Jubilei ya Miaka 100 ya Jimbo La Kijeshi Italia: 1926-2026: Haki, Amani na Utulivu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mama Kanisa daima ametaka kutoa huduma ya maisha ya kiroho kwa Askari kwa bidii ya kusifiwa na kwa namna inayolingana na mahitaji mbalimbali. Askari, kwa hakika wanaunda tabaka mahususi la kijamii kutokana na hali mahususi ya maisha yao ya kijeshi iwe kwa hiari au kwa mujibu wa sheria za nchi; wanahitaji aina madhubuti na maalum ya usaidizi wa shughuli za kichungaji na kwamba, Mababa wa Kanisa wameona na kutambua hitaji hili muhimu katika maisha na utume wa Askari sehemu mbalimbali za dunia, kama walivyoagiza Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Lengo kuu ni kujenga na kudumisha amani, usalama na uhuru wa watu wa Mungu, ili hatimaye, Askari waweze kuchangia katika muktadha wa amani na utulivu. Hii ni kutokana na kuwepo kwa mabadiliko makubwa ya taaluma ya kijeshi, katika uhalisia wa maisha ya mwanadamu. Ndiyo maana Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walishauri kuanzishwa kwa majimbo ya kijeshi, ili Kanisa lisaidie utendaji wa shughuli za kichungaji wenye lengo la kunufaisha mema ya roho za wanajeshi. Rej. Christus domini, 43. Majimbo ya Kijeshi ndani ya Kanisa Katoliki yalianzishwa kunako tarehe 6 Machi 1925. Mtakatifu Yohane Paulo II kunako tarehe 26 Aprili 1986 akachapisha Katiba ya Kichungaji Kuhusu Huduma ya Kiroho Kwa Askari Jeshi: “Spirituali Militum Curae.” Kwa hakika, Mapadre wahudumu wa maisha ya kiroho kwenye Majimbo ya Kijeshi ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na maridhiano; ni walinzi na watunzaji wa Injili ya matumaini kwa watu waliovunjika na kupondeka moyo. Jimbo la Kijeshi nchini Italia: “Ordinariato militare per l'Italia” linaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwake kunako mwaka 1926, kwa ushiriki wa Baba Mtakatifu Leo XIV ambaye katika maisha na utume wake, anayendelea kujipambanua kuwa ni shuhuda wa haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa.
Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Jimbo la Kijeshi nchini Italia yananogeshwa na kauli mbiu “Inter, Arma, Caritas” Yaani: “Kati ya Silaha, Upendo.” Lengo ni kumleta Kristo Yesu katika mishipa ya ubinadamu, kupyaisha na kushiriki utume, kwa kuangalia siku zijazo kwa utulivu na kwa kufanya maamuzi ya ujasiri. Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Jimbo la Kijeshi nchini Italia ni tukio linalohifadhi kumbukumbu muhimu na unabii. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi tarehe 7 Machi 2026 amekutana na wajumbe wanaounda Jimbo la Kijeshi nchini Italia na kuwatia shime kuendeleza majadiliano na ushirikiano na Majimbo megine ya kijeshi yaliyo enea sehemu mbalimbali za dunia. Baba Mtakatifu Leo XIV katika hotuba yake amekazia umuhimu wa Jamii kutunza kumbukumbu yake na kwamba, kwa Mama Kanisa, hii ni dhamana inayozalisha unabii, kielelezo cha Mwenyezi Mungu anayeingia katika historia ya mwanadamu, kwani imani kwa Kristo Yesu inafumbatwa katika historia halisi katika Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai.
Jubilei ya Miaka Mia Moja tangu kuanzishwa kwa Jimbo la Kijeshi nchini Italia, ni historia ambayo imeundwa na wanajeshi, wanaotembea ndani ya Kanisa, huku wakisindikizwa na viongozi wao wa kiroho katika siku za mwanga wa amani pamoja na zile siku za “kimbembe cha vita”, kwa sadaka kubwa, ujasiri na majitoleo ambayo yamesaidia sana kukua na kuendelea kwa jamii na wakati mwingine hata kwa sadaka ya maisha yao! Kadiri ya Mafundisho ya Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa anasema, historia ni mahali pa kujenga utamaduni wa upendo kwa kutekeleza kwa dhati Amri ya Kristo Yesu ya kupendana kama alivyowapenda. Rej. Yn 15:12 na kwamba, viongozi wa maisha ya kiroho wamemwilisha ndani mwao, wakaushuhudia na hata wakati mwingi wakayamimina maisha yao. Katika huduma zao za kichungaji, Kristo Yesu anaendelea kuwachunga kondoo wake, kwa njia ya ushuhuda wa maisha, katika kutangaza na kushuhudia Injili; katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu na Sakramenti nyingine za Kanisa; katika usikivu wenye uvumilivu na kwamba, amani ni tunda la haki.
Dhamana na nafasi ya wahudumu wa maisha ya kiroho kwenye kambi za kijeshi inajionesha hasa katika kuunda dhamiri nyofu na kwamba, viongozi hawa wanakuwa ni vyombo vya huduma ya majadiliano kati ya watu wa Mataifa, tamaduni, dini, kwa kushuhudia Kanisa ambalo linalenga kujenga umoja; kukuza na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, bila kusahau amani jamii inayohitaji malezi na majiundo ya haki na upendo. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, wanadamu, maadamu ni wakosefu, wapo na wataendelea daima kuwa chini ya tishio la vita, hadi Kristo Yesu atakapokuja. Lakini madhali wanaweza kuishinda dhambi wakiunganika katika upendo, wanaweza pia kuushinda utumiaji nguvu, kiasi cha kufua panga zao ziwe majembe na mikuki yao iwe miundu na kwamba, hawatajifunza vita tena kamwe. Rej GS 78. Mwanajeshi Mkristo anayo dhamana ya kuwalinda wanyonge; kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na utulivu na kwamba, huu ni wito unaojikita katika dhamiri nyofu. Utambulisho wa mwanajeshi unafumbatwa katika ukarimu na moyo wa huduma, mambo yanayohitaji msingi wa neema na upendo. Ni mtu ambaye anatekeleza kwa dhati kabisa utume wake ndani ya jeshi kwa kuhakikisha kwamba, anamwilisha tunu msingi za Kiinjili, Sheria, Kanuni na Taratibu za Kijeshi kwani huduma ya ulinzi, usalama na amani; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza.
Mtakatifu Yohane Paulo II anasema, Majimbo ya Kijeshi yanawajibu wa kuvisindikiza vikosi vya ulinzi na usalama; kuwalinda na kuwatetea wanyonge ndani ya jamii; watu waaminifu ili kukuza na kujenga misingi ya amani na utulivu; kuondoa hatari na hivyo kukoleza moyo wa haki na amani. Mintarafu Mafundisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, Kanisa linatangaza Injili ya amani, tayari kushirikiana na watu wote mapenzi mema kulinda ustawi wa wengi, Linataka kuwa ni maabara ya utendaji wa Mungu mintarafu majiundo makini yanayoongozwa na sheria na kanuni ya umoja, haki, ukweli na upendo na kwamba, Baba Mtakatifu Leo XIV anapenda kuyaalika Majimbo ya Kijeshi kuwa na mwingiliano wa masomo, ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo zinazojikita katika mchakato wa uinjilishaji wa tamaduni na utamadunisho wa Injili unaoiwezesha Habari Njema ya Kristo Yesu kuingia na kupenyeza mizizi yake katika tamaduni mbalimbali, ikiikubali, ikiisafisha, na kuipatia maana mpya bila kuharibu utambulisho wa watu. Lengo ni kufanya Injili ya Kristo Yesu uwe ni ujumbe unaozungumza lugha na tajiriba ya watu mahalia. Huu ni mchakato wa kuiangalia Injili, Tamaduni, pamoja na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia
Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe wake kwa Siku ya 59 ya Kuombea Amani Duniani tarehe Mosi, Januari 2026 ulionogeshwa na kauli mbiu: "Amani iwe nanyi nyote: Kuelekea amani "Isiyo na Silaha na inayopokonya Silaha" anawaalika viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika kuelekea kwenye amani isiyo na silaha, na inayopokonya silaha. Hii ni amani inayopata chimbuko lake kutoka kwa Kristo Mfufuka, changamoto kwa wafuasi wa Kristo kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na maridhiano. Amani ni mchakato, ni safari na mwanga wa mapito katika maisha. Amani ni zawadi kutoka kwa Kristo Yesu: “Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga.” Yn 14:27. Hata katika hali ya kutisha, Kristo Yesu alimwambia Mtume Petro: “Rudisha upanga alani mwake.” Yn 18:11.
Amani ni ukweli unaopaswa kumwilishwa katika maisha. Mabilioni ya Dola za Kimarekani yanayotumika kununulia silaha yangeweza kusaidia kuboresha maisha ya watu wengi duniani, kumbe kuna haja ya kuzuia ukatili wa vita kwa sababu maendeleo ya silaha za kisayansi yameongeza sana ubaya na ukatili wa vita. Rej. Gauium et spes, 80. Baba Mtakatifu Leo XIV anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kujielekeza katika amani inayopokonya Silaha; amani inayosimikwa katika tunu msingi za Kiinjili; kwa kuheshimiana, kuthamininiana pamoja na kuheshimiana. Huu ni mwaliko wa kujikita katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi na kwamba, amani si swala la kufirikika tu, bali ni jambo linalo simikwa katika: maelewano na utekelezaji wa majukumu yanyofikiwa. Ni amani inayosimikwa katika diplomasia, majadiliano, kanuni na sheria za Kimataifa kwa kuimarisha taasisi za Kimataifa katika utekelezaji wa majukumu yake. Haki, Amani, Utu na Heshima ya binadamu ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee, ili kurejesha tena Injili ya matumaini kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo na kwamba, binadamu wajifunze kusaidiana!
Askofu mkuu Gian Franco Saba wa Jimbo la Kijeshi nchini Italia katika mahojiano maalum na Gazeti la L’Osservatore Romano linalomilikiwa na kuchapishwa na Vatican anasema kuna umuhimu wa kuwa na sera pamoja na mipango mikakati ya shughuli za kichungaji kwa wanajeshi wa vikosi vya ulinzi na usalama, kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima kiroho na kimwili na kama kielelezo cha ukaribu wa Kanisa kwa wanajeshi. Hii ni sehemu muhimu sana ya uinjilishaji wa watu wa Mungu na inakita mizizi yake katika ufahamu wa watu wa Mungu. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, hata wanajeshi wanayo dhamana na wajibu wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Jambo la msingi kwa Mama Kanisa ni kuhakikisha kwamba, anasaidia kufunda dhamiri safi na nyofu miongoni mwa Maaskari, ili kuwawezesha kushiriki katika kukuza na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Maaskari wa vikosi vya ulinzi na usalama sio kila wakati wanapaswa kuhusianishwa na vita na kwamba, vita iwe ni hatua ya mwisho katika maamuzi ya binafamu. Kumbe, Askari wa vikosi vya ulinzi na usalama ni watu walioandaliwa katika mchakato wa kukuza na kudumisha: Ulinzi, Usalama; Haki msingi za binadamu, uhuru pamoja na tunu msingi za kijamii. Uwepo wa Mapadre wa Jimbo la Kijeshi nchini Italia ni ushuhuda hai wa ukaribu wa Kiinjili; vyombo, wahudumu na walinzi wa matumaini kando ya walioanguka, waliojeruhiwa, wafungwa, na wanaoteseka. Huu ni uinjilishaji unaokita mizizi yake katika: Upendo, faraja, na amani. Urithi muhimu wa kihistoria, wa kiroho na wa Kikristo ulioendelezwa kwa zaidi ya miaka mia moja ya Jimbo la Kijeshi nchini Italia sanjari na kanuni maadili na utu wema kwa wanajeshi. Watambue kwamba, wao ni wahudumu wa Injili inayounganisha “Kumbukumbu na Unabii.”
