Tafuta

Tarehe Mosi, Februari 2026 wananchi wa Uswisi wameadhimisha Ibada ya Kiekumene, ili kuwakumbuka na kuwaombea vijana 41 waliopteza maisha katika janga hili na wengine 115 kujeruhiwa vibaya. Tarehe Mosi, Februari 2026 wananchi wa Uswisi wameadhimisha Ibada ya Kiekumene, ili kuwakumbuka na kuwaombea vijana 41 waliopteza maisha katika janga hili na wengine 115 kujeruhiwa vibaya.   (AFP or licensors)

Papa Leo XIV: Fumbo la Kifo Katika Maisha ya Mwanadamu!

Tarehe Mosi, Februari 2026 wananchi wa Uswisi wameadhimisha Ibada ya Kiekumene, ili kuwakumbuka na kuwaombea vijana 41 waliopteza maisha katika janga hili na wengine 115 kujeruhiwa vibaya. Baba Mtakatifu Leo XIV ametuma ujumbe maalum katika Ibada hii, akiwatia shime wale waliofikwa na msiba huu mzito, wagonjwa wanaoendelea kuteseka na wale ambao wamepata vilema vya kudumu. Msaada wa hali na mali unahitajiwa ili kuweza kulikabili janga hili!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Kanisa wanasema, maana ya Kikristo ya kifo imefunuliwa katika mwanga wa Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu ambaye ndani yake mna tumaini la Wakristo. Mkristo anayekufa katika Kristo Yesu huuacha mwili ili kwenda kukaa pamoja na Mwenyezi Mungu, milele yote! Kwa Mkristo, siku ya kifo huanzisha, mwishoni mwa maisha yake ya Kisakramenti, utimilifu wa kuzaliwa kwake upya kulikoanzishwa na Sakramenti ya Ubatizo, kufanana kamili na sura ya Mwana, kulikotolewa kwa Mpako wa Roho Mtakatifu na ushirika katika karamu ya Ufalme, uliotangulizwa katika Ekaristi, hata kama ana lazima bado kutakaswa zaidi ili kuvikwa vazi la arusi! Waamini wanahamasishwa kulitafakari Fumbo la kifo, kama sehemu ya matumaini ya Kikristo kwani, Kristo Yesu mwenyewe anasema, ndiye ufufuo na uzima na kwamba, yeyote anayemwamini ajapokufa atakuwa anaishi na kwamba, heri yao wale wote wanaokufa katika Kristo Yesu. Matumaini ya Kikristo yawasaidie waamini kukabiliana na Fumbo la kifo kwa imani na matumaini na kwamba, hata ustaarabu wa watu wa kale umepitia katika fumbo hili na kwa hakika, ibada ya kifo ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya binadamu. Mzaburi anasema, “Basi, utujulishe kuzihesababu siku zetu, tujipatie moyo wa hekima.” Haya ni maneno yanayowatia waamini matumaini badala ya kujisikia kuwa wanyonge wanapoyaona maisha yao yana yoyoma na kutoweka mara kama ndoto ya mchana. Kifo kinayaanika maisha ya binadamu na kumwondolea kiburi na kuwahimiza watu kujenga na kudumisha upendo, kutafuta na kuambata mambo msingi katika maisha, ili sadaka na majitoleo yao yaweze kuwapatia amani na utulivu wa ndani wanapokabiliana na Fumbo la Kifo!  Kristo Yesu anapenda kuimarisha matumaini ya waja wake kwamba, Yeye ndiye ufufuo na uzima! Jambo la msingi ni wao kumwamini.

Vijana 41 walifariki dunia na wengine 115 walijeruhiwa vibaya
Vijana 41 walifariki dunia na wengine 115 walijeruhiwa vibaya   (AFP or licensors)

Takribani watu 41 walifariki dunia na wengine 115 kujeruhiwa, wengi wao vibaya, baada ya moto mkubwa kuteketeza baa wakati wa Sherehe za Mwaka Mpya yaani tarehe 31 Desemba 2025 katika Kituo cha Mapumziko cha Milimani cha Crans-Montana nchini Uswisi. Moto huo ulizuka chini ya saa mbili baada ya kuingia mwaka mpya, na kugeuza baa ya “Le Constellation” kutoka eneo la shangwe hadi kuwa kitovu cha simanzi na majonzi. Tangu wakati huo, watu wa Mungu nchini Uswisi wamekuwa katika kipindi cha sala, umoja na heshima kwa vijana waliofariki dunia na wale waliojeruhiwa. Wamekabiliana na janga hili kwa ujasiri na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Tarehe Mosi, Februari 2026 wananchi wa Uswisi wameadhimisha Ibada ya Kiekumene, ili kuwakumbuka na kuwaombea vijana 41 waliopoteza maisha katika janga hili na wengine 115 kujeruhiwa vibaya. Baba Mtakatifu Leo XIV ametuma ujumbe maalum katika Ibada hii, akiwatia shime wale waliofikwa na msiba huu mzito, wagonjwa wanaoendelea kuteseka na wale ambao wamepata vilema vya kudumu. Kwa wote hawa amependa kuonesha uwepo wake wa karibu pamoja na huruma ya Kanisa zima, ili kuwaimarisha katika imani kwa Kristo Yesu, wakati huu wa majaribu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Leo XIV kwamba, waathirika hawa wataweza kuonja msaada wa kidugu na kiroho kutoka kwa jirani zao ili kuweza kukabiliana na kipindi hiki cha majonzi kwa ujasiri mkubwa. Kwa hakika nyoyo zao zimejeruhiwa sana kwa mateso na hali inayowapelekea kujisikia kwamba, wametelekezwa.

Papa Leo XIV ametuma ujumbe wa faraja na matumaini.
Papa Leo XIV ametuma ujumbe wa faraja na matumaini.   (AFP or licensors)

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Leo XIV anapenda kuwakabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mateso, ili aweze kuwalinda wakati huu wa majonzi, ili kwa pamoja, waweze kuuangalia Msalaba wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, ili hatimaye, waweze kushiriki katika utukufu na ufufuko wake. Mama Kanisa anatangaza na kushuhudia kwamba, kwa hakika Kristo Yesu amefufuka, chemchemi ya matumaini kwa waja wake; atawafuta machozi na hatimaye furaha itaweza kurejea tena katika nyoyo zao. Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa anasema: “Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.” Rum 8:38-39. Baba Mtakatifu Leo XIV anawatia shime kwamba: mema na mazuri yote walioishi na wapendwa wao, kamwe hayatasahaulika. Katika kipindi hiki cha: majonzi, giza na utupu, Bikira Maria anawaalika kuuangalia Msalaba wa Kristo Yesu, chemchemi ya matumaini na hapo wataweza kupata nguvu na ujasiri wa kuendelea kutekeleza safari yao. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, nia hii ameiweka moyoni mwake na kwamba, anaendelea kuwakumbuka na kuwaombea marehemu wao waweze kupumzika katika usingizi wa amani, wakiwa na matumaini ya ufufuko kwa wafu na uzima wa milele amina. Anawaombea wagonjwa wapate nafuu katika mahangaiko yao! Mwishoni amewapatia baraka zake za kitume.

Janga la Moto

 

02 Februari 2026, 14:36