Tafuta

Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Bikira Maria wa Lourdes sanjari na Siku ya 34 ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2026 yanafanyika Jumatano tarehe 11 Februari 2026. Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Bikira Maria wa Lourdes sanjari na Siku ya 34 ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2026 yanafanyika Jumatano tarehe 11 Februari 2026.   (ANSA)

Maadhimisho ya Siku ya 34 ya Wagonjwa Duniani 2026: Msamaria Mwema!

Maadhimisho ya Siku ya 34 ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2026 yananogeshwa na kauli mbiu “Huruma ya Msamaria Mwema: Kupenda kwa Kubeba Maumivu ya Mwingine.” Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kauli mbiu hii inalenga kupyaisha sura ya Msamaria Mwema, wakati huu, kugundua uzuri wa upendo na mwelekeo wa kijamii wa huruma ya Mungu kwa ajili ya wahitaji, wagonjwa na wale wanaoteseka. Kardinali Michael Czerny, anamwakilisha Papa Leo XIV.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Siku ya Wagonjwa Duniani, ilianzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako tarehe 13 Mei 1992 na kuadhimishwa kwa mara ya kwanza kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Lourdes nchini Ufaransa kunako tarehe 11 Februari 1993. Siku ya Wagonjwa Duniani ni nafasi ya kutafakari kanuni maadili na utu wema; sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya wagonjwa na wazee, tayari kusoma alama za nyakati kwa kusikiliza na kujibu kilio cha wagonjwa na wale wanaoteseka. Hii ni siku maalum kwa ajili ya kukoleza uragibishaji na maadhimisho yanayokusudia kuwasaidia waamini kusali na kushiriki mateso ya wagonjwa; na kwa wagonjwa wenyewe kutolea mateso na mahangaiko yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo Yesu na hatimaye, kuwakumbusha wagonjwa kuwa wao ni sura na ufunuo wa Kristo Yesu, anayeteseka kati pamoja nao. Hii ni siku inayopania kuamsha tena na tena huruma na upendo kwa wagonjwa, ili kuwatunza kwa mapendo ya dhati. Ni siku inayopania kukuza na kudumisha kanuni maadili, utu wema pamoja na haki msingi za wagonjwa, sanjari na kuangalia changamoto wanazokabiliana nazo wagonjwa na katika sekta ya afya kwa ujumla wake, ili kuweza kuzipatia ufumbuzi wa kudumu.

Papa Leo XIV akizungumza na ujumbe kutoka Jimbo la Chiclayo, Peru
Papa Leo XIV akizungumza na ujumbe kutoka Jimbo la Chiclayo, Peru   (@Vatican Media)

Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Bikira Maria wa Lourdes sanjari na Siku ya 34 ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2026 yanafanyika Jumatano tarehe 11 Februari 2026. Kimataifa maadhimisho haya yanafanyika kwenye Madhabahu ya Bikira Maria, Mama Yetu wa Amani, Jimbo Katoliki la Chiclayo, nchini Perù: “Nuestra Señora de la Paz en Chiclayo.” Ujenzi wa Madhabahu haya ni jitihada za maisha ya kiroho na kichungaji zilizoasisiwa na Mtakatifu Yohane Paulo II. Maadhimisho ya Siku ya 34 ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2026 yananogeshwa na kauli mbiu “Huruma ya Msamaria Mwema: Kupenda kwa Kubeba Maumivu ya Mwingine.” Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kauli mbiu hii inalenga kupyaisha sura ya Msamaria Mwema, wakati huu, kugundua uzuri wa upendo na mwelekeo wa kijamii wa huruma ya Mungu kwa ajili ya wahitaji, wagonjwa na wale wanaoteseka.

Maadhimisho ya Siku ya 34 ya Wagonjwa Duniani, 2026
Maadhimisho ya Siku ya 34 ya Wagonjwa Duniani, 2026

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu amemteuwa Kardinali Michael Czerny, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu, kuwa ni Mwakilishi wake wa Kitume katika Maadhimisho ya Siku ya 34 ya Wagonjwa Duniani, huku akiambatana na Askofu mkuu Paolo Rocco Gualtieri, Balozi wa Vatican nchini Perù pamoja na wajumbe wa shughuli za kichungaji kwa ajili ya wagonjwa kutoka katika Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini na Karibea; CELAM linalounganisha Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kutoka katika nchi 22. (Consejo Episcopal Latinoamericano y Caribeño). Katika barua ya uteuzi huu, Baba Mtakatifu Leo XIV hata baada ya kuchaguliwa kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, mara nyingi moyo, upendo na akili zinaiendea nchi ya Peru, ambako watu waaminifu wa Mungu wakiongozwa na utauwa na upendo, wanakimbilia kwa ujasiri na utauwa ulinzi na tunza ya Bikira Maria. Baba Mtakatifu Leo XIV anakiri kwamba, miaka kumi na miwili iliyopita, aliwekwa wakfu kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Chiclayo na tangu wakati huo akajiweka wakfu kwa ulinzi na tunza ya Bikira Maria na kwa sasa utume wake kwa Kanisa zima, kwa ajili ya Ukristo na Utakatifu wa maisha. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, ameridhia uamuzi wa maadhimisho haya uliokuwa umekwisha kutolewa na Hayati Baba Mtakatifu Francisko kwa kushirikiana na Baraza la Maaskofu Katoliki Peru wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo. Hapa ni mahali ambapo anasema Baba Mtakatifu Leo XIV pamekuwa ni mahali pake pa sala. Tukio hili ni kielelezo cha umoja na ushirika wa Mama Kanisa katika sala kwa ajili ya waamini wagonjwa, wanaoteseka na wale ambao ni dhaifu, ili kwa sala za waamini kutoka sehemu mbalimbali za dunia, waonje huruma na amani iweze kutawala duniani.

Siku ya Wagonjwa Duniani: Sala, Misa, Upendo na Mshikamano
Siku ya Wagonjwa Duniani: Sala, Misa, Upendo na Mshikamano   (ANSA)

Baba Mtakatifu Leo XIV anawaombea wagonjwa waweze kupata amani na utulivu wa ndani unaobubujika kutoka katika upendo wa Mungu. Baba Mtakatifu Leo XIV anapenda kumwambia Kardinali Michael Czerny, kwamba, amemteuwa ili kumwakilisha katika Maadhimisho ya Siku ya 34 ya Wagonjwa Duniani, kwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu, awape amani na faraja ya Injili, aoneshe moyo wa umoja na ushirika unaopata chimbuko lake kutoka kwa Kristo Yesu mwenyewe aliyesema: “Na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.” Mt 28:20. Hatimaye, Baba Mtakatifu anamwomba Kardinali Michael Czerny, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu kumfikishia salam na matashi mema kwa watu watakatifu wa Mungu nchini Perù. Hii iwe ni fursa ya kutoa ushuhuda wa imani, matumaini na mapendo, huku akionesha uwepo wake wa karibu kibinadamu na kikristo kwa wahitaji, huku wakisaidiana kubeba mizigo ya mateso na mahangaiko yao, ili kutimiza Sheria ya Kristo Yesu kutoka katika vilindi vya nyoyo zao. “Mchukuliane mizigo na kuitimiza hivyo sheria ya Kristo.” Gal 6:2. Mwishoni, Baba Mtakatifu Leo XIV ameukabidhi utume huu wa Kardinali Michael Czerny kwa ulinzi na tunza ya Bikira Maria Malkia wa Amani na hatimaye, akawapatia wote baraka zake za kitume kwa wote wanaoshiriki katika Maadhimisho ya Siku ya 34 ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2026.

Siku ya 34 ya Wagonjwa
09 Februari 2026, 15:05