Papa atakutana na Parokia ya Maria Malkia wa Amani ,Dominika Februari 15
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Parokia ya Mtakatifu Maria Regina Pacis (Malkia wa Amani) huko Ostia Lido itakuwa ya kwanza kupokea ziara ya kichungaji ya Papa Leo XIV, Dominika 15 Februari 2026, ambapo Baba Mtakatifu atakuwa katika jumuiya iliyokabidhiwa kwa Shirika la Utume Katoliki wajuliakanao (Mapadre wa Pallottini). Anatarajia kufika saa 10:00 jioni, masaa ya Ulaya na atakutana mara moja na watoto wa katekisimu na vijana, jumla ya takriban 400, watakaomkaribisha uwanja wa nyuma ya Kanisa. Kisha itakuwa zamu ya wazee, wagonjwa, maskini, na watu wa kujitolea wa Caritas (jumla ya watu 400), watakaomsubiri kwenye ukumbi wa mazoezi.
![]()
Parokia ya Mtakatifu Maria Malkia wa Amani huko Ostia,Roma
Saa 11:00 jioni, Papa Leo XIV ataongoza Misa Takatifu, ambayo atashirikiana na Makamu wake, Kardinali Baldo Reina, Askofu wa Sekta ya Kusini, Askofu Renato Tarantelli Baccari, na paroko wa Parokia hiyo, Padre Giovanni Vincenzo Patanè. Miongoni mwa wengine, mapadre wa Parokia ya Ostia, Msimamizi wa Kikanisa cha Jeshi ya Kodi ya mapato Padre Francesco Chiantera, na wakuu wa sekta ya Kusini pia watakuwepo. Mwishoni mwa Maadhimisho Papa atakutana na baraza la wachungaji katika ukumbi wa Parokia. Kisha, kabla ya kurudi Vatican atasimama kuwasalimia waamini watakaobaki nje, ambao watakuwa wamefuatilia Misa kupitia skrini kubwa itakayoandaliwa kwa ajili ya hafla hiyo.
"Ni muhimu kwamba parokia ya kwanza iliyochaguliwa na Baba Mtakatifu kwa ziara zake za kichungaji imejitolea kwa Maria, Malkia wa Amani," anasema kuhani wa parokia. "Tangu mwanzo wa upapa wake, Papa Leo ameonesha umakini mkubwa kwa mada hiyo na kuzungumzia 'amani isiyo na silaha na kupokonya silaha.” Zaidi ya hayo, licha ya kuwa sehemu ya Jimbo la Roma, “ina sifa ya kuwa na Mtakatifu wake mlinzi, Mtakatifu Augustine, ambaye ni mpendwa sana kwa Papa wetu, ambaye ni Muagostiniani,” alisema. Habari za ziara hii ya kichungaji, Padre Patanè aliendelea kusema, zilipokelewa kwa hisia kubwa na jumuiya nzima ya Parokia. "Ili kuepuka tofauti, tuligawa tiketi kwa kura," alielezea. "Tunaona ni fursa nzuri kuwa jumuiya ya kwanza ambayo Baba Mtakatifu anatembelea... pia ni fursa nzuri ya kusafisha majengo na kusafisha vitu vichache!" Padre huyo alitania. "Yeye ni Papa, lakini kwetu sisi, kwanza kabisa ni Askofu wetu, mchungaji anayetembelea kanisa lake."
Asante kwa kusoma makala haya. Ukitaka kuendelea kupata taarifa mpya, tunakualika ujiandikishe kwa jarida kwa kubofya hapa: cliccando qui
