Tafuta

Baba Mtakatifu Leo XIV, Dominika ya Pili ya Kipindi cha Kwaresima, tarehe Mosi, Machi 2026 ametembelea Parokia ya Kupaa Bwana Mbinguni, huko Quarticciolo, Mashariki mwa mji wa Roma. Baba Mtakatifu Leo XIV, Dominika ya Pili ya Kipindi cha Kwaresima, tarehe Mosi, Machi 2026 ametembelea Parokia ya Kupaa Bwana Mbinguni, huko Quarticciolo, Mashariki mwa mji wa Roma.  (@Vatican Media)

Hija ya Kichungaji Ya Papa Leo XIV Parokia ya Kupaa Bwana Mbinguni: Ushuhuda wa Imani

Baba Mtakatifu Leo XIV aliwashukuru na kuwapongeza kwa moyo wao wa ukarimu na mapokezi makubwa waliyomwonesha. Amewataka wawe ni mwanga na nuru inayobubujika kutoka katika undani wa maisha yao, kwa kutambua kwamba, kwa njia ya Imani, Kristo Yesu amewakirimia zawadi ya imani, nuru hii inawawezesha kuwa ni mashuhuda wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kipindi cha Kwaresima kinasimikwa katika nguzo kuu nne: yaani; Sala, Kufunga, Neno la Mungu na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo cha imani tendaji. Kipindi hiki cha Kwaresima ni mwaliko wa kupanda juu Mlimani Tabor ili kupata mang’amuzi ya maisha ya kiroho na kiutu, ili hatimaye kuweza kuzama zaidi katika Fumbo la maisha ya Kristo Yesu kama utimilifu wa Sheria na Unabii. Ni mwaliko wa kumsikiliza Kristo Yesu kwa umakini mkubwa kama mtindo wa maisha ya Kanisa la Kisinodi na Kimisionari. Waamini wapambane na changamoto za maisha na utume wao kwa ari, ujasiri na moyo mkuu, ili kwamba, Fumbo la Msalaba liwasaidie kukuza imani, matumaini na mapendo, ili hatimaye, waweze kuwa ni mashuhuda na wajenzi wa Kanisa la Kimisionari na la Kisinodi. Baba Mtakatifu Leo XIV, Dominika ya Pili ya Kipindi cha Kwaresima, tarehe Mosi, Machi 2026 ametembelea Parokia ya Kupaa Bwana Mbinguni, “Parrocchia dell'Ascensione di Nostro Signore Gesù Cristo” huko Quarticciolo, Mashariki mwa mji wa Roma. Papa Leo XIV anakuwa ni Baba Mtakatifu wa tatu kutembelea na kusali Parokiani hapo. Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Yohane XXIII alitembelea Parokiani hapo tarehe 3 Machi 1963 na Mtakatifu Yohane Paulo II hapo tarehe 3 Februari 1980. Wenyeji wa eneo hili ni watu ambao wamejiajiri katika shughuli zao binafsi na kuna idadi kubwa ya wazee na wastaafu na sehemu kubwa ya wakazi hawa wanakabiliana na changamoto ya uvunjifu wa amani na vitendo vya uhalifu na jinai. Parokia hii inahudumiwa na Mapadre wa Moyo Mtakatifu wa Yesu, katika nafsi ya Padre Daniele Canali. Parokia hii ilianzishwa mwaka 1948 na Kanisa la Parokia kujengwa kunako mwaka 1954.

Kanisa la Parokia lilijengwa mwaka 1954.
Kanisa la Parokia lilijengwa mwaka 1954.   (@Vatican Media)

Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, kumekuwepo na maendeleo makubwa: kiroho na kimwili, baadaye maendeleo haya yakaathiriwa na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, watu wakafunga maduka na shughuli zao; vijana wakaondoka katika eneo hili kutafuta fursa za maendeleo sehemu nyingine za Italia. Eneo hili likawa ni makao ya mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo, mambo yanayosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kimsingi hili ni eneo hatari kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na kwamba, watu wengi wanakabiliana na hali duni ya maisha. Baba Mtakatifu Leo XIV akiwa Parokiani hapo, amepata fursa ya kukutana na kuzungumza na watoto, wazee na wagonjwa pamoja na Baraza la Halmashauri ya Parokia na hatimaye, akaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, Dominika ya Pili ya Kipindi cha Kwaresima. Baba Mtakatifu Leo XIV aliwashukuru na kuwapongeza kwa moyo wao wa ukarimu na mapokezi makubwa waliyomwonesha. Amewataka wawe ni mwanga na nuru inayobubujika kutoka katika undani wa maisha yao, kwa kutambua kwamba, kwa njia ya Imani, Kristo Yesu amewakirimia zawadi ya imani, nuru hii inawawezesha kuwa ni mashuhuda wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Papa Leo XIV amekutana na kuzungumza na watoto Parokiani hapo
Papa Leo XIV amekutana na kuzungumza na watoto Parokiani hapo   (@Vatican Media)

Amewashukuru waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwa ushujaa na ushuhuda wanaoutoa katika mazingira yao kwa hakika anasema Baba Mtakatifu Leo XIV wanapaswa kuwa: “Ni chumvi ya dunia; lakini chumvi ikiwa imeharibika itatiwa nini hata ikolee? Haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu. Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima. Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani. Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.” Mt 5:13-16. Kumbe, hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Leo XIV katika Parokia hii imekuwa ni muda muafaka wa kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo; amewatia shime ili waweze kuwa ni mashuhuda wa Fumbo la Pasaka. Baba Mtakatifu Leo XIV katika mahubiri yake amewakumbusha waamini kwamba, maisha ni safari inayodai imani sanjari na kujiaminisha katika Neno la Mungu, bila kushikwa na kishawishi cha kutaka kukimbia changamoto za maisha, bali kuwa na ujasiri wa kuweza kugundua: “hazina iliyositirika katika shamba; ambayo mtu alipoiona, aliificha; na kwa furaha yake akaenda akauza alivyo navyo vyote, akalinunua shamba lile.” Mt 13:44. Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya Pili ya Kipindi cha Kwaresima Mwaka A wa Kanisa inasimikwa katika safari ya wito wa Abramu: Kut 12: 1-4; na Tukio la Kristo Yesu kugeuka sura Mt 17:1-9. Mitume wa Kristo Yesu iliwabidi kufunga safari huku wakiandamana na Mwalimu wao, safari ambayo ingepata hitimisho lake pale juu Mlimani Kalvari, yaani kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu uletao maisha na uzima wa milele.

Papa Leo XIV amewashukuru kwa ushuhuda wenye mvuto na mashiko
Papa Leo XIV amewashukuru kwa ushuhuda wenye mvuto na mashiko   (@Vatican Media)

Hii ilikuwa ni changamoto kwa Mtakatifu Petro, Mtume pamoja na wafuasi wengine wa Kristo kukubali Fumbo la Kifo katika maisha ya Kristo Yesu aliyejisadaka katika Fumbo la Ekaristi, ili kutoa Mwili wake uwe ni chakula na Damu yake Azizi iwe ni kinywaji cha maisha ya kiroho, akawa tayari kufa, ili kuwa ni chemchemi ya maisha mapya yanayoibukia kwenye uzima wa milele. Kumbe, Dominika ni siku maalum kwa waamini kukutana na Kristo Yesu katika Neno na Ekaristi na kwamba; “Hakuna mtu mwenye upendo mkuu kuliko huu, mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.” Yn 15:13. Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu ndicho kilele cha safari ya maisha na utume wake hapa ulimwenguni, jambo ambalo kwa Mtakatifu Petro, lilikuwa ni kashfa, lakini Kristo Yesu anamwonya Petro kwa kumwambia kwamba; “Nenda nyuma yangu, Shetani; u kikwazo kwangu; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.” Mt 16:23. Kumbe, tukio la Kristo Yesu kugeuka sura lilipania kuwaimarisha Mitume wa Yesu katika imani, matumaini na mapendo, kwani wao mateso na kifo cha Masiha wa Bwana, ni tukio ambalo lilikuwa haliingii kichwani mwao kabisa!

Papa Leo XIV amezungumza na Halmashauri ya Parokia
Papa Leo XIV amezungumza na Halmashauri ya Parokia   (@Vatican Media)

Kristo Yesu Mlimani Tabor anadhihirisha utukufu wake, pembeni mwake wakiwepo Musa na Eliya: Sheria na Unabii kielelezo cha utimilifu wa Ufunuo wa Mungu kwa binadamu. Rej Mt 17: 2-3. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kilele cha safari ya maisha ya waamini kimesheheni nuru inayomwonesha Kristo Yesu: Mtu kweli na Mungu kweli na kwamba, Mtakatifu Petro alikuwa hana budi kuendelea na safari hadi Mjini Yerusalemu, pale Mlimani Kalvari. “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye; msikieni yeye.” Kristo Yesu bado anaendelea kufanya hija na wafuasi wake, anawafundisha mantiki ya upendo usiokuwa na ukomo; kwa kujiachilia mikononi mwa Mungu ili hatimaye, hata waamini waweze kuwa ni mwanga wa Mataifa. Ndani ya Parokia hii anasema Baba Mtakatifu Leo XIV kuwa wahudumu wa Mwanga; watu wenye furaha ya kutumikia. Tukio la Kristo Yesu kung’ara Uso wake ni mwendelezo wa safari ya Yesu, Safari ya Kanisa na Parokia katika ujumla wake, kutekeleza dhamana na utume wa Kkristo Yesu, licha ya matatizo, changamoto na fursa zilizopo. Hii ni nuru iliyoko katika moyo wa mwanadamu, changamoto na mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanamwilisha ndani mwao: mateso ya Ktisto Yesu, wanashirikisha amana na utajiri wa Yesu; wanatumia kipaji cha ugunduzi ili kuganga na kutibu majeraha yaliyoko katika makazi yao. Baba Mtakatifu anawapongeza waamini wa Parokia ya Kupaa Bwana Mbinguni, “Parrocchia dell'Ascensione di Nostro Signore Gesù Cristo” huko Quarticciolo, Mashariki mwa mji wa Roma kwa kuendelea kuwa hai licha ya changamoto kubwa wanazokumbana nazo, lakini bado wameendelea kushuhudia tunu msingi za Kiinjili kwa ujasiri mkubwa.

Amewataka vijana kusadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo
Amewataka vijana kusadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo   (@Vatican Media)

Hii ni Parokia inayokita mizizi yake katika ukarimu na ujenzi wa Jumuiya, kwa kukazia utambulisho wa wanaparokia wake, tayari kujikita katika mchakato wa kuganga na kuponya majeraha na kwamba, ni matumaini ya Baba Mtakatifu Leo XIV kwamba, watu wengine watawaunga mkono, ili kweli waweze kuwa ni chachu ya wema na haki. Huu ni mwaliko kwa vijana kuchagua Injili ya uhai kwa kumfuata Kristo Yesu, Mwalimu wao wa maisha. Hii ni Jumuiya ambayo ni chemchemi ya matumaini yanayomwilishwa katika maisha na utume wao, dhidi ya ubaya na uwepo wa dhambi. Kumbe, huu ni mwaliko wa kuendelea kutoa utambulisho wao kama Wakristo, watu wanaotaka kujikita katika ujenzi wa ufalme wa Mungu unaosimikwa katika haki, amani, udugu na mshikamano. Wawe ni mashuhuda wa imani, ili kuwasaidia wale ambao hawajamtabua Yesu, waweze kumtambua kuwa ni nuru kweli na furaha ya kweli. Waamini waendelee kutangaza na kushuhudia Injili inayong’ara na kutoa maisha. Bikira Maria Mama wa Kanisa awasindikize na kuwaombea daima.

Papa Leo XIV amekutana na Halimashauri walei Parokiani hapo.
Papa Leo XIV amekutana na Halimashauri walei Parokiani hapo.   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV alipokuwa anazungumza na watoto Parokiani hapo amewaambia kwamba, Kristo Yesu aliyepaa mbinguni, amechukua pia Mwili wake wa kibinadamu sasa amekaa mkono wa kulia mwa Baba yake wa mbinguni. Waendelee kuwa ni mashuhuda wa nuru kwa kuchagua kutenda mema; kukuza na kudumisha udugu wa kibinadamu na upendo mambo ambayo wanapaswa kuyaadhimisha, daima wachague kutenda mema. Baba Mtakatifu Leo XIV amewapongeza vijana wanaounda “Jumuiya ya Magis” mashuhuda wa Injili wanaoweza kuleta mabadiliko katika maisha; wawe ni mashuhuda, vyombo na wajenzi wa amani ya Kristo Yesu kwa watu wote. Watoto wanahimizwa kuendelea kusali sana kwa ajili ya amani na umoja kati yao, wakishinde kishawishi cha kuwatenda vibaya jirani zao, daima wachague kutenda mema na watiifu kwa wazazi wao; waendelee kujikita katika upatanisho, ushirika na urafiki ili kuwa kweli ni wajenzi wa amani. Kuna watoto ambao wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi, hawana mahitaji msingi; wengi wao ni wale wanaotoka katika maeneo ya vita kama ilivyo Ukanda wa Gaza. Wawe ni mashuhuda wa kutenda mema, na kukataa ubaya wala kujihusisha na matumizi haramu ya dawa za kulevya. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Leo XIV kwamba Parokia hii itaendelea kuwa ni nuru na shuhuda wa imani tayari kujifunza na kuwafunda wengine Injili ya upendo, kwa ujasiri waweze kumkubali na kumpokea Kkristo Yesu katika maisha yao.

Wanaparokia wawe ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu
Wanaparokia wawe ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu alipokutana na kuzungumza na wazee pamoja na wagonjwa Parokiani hapo, amewapongeza kwa kuunda Jumuiya yenye changamoto mbalimbali za kiafya: Uzee na ulemavu na kwamba, upendo wa Mungu unawakirimia nguvu ya kufanyika kuwa ni familia na hivyo kuweza kutembea kwa pamoja kama wamoja. Baba Mtakatifu anawaalika wazee na wagonjwa kusali kwa ajili ya kuwaombea watu wanaoathirika kwa vita sehemu mbalimbali za dunia. Kama waamini wasimame kidete kutetea ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kwa kuishi na kufanya kazi kwa pamoja, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda wa Kristo Yesu. Baba Mtakatifu Leo XIV amewashukuru wajumbe wa Baraza la Halmashauri ya Parokia kwa mapokezi makubwa, kwa Ibada ya Bikira Maria na kwamba, kwa hakika wao ni mashuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake na kwamba, maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu yanawawezesha kujenga na kudumisha Jumuiya ya waamini, chimbuko la maisha, upendo na udugu wa kibinadamu. Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu ni utimilifu wa ushirika kati ya waamini. Anawashukuru na kuwapongeza kwa ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Papa Leo XIV Hija ya Kichungaji
02 Machi 2026, 15:48