Wamisionari wa Oblati wa B. Maria, Miaka 200; Masista wa Bibi Yetu wa Mitume, Miaka 150 ya Utume
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume ni kipindi muafaka cha watawa kukutana katika: Sala, tafakari na mang’amuzi ya kina mintarafu amana na utajiri wa mashirika na wanashirika wenyewe. Ni wakati muafaka kwa wanashirika kufanya upembuzi yakinifu kuhusu: Maisha na utume wa mashirika yao, kwa kuangalia changamoto, matatizo na fursa zilizopo kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Huu ni wakati muafaka wa kusoma alama za nyakati na kuangalia wapi ambapo Roho Mtakatifu anawataka kwenda baada ya mikutano yao mikuu. Lengo kuu ni kuhakikisha kwamba, watawa wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili; kwa kujikita katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu kama chemchemi ya furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake tayari kujenga Kanisa na Kisinodi na Kimisionari. Shirika la Wamisionari wa Oblati wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili: “La Congregazione dei Missionari Oblati di Maria Immacolata, OMI. Lilianzishwa tarehe 25 Januari 1816 huko “Aix-en-Provence” nchini Ufaransa na Mtakatifu Eugenio de Mazenod na kuidhinishwa na Papa Leo XII kunako tarehe 17 Februari 1826, kwa kujikita katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Mwaka huu 2026 linaadhimisha Kumbukizi ya Miaka 200 tangu Papa Leo XII alipopitisha Mwongozo na Katiba ya Shirika.
Shirika la Masista wa Bibi Yetu wa Mitume, “Suore di Nostra Signora degli Apostoli, NSA” wanajiweka wakfu kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, wakijitahidi kuwa ni mbegu ya matumaini katika Ulimwengu mamboleo, ili watu wa Mungu waweze kuwa ni wakamilifu zaidi. Watawa hawa wanashiriki katika maisha na utume wa Kanisa kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Ulimwengu mpya mintarafu mpango wa Mungu. Shirika hili lilianzishwa kunako mwaka 1876 huko Lione, Ufaransa na Padre Agostino Planque. Mwaka 2026 linaadhimisha Kumbukizi ya Miaka 150 tangu kuanzishwa kwao!
Shirika la Wamisionari wa Oblati wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili pamoja na Shirika la Masista wa Bibi Yetu wa Mitume, tarehe 21 Februari 2026 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Leo XIV mjini Vatican na kuwataka kutoa kipaumbele cha pekee kwa Injili ya upendo kama kioo cha huruma na upendo wa Mungu Ulimwenguni. Pamoja na tofauti zao msingi, lakini Mashirika yote haya mawili yalianzishwa nchini Ufaransa na kwamba, yanasimikwa katika wito wa kimisionari wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa na hasa kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Mtakatifu Eugenio de Mazenod katika maisha na utume wake, alisimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za wafanyakazi na wakulima, waliokuwa wananyonywa kwa kukosa elimu, ujuzi na maarifa. Akahakikisha kwamba, Shirika lake linachanua kwa kasi kubwa nchini Canada, Ulaya na Barani Afrika.
Zote hizi anasema Baba Mtakatifu Leo XIV, ni juhudi za ukarimu wa kimisionari na ushuhuda wenye mvuto na mashiko ukawa ni msingi wa ukuaji wa Shirika sehemu mbalimbali za dunia. Ni Shirika ambalo limejikita katika mchakato wa kutamadunisha Injili ili kuinjilisha tamaduni mintarafu tunu msingi za Kiinjili. Juhudi zote hizi zinakwenda sanjari na majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji msingi ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Huu ni mwaliko wa kupenda na kujisadaka katika shughuli za kimisionari na hivyo kwenda pembezoni mwa ulimwengu, kwa ajili ya maskini na kwa wale wasiofikiwa na wengi, huku wakiwa chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria na kwa kuongozwa na kauli ya maneno kutoka katika Kitabu cha Matendo ya Mitume inayoionesha Jamii ya Mitume kumi na mmoja wakidumu kwa moyo mmoja katika kusali pamoja na “Bikira Maria Mama Yake Yesu.”
Wasichana na wanawake wengi wamepokea changamoto hii ya kukaa kati pamoja na Bikira Maria, ili kuwa ni mashuhuda wa Kristo Yesu pamoja na Mitume wake, sehemu mbalimbali za dunia. Wengi wa watawa hawa wamesadaka maisha yao hadi kifo kutokana na magonjwa, dhuluma na nyanyaso na kwamba, hata wao bado wanaendelea kutoa huduma katika mazingira magumu, tete na hatarishi. Baba Mtakatifu Leo XIV amewatia shime kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu katika kutekeleza dhamana na utume wao, kama mashuhuda wa udugu wa kibinadamu, haki na amani. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Leo XIV amewataka kujenga na kudumisha maisha ya kijumuiya yanayosimikwa katika moyo na ukarimu wa maisha ya kifamilia; wajitahidi kukutana na Kristo Yesu katika: Sala, Neno na maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa na hasa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho; Katika Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu; kwa kushirikiana na kushikamana kwa hali na mali; kwa kujenga na kudumisha udugu na ujirani mwema, ushuhuda wa upendo wa Mungu ulimwenguni na kwamba, anawasindikiza kwa sala na sadaka yake.
