Tafuta

2026.03.18 Udienza Generale

Katika kumbukizi ya Amoris laetitia,Papa aitisha Mkutano na marais wa Maaskofu Oktoba 2026

Katika fursa ya maadhimisho ya miaka 10 tangu kuchapishwa kwa Waraka wa Kitume wa Papa Francisko wa Amoris Laettia,Papa Leo XIV amewaalika Marais wa Mabaraza ya Maaskofu Ulimwenguni kwa Mkutano mnamo Oktoba 2026 ili kusikilizana na ufahamu wa Sinodi kuhusu hatua zinazohitajika kutangaza Injili kwa familia leo hii zilizoathiriwa na mabadiliko mengi na kushirikisha kile kinachofikiriwa katika Makanisa mahalia.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

"Kwa kutambua mabadiliko yanayoendelea kuathiri familia, nimeamua kuwaita Marais wa Mabaraza ya Maaskofu kutoka ulimwenguni kote mnamo Oktoba 2026, ili kuendelea, kupitia kusikilizana kwa pamoja, na utambuzi wa sinodi kuhusu hatua zinazohitajika kutangaza Injili kwa familia leo, kwa kuzingatia Amoris Laetitia na kuzingatia kile kinachotimizwa katika Makanisa mahalia.” Ndivyo unahimimishwa Ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV uliotolewa tarehe 19 Machi 2026, wakati Mama Kanisa akiwa anadhimisha siku Kuu ya Mtakatifu Yosefu, Mlezi na Msimamizi wa Familia Takatifu ya Nazareti na miaka 10 tangu kuchapishwa kwa Waraka wa Papa Francisko kuhusu Upendo wa Ndoa ndani ya Familia.

"Familia ni msingi wa jamii na zawadi kutoka kwa Mungu"

Kwa njia hiyo katika ujumbe huo, Papa anaanza kusema  "Kaka  na dada wapendwa! Mnamo tarehe 19 Machi 2016, Papa Francisko alilipatia Kanisa lote ujumbe wa mng'ao wa matumaini kuhusu upendo wa ndoa na familia: Wosia wa Kitume wa Amoris Laetitia, matunda ya miaka mitatu ya utambuzi wa Sinodi ulioungwa mkono na Mwaka Mtakatifu wa Huruma.  Baba Mtakatifu katika ujumbe huo anabainisha kuwa “Katika maadhimisho haya ya miaka kumi, tunataka kumshukuru Bwana kwa msukumo uliotolewa kwa ajili ya kujifunza na uongofu wa kichungaji wa Kanisa na kumwomba ujasiri wa kuendelea na safari hii, tukiikaribisha Injili upya kila wakati, katika furaha ya kuweza kuitangaza kwa wote. Kama Mtaguso wa Pili wa Vatican unavyofundisha, familia ni "msingi wa jamii," zawadi kutoka kwa Mungu, na "shule ya utajiri wa binadamu." Kupitia Sakramenti ya Ndoa, wanandoa Wakristo huunda aina ya "Kanisa la nyumbani," ambalo jukumu lake ni muhimu kwa elimu na uenezaji wa imani. Baada ya msukumo wa Mtaguso, Nyaraka mbili za  Kitume: Familiaris consortio wa Mtakatifu Yohane Paulo II kunako  1981 na  Amoris laetitia (AL). Zote mbili zimechochea kujitolea kwa Kanisa kimafundisho na kichungaji katika kuwahudumia vijana, wenzi wa ndoa, na familia. Kutambua "mabadiliko ya kianthropolojia na kiutamaduni," (AL, 32).

"Kusikiliza furaha na matumaini yao, huzuni na wasiwasi wao"

Baada ya kuimarika zaidi katika kipindi cha miaka thelathini na mitano iliyopita, Papa Francisko alijitahidi zaidi kulihusisha Kanisa katika njia ya utambuzi wa sinodi. Hotuba yake mnamo 17 Oktoba 2015, iliyotolewa wakati wa Mkutano Mkuu wa Kawaida wa XIV wa Sinodi ya Maaskofu kuhusu Familia, ilitoa wito wa "kusikilizana kwa pamoja" ndani ya Watu wa Mungu, "wote wakimsikiliza Roho Mtakatifu, 'Roho wa Ukweli' (Yn 14:17), ili kujua 'anachowaambia Makanisa' (Ufu 2:7)."Alifafanua kwamba "haiwezekani kuzungumza kuhusu familia bila kushauriana na familia, kusikiliza furaha na matumaini yao, huzuni na wasiwasi wao." Kwa kukusanya matunda ya utambuzi wa sinodi, Amoris laetitia unatoa fundisho la thamani ambalo tunapaswa kuendeleza kulitia ndani leo hii: tumaini la kibiblia la uwepo wa Mungu wenye upendo na  Huruma, ambao unaturuhusu kuishi "historia za mapendo” hata  zinapopitiwa na migogoro ya kifamilia" (AL8); mwaliko wa kukubali "mtazamo wa Yesu" (AL, 60) na kuhimiza bila kuchoka "kukua, kuimarisha na kuzidisha upendo wa ndoa na familia" (AL, 89); wito wa kugundua kwamba upendo katika ndoa "hutoa uhai kila wakati" (AL, 165) na kwamba ni "halisi" hasa katika njia yake "iliyo na kikomo na ya kidunia" (AL, 113), kama fumbo la Umwilisho linavyotufundisha.

Ili kuhudumia utume wa kutangaza Injili kwa vizazi,lazima kujifunza kuamsha uzuri wa wito wa ndoa

Papa Francisko anathibitisha "hitaji la kuendeleza njia mpya za kichungaji" (AL, 199) na "kuimarisha elimu ya watoto" (AL, sura ya VII), huku akilialika Kanisa "kusindikiza, kutambua na kuunganisha udhaifu" (AL, sura ya VIII), kushinda dhana ya kupunguza uzito wa kawaida, na kukuza "kiroho kinachotokana na maisha ya familia" (AL, 313). Kama nilivyopata fursa ya kuwaambia vijana waliokusanyika huko Tor Vergata wakati wa Jubilei ya Matumaini, "udhaifu [...] ni sehemu ya ajabu tuliyo nayo": hatukuumbwa "kwa ajili ya maisha ambapo kila kitu kinachukuliwa kuwa cha kawaida na kimetengenezwa, bali kwa ajili ya uhai unaozaliwa upya kila mara katika kutoa, kwa upendo." Ili kutumikia utume wa kutangaza Injili ya familia kwa vizazi vichanga, ni lazima tujifunze kuamsha uzuri wa wito wa ndoa hasa kwa kutambua udhaifu wetu, ili kuamsha "imani katika neema" (AL, 36) na hamu ya Kikristo ya utakatifu. Pia tunapaswa kusaidia familia, hasa zile zinazoteseka kutokana na aina nyingi za umaskini na vurugu zilizopo katika jamii ya kisasa.

"Mabadiliko ya sasa ya haraka yanahitaji umakini maalum wa kichungaji kwa familia"

Tunamshukuru Bwana kwa familia ambazo, licha ya magumu na changamoto, zinaishi "kiroho cha upendo wa familia [...] unaoundwa na maelfu ya ishara halisi na kweli" (AL, 315). Pia ninatoa shukrani zangu kwa Wachungaji, wafanyakazi wa kichungaji, Vyama vya Waamini, na Harakati za Kikanisa zinazohusika katika huduma ya familia. Wakati wetu unaoneshwa na mabadiliko ya haraka ambayo, hata zaidi ya miaka kumi iliyopita, yanahitaji uangalifu maalum wa kichungaji kwa familia, ambazo Bwana amewakabidhi jukumu la kushiriki katika utume wa Kanisa wa kutangaza na kushuhudia Injili. Hakika, kuna maeneo na hali ambazo Kanisa "haliwezi kuwa chumvi ya dunia" isipokuwa kupitia waamini walei na, hasa, familia.

Oktoba 2026 Marais wa Mabaraza ya Maaskofu wanaitwa Roma

Kwa hivyo, kujitolea kwa Kanisa katika eneo hilo lazima kupyaishwe  na kuimarishwa, ili wale ambao Bwana anawaita kwenye ndoa na familia waweze kuishi upendo wao wa ndoa katika Kristo na vijana waweze kuhisi kuvutiwa na nguvu ya wito wa ndoa katika Kanisa. Kwa kutambua mabadiliko yanayoendelea kuathiri familia, nimeamua kuwaita Marais wa Mabaraza ya Maaskofu kutoka ulimwenguni kote mnamo Oktoba 2026, ili kuendelea, kupitia kusikilizana kwa pamoja, na utambuzi wa sinodi kuhusu hatua zinazohitajika kutangaza Injili kwa familia leo, kwa kuzingatia Amoris Laetitia na kuzingatia kile kinachotimizwa katika Makanisa mahalia.”Papa anahitimisha akikabidhi safari hiyo  kwa maombezi ya Mtakatifu Yosefu, mlezi wa Familia Takatifu ya Nazareti.

BARUA YA PAPA

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku bonyeza hapa: Just click here.

19 Machi 2026, 12:17