Tafuta

Baba Mtakatifu Leo XIV katika maisha na utume wake anasisitizia juu ya ukweli wa kimsingi kwamba, huduma ya Khalifa wa Mtakatifu Petro katika undani wa moyo wake inasimikwa katika mahusiano! Baba Mtakatifu Leo XIV katika maisha na utume wake anasisitizia juu ya ukweli wa kimsingi kwamba, huduma ya Khalifa wa Mtakatifu Petro katika undani wa moyo wake inasimikwa katika mahusiano!  (© Archdiocese of Malta)

Kumbukizi ya Miaka 60 ya Uhusiano wa Kidiplomasia Kati ya Malta na Vatican: 1965-2026

Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican “Holy See” na Jamhuri ya Malta, ulianzishwa tarehe 15 Desemba 1965 takribani miaka 60 iliyopita, wakati wa Mapambazuko ya Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, Kanisa katika Ulimwengu mamboleo. Uhusiano huu una nguvu ya kipekee, umejikita katika mahusiano ya kina ya kihistoria na kidini, ambayo mara nyingi yanaoneshwa kwa ziara za kitume zinazotekelezwa na Khalifa wa Mtakatifu Petro. 1965-2026.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Diplomasia ya Vatican na Kanisa Katoliki katika ujumla wake, kimsingi inakazia kwa namna ya pekee kabisa: huduma makini ya maendeleo fungamani ya binadamu; kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Mambo mengine msingi ni: amani na maridhiano kati ya watu; huduma makini kwa wakimbizi na wahamiaji duniani; elimu, afya, biashara, mawasiliano, ushirikiano na mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa pamoja na haki miliki ya kiakili. Hizi ni kanuni msingi zinazofumbatwa katika Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayotoa dira na mwongozo makini kwa Jumuiya ya Kimataifa katika mchakato wa kukuza na kudumisha utamaduni wa amani, haki, ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu. Hii ni sehemu muhimu sana ya utangazaji na ushuhuda wa Habari Njema ya Wokovu miongoni mwa Jumuiya ya Kimataifa. Vatican katika masuala ya kidiplomasia ya Kimataifa inafuata kwa makini sana: Sheria za Kimataifa, taratibu na kanuni za Jumuiya ya Kimataifa sanjari na kuendelea kuwa ni sauti ya kinabii inayojikita katika kanuni maadili na ushirikiano unaosimamiwa na kuratibiwa na kanuni auni. Amani haiwezi kufikiwa mara moja kwa daima, bali inadaiwa kujengwa siku kwa siku. Amani ni matokeo ya haki inayomwilishwa katika upendo, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Rej. GS 78.

Kumbukizi ya Miaka 60 ya Uhusiano wa Kidiplomasia: Vatican na Malta
Kumbukizi ya Miaka 60 ya Uhusiano wa Kidiplomasia: Vatican na Malta   (ANSA)

Amani ya kweli inakolezwa katika urafiki wa udugu wa kibinadamu na kwamba, upatanisho ni mchakato unaopania kuboresha maisha ya mbeleni na unafumbatwa katika toba, msamaha na wongofu wa ndani, ili kujenga na kudumisha utamaduni wa upendo, chemchemi ya amani ya kudumu. Takwimu zinaonesha kwamba, hadi kufikia Januari 2026 Vatican ina uhusiano wa kidiplomasia na nchi 184 duniani kote. Mabalozi wakazi wanaoishi mjini Roma kwa sasa ni 89, wengine, ni mabalozi wanaowakilisha nchi zao wakiwa wanatoka nje ya Roma. Kuna Mashirika ya Kimataifa kama vile, Shirikisho la Nchi za Kiarabu pamoja na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR yote haya yanafanya idadi yake ifikie 93. Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican “Holy See” na Jamhuri ya Malta, ulianzishwa tarehe 15 Desemba1965 takribani miaka 60 iliyopita, wakati wa Mapambazuko ya Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, Kanisa katika Ulimwengu mamboleo. Uhusiano huu una nguvu ya kipekee, umejikita katika mahusiano ya kina ya kihistoria na kidini, ambayo mara nyingi yanaoneshwa kwa ziara za kitume zinazotekelezwa na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Uhusiano huu, unasimamiwa na Baraza la Kitume huko Malta, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ikiwa ni pamoja na elimu, afya mali ya Kanisa, na masuala ya ustawi wa jamii licha ya mivutano ya zamani na ya kihistoria.

Papa Francisko mwaka 2022 alitembelea nchini Malta
Papa Francisko mwaka 2022 alitembelea nchini Malta   (Vatican Media)

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kama sehemu ya maadhimisho ya Kumbukizi ya Miaka 60 ya Uhusiano wa Kidiplomasia kati ya Jamhuri ya Malta na Vatican amesema, Baba Mtakatifu Leo XIV katika maisha na utume wake anasisitizia juu ya ukweli wa kimsingi kwamba, huduma ya Khalifa wa Mtakatifu Petro katika undani wa moyo wake inasimikwa katika mahusiano kama ilivyojitokeza kwenye Kitabu cha Matendo ya Mitume: “Na Petro, akimkazia macho, pamoja na Yohane, akasema, “Tutazame sisi.” Akawaangalia, akitaraji kupata kitu kwao. Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende. Akamshika mkono wa kuume, akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikatiwa nguvu.” Mdo 3:4-7. Huu ni mwaliko wa kuingia katika uhusiano wa kutambuliwa na unaojengwa katika matumaini, kama asili bainifu ya diplomasia ya Vatican inayotekelezwa katika: huduma ya ushirika, inayozingatia watu na tamaduni zao; utu, heshima na haki msingi za binadamu; ushirika latika imani, maadili na utu wema. Malta inautajiri na amana kubwa katika maisha na utume wa Kanisa kwani hapa ni mahali ambapo Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa alijifunga kibwebwe kuwainjilisha watu wa Mataifa, akaonja ukarimu, akawaponya watu sanjari na kudumisha imani.

Kardinali Parolin akiadhimisha Ibada ya Misa Takatifu nchini Malta
Kardinali Parolin akiadhimisha Ibada ya Misa Takatifu nchini Malta

Mabalozi wa Vatican nchini Malta wamekuwa ni alama ya ushirika kati ya Mtakatifu Petro na Kanisa mahalia na kwamba, wameendelea kusaidia na kudumisha uhuru wa Kanisa katika maisha na utume wake na kwamba, makubaliano kati ya Vatican na Malta yametambua umuhimu wa elimu, tunu msingi za maisha ya ndo ana familia; mali ya Kanisa sanjari na majiundo ya Kitaalimungu na kwamba, uhusiano kati ya Kanisa na Serikali unasimikwa katika kuheshimiana, kila upande ukitekeleza dhamana na wajibu wake katika misingi ya ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Malta imekuwa ni mfano mzuri wa ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji na imeendelea kukita mizizi yake katika majadiliano, kwa kusikiliza kwa makini pamoja na uaminifu kwa tunu zake msingi za kijamii. Kimekuwa ni kisiwa cha amani, maridhiano na mapenzi mema, mambo msingi yanayosimamia na kuratibu uhusiano wa Kimataifa. Hii ni changamoto kwa mahusiano ya kidiplomasia kukita mizizi yake katika utu, kanuni maadili, utu wema na matumaini. Maadhimisho ya Kumbukizi ya Miaka 60 ya uhusiano wa Kidiplomasia kati ya Vatican na Malta, ni fursa ya kuendelea kujizatiti katika kuzipatia ufumbuzi changamoto katika ulimwengu mamboleo yaani: Ongezeko la Wakimbizi na Wahamiaji; Mafungamano ya kijamii; Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; Mabadiliko ya Sayansi na teknolojia, pamoja na ulinzi na amani katika utekelezaji wa kanuni ya Kimataifa “International Order.” Kardinali Parolin amesema Mtakatifu Paulo alifika kisiwa cha Malta baada ya meli yake kuvunjika wakati akisafirishwa kwenda Roma kama mfungwa (Matendo 28). Wenyeji walionesha fadhila za kipekee, na Paulo Mtume alinusurika kuumwa na nyoka, jambo lililowashangaza. Alikaa hapo kwa miezi mitatu, akiponya wagonjwa. Hata viongozi wakuu wa Kanisa Katoliki waliobahatika kutembelea Malta, wamepokelewa kwa imani na matumaini, changamoto na mwaliko wa kuendelea kukuza na kudumisha ushirikiano na mshikamano wa kidiplomasia; kwa kusimama kidete kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu; ustawi na maendeleo yake. Miaka hii 60 ya uhusiano wa Kidiplomasia uziwezeshe nchi hizi mbili kuwa ni madaraja ya uvumilivu na unyenyekevu katika huduma ya amani ulimwenguni.

Waziri mkuu Robert Abel wa Mlta mwaka 2025 alitembelea Vatican.
Waziri mkuu Robert Abel wa Mlta mwaka 2025 alitembelea Vatican.   (@VATICAN MEDIA)

Katika mahubiri yake, Dominika tarehe Mosi, Februari 2026 amekazia kuhusu safari ya Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa, jinsi walivyokumbana na dhoruba na hatimaye, wakafika nchini kavu salama na kwamba, akiwa nchini Malta alionja fadhila ya: upendo na ukarimu; tukio ambalo linaonesha: Uaminifu, uwajibikaji na mahusiano katika hatari, tayari kuchukua maamuzi magumu, daima wakimtumainia Mungu muweza wa yote katika maisha yao. Udhaifu wa binadamu hapa unakumbana na kuonja ukarimu wa watu wa Mungu. Mdo 27-28. Hiki ni kielelezo makini cha umoja na ushirika kati ya Watakatifu Petro na Paulo wanaosimika maisha na utume wao kwa kukutana na watu, ushuhuda wa imani; Umoja, mwendelezo na ushirika. Kumbe, uhusiano wa kidiplomasia kati ya Malta na Vatican unapaswa kueleweka katika misingi hii kwa kuendelea kujikita katika ujenzi wa madaraja yanayowakutanisha watu, majadiliano katika ukweli na uwazi sanjari na ushirikiano katika uaminifu. Huu ni mwaliko wa kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: hifadhi, usalama na ustawi wa maisha yao. Mama Kanisa katika maisha na utume wake, anapenda kuona watu wote wakiokolewa, kwamba, amani inadumu sehemu mbalimbali za dunia na kwamba majadiliano yaweze kuzaa matunda yanayokusudiwa yaani: haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Kumbukizi hii ya Miaka 60 ya Uhusiano wa Kidiplomasia kati ya Vatican na Malta uendelee kuimarishwa katika historia, imani na wajibu shirikishi; kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu.

Uhusiano wa Kidiplomasia kati ya Vatican na Malta unaendelea
Uhusiano wa Kidiplomasia kati ya Vatican na Malta unaendelea   (@VATICAN MEDIA)

Mikataba iliyotiwa saini kati ya pande hizi mbili imeendelea kuimarisha umuhimu wa elimu, tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; mali ya Kanisa; maendeleo na majiundo ya watu wa Mungu. Mikataba hii inapania pamoja na mambo mengine, kuwahudumia watu wa Mungu kwa kuwajibika barabara bila mkanganyiko wowote na kwamba, yote haya yanafanyika katika msingi wa majadiliano  na uhalisia wa mambo. Hija za kitume ambazo zimefanywa na viongozi wakuu wa Kanisa Katoliki nchini Malta, zimekuwa ni muda muafaka wa kuonesha ukarimu na moyo wa sala. Kardinali Pietro Parolin, amewashukuru watu wa Mungu kutoka Malta ambao wameendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya shughuli za kichungaji kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican. Kumbe, uhusiano wa kidiplomasia pamoja na mambo mengine unalenga kukuza na kudumisha: umoja na ushirika na hivyo kuliwezesha Kanisa kutekeleza dhamana na wajibu wake wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kwa ajili ya wokovu wa roho za watu; utu, heshima na haki msingi za binadamu zikipewa kipaumbele cha kwanza, ili Kristo Yesu anayeishi ndani ya waja wake, aendelee kuonesha uwepo wake angavu.

Miaka 60 ya uhusiano wa kidiplomasia
02 Februari 2026, 16:07