Tafuta

Kardinali Polycarp Pengo ni Jabali la imani, maadili, utu wema na shughuli za kichungaji, mfano bora wa kuigwa Kardinali Polycarp Pengo ni Jabali la imani, maadili, utu wema na shughuli za kichungaji, mfano bora wa kuigwa 

Kardinali Polycarp Pengo: Jabali la: Imani, Maadili na Utume

Kardinali Pengo alikuwa ni zawadi adimu na adhimu kutoka kwa Mungu kwa ajili ya Tanzania. Alikuwa ni mtu mwenye imani thabiti iliyomwilishwa katika ukweli na upendo na kwamba, ukweli na upendo ni chanda na pete. Nguvu ya maisha na ushuhuda wake anasema Askofu Wolfgang Pisa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), ilipata chimbuko lake katika: Neno la Mungu, Maisha ya Sala, Tafakari ya Rozari Takatifu na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu.

Na Sarah Pelaji na Veranda Malima Kigeso – Pugu, Dar es Salaam, Tanzania

Askofu Wolfgang Pisa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), anasema Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, alikuwa ni zawadi adimu na adhimu kutoka kwa Mungu kwa ajili ya Kanisa la Tanzania. Alibahatika kuwa na vipaji pekee alivyovitumia kikamilifu tangu akiwa Padre, hadi Kardinali, akaonesha ukomavu wa imani, chachu ya mabadiliko; maadili na utu wema. Kardinali Pengo alikuwa ni mtu mkweli, Mwalimu na Mfuasi amini wa Kristo Yesu aliyewashirikisha wengine, katika uongozi wake: Utoto Mtakatifu, WAWATA na UWAKA wakapata nyajibu katika maisha na utume wa Jimbo kuu la Dar es Salaam. Mchakato wa tegemeza Jimbo ulioasisiwa kunako mwaka 1994 kwa sasa umeigwa na Majimbo mbalimbali nchini Tanzania. Kardinali Pengo alikuwa ni mtu mwenye imani thabiti ikamwilishwa katika ukweli na upendo na kwamba, ukweli na upendo ni chanda na pete. Nguvu ya maisha na ushuhuda wake anasema Askofu Wolfgang Pisa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), ilipata chimbuko lake katika: Neno la Mungu, Maisha ya Sala, Tafakari ya Rozari Takatifu na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu. Kardinali Pengo alijinasua na malimwengu, kiasi kwamba, ameaga dunia bila ya kuacha akaunti yoyote ya Benki!

Hayati Kardinali Pengo Askofu Mkuu Mstaafu Jimbo kuu la Dar es Salaam.
Hayati Kardinali Pengo Askofu Mkuu Mstaafu Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Tanzania imeungana na Kanisa Katoliki Barani Afrika na dunia kwa ujumla kumuaga kwa heshima na taadhima Hayati Polycarp Kardinali Pengo, aliyefariki Februari 19, 2026 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, JKCI, na kuzikwa katika Kituo cha Hija cha Pugu, Jimbo kuu la Dar es Salaam, Jumamosi tarehe 28 Februari 2026. Maelfu ya waombolezaji walijitokeza kushiriki Misa ya Mazishi iliyoongozwa na Askofu mkuu Yuda Thaddaeus Ruwa'ichi wa Jimbo kuu la Dar Es Salaam. Sala ya buriani ilitolewa na Kardinali Protase Rugambwa, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora na Ibada ya mazishi iliongozwa na Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar (SECAM), Kardinali Fridolin Ambongo Besungu, akishirikiana na viongozi wengine waandamizi wa Kanisa kutoka Afrika Mashariki na Kati. Mavazi meupe yaliyotumika katika Ibada ya Mazishi ya Kardinali Pengo, ni kielelezo cha imani na matumaini juu ya Ufufuko wa wafu, maisha na uzima wa milele. Hiki ni kielelezo cha ushindi wa Kristo Yesu dhidi ya dhambi na mauti. Mkazo unawekwa kwenye chemchemi ya maisha mapya kutoka kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, badala ya kubaki katika mtazamo wa maombolezo tu! Miongoni mwa wageni wa kimataifa waliohudhuria ni Kardinali Antoine Kambanda, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Kigali, Rwanda, pamoja na Askofu Charles Kasonde, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA.  Serikali ya Tanzania iliwakilishwa na Makamu wa Rais, Dr. Emmanuel Nchimbi, aliyetoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Hayati Kardinali Pengo alikuwa Jabali la: Imani, Maadili na Utume
Hayati Kardinali Pengo alikuwa Jabali la: Imani, Maadili na Utume

Tumaini Katika Imani: Katika mahubiri yake, Askofu mkuu Ruwa’ichi alisema majaribu ya maisha ni njia ya utakaso na kuimarishwa na siri ya Mungu aliweka msisitizo juu ya tumaini la Kikristo akijibu swali, “Kwa nini watu wema wanakufa?” Alieleza kuwa kifo si ishara ya kuachwa na Mungu bali ni sehemu ya safari ya utakaso na kuungana naye. Akirejea simulizi la Kibiblia la Lazaro, alikumbusha waamini maneno ya Yesu: “Mimi ndimi ufufuo na uzima” Alisisitiza kuwa maisha ya mwanadamu hayaishii duniani, bali yanaendelezwa katika maisha na uzima wa milele. Kristo Yesu katika majadiliano na Martha dada yake Lazaro alimfunulia kuhusu Fumbo la Kifo, Maisha na Uzima wa milele. Wakristo wanamwamini Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu; msindi na mtukufu; Mmwokozi, tegemeo na kimbilio la waamini na kwamba, Kristo Yesu ni chemchemi ya uzima mpya. Mtu wa Mungu anapata ukamilifu kupitia imani, uadilifu na uchaji wa Mungu; kwa kujenga maisha ya fadhila: Upendo, haki, ukweli, huruma na upendo pamoja na watu wengine. Hata Kardinali Polycarp Pengo ataishi pamoja na Kristo Yesu, msingi wa imani, utume wake wa uinjilishaji na ushuhuda wa tunu msingi za Kiinjili, kwa maneno lakini Zaidi kwa njia ya ushuhuda wa maisha yake adili na matakatifu “Tunapomsindikiza Kardinali Pengo, tujenge fadhila zinazompendeza Mungu,” alihimiza.

Kardinali Pengo alisimama kidete kutetea haki, amani na utulivu
Kardinali Pengo alisimama kidete kutetea haki, amani na utulivu

Miaka ya Huduma na Uongozi: Kardinali Pengo alitumikia Kanisa kwa zaidi ya miaka 55 ya upadri na zaidi ya miaka 40 kama Askofu, akihudumu katika majimbo mbalimbali kabla ya kuliongoza Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Alijulikana kwa msimamo wake thabiti katika maadili, uwajibikaji wa kijamii na mshikamano wa kitaifa. Akizungumza wakati wa Ibada ya mazishi, Kardinali Ambongo alimwelezea Marehemu Pengo kama “Nabii wa utu na amani barani Afrika,” aliyekuwa na sauti ya maadili katika masuala ya haki msingi za binadamu, maridhiano na heshima ya maisha. Wakati wa uongozi wake ndani ya SECAM (2007–2009), alihamasisha ukuaji wa Kanisa Barani Afrika, akisisitiza kuwa uinjilishaji hauwezi kutenganishwa na haki, amani na utu wa binadamu. Kwa upande wake, Askofu Kasonde alisema AMECEA itamkumbuka Kardinali Pengo kwa mchango wake mkubwa katika kuimarisha mshikamano wa kikanda na kujitegemea kwa Kanisa la Afrika Mashariki. Kiongozi wa Taifa na Daraja la Maridhiano: Akitoa salamu za serikali, Makamu wa Rais Nchimbi alimwelezea Kardinali Pengo kama kiongozi aliyesisitiza mambo matatu makuu: uadilifu wa binafsi, nidhamu ya kichungaji, na huduma kwa wanyonge. Alisema marehemu alifundisha na kuishi maadili aliyoyahubiri, akibaki imara hata katika udhaifu wa mwili. “Kanisa limechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya taifa kupitia elimu, afya na huduma za kijamii. Kardinali Pengo alikuwa sehemu ya mchango huo,” alisema Nchimbi, akihimiza Watanzania kuenzi urithi wake kwa kuishi kwa uwajibikaji na mshikamano badala ya migawanyiko ya kisiasa.

Hili ni tukio ambalo limewakusanya watanzania wengi katika umoja na utofauti wao
Hili ni tukio ambalo limewakusanya watanzania wengi katika umoja na utofauti wao

Askofu Wolfgang Pisa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), ametoa salamu za rambirambi kwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Yuda Thaddaeus Ruwa'ichi, Askofu msaidizi, mapadri, watawa na waamini wote wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam pamoja na Kanisa lote Tanzania kufuatia kifo cha Hayati Polycarp Kardinali Pengo. Askofu Pisa amesema Kanisa linamshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha ya Kardinali Pengo, akimtaja kama mchungaji na kiongozi aliyekuwa mfano wa kuigwa katika utume wake wa kuhubiri na kuishi Injili kwa matendo. Alikumbusha safari yake ya utumishi kuanzia Jimbo Katoliki la Sumbawanga hadi Jimbo kuu la Dar es Salaam, ambako alihitimisha huduma yake ya kichungaji kwa uaminifu na bidii. “Tunasherehekea utume wake na tunamuombea Mungu amjalie tuzo ya milele,” alisema Askofu Pisa, akirejea mfano wa Mtakatifu Polycarp Askofu na Shahidi kama ishara ya uaminifu wa kudumu kwa Kristo. Aliongeza kuwa marehemu aliitumikia Kanisa bila kuchoka na alisimama imara katika wito wake hadi mwisho wa maisha yake. Amewahimiza waamini kutumia kipindi hiki kama muda wa toba, sala na kutafakari, wakidumu katika imani na matumaini.

Askofu mkuu mkuu Angelo Accatino ametoa salam za Papa Leo XIV
Askofu mkuu mkuu Angelo Accatino ametoa salam za Papa Leo XIV

Kwa upande wake, Askofu mkuu Angelo Accattino, Balozi wa Vatican nchini Tanzania amesema Kanisa linaomboleza kwa huzuni kubwa lakini pia kwa shukrani kwa mchango wa Kardinali Pengo. Alimwelezea marehemu kama zawadi kwa Kanisa la Tanzania akiwa: Padri, Askofu na hatimaye kama Kardinali.Askofu Mkuu Accattino alikumbusha kuwa Kardinali Pengo, aliyekuwa Padri wa Jimbo la Sumbawanga, anakumbukwa kwa juhudi zake za kichungaji na kielimu, hususan katika eneo la Seminari kuu ya Kipalala alikohudumu kama Jaalimu mwenye bidii. Alitaja pia huduma yake kama Askofu wa Nachingwea na baadaye Askofu Mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, akisisitiza mchango wake mkubwa katika kukuza Kanisa na kuimarisha majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni kati ya Kanisa na Serikali. Alibainisha kuwa karama na uongozi wake vilimwezesha kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya Kanisa Barani Afrika na Vatican, ikiwemo uongozi ndani ya SECAM (2007–2009), ambapo alijitokeza kama mtetezi wa haki za kijamii, umoja na uwajibikaji wa kimaadili katika kukabiliana na changamoto za kijamii. Ubalozi wa Vatican nchini Tanzania umetoa pole kwa familia ya marehemu, Jimbo Kuu la Dar es Salaam na waamini wote, ukimwombea Kardinali Pengo apokee rehema ya Mungu na uzima wa milele.

Askofu Ruwa'ichi ameongoza Ibada ya Misa Takatifu
Askofu Ruwa'ichi ameongoza Ibada ya Misa Takatifu

Salamu za rambirambi pia zimetumwa na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kutoka Uganda, Kenya, Zambia, Malawi na Ethiopia, yakionesha mshikamano wa Kikanda na Kimataifa na Kanisa la Tanzania katika kipindi hiki cha maombolezo. Kwa niaba ya Mufti mkuu wa Tanzania, mwakilishi wake amesema taifa linamsindikiza kiongozi aliyelitumikia kwa moyo wa kujitoa na kwa maslahi mapana ya Tanzania. Alisisitiza kuwa kumuenzi Kardinali Pengo ni kuenzi hekima, utu na uzalendo aliouishi. “Ubora wa mtu hupimwa kwa uwezo wake wa kuleta umoja na maelewano kati ya watu,” alisema, akiongeza kuwa marehemu alipendeza mbele za Mungu na wanadamu kwa maisha yake ya huduma na maadili. Kwa ujumla, viongozi wa dini na serikali wamekubaliana kuwa urithi wa Kardinali Pengo utaendelea kuishi katika historia ya Kanisa na Taifa kama alama ya uongozi wa kiroho uliosimama juu ya imani, uadilifu na mshikamano na upendo. Sauti ya Kinabii Barani Afrika: Katika hotuba yake, Kardinali Ambongo alieleza kuwa Bara la Afrika limepoteza sauti yenye busara na mamlaka ya kimaadili. Alikumbusha jinsi Kardinali Pengo alivyoeleza Kanisa la Afrika kama “Kanisa changa katikati ya uinjilishaji,” akihamasisha Jumuiya Ndogondogo za Kikristo kama uti wa mgongo wa ukuaji wa Kanisa Barani Afrika. Alisisitiza kuwa kwa Kardinali Pengo, tunu msingi za Kiinjili sanjari na Maadili ya Kikristo yaliendana na maadili ya kijamii yanayolenga kujenga na kukuza: umoja, haki na heshima kwa kila mtu.

Kardinali Protase akaongoza Sala ya Buriani
Kardinali Protase akaongoza Sala ya Buriani

Urithi wa Elimu; Maadili Na Utu wema: Mbali na huduma yake ya kichungaji, Kardinali Pengo alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino Tanzania (SAUT), akichangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya elimu ya juu nchini. Alikumbukwa pia kwa mchango wake katika kuimarisha majukwaa ya mazungumzo ya kidini, akiamini kuwa ushirikiano ni msingi wa amani na maendeleo. Viongozi wa dini ya Kiislamu waliwakilishwa katika mazishi hayo na kumpongeza kwa kujitolea kwake kwa maslahi mapana ya taifa. Walisema kuondoka kwake ni wito kwa Watanzania kuendeleza hekima, utu na uzalendo aliouishi. Familia ya hayati Kardinali Pengo imeongozwa na dada yake, bibi Helena Khamsini ambaye kwa niaba ya familia amelishukuru kanisa kwa kumlea na kumtunza kaka yake toka alipokuwa na umri wa miaka 27 (alipopata daraja la upadre) hadi alipofariki dunia Februari 19, 2026 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), jijini Dar es salaam. Mwisho wa Safari na Mwanzo wa Urithi: Akihitimisha Ibada, Askofu mkuu Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam aliwashukuru waamini na viongozi wote kwa kujitokeza kwa wingi, akiwahimiza kuendeleza moyo wa kujituma na kujitoa aliouonesha Kardinali Pengo hadi mwisho wa maisha yake. “Tumwombee apate pumziko la milele, na sisi tuishi kwa imani na matumaini kama alivyoishi yeye,” alisema. Kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla, mazishi ya Kardinali Polycarp Pengo hayakuwa tu tukio la maombolezo, bali pia yalikuwa Tamko la kitaifa na kimataifa kuhusu nguvu ya uongozi wa kiroho unaojengwa juu ya maadili, haki na huduma kwa wote. Urithi wake unabaki kuwa mwanga angavu kwa kizazi cha sasa na kile kijacho.

Kardinali Abongo, SECAM akaongoza Ibada ya Maziko
Kardinali Abongo, SECAM akaongoza Ibada ya Maziko

Ni katika muktadha wa Fumbo la Kifo katika maisha ya mwanadamu, Baba Mtakatifu Leo XIV amemtumia salam za rambirambi Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania kufuatia kifo cha Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar Es Salaam kilichotokea tarehe 19 Februari 2026 majira ya Saa 4:00 Usiku, akiwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Jijini Dar es Salaam. Baba Mtakatifu Leo XIV anapenda kutoa salama zake za rambirambi kwa familia ya Mungu Jimbo kuu la Dar es Salaam. Anamshukuru Mungu kwa huduma ya Kiaskofu aliyoitekeleza katika majimbo kadhaa nchini Tanzania. Anamkumbuka hasa kwa sadaka na majitoleo yake katika malezi na majiundo ya awali na endelevu ya Makleri, Jimbo kuu la Dar es Salaam. Kati ya Mwaka 2007 hadi mwaka 2009 alichaguliwa kuwa Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM, akafanikiwa kuwaunganisha Maaskofu wa Kusini mwa Afrika na Kaskazini, kwa kukazia moyo wa SECAM kujitegemea kwa rasilimali watu na vitu. Na katika maisha na utume wake kama Kardinali, aliteuliwa kuwa Mjumbe wa Mabaraza mbalimbali ya Kipapa kwa ajili ya huduma kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu Leo XIV anapenda kuiweka roho ya Kardinali Polycarp Pengo, Mchungaji mnyenyekevu, katika huruma ya Kristo Yesu, Mchungaji Mwema. Kwa waombolezaji na wote walioguswa na msiba huu mzito, huku wakiwa na tumaini la ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele, anapenda kuwapatia faraja na baraka zake za kitume!

Buriani Kardinali Pengo
01 Machi 2026, 17:51