Siku ya 48 ya Uhai Kitaifa Nchini Italia: Watoto Kwanza
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe Mosi, Februari 2026 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, aliwakumbusha waamini kwamba, nchini Italia, walikuwa wanaadhimisha “Siku ya Kitaifa ya Kuwakumbuka Waathirika wa Kiraia wa Vita na Migogoro Duniani.” Mpango mkakati huu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, unaendana na hali halisi kwani kila siku kuna waathirika wa vitendo hivi vinavyotumia silaha ambavyo kimsingi vinakiuka waziwazi kanuni maadili na sheria. Watu waliopoteza maisha yao na kujeruhiwa, wataheshimiwa kikweli, dhuluma hii isiyoweza kuvumiliwa itakapokomeshwa. Mtakatifu Yohane Paulo II katika Wosia wake wa Kitume, “Evangelium vitae” yaani “Injili ya uhai” kwa ufupi anakazia kuhusu: Thamani ya maisha, ukuu na utu wa binadamu kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hii ni Injili ya upendo wa Mungu kwa binadamu; Utu na heshima yake, mambo msingi yanayofumbatwa katika Injili. Katika ulimwengu mamboleo kuna mambo ambayo yanaendelea kutishia Injili ya uhai kwa kukumbatia utamaduni wa kifo. Haya ni matokeo ya watu kukengeuka pamoja na kuporomoka kwa kanuni maadili na utu wema. Kuna sera na mikakati mbalimbali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii inayotishia Injili ya uhai, ustawi na maendeleo ya wengi. Mtakatifu Yohane Paulo II anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete: kuheshimu, kulinda na kuhudumia Injili ya uhai, ili kukuza na kudumisha haki, maendeleo fungamani ya binadamu, uhuru wa kweli, amani na furaha ya kweli inayobubujika kutoka katika sakafu ya maisha ya mwanadamu. Waamini wanapaswa kujipambanua kuwa ni watu wanaotetea Injili ya uhai kwa ajili ya maisha dhidi ya utamaduni wa kifo.
Ni katika muktadha huu, Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI., Dominika tarehe Mosi Februari 2026 limeadhimisha Siku ya 48 ya Uhai Kitaifa nchini Italia kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Watoto Kwanza.” Maandiko Matakatifu yanasema: “Angalieni msidharau mmojawapo wadogo hawa; kwa maana nawaambia ya kwamba malaika wao mbinguni siku zote huutazama uso wa Baba yangu aliye mbinguni.” Mt 18:10. Ukarimu wa Kristo Yesu kwa watoto ni jambo ambalo liliwashangaza wengi, changamoto na mwaliko wa kuwaheshimu na kuwajali watoto wadogo, kielelezo makini kinachoakisi upendo wa Mungu kwa waja wake; upendo ambao huchukua nafasi, kwa kuwapenda watoto jinsi walivyo. Hii ni tabia inayowaruhusu watoto kupendwa, kutumikiwa pamoja na kujitambua kwamba, wao ni tegemezi. Huu ni mwaliko kwa waamini kutoa kipaumbele cha kwanza kwa sheria za moyo, pamoja na kutamani mema. Kristo Yesu anakaza kusema: “Nawaambieni kweli, msipogeuka na kuwa kama watoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni. Yeyote anayejinyenyekesha kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkubwa katika ufalme wa mbinguni. Yeyote anayempokea mtoto mmoja kama huyu kwa jina langu, ananipokea mimi. “Yeyote atakayemkosesha mmoja wa hawa wadogo wanaoniamini, ingekuwa afadhali afungwe shingoni jiwe kubwa la kusagia na kuzamishwa kwenye kilindi cha bahari.” Mt 18:3-6. Huu ni mwaliko wa kuacha majivuno, kiburi, kutafuta ukuu na madaraka na badala yake, watu wajiaminishe na kumtegemea Mungu kikamilifu. Watoto kamwe hawapaswi: kudhararuliwa, kutwezwa na kutupiliwa mbali kwani Mwenyezi Mungu anawatunza kwa namna ya pekee, mwaliko wa kukuza na kudumisha utamaduni bora unaotoa kipaumbele cha pekee kwa maslahi bora ya watoto: kwa kukaribishwa, kulindwa, kutunzwa pamoja na familia zao, ili hatimaye, waweze kukua wakiwa huru na wenye furaha, msingi bora wa malezi na makuzi ya watoto kwa sasa na kwa siku za usoni.
Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI linasema, kuna watoto ambao wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi; watoto wanaopelekwa mstari wa mbele vitani kama chambo; watoto wanaouwawa hata kabla ya kuzaliwa, watoto wanaotekwa nyara; watoto wanaozalishwa kwenye maabara na hivyo kunyimwa haki ya kuwafahamu wazazi wao wa kibaiolojia, au Mama aliyewabeba mimba; kuna maelfu ya watoto wanaoishi peke peke baada ya wazazi wao kutengana; baadhi yao wanatumika kama silaha za kulipiza kisasi. Kuna watoto wanaotumbukizwa kwenye biashara ya ngono na utalii; wanaoajiriwa kwenye kazi za suluba kwa ujira “kiduchu”; watoto ambao wamekosa fursa ya kwenda shule na kupata huduma bora za afya. Kuna watoto wanao nyanyasika hata katika familia zao wenyewe; watoto ambao wananyofolewa viungo vyao kama sehemu ya biashara haramu ya binadamu na viungo vyake. Kuna makundi makubwa ya watoto yanayothubutu kuzikimbia familia na nchi zao; kuna watoto ambao wametumbukizwa katika itikadi kali ili kutekeleza maslahi ya wenye nguvu. Kwa hakika, amani, uhuru na demokrasia ya kweli inaweza kuanza kwa kuwajali na kuwathamini watoto wadogo. Lakini, pale ambapo jamii inapoteza hisia ya ukarimu, inaanza kuwanyonya watoto wake, badala ya kuwatumikia na kuwapa uhai, huo ni mwanzo wa kuvunjika kwa haki msingi za binadamu, utu wema, ustawi, maendeleo na mafao ya watoto. Huu ni mwaliko kwa jamii kuwapenda na kuwathamini watoto. Jumuiya za Kikristo zinapaswa kuwa mstari wa mbele katika malezi na makuzi ya watoto ndani ya Jamii kwa kujikita katika ukarimu, kwa kuwashirikisha watoto katika maisha na utume wa Kanisa; kwa kuwarithisha imani, maadili na utu wema. Kwa hakika watoto wanahitaji kuona mifano bora ya maisha kutoka kwa wazazi wao, tayari kukaribishwa katika Jumuiya ya waamini kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo. Kanisa linapaswa kushirikiana na kushikamana na watu pamoja na taasisi zinazojipambanua kwa ulinzi na tunza ya watoto; zinazotoa elimu na malezi bora; zinazosimamia haki msingi za watoto, maadili na utu wema.
Watu na taasisi kama hizi zinapaswa kushukuriwa, kwani zinaendelea kujibidiisha katika ujenzi wa Ulimwengu, ili uweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi watoto. Hii ni changamoto kwa Jamii kuendelea kusimama kidete kutafuta, kulinda na kudumisha haki msingi za watoto, jambo linalohitaji toba na wongofu wa ndani, tayari kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na sera za utoaji mimba. Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linasema kwamba, kuna idadi ndogo sana ya watoto wanaozaliwa nchini Italia. Watoto hawa katika maisha yao ya baadaye, wataelemewa sana na madeni; uharibifu wa mazingira sanjari na athari za mabadiliko ya tabia nchi; upweke hasi pamoja na migogoro inayoendelea kuibuliwa bila kujali mustakabali wa Ulimwengu. Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, linasema, Mama Kanisa tarehe 25 Machi ya kila mwaka anaadhimisha Siku kuu ya Bikira Maria kupashwa habari kwamba, atakuwa ni Mama wa Mkombozi, mwanzo wa Fumbo la Umwilisho, hii ni Siku ya Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo “Pro Life.” Kuna uhusiano wa karibu kati ya Fumbo la Umwilisho na utume wa familia. Kadiri ya mpango wa Mungu, Kristo Yesu alizaliwa na kukulia katika familia ya binadamu iliyoundwa na Mtakatifu Yosefu pamoja na Bikira Maria. Kanisa linapoadhimisha Siku ya Uhai, linapenda kukazia kuhusu umuhimu wa: Maisha, utu na heshima ya kila binadamu. Tangu mwanzo, Mwenyezi Mungu alipenda kuibariki familia na kuipatia dhamana ya kuendeleza kazi ya uumbaji; ili kweli iweze kuwa ni Jumuiya ya maisha na upendo katika moyo wa jamii. Jumuiya ya Kimataifa inahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, inajenga na kudumisha utamaduni wa uhai kwani huu ni urithi wa binadamu wote dhidi ya utamaduni wa kifo! Hii iwe ni fursa ya kukuza na kudumisha dhamiri nyofu; iwe ni siku ya kutetea watoto ambao hawajazaliwa pamoja na kuwaenzi watoto katika maisha, malezi, makuzi na matamanio yao halali.
