Kwaresima Ni Hija ya Maisha ya Kiroho: Toba, Wongofu wa Ndani Na Huruma
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka huu 2026 kinanogeshwa na ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV kwa kauli mbiu: “Kusikiliza na kufunga: Kwaresima kama Kipindi cha Wongofu wa ndani.” Kwaresima ni kipindi ambacho Kanisa kama Mama na Mwalimu, anawaalika watoto wake kutoa kipaumbele cha pekee kwa Fumbo la Mungu katikati ya maisha yao, ili imani ipate tena nguvu na mioyo ya waamini isipotee katikati ya mahangaiko na bughudha za maisha ya kila siku. Kila safari ya wongofu wa ndani huanza pale waamini wanaporuhusu Neno la Mungu liwafikie na kulikaribisha kwa moyo wa unyenyekevu. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kuna uhusiano kati ya karama ya Neno la Mungu, Nafasi ya Ukarimu na mabadiliko ambayo Neno hili linaleta. Kwa sababu hiyo, safari ya Kwaresima inakuwa ni fursa muafaka ya kusikiliza sauti ya Mungu na hivyo kupyaisha tena maamuzi ya kumfuasa Kristo Yesu, kwa kutembea katika njia ile iendayo Yerusalemu ambako Fumbo la Pasaka yaani: Mateso, kifo na ufufuko vinapata utimilifu wake. Kipindi cha Kwaresima kimsingi kinasimikwa katika nguzo kuu nne: Sala na Kufunga; Tafakari ya Neno la Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.
Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 4 Machi 2026 amewakumbusha waamini kwamba, Kwaresima ni hija ya maisha ya kiroho inayosimikwa katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani; kwa kuomba huruma na amani ya Mungu ili iweze kutawala akili na nyoyo za watu. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kumfungulia Mungu akili na nyoyo zao, tayari kupokea neema na baraka, zinazowawesha kuwa kweli ni mashuhuda wa furaha ya Injili. Kipindi cha Kwaresima ni fursa ya kupyaisha maisha ya kiroho kama mtu binafsi na kama familia, ili waweze kuwa ni vyombo vya Mungu katika ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa na hivyo kuendelea kumtambua na kumkiri Kristo Yesu kuwa ni utimilifu wa matumaini ya Kikristo. Huu ni mwaliko kwa namna ya pekee kwa vijana wa kizazi kipya kuwa ni vyombo na mashuhuda amini wa Injili ya Kristo Yesu inayomwilishwa katika medani mbalimbali za maisha ya waamini. Kwa wagonjwa, Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika kumwilishwa ndani mwao fadhila uvumilivu, huku wakiunganisha mateso yao na yale ya Kristo Yesu aliyejitoa sadaka Msalabani ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.
Baba Mtakatifu Leo XIV anakaza kusema, Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanazisaidia familia kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia, kwa kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Baba Mtakatifu Leo XIV anawataka wanafamilia kujenga na kudumisha utamaduni wa sala ndani ya familia waliyoianzisha.
Baba Mtakatifu Leo XIV amewakumbusha waamini kwamba, tarehe 4 Machi, Mama Kanisa anaadhimisha Kumbukumbu ya Mtakatifu Casmiri, Mfalme wa Poland, aliyezaliwa tarehe 3 Oktoba mwaka 1458, huko Wawel, Krakow, Poland. Alikuwa ni mwana wa mfalme Casimir IV, ambaye katika maisha yake, alijitesa sana kama kielelezo cha toba na wongofu wa ndani. Akafariki dunia tarehe 4 Machi 1884 huko Lithuania na kutangazwa kuwa Mtakatifu na Papa Leo X kunako mwaka 1521. Alipenda kusali kwa maneno yafuatayo: “Omni die dic Mariae” Yaani: “Mwambie Bikira Maria Kila Siku”, kielelezo cha kujiweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa.
