Papa Leo XIV:Umoja wa Kikristo unaweza kuwa chachu ya amani duniani na upatanisho kwa wote
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu alikutana mjini Vatican na washiriki wa mafunzo ya mapadre vijana na wamonaki wa Makanisa ya Kiorthodox ya Mashariki tarehe 5 Februari 2026, ambao ni mpango unaotekelezwa na Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Kikiristo. "Amani iwe nanyi nyote mlio katika Kristo!" (1 Pt 5:14). Kwa maneno haya ya Mtakatifu Petro, ninawakaribisha ninyi, mapadre na watawa wanaowakilisha Makanisa ya Kiorthodox ya Armenia, Coptik, Ethiopia, Eritrea, Malankara na Siria. Pia ninatoa salamu za kidugu kwa Askofu Mkuu Khajag Barsamian na Askofu Mkuu Barnaba El-Soryani, wanaowasindikiza.”
Papa alipenda kutoa heshima na shukrani zake kwa viongozi wa heshima wa Makanisa yao ya Kiorthodox ya Mashariki, ambao wamewateua kushiriki katika ziara hii ya masomo iliyoandaliwa na Baraza la Kipapa la Kuhamaisha Umoja wa Kikristo. Ni matumaini wamefurahia ziara hiyo ambayo ilikusudiwa kuwapa fursa ya kujifunza zaidi kuhusu Kanisa Katoliki, hasa Baraza la Wawakilishi la Roma na taasisi za elimu za Roma. Kadhalika Papa ana uhakika kwamba ziara yao pia imekuwa baraka kwa wale wote waliokutana nao hapa, kuwawezesha kujifunza zaidi kuhusu Makanisa yao.
Tumesherehekea Juma la Kuombea Umoja wa Kikristo
Hivi karibuni, Papa alieleza “ tulivyosherehekea Juma Maombi kwa ajili ya Umoja wa Kikristo, ambalo mada yake ilichukuliwa kutoka katika barua ya Mtakatifu Paulo kwa Waefeso, ambapo Mtume anasisitiza umuhimu wa kuungana katika Imani kwamba : "Kuna mwili mmoja na Roho mmoja, kama vile mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu" (Efe 4:4). Kama tunavyojua, “Mtakatifu Paulo alisafiri sana Israeli, Asia Ndogo, Siria, Arabia na hata Ulaya. Kwa kuanzisha na kutembelea jumuiya nyingi za Kikristo, aligundua sifa za kila kanisa, yaani kabila lao, desturi zao, pamoja na changamoto na wasiwasi.” Mtume aligundua kwamba jumuiya hizo zinaweza kuwa na mtazamo wa ndani sana, zikizingatia matatizo yao mahususi. Matokeo yake, katika barua zake zote, Mtakatifu Paulo aliazimia kuwakumbusha kwamba walikuwa sehemu ya Mwili mmoja wa Fumbo la Kristo.
Kwa kufanya hivyo, aliwatia moyo kusaidiana na kudumisha umoja wa imani na mafundisho yanayoakisi asili isiyo na kifani na umoja wa Mungu. Kwa hiyo Papa alisema tofauti za kihistoria na kiutamaduni katika Makanisa yetu zinawakilisha mfano mzuri wa urithi wetu wa Kikristo wa pamoja, jambo ambalo sote tunaweza kuthamini. Wakati huo huo, tunapaswa kuendelea kusaidiana, ili tuweze kukua katika imani yetu ya pamoja katika Kristo, ambaye ndiye chanzo kikuu cha amani yetu (taz. Efe 2:14). Hili linahitaji tujifunze "kujivua silaha." Kama Patriaki Athenagoras, mwanzilishi wa harakati ya kiekumeni, alivyosema katika sala nzuri kwamba: "Nimeondolewa haja ya kuwa sahihi, kujihesabia haki kwa kuwahukumu wengine," kwa kupigana "vita ngumu zaidi, vita dhidi yangu mwenyewe." Tunapoondoa ubaguzi tunaobeba ndani yetu, na kuivua silaha mioyo yetu, tunakua katika upendo, tunafanya kazi kwa karibu zaidi pamoja na kuimarisha vifungo vyetu vya umoja katika Kristo. Kwa njia hii, umoja wa Kikristo pia unakuwa chachu ya amani duniani na upatanisho wa wote. Papa Leo XIV kwa kuhitimisha alisema huku akisasisha shukrani zake kwa ziara yao kwamba “ninawahakikishia ukumbusho wangu katika sala. Bwana awabariki na Bikira Maria Mwenyeri, Mama wa Mungu, awalinde ninyi na Makanisa yenu pendwa.”
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku: Just click here
