Tafuta

Kardinali Marcello Semeraro tarehe 7 Februari 2026 amemtangaza Mtumishi wa Mungu Padre Salvador Valera Parra, kuwa ni Mwenyeheri. Kardinali Marcello Semeraro tarehe 7 Februari 2026 amemtangaza Mtumishi wa Mungu Padre Salvador Valera Parra, kuwa ni Mwenyeheri.  

Mwenyeheri Padre Salvador Valera Parra: Injili Hai Ya Kristo Yesu!

Padre Salvador Valera Parra alikuwa ni Paroko aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu waliokuwa chini ya usimamizi na uongozi wake. Alibahatika kujivika fadhila ya unyenyekevu na kujitosa barabara katika upendo wa shughuli za kichungaji Parokiani mwake. Hayo yamesemwa na Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 8 Februari 2026 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mt. Petro.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Marcello Semeraro, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu, huko Huércal-Overa, nchini Hispania, Jumamosi tarehe 7 Februari 2026 kwa niaba ya Baba Mtakatifu Leo XIV amemtangaza Mtumishi wa Mungu Padre Salvador Valera Parra, kuwa ni Mwenyeheri. Padre Salvador Valera Parra alikuwa ni Paroko aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu waliokuwa chini ya usimamizi na uongozi wake. Alibahatika kujivika fadhila ya unyenyekevu na kujitosa barabara katika upendo wa shughuli za kichungaji Parokiani mwake. Hayo yamesemwa na Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 8 Februari 2026 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Mwenyeheri Padre Salvador Valera Parra ni mfano bora wa kuigwa na Mapadre wengine, kwani alikita maisha yake ya kichungaji katika mambo muhimu na hatimaye akajitahidi kuyasimika maisha yake katika hali ya unyekevu, majitoleo na sadaka kubwa. Kwa hakika alikuwa ni mchamungu, mtu wa sala iliyorutubishwa kwa Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 13 Machi 1840 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Karama, amana na utajiri wake wa maisha ya kiroho vilianza kuonekana mara baada ya kuhamishiwa kwenye Parokia ya “San Làzaro ad Alhama Murcia” baada ya kifo cha Paroko aliyekuwepo. Akajipambanua katika maadhimisho ya Liturujia na Ibada mbalimbali za Kanisa; akajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa na wazee, kwa kuwatembelea na kuwapatia Sakramenti za Huruma ya Mungu; akawaonjesha watu wa Mungu Injili ya upendo iliyosimikwa katika unyenyekevu.

Mwenyeheri Padre Salvador Valera Parra, Injili Hai ya Kristo Yesu
Mwenyeheri Padre Salvador Valera Parra, Injili Hai ya Kristo Yesu

Mwenyeheri Padre Salvador Valera Parra katika maisha na utume wake, alijipambanua kuwa ni mhudumu wa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii, kiasi kwamba Serikali ya Hispania ikatambua mchango wake na kumpatia Nishani ya Mfalme Carlos III “Cruz de la Real Orden de Carlos III.” Kwa hakika alijitosa kuwasaidia na kuwahudumia waathirika wa ugonjwa wa Kipindupindu, kiasi hata cha kuhatarisha maisha yake; akawa mstari wa mbele kutoa huduma kwa wafungwa na wale waliokuwa wameathirika kwa mafuriko, matetemeko ya ardhi pamoja na majanga ya moto, kiasi cha kuanzisha Kituo cha Huduma kwa Watawa Wazee na wale waliokuwa wanasahaulika. Kwa hakika alikuwa ni Padre aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya huduma ya roho za waamini wake: “Cura animarum.” Na ilipogota tarehe 15 Machi 1889 Mwenyeheri Padre Salvador Valera Parra akaitupa mkono dunia akiwa na umri wa miaka 72. Hili likawa ni tukio la shukrani kwa Mwenyezi Mungu kutoka kwa wanaparokia wake, walioonja katika maisha na utume wake kama Padre ushuhuda wa utakatifu wa maisha, akawakirimia amani na utulivu wa ndani, wale wote aliobahatika kukutana naye! Lengo lake kuu lilikuwa ni kuwasindikiza watu wa Mungu kukutana na Mwenyezi Mungu katika hija ya maisha yao; huku akihakikisha kwamba, anawajalia upendo na neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu; huku akimwilisha katika maisha na utume wake kwa fadhila mbalimbali. Mababa wa Kanisa wanasema kwamba, fadhila ni tabia ya kawaida na imara ya kutenda mema. Yamruhusu mtu si kutenda mema tu bali kutoa kilicho chema kabisa cha nafsi yake. Mtu wa fadhila huelekea mema kwa hisi zake zote pamoja na nguvu za kiroho. Hutafuta mema na kuyachagua kwa matendo halisi.

Mwenyeheri Salvador Valera Parra
Mwenyeheri Salvador Valera Parra

Kuna fadhila za kibinadamu ambayo ni hali thabiti, maelekeo imara, ukamilifu wa kawaida wa akili na utashi zinazotawala matendo ya binadamu, zinazoratibu harara na kuongoza mwenendo kufuata akili na imani. Zinawezesha raha, kujitawala na furaha katika kuishi maisha mema kimaadili. Fadhila adili hupatikana kwa juhudi za kibinadamu kuungana na upendo wa Mungu. Shabaha ya mtu mwenye fadhila ni kuwa kama Mungu. Kuna fadhila kuu ambazo hutenda kazi kama bawaba nazo ni: Busara, haki, nguvu, na kiasi. Rej. KKK 1803-1803. Kuna fadhila tatu za Kimungu: imani, matumaini na mapendo. Alijitahidi kumwilisha mashauri ya Kiinjili yaani: Ufukara, Utii na Usafi kamili; mambo yaliyofumbatwa katika fadhila ya unyenyekevu, huku akijiachilia mikononi mwa Mungu. Kwa hakika watu wa Mungu nchini Hispania wanamshukuru na kumtukuza Mungu kwa utakatifu, unyenyekevu na unyoofu wa maisha ya Mwenyeheri Padre Salvador Valera Parra. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 18 Machi 2021 akatambua fadhila zake na hivyo kuitwa Mtumishi wa Mungu. Huu ni muujiza wa kwanza kutambuliwa na Baba Mtakatifu Leo XIV baada ya kuchaguliwa kwake kuliongoza Kanisa Katoliki Baba Mtakatifu Leo XIV, tarehe 20 Juni 2025 akaridhia kwamba, atangazwe kuwa ni Mwenyeheri, Ibada iliyoadhimishwa na Kardinali Marcello Semeraro, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu, huko Huércal-Overa, nchini Hispania, Jumamosi tarehe 7 Februari 2026 kwa niaba ya Baba Mtakatifu Leo XIV.

Mwenyeheri Padre Salvador Valera Parra: Ushuhuda wa Utakatifu
Mwenyeheri Padre Salvador Valera Parra: Ushuhuda wa Utakatifu

Kardinali Marcello Semeraro, katika mahubiri yake amemtaja Mwenyeheri Padre Salvador Valera Parra kuwa ni chombo na shuhuda hai wa Injili ya Kristo Yesu, Mchungaji mwema, mfano bora wa kuigwa na Mapadre katika ulimwengu mamboleo. Katika mazingira yalionesha uchoyo, ubinafsi na haraka ya kutenda kupita kiasi na kwa juu juu tu bila kuzama katika undani wake, Mwenyeheri Padre Salvador Valera Parra alikuwa ni shuhuda wa maisha ya unyofu, sadaka na majitoleo yaliyofanyika katika hali ya ukimya sanjari na udumifu katika fadhila ya uaminifu, akajitahidi kuandika Injili ya Tano, changamoto kwa kila mwamini kuandika Injili hii kwa njia ya ushuhuda wa maisha yake adili na matakatifu; akawa ni kielelezo cha jicho la Kristo Yesu kwa maskini na wahitaji zaidi; na kupenda kama Kristo Yesu alivyopenda; mfano bora wa kuigwa kutoka kwa watakatifu.

Mwenyeheri Salvador

 

12 Februari 2026, 14:35