Tafuta

Askofu  Luis Marín de San Martín,ametuliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Upendo. Askofu Luis Marín de San Martín,ametuliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Upendo. 

Marín de San Martín ateuliwa kuwa Mkuu mpya wa Sadaka ya Papa

Nafasi ya Kardinali Krajewski aliyeteuliwa kuwa Askofu Mkuu Łódź nchini Poland inachukuliwa na Askofu Luis Marín de San Martín(OSA)ambaye hadi uteuzi huo alikuwa Katibu Mkuu Msaidizi wa Sinodi na moja kwa moja anakuwa Askofu Mkuu.

Vatican News

Askofu wa Kiagostiniani wa Hispania Luis Marín de San Martín ndiye Msimamizi mpya wa Sadaka ya Papa. Askofu mpya mwenye umri wa miaka 64, ambaye Papa Francisko alimteua kuwa katibu Mkuu msaidizi wa Sekretarieti Kuu ya Sinodi mnamo 2021, aliteuliwa tarehe 12 Machi 2026 na Baba Mtakatifu Leo XIV,  kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Upendo, akimrithi Kardinali Konrad Krajewski, ambaye alikuwa ameshikilia wadhifa huo tangu 2013. Wakati huo huo, Papa alimteua Kardinali wa Poland kuwa Askofu Mkuu mpya wa jiji la Łódź, katika nchi yake alikozaliwa. Msimamizi wa Sadaka ya Kipapa Mpya Askofu, alizaliwa tarehe 12 Agosti 1961, huko Madrid nchini Hispania. Baada ya Kujiunga na Shirika, Marín de San Martín alifunga nadhiri za kwanza katika Shirika la Mtakatifu Agostino mnamo tarehe 5 Septemba  1982, na nadhiri za daima mnamo tarehe 1  Novemba 1985.  

Wadhifa wake

Alipewa daraja la Upadre mnamo tarehe 4 Juni 1988, na baada ya mafunzo akapata shahada ya udaktari katika Taalimungu Takatifu, kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Comillas katika mji mkuu wa Hispania. Alikuwa Mkufunzi katika Seminari Kuu ya Tagaste, Los Negrales (1996-1999), Mkuu wa Kanda ya Shirika (1999-2002), na Mkuu wa Monasteri ya Mtakatifu  María de La Vid (2002-2008). Pia alihudumu kama Profesa wa Taalimungu katika vitivo vya Kiagostiniani huko Los Negrales, Mtakatifu Laurent de El Escorial, na Valladolid. Tangu 2004, amekuwa Profesa mgeni katika Kitivo cha Taalimungu cha Kaskazini mwa Hispania huko Burgos. Yeye ndiye mwandishi mkuu wa kumbukumbu ya Shirika lake la Mtakatifu Agostino, na msaidizi Mkuu wa Shirika hilo la Waagostiniani, wakati  anakaa katika Taasisi ya Tasaufi ya Kiagostiniani.

Mwanzo wa Safari

"Sasa ninaanza safari yangu kama mchungaji utume wa Sadaka ya Papa na Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Upendo. Huduma nzuri na inayohitaji juhudi," aliandika Mwenyekiti mpya katika chapisho refu kwenye akaunti yake ya kibinafsi ya Facebook. "Natumaini kuendeleza juhudi na kazi nzuri iliyofanywa na Kardinali Konrad Krajewski katika miaka ya hivi karibuni. Ninataka kuwaweka maskini katikati na kujiruhusu kupingwa na kilio chao, ambacho ni cha Kristo. Kama Mkristo, kama mchungaji, lazima nifichue uso wa kweli wa upendo wa kimungu." "Ninajua siko peke yangu," aliandika Askofu huyo. " Mimi ni mtoto wa Kanisa, mimi ni sehemu ya watu wa Mungu. Tutembee pamoja. Kwa hivyo, kwa unyenyekevu na uaminifu, ninawaomba marafiki zangu na wote wanaotaka kunisaidia kuniombea. Ninahitaji msaada thabiti wa maombi. Kwa mengine yote, ninajua kwamba huduma kwa maskini inahusiana na Injili. Wanatuinjilisha."

Katibu Msaidizi wa Sekretarieti ya Sinodi:Miaka ya utajiri Mkubwa

Katika chapisho hilo hilo, Askofu Marín de San Martín pia anakumbuka miaka yake kama katibu msaidizi wa Sinodi: miaka "ya utajiri mkubwa. Ninasisitiza uhai wa Kanisa, ambao huondoa vivuli vya kukata tamaa na kujiuzulu. Nimekutana na 'watakatifu wengi wa karibu' ambao, kwa unyenyekevu, ujasiri, na furaha, wanaishi na kutoa ushuhuda wa imani yao na kupanda Injili," ameandika. Anatoa heshima maalum kwa Kardinali Mario Grech na "wenzake wote wa Sekretarieti Kuu ya Sinodi." Askofu pia anatoa shukrani zake kwa Papa Francisko ambaye hasahauliki, ambaye aliniita kushirikiana katika wakati huu wa upya na matumaini. Kwa nia njema, nimejitahidi kuimarisha ushirika, kukuza uwajibikaji wa pamoja uliotofautiana, na kukuza utume wa uinjilishaji.

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku bonyeza hapa: Just click here.

12 Machi 2026, 15:20