Nia Za Baba Mtakatifu Leo XIV Kwa Mwezi Februari 2026: Watoto Wagonjwa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Maadhimisho ya Siku ya 34 ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2026 yamenogeshwa na kauli mbiu “Huruma ya Msamaria Mwema: Kupenda kwa Kubeba Maumivu ya Mwingine.” Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe wake anakazia zaidi: Zawadi ya kukutana, furaha ya kuonesha ujirani mwema na uwapo katika huduma; Utume shirikishi katika huduma kwa wagonjwa; Kwa kusukumwa na upendo wa Mungu, ili kuwawezesha watu kukutana wao wenyewe sanjari na ndugu zao katika Kristo Yesu. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kauli mbiu hii inalenga kupyaisha sura ya Msamaria Mwema, wakati huu, kugundua uzuri wa upendo na mwelekeo wa kijamii wa huruma ya Mungu kwa ajili ya wahitaji, wagonjwa na wale wanaoteseka.
Baba Mtakatifu Leo XIV katika Nia zake kwa Mwezi Februari 2026 zinazosambazwa na Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa kwa kushirikiana na Baraza la Kipapa la Mawasiliano Jamii, anaawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kwa muda, ili kusali pamoja naye kuwaombea watoto wenye magonjwa yasiyotibika. Takwimu zinaonesha kwamba, kila mwaka watoto na vijana wenye umri wa miaka 19 wapatao 400, 000 wanateseka kwa ugonjwa wa Saratani na kwamba, wengi wao hawana uwezo wa kupata tiba ya magonjwa yanayowasibu. Kati ya vijana wenye umri wa miaka 21 wanateseka na magonjwa yasiyokuwa na tiba kama vile: Kisukari, Magonjwa ya Moyo na yale yaliyoko kwenye mfumo wa kupumlia.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kwa hakika watu wanawafahamu watoto na familia zao, jinsi wanavyoteseka na hata wakati mwingine kujikatia tamaa; lakini pia wanaweza kuonja upendo mkuu na tumaini katika shida na mahangaiko yao. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuungana naye leo na baadaye, wawashirikishe wengine kusali kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea watoto hawa pamoja na watoto wengine wote wanaoteseka kutokana na magonjwa mbalimbali. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaombea watoto hawa na familia zao, ili kamwe wasitindikiwe tiba na huduma ya afya; mshikamano wa udugu wa kibinadamu na upendo unaoshuhudiwa na jumuiya ya waamini, ili watoto hawa na familia zao, waweze kuimarika katika imani; Mwenyezi Mungu aweze kubariki kazi ya mikono ya madaktari kwa ajili ya tiba kwa watoto wagonjwa na kwamba, Roho Mtakatifu awakirimie mapaji na karama zake, ili kuwapatia madaktari na wauguzi hekima na busara ya kuweza kufanya maamuzi magumu na waendelee kuwahudumia wagonjwa kwa kuthamini utu, heshima na haki zao msingi.
Baba Mtakatifu Leo XIV anamwomba Mwenyezi Mungu aweze kuwarimia watoto wagonjwa na familia zao faraja, imani na matumaini ya maisha mapya. Itakumbukwa kwamba, Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa umeenea katika nchi zaidi ya 90 na unaowaunganisha waamini zaidi ya milioni 22 wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya utume wa Kristo Yesu na Kanisa lake anasema Padre Cristóbal Fones, SJ., Mkurugenzi wa Utume wa Sala Kimataifa. Huu ni mshikamano wa udugu wa kibinadamu unaofumbatwa katika uhalisia wa maisha ya watu; kwa kuwasindikiza watoto wagonjwa sanjari na kuwaenzi wazazi pamoja na familia zao.
