Waraka wa Kitume wa Papa Leo XIV Kwa Wanamichezo ya 25 ya Olimpiki 2026
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Michezo ya Olimpiki kwa mara ya kwanza ilifanyika kunako Mwaka 776 Kabla ya Kristo, huko mjini Olympia, nchini Ugiriki. Haya yalikuwa ni mashindano kwa ajili ya wanamichezo mahalia tu na wala hayakuwa na umaarufu wowote Kimataifa. Lakini kadiri muda ulivyokuwa unazidi kuyoyoma, michezo mingi zaidi iliendelea kuongezwa katika mashindano haya, kiasi kwamba, hata muda wa mashindano yenyewe ukaongezeka maradufu. Kipindi chote cha mashindano ya Olimpiki, vita na misigano yote ya kisiasa na kijamii ilisitishwa ili kutoa fursa kwa wananchi kufurahia michezo nchini Ugiriki. Kumbe tangu mwanzo, tunu ya amani na maridhiano imekuwa ni kati ya mambo yanayotiliwa mkazo wakati wa michezo ya Olimpiki. Michezo hii ilianza kupata umaarufu wa pekee mara baada ya utawala wa Kirumi kuanza kushika hatamu za uongozi nchini Ugiriki. Hapa Ukristo ukatambuliwa rasmi kwamba, ndiyo dini iliyokuwa inaongoza kwenye utawala wa Kirumi. Wakati wote huu, michezo hii ilionekana kuwa na sura ya kipagani zaidi na wala hakuna masuala ya kidini yaliyogusiwa wakati huo. Kunako mwaka 393 Baada ya Kristo wakati wa Michezo ya Olimpiki huko Thesalonike, kulitokea maafa makubwa yaliyopelekea Mfalme Theodor wa kwanza kusitisha michezo hiyo! Hapa kukawa ni mwanzo wa kuyumba na kuchechemea kwa historia ya michezo ya Olimpik iliyokuwa imedumu kwa takribani Karne moja Kabla ya Kristo! Mwaka 1894 Bwana Pierre de Coubertin akajitosa kuhamasisha tena michezo hii miongoni mwa Jumuiya ya Kimataifa kwa kuanzisha mashindano ya michezo mbalimbali, ikiongozwa na kauli mbiu iliyojulikana kwa lugha ya Kilatini kuwa ni "Citius, Altius, Fortius" yaani, Kasi, hapa Waswahili wangesema "Mchomoko", Lenga juu zaidi na kwa nguvu." Lengo kuu likiwa ni mchakato wa ujenzi wa mahusiano na mafungamano miongoni mwa vijana nchini Ufaransa.
Mashindano ya Olimpiki yameendelea kuboreka mwaka hadi mwaka. Lakini pia yamekuwa yakikabiliana na changamoto mbalimbali zikiwemo za ulinzi na usalama wa wanamichezo na watazamaji wanaohudhuria katika mashindano haya. Hii ni dhamana nyeti sana kwa wenyeji wa mashindano haya na kwa Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake. Ndiyo maana kuna hatua kali sana za kinidhamu zinazochukuliwa ili kuwa na ulinzi makini zaidi hasa kutokana na kuongezeka kwa vitendo vya kigaidi sehemu mbalimbali za dunia. Baadhi ya wafanyabiashara haramu ya dawa za kulevya wamekuwa wanataka kutumia mwanya wa michezo hii ya Kimataifa kwa ajili ya kueneza biashara haramu ya matumizi ya dawa za kulevya, matukio yanayowahusisha wanamichezo wenyewe, kiasi cha kukiuka malengo na kanuni za michezo. Kashfa hizi zimekuwa ni aibu kwa wanamichezo na nchi wanamotoka pale inapobainika kwamba, ushindi walioupata ni kutokana na matumizi haramu ya dawa za kulevya. Michezo hii imeongeza pia kasi ya biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo unaowatumbukiza wanawake na wasichana katika utumwa na utalii wa ngono. Mama Kanisa anaona kwamba, matukio kama haya ni mahali muafaka pa kuendeleza mchakato wa Uinjilishaji Mpya. Ndiyo maana mikakati ya maisha ya kiroho kwa ajili ya wanamichezo na mashabiki wao inapewa kipaumbele cha pekee, kwa kutambua kwamba, mwanadamu ameumbwa mwili na roho! Hii ni fursa ya kujenga na kudumisha umoja, mshikamano na upendo wa udugu wa kibinadamu pamoja na maridhiano kati ya watu wa Mataifa.
Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Michezo ya Olympiki kuanzia tarehe 6 Februari hadi tarehe 22 Februari 2026 na kuanzia tarehe 6 Hadi tarehe 15 Machi 2026 inafanyika Michezo ya Olimpiki, huko Milano na Cortina, Kaskazini mwa Italia, Baba Mtakatifu Leo wa XIV amewatumia barua washiriki wa michezo hii huku akionesha: Thamani ya michezo: Michezo na ujenzi wa amani; tunu msingi za michezo katika majiundo; Mchezo, shule ya maisha na ya kisasa; Michezo na maendeleo binafsi; Mambo yanayohatarisha tunu msingi za michezo; Mashindano na utamaduni wa watu kukutana; Michezo, Mahusiano na mang’amuzi; sanjari na Mpango mkakati wa michezo kwa ajili ya kuwa na maisha tele! Kipindi chote cha mashindano ya Olimpiki, vita na misigano yote ya kisiasa na kijamii ilisitishwa ili kutoa fursa kwa wananchi kufurahia michezo na hivyo michezo ikawa ni fursa ya kujenga na kudumisha amani; ukuaji wa udugu wa kibinadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na kwamba, vita, kinzani na mipasuko ni dalili za kushindwa kwa ubinadamu. Dunia ina kiu ya amani kumbe. Kuna haja ya kutumia nyenzo zitakazo saidia kusitisha matumizi mabaya ya madaraka na hivyo kujikita katika utawala wa haki na sheria. Tunu msingi za michezo katika majiundo ili kuweza kuwa na maisha tele pamoja na utimilifu wake. Rej. Yn 10:10. Mama Kanisa hana budi kutekeleza dhamana na utume wake hapa ulimwenguni, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu katika michezo kama anavyosema Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa kuhusu utaratibu kwa wanariadha: “Je! Hamjui, ya kuwa wale washindanao kwa kupiga mbio, hupiga mbio wote, lakini apokeaye tuzo ni mmoja? Pigeni mbio namna hiyo, ili mpate. Na kila ashindanaye katika michezo hujizuia katika yote; basi hao hufanya hivyo kusudi wapokee taji iharibikayo; bali sisi tupokee taji isiyoharibika.” 1Kor 9:24-25. Hiki ni kielelezo cha mashindano ya kiroho; na kwamba Binadamu ni umoja wa mwili, roho na nafsi na hivyo Mama Kanisa anakazia umuhimu wa michezo katika maisha ya mwanadamu kama mambo muhimu sana katika kuhubiri na kufundisha.
Mchezo, shule ya maisha na ya kisasa mambo ambayo yamepewa kipaumbele cha pekee na walezi katika maisha na kazi; Ustawi na maendeleo ya mtu mzima: kiroho na kimwili na kwamba, Mama Kanisa anaona michezo kama fursa ya kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha kama vile: Udugu wa kibinadamu, mshikamano na amani. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema mapumziko yatumike kuimarisha afya ya kiroho na kimwili na kwamba, michezo pia inaweza kuimarisha, kustawisha na kukuza mahusiano ya kidugu kati ya wanadamu wa hali zote, mataifa na makabila mbalimbali. Kumbe, wakristo wanahimizwa kushiriki katika michezo, huku ikikolezwa na roho ya kiutu na ya kikristo. Rej. Gaudium et spes, n.61. Katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, Mama Kanisa amekazia pia umuhimu wa michezo, utamaduni na elimu na kwamba, michezo ni lugha inayofahamika na wengi na kikolezo cha watu kukutana; kujadiliana na kwamba, bado kuna mengi ya kujifunza kutoka katika tamaduni za watu mbalimbali, ili kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekumene, kidini na kitamaduni. Michezo na maendeleo binafsi: Michezo ni chanzo cha furaha, mahali mtu anapoweza kujieleza kutoka katika undani wake; ni mahali pa kuonesha umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu unaovunjilia mbali uchoyo na ubinafsi, unajielekeza katika mafao ya wengi; michezo inatoa fursa ya watu kukutana na hivyo kukuza na kudumisha udugu; ni mahali pa kuratibu kinzani na migogoro, kwa kusameheana na kusahau. Makocha wanayo kazi na dhamana nyeti katika kujenga umoja kama timu, kati ya wachezaji. Michezo inamwendeleza mtu mmoja mmoja sanjari na kujenga mahusiano na mafungamano ya kijamii; kumbe michezo lazima ijitahidi kuwalenga watu wote ndani ya jamii, kwani ni sehemu muhimu sana ya maendeleo ya binadamu.
Mambo yanayohatarisha tunu msingi za michezo ni pamoja na: Rushwa, michezo kufungamanishwa sana na masilahi ya kiuchumi na kifedha; kwa kujikita zaidi katika kutafuta na kupata ushindi kwa njia zozote zile, ambazo nyingine zinakwenda kinyume kabisa cha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Masilahi ya kibiashara yanaonekana kufifisha tunu msingi za michezo zinazopaswa kulindwa na kudumishwa. Michezo kwa sasa inaonekana kuzima kiu ya uchu wa mali na fedha katika hili Mwinjili Mathayo anasema: “Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu, na kumpenda huyu; ama atashikamana na huyu, na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali.” Mt 6:24-26. Uchu wa mali na fedha unadhalilisha tasnia ya michezo na kuitumbukiza katika rushwa, kama ilivyo pia kwa jamii nzima. Mashindano na utamaduni wa watu kukutana na kukua kwa pamoja; kujenga na kudumisha mahusiano ya amani; kwa kutambua mapungufu ya kila mmoja; kwa kuheshimiana na kwamba, ushindi ni matokeo ya nidhamu, udumifu na uaminifu. Mashindano ni mchakato wa kusafiri kwa pamoja katika furaha, mafanikio na hata kushindwa kwao; tayari kujenga na kuimarisha umoja, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Kumbe, michezo inapaswa kuwa ni chemchemi ya umoja katika tofauti zake msingi; zinazopania pamoja na mambo mengine kujenga familia ya binadamu inayosimikwa katika ukarimu, majadiliano na hali ya kuaminiana. Michezo, Mahusiano na mang’amuzi mintarafu ushindi na kushindwa, mambo yanayopaswa kusimikwa katika ukweli na unyenyekevu. Wanamichezo wajifunze kukubali matokeo, bila kukata wala kukatishwa tamaa; Kukubali ushindi, bila majivuno wala kejeli, bali wapokee ukweli katika hali ya ukomavu, kwa kutambua udhaifu wao na fursa ambazo ziko mbele yao daima. Kamwe michezo isichukue nafasi ya dini katika maisha ya mwanadamu, kwani itapoteza utambulisho wake na kwamba, wanamichezo watambulike kuwa ni watu wenye: mwili, roho na nafsi.
Mtakatifu Giorgio Frassati (1901-1925) alijitahidi kuunganisha: Michezo, Imani, Sala na Sadaka yake katika Michezo, mambo yaliyomwezesha kutafakari matendo makuu ya Mungu katika maisha yake. Baba Mtakatifu anaonya matumizi makubwa ya akili unde katika tasnia ya michezo sehemu mbalimbali za dunia. Teknolojia inapaswa kuwa ni kwa ajili ya huduma kwa binadamu; teknolojia iwe ni fursa inayowawezesha watu wote kushiriki katika michezo na kwamba, teknolojia kiwe ni chombo cha kuendeleza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu pamoja na mafungamano yake. Michezo ijenge mahusiano na ukaribu miongoni mwa watu; iwe ni chombo cha kuwasindikiza watu na kwamba, mashindano ni safari ya pamoja! Tunu msingi za michezo iwe ni shule ya ubinadamu na wala isiwe ni chombo cha ulaji wa kupindukia!Mpango mkakati wa michezo kwa ajili ya kuwa na maisha tele kwa kujikita katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji inayotekelezwa na Makanisa mahalia sanjari na kutambua kwamba, michezo ni fursa ya kufanya mang’amuzi, kwa kuwasindikiza pamoja na kuwapatia wanamichezo mwongozo wa maisha ya kiroho. Baba Mtakatifu Leo XIV anashauri Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbalimbali za dunia kuwa na Idara au Tume ya Michezo itakayokuwa na dhamana ya kuratibu, kuelimisha na kuwakutanisha wanamichezo katika ngazi mbalimbali, ili kukuza na kudumisha utakatifu wa michezo katika mahusiano na mafungamano ya watu. Ukaribu na uwepo wa Kanisa katika tasnia ya michezo ikazie kanuni maadili na utu wema; uwiano mzuri kati ya mwili, roho na nafsi katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Michezo ni mahali pa kujenga mahusiano ya kijamii, kitamaduni na kimwili; ni chemchemi ya furaha; mahali pa kusaidiana na kwamba, michezo ni fursa ya kujenga na kudumisha maridhiano ya kijamii.
Michezo iwe ni fursa ya mtu kukubali kushindwa, bila ya kukata tamaa; kushinda bila ya kuwa na kiburi na majivuno na kwamba, mazoezi yawe ni sehemu ya majiundo ya kiutu na kibinadamu. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, katika mtazamo wa shughuli za kichungaji, hii ni changamoto kwa Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, anashiriki kikamilifu katika tasnia ya michezo, kwa kuwasindikiza, kuwapatia wanamichezo mang’amuzi na matumaini. Ni katika muktadha huu, michezo kweli inaweza kuwa ni shule ya maisha, mahali pa kushirikishana tunu msingi za maisha; kwa kuheshimiana na wengine na kwa furaha ya kweli kutembea kwa pamoja!
