Tafuta

Siku ya Wagonjwa Duniani  ni siku ya Sala, Ibada ya Misa Takatifu pamoja na kutoa Sakramenti ya Mpako kwa wagonjwa na wazee. Siku ya Wagonjwa Duniani ni siku ya Sala, Ibada ya Misa Takatifu pamoja na kutoa Sakramenti ya Mpako kwa wagonjwa na wazee.   (ANSA)

Ujumbe wa Papa Leo XIV Kwa Siku ya 34 ya Wagonjwa Duniani 2026

Maadhimisho ya Siku ya 34 ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2026 yananogeshwa na kauli mbiu “Huruma ya Msamaria Mwema: Kupenda kwa Kubeba Maumivu ya Mwingine.” Papa Leo XIV katika ujumbe wake anakazia zaidi: Zawadi ya kukutana, furaha ya kuonesha ujirani mwema na uwapo katika huduma; Utume shirikishi na huduma kwa wagonjwa; Kwa kusukumwa na upendo wa Mungu, ili kuwawezesha watu kukutana wao wenyewe sanjari na ndugu zao katika Kristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Kanisa wanasema, kwa Mpako Mtakatifu wa wagonjwa na sala za Makuhani, Mama Kanisa huwakabidhi wagonjwa kwa Kristo Yesu, aliyeteswa na kutukuzwa ili awainue na kuwaokoa. Mama Kanisa anawaalika wagonjwa na wazee kujiunga kwa hiari na mateso na kifo cha Kristo Yesu, ili kutoa mchango wao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Rej. KKK. 1499. Mpako wa wagonjwa hutimiliza kufananishwa kwa waamini kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu kama Sakramenti ya Ubatizo inavyoanza. Siku ya Wagonjwa Duniani, ni wakati wa kusali na kuwaombea wagonjwa na familia zao; kwa kuwaenzi wahudumu katika sekta ya afya pamoja na watu wanaojitolea usiku na mchana, kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa na wazee sehemu mbalimbali za dunia. Ni muda muafaka wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya wito wa huduma ya afya, ili kuweza kuwasindikiza wagonjwa na wanaoteseka katika shida na mahangaiko yao. Ni fursa kwa Kanisa kupyaisha tena na tena huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hii ni siku ya Sala, Ibada ya Misa Takatifu pamoja na kutoa Sakramenti ya Mpako kwa wagonjwa na wazee.

Siku ya Wagonjwa Duniani: Mshikamano wa huruma na upendo
Siku ya Wagonjwa Duniani: Mshikamano wa huruma na upendo

Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Bikira Maria wa Lourdes sanjari na Siku ya 34 ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2026 yanaadhimishwa Jumatano tarehe 11 Februari 2026. Kimataifa maadhimisho haya yanafanyika kwenye Madhabahu ya Bikira Maria, Mama Yetu wa Amani, Jimbo Katoliki la Chiclayo, nchini Perù: “Nuestra Señora de la Paz en Chiclayo.” Ujenzi wa Madhabahu haya ni jitihada za maisha ya kiroho na kichungaji zilizoasisiwa na Mtakatifu Yohane Paulo II. Maadhimisho ya Siku ya 34 ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2026 yananogeshwa na kauli mbiu “Huruma ya Msamaria Mwema: Kupenda kwa Kubeba Maumivu ya Mwingine.” Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe wake anakazia zaidi: Zawadi ya kukutana, furaha ya kuonesha ujirani mwema na uwapo katika huduma; Utume shirikishi katika huduma kwa wagonjwa; Kwa kusukumwa na upendo wa Mungu, ili kuwawezesha watu kukutana wao wenyewe sanjari na ndugu zao katika Kristo Yesu.

Maadhimisho ya Siku ya 34 ya Wagonjwa Duniani 2026
Maadhimisho ya Siku ya 34 ya Wagonjwa Duniani 2026   (AFP or licensors)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kauli mbiu hii inalenga kupyaisha sura ya Msamaria Mwema, wakati huu, kugundua uzuri wa upendo na mwelekeo wa kijamii wa huruma ya Mungu kwa ajili ya wahitaji, wagonjwa na wale wanaoteseka. Kilele cha maadhimisho haya, kinayashirikisha Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume nchini Perù, sanjari na wadau mbalimbali wa sekta ya afya, bila kuwasahau wagonjwa ambao ndio wahusika wakuu. Wagonjwa na wazee, katika maadhimisho haya, wanapewa Sakramenti ya Mpako Mtakatifu wa Wagonjwa, kwani kwa hakika upendo hauna budi kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya wagonjwa. Magonjwa haya, kwa sehemu kubwa ni matokeo ya umaskini, upweke hasi, ndiyo maana wote hawa wanaalikwa kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Siku ya 34 ya Wagonjwa Duniani. Hayati Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume: “Misericordia et misera” yaani “Huruma na amani” anasema, huruma ni kielelezo makini cha upendo wa Mungu unaosamehe, unaoongoa, unaopyaisha na kubadili mwelekeo wa maisha. Ni kielelezo cha ufunuo wa Fumbo la Mungu ambalo ni huruma ya milele, inayowakumbatia na kuwaambata watu wote pasi na ubaguzi, kiasi cha kuwakirimia maisha mapya, chemchemi ya furaha na matumaini mapya, yanayovunjilia mbali ubaguzi, ubinafsi na uchoyo ili kutenda wema, kufikiri vyema na kuondoa huzuni moyoni. Huruma ya Mungu inajidhihirisha kwa namna ya pekee katika: Maadhimisho ya Sakramenti za Uponyaji yaani: Sakramenti ya Upatanisho na Mpako wa Wagonjwa. Sakramenti ya Upatanisho inawaonjesha waamini huruma, upendo na msamaha wa dhambi; mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, ili kumwilisha upendo wa Mungu katika maisha, tayari kuwaonjesha majirani huruma na upendo huo kama ilivyokuwa kwa mfano wa Msamaria mwema, maarufu kama Injili ya Msamaria mwema.

Huruma ya Msamaria Mwema: Kupenda Kwa Kubeba Maumivu ya Wengine
Huruma ya Msamaria Mwema: Kupenda Kwa Kubeba Maumivu ya Wengine   (ANSA)

“Naye akitaka kujidai haki, alimwuliza Yesu, Na jirani yangu ni nani? Yesu akajibu akasema, Mtu mmoja alishuka toka Yerusalemu kwenda Yeriko, akaangukia kati ya wanyang’anyi; wakamvua nguo, wakamtia jeraha, wakaenda zao, wakimwacha karibu ya kufa. Kwa nasibu kuhani mmoja alishuka kwa njia ile; na alipomwona alipita kando. Na Mlawi vivyo hivyo, alipofika pale akamwona, akapita kando. Lakini, Msamaria mmoja katika kusafiri kwake alifika hapo alipo; na alipomwona alimhurumia, akakaribia, akamfunga jeraha zake, akizitia mafuta na divai; akampandisha juu ya mnyama wake, akampeleka mpaka nyumba ya wageni, akamtunza. Hata siku ya pili akatoa dinari mbili, akampa mwenye nyumba ya wageni, akisema, Mtunze huyu, na cho chote utakachogharimiwa zaidi, mimi nitakaporudi nitakulipa. Waonaje wewe, katika hao watatu, ni yupi aliyekuwa jirani yake yule aliyeangukia kati ya wanyang’anyi? Akasema, Ni huyo aliyemwonea huruma. Yesu akamwambia, Enenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo.” Lk 10: 25-37. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema kwa ufupi kabisa, Msamaria mwema: Alipomwona alimhurumia, akakaribia, akamfunga jeraha zake; akazitia mafuta na divai; akampandisha juu ya mnyama wake, akampeleka mpaka nyumba ya wageni, akamtunza. Huu ndio mwelekeo alionao Kristo Yesu kwa binadamu, anayewaonesha huruma, upendo na ujirani mwema na kwamba, kwa njia ya huruma na upendo, waamini wanaweza kugeuka na kuwa ni majirani wema kwa wagonjwa na wenye shida. Kristo Yesu ni Msamaria kutoka mbinguni aliyemwonea huruma mwanadamu akamsogelea, akajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kumfunga mwanadamu majeraha yake. Upendo huu unarutubishwa kwa mwanadamu kukutana na Kristo Yesu, kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Francisko wa Assisi katika huduma kwa wakoma, akapata furaha ya kupenda kama ilivyokuwa kwa Msamaria Mwema.

Mateso na mahangaiko ya watoto wa Yemen: Madhara ya vita
Mateso na mahangaiko ya watoto wa Yemen: Madhara ya vita   (AFP or licensors)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, huruma inamsukuma mwamini kuguswa na mateso na mahangaiko ya jirani zake, kama ilivyokuwa kwa Msamaria mwema akakaribia, akamfunga jeraha zake; akazitia mafuta na divai. Utume huu ni shirikishi kama Wasamaria wema, mtunza nyumba ya wageni, ndugu na jamaa na kwamba, huduma kwa wagonjwa na dhaifu ni sehemu ya utume wa Mama Kanisa Ulimwenguni, watu wote wenye mapenzi mema, wanapaswa kushiriki kikamilifu, kila mmoja kadiri ya wito na huruma yake kwa wagonjwa, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kwa kusukumwa na upendo wa Mungu, ili kuwawezesha watu kukutana wao kwa wa sanjari na ndugu zao katika Kristo Yesu, kielelezo cha upendo kwa Mungu unaomwilishwa katika upendo kwa jirani, chanda na pete, kinachomweza mwamini kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa jirani yake, kielelezo cha upendo kwa Mungu unaomwilishwa katika matendo, kielelezo cha imani tendaji; kwa kutambua na kuthamini: utu, heshima na haki msingi za binadamu; kwa kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya udugu wa kibinadamu sanjari na upendo kwa Mungu. Baba Mtakatifu Leo XIV anapenda kuwahimiza waamini kuhakikisha kwamba, katika maisha na utume wao, waendelee kujkikita katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu unaosimikwa katika dhana ya “Msamaria Mwema” inayofumbata pamoja na mambo mengine: Ujasiri, Uwajibikaji, Upendo na Mshikamano wa udugu wa kibinadamu unaopata chimbuko lake katika ushirikiano na Mwenyezi Mungu na imani kwa Kristo Yesu. Na kwa njia hii, waamini wanaweza kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya wagonjwa, wazee na wote wanaoteseka.

Siku ya 34 ya Wagonjwa Duniani 11 Februari 2026
Siku ya 34 ya Wagonjwa Duniani 11 Februari 2026

Mwishoni mwa ujumbe wake kwa Siku ya 34 ya Wagonjwa Ulimwenguni kwa Mwaka 2026, Baba Mtakatifu Leo XIV anapenda kuinua sala zake kwa Bikira Maria Afya ya Wagonjwa, akiomba huruma na msaada kwa wagonjwa na wote wanaoteseka; awalinde na kuwaombea ili wapate baraka kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Anapenda kutoa baraka zake za Kitume kwa wagonjwa wote, ndugu na jamaa zao; madaktari, wauguzi pamoja na wafanyakazi wote katika sekta ya afya, na kwa namna ya pekee, wale wanaoshiriki kikamilifu katika Maadhimisho ya Siku ya 34 ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2026.

Ujumbe wa Papa Leo XIV Wagonjwa
10 Februari 2026, 15:05