Tafuta

Baba Mtakatifu Leo XIV Dominika tarehe 15 Februari 2026 ameanza kutembelea Parokia ya Bikira Maria Malkia wa Amani huko Ostia Lido, Kusini mwa Roma. Baba Mtakatifu Leo XIV Dominika tarehe 15 Februari 2026 ameanza kutembelea Parokia ya Bikira Maria Malkia wa Amani huko Ostia Lido, Kusini mwa Roma.   (ANSA)

Hija ya Kichungaji ya Papa Leo XIV Parokia ya Bikira Maria Malkia wa Amani, Ostia Lido

Papa Leo XIV: Amekazia kuhusu Amri Mpya iliyotolewa na Kristo Yesu, kama utimilifu wa Torati na Manabii katika Agano la Kale. Amri za Mungu ni sehemu ya safari ya ukombozi wa watu wa Mungu; ni dira na mwongozo wa maisha; kielelezo cha upendo wa Mungu kwa waja wake, ili kudumisha uhuru wa watoto wa Mungu, sanjari na utimilifu wa maisha kama linavyojionesha Somo la Pili. Vijana wajifunze kuwa wakweli, waaminifu, wakarimu na wenye upendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa anasema, Kipindi cha Kwaresima, ambacho kwa mwaka huu kinanogeshwa na ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV kwa kauli mbiu: “Kusikiliza na kufunga: Kwaresima kama Kipindi cha Wongofu wa ndani.” Itakumbukwa kwamba, Kwaresima ni kipindi ambacho Kanisa kama Mama na Mwalimu, anawaalika watoto wake kutoa kipaumbele cha pekee kwa Fumbo la Mungu katikati ya maisha yao, ili imani ipate tena nguvu na mioyo ya waamini isipotee katikati ya mahangaiko na bughudha za maisha ya kila siku. Kila safari ya wongofu wa ndani huanza pale waamini wanaporuhusu Neno la Mungu liwafikie na kulikaribisha kwa moyo wa unyenyekevu. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kuna uhusiano kati ya karama ya Neno la Mungu, Nafasi ya Ukarimu na mabadiliko ambayo linaleta. Kwa sababu hiyo, safari ya Kwaresima inakuwa fursa muafaka ya kusikiliza sauti ya Mungu na hivyo kupyaisha tena maamuzi ya kumfuasa Kristo Yesu, kwa kutembea katika njia ile iendayo Yerusalemu ambako Fumbo la Pasaka yaani: Mateso, kifo na ufufuko vinapata utimilifu wake.

Vijana ni chumvi na nuru ya Ulimwengu
Vijana ni chumvi na nuru ya Ulimwengu   (@Vatican Media)

Ni fursa ya kuamsha na kupyaisha ari na mwamko wa kimisionari pamoja na wongofu wa shughuli za kichungaji tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Huu ni mwaliko wa kuwakumbuka na kuwaombea wainjilishaji wote, ili waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa kile wanacho amini, kufundisha na kuadhimisha. Iwe ni fursa ya kugundua na kutambua kwamba, wao kama waamini ni Mitume wa Yesu, changamoto na mwaliko wa kutafuta na kuambata mapenzi ya Mungu katika maisha. Kwaresima ni kipindi cha kuimarisha na kuboresha imani, matumaini na mapendo kwa: kufunga na kusali; kwa kufanya toba na malipizi ya dhambi; kwa kushiriki kikamilifu katika Sakramenti za Kanisa; Kwa kusoma, kutafakari na hatimaye, kumwilisha Neno la Mungu katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo makini cha imani tendaji. Lengo ni kujitakasa na kuambata utakatifu wa maisha, ili hatimaye, kushiriki furaha ya Kristo Mfufuka wakati wa Sherehe ya Pasaka ya Bwana, huku wakiwa wamepyaishwa kwa neema ya Roho Mtakatifu.

Waamini wawe ni vyombo na mashuhuda wa tunu msingi za Injili
Waamini wawe ni vyombo na mashuhuda wa tunu msingi za Injili   (@Vatican Media)

Waamini watambue kwamba wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao kwa watu wanaowazunguka na wale wote ambao Mwenyezi Mungu anawajalia fursa ya kukutana nao katika hija ya maisha yao, ili waweze kujaliwa mwanga na furaha ya Injili katika maisha yao. Mateso na kifo cha Kristo Msalabani, kiwe ni kikolezo cha toba na wongofu wa ndani kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa anayesema: “Lakini sikujulikana uso wangu na makanisa ya Uyahudi yaliyokuwa katika Kristo; ila wamesikia tu ya kwamba huyo aliyetuudhi hapo kwanza, sasa anaihubiri imani ile aliyoiharibu zamani. Wakamtukuza Mungu kwa ajili yangu.” Gal 1: 22-24. Waamini wajitahidi kuwa na kumbukumbu hai ya kukutana na Kristo Yesu katika maisha na utume wao. Ni wakati wa kuuvua utu wa kale na kuanza kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka. Kipindi cha Kwaresima kinasimikwa katika nguzo kuu nne: yaani; Sala, Kufunga, Neno la Mungu na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo cha imani tendaji. Kipindi hiki cha Kwaresima ni mwaliko wa kupanda juu Mlimani Tabor ili kupata mang’amuzi ya maisha ya kiroho na kiutu, ili hatimaye kuweza kuzama zaidi katika Fumbo la maisha ya Kristo Yesu kama utimilifu wa Sheria na Unabii. Ni mwaliko wa kumsikiliza Kristo Yesu kwa umakini mkubwa kama mtindo wa maisha ya Kanisa la Kisinodi na Kimisionari. Waamini wapambane na changamoto za maisha na utume wao kwa ari, ujasiri na moyo mkuu, ili kwamba, Fumbo la Msalaba liwasaidie kukuza imani, matumaini na mapendo, ili hatimaye, waweze kuwa ni mashuhuda na wajenzi wa Kanisa la Kimisionari na la Kisinodi.

Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilelel cha maisha na utume wa Kanisa
Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilelel cha maisha na utume wa Kanisa   (@Vatican Media)

Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2026, Baba Mtakatifu Leo XIV Dominika tarehe 15 Februari 2026 ameanza kutembelea Parokia ya Bikira Maria Malkia wa Amani huko Ostia Lido, Kusini mwa Roma. Hii ni mara yake ya kwanza kutembelea Parokia tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki. Hili ni Kanisa lililobuniwa na Baba Mtakatifu Benedikto XV, wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Kanisa hili likabahatika kutembelewa na Papa Yohane XXIII mwaka 1963, Paulo VI Mwaka 1968; Mtakatifu Yohane Paulo II 1980, pamoja na Papa Francisko mwaka 2015. Parokia hii inahudumiwa na Mapadre wa Shirika la Wapallotini katika nafsi ya Padre Giovanni Patanè, Paroko. Baba Mtakatifu Leo XIV amekutana na kuzungumza na: Watoto na Vijana wapatao 300 wanaojiandaa kwa ajili ya Kupokea Sakramenti za Kanisa; Wazee na Wagonjwa; Maskini, Wahamiaji na Wakimbizi. Watu wa Mungu Parokia ya Bikira Maria Malkia wa Amani huko Ostia Lido, Kusini mwa Roma wamesubiria ujio huu kwa sala na kuhitimishwa kwa Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu. Pamoja na ubora wake, hii ni Parokia inayokabiliana na changamoto pevu ya uwepo wa mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo. Katika mahubiri yake, amekazia kuhusu Amri Mpya iliyotolewa na Kristo Yesu, kama utimilifu wa Torati na Manabii katika Agano la Kale. Amri za Mungu ni sehemu ya safari ya ukombozi wa watu wa Mungu; ni dira na mwongozo wa maisha; kielelezo cha upendo wa Mungu kwa waja wake, ili kukuza na kudumisha uhuru wa watoto wa Mungu, sanjari na utimilifu wa maisha kama linavyojionesha Somo la Pili.

Vijana ni chumvi ya dunia na matumaini ya Kanisa
Vijana ni chumvi ya dunia na matumaini ya Kanisa   (@Vatican Media)

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, uchungu na fadhaa ya wanadamu wa nyakati zetu, hasa ya maskini na ya wale wote wanaoteswa, yote ni furaha na matumaini, uchungu na fadhaa ya wafuasi wa Kristo pia. Rej. Gaudium et spes, 1. Haya ni mafundisho yanayochota amana na utajiri wake kutoka katika Heri za Mlimani, kielelezo cha utimilifu wa Sheria ya Mungu, changamoto na mwaliko kwa waamini kuwa waaminifu kwa Sheria ya Mungu na kuondokana na mambo yale yanayokwenda kinyume cha Sheria hii na kwamba, mambo mabaya yanayojionesha ulimwenguni yanapata chimbuko lake katika moyo wa baridi, mgumu na usiokuwa hata na chembe ya huruma. Baba Mtakatifu Leo XIV amesikitishwa sana na vitendo vya uvunjifu wa amani, matumizi haramu ya dawa za kulevya, kuenea kwa mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo; mambo yanayosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu sanjari na kuwatumbukiza watu katika vitendo vya jinai. Baba Mtakatifu anasema, katika hali na mazingira kama haya, waamini wote wanapaswa kushirikiana na kushikamana katika kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili, kwa kukazia haki, amani na utulivu. Huu ni mwaliko kwa jamii kuwekeza katika mfumo wa elimu makini kwa watoto na vijana. Vijana wa Parokia wajifunze kuwa wakweli na waaminifu; wakarimu na wenye upendo; wajenge moyo wa kuwasaidia wengine na kwamba, wajifunze kuhakikisha kwamba, wanamwilisha imani yao katika matendo adili na matakatifu; wawe ni vyombo na mashuhuda wa upatanisho. Rej Mt 5:23-24.

Jamii iwekeze katika elimu na afya njema
Jamii iwekeze katika elimu na afya njema   (@Vatican Media)

Parokia iwe ni mahali ambapo waamini wanakutana na Mwenyezi Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Jina la Parokia hii ya Bikira Maria Malkia wa Amani ni jitihada za Baba Mtakatifu Benedikto XV, mara baada ya Vita kuu ya Kwanza ya Dunia, iwe ni faraja na mwanga wa matumaini kwa watu wanaoteseka. Huu ni mwaliko kwa waamini kuendelea kusali kwa ajili ya kuombea amani duniani na kwamba, amani yao ya kweli ni Kristo Yesu. Baba Mtakatifu Leo XIV amewaambia vijana wa kizazi kipya kwamba wao ni chemchemi ya matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Bikira Maria Malkia wa amani, daima anawasindikiza katika maisha yao. Maadhimisho ya Ekaristi Takatifu ni mahali pa waamini kupyaisha imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kristo Yesu yu hai kati pamoja na waja wake, kiasi cha kuwakirimia matumaini ili waishi katika amani, upendo na urafiki wa kidugu; ili hatimaye, wao wenyewe waweze kuwa ni chemchemi ya amani na furaha kwa watu wa Mungu mjini Ostia. Baba Mtakatifu amewaalika vijana kumwomba Bikira Maria Malkia wa amani, ili aweze kuwakirimia amani katika nyoyo zao, familia na watu wote katika ujumla wao.Baba Mtakatifu Leo XIV akizungumza na Baraza la Shughuli za Kichungaji Parokia ya Bikira Maria Malkia wa Amani huko Ostia Lido, Kusini mwa Roma, amewataka watambue kwamba, wako Parokiani kwa ajili ya huduma ya Parokia na kwamba, wao ni sehemu ya Jumuiya hai ya imani, inayotangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili na kwamba, sadaka na majitoleo yao ni muhimu katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wao. Watoe kipaumbele cha kwanza kama mashuhuda wa Injili, huku wakijitahidi kutembea pamoja kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, tayari kuisaidia Jumuiya kuwa na mang’amuzi ya imani katika ujenzi wa umoja na ushirika kwa ajili ya Jimbo kuu la Roma na hatimaye kwa Kanisa la Kristo Yesu katika ujumla wake.

Watoto ni amana na utajiri wa Kanisa
Watoto ni amana na utajiri wa Kanisa   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV amepata nafasi ya kukutana na kuzungumza na wazee pamoja na wagonjwa Parokiani hapo na kwamba, wao ni alama hai ya maisha na utume wa Parokia; mahali ambapo waamini wanajifunza kuwa na ukarimu kwa watu wote wa Mungu. Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Michezo ya Olympiki kuanzia tarehe 6 Februari hadi tarehe 22 Februari 2026 na kuanzia tarehe 6 Hadi tarehe 15 Machi 2026 inafanyika Michezo ya Olimpiki, huko Milano na Cortina, Kaskazini mwa Italia, Baba Mtakatifu Leo wa XIV amewatumia barua washiriki wa michezo hii huku akionesha: Thamani ya michezo: Michezo na ujenzi wa amani; tunu msingi za michezo katika majiundo; Mchezo, shule ya maisha na ya kisasa; Michezo na maendeleo binafsi; Mambo yanayohatarisha tunu msingi za michezo; Mashindano na utamaduni wa watu kukutana; Michezo, Mahusiano na mang’amuzi; sanjari na Mpango mkakati wa michezo kwa ajili ya kuwa na maisha tele! Kipindi chote cha mashindano ya Olimpiki, vita na misigano yote ya kisiasa na kijamii ilisitishwa ili kutoa fursa kwa wananchi kufurahia michezo na hivyo michezo ikawa ni fursa ya kujenga na kudumisha amani; ukuaji wa udugu wa kibinadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na kwamba, vita, kinzani na mipasuko ni dalili za kushindwa kwa ubinadamu. Dunia ina kiu ya amani kumbe. Kuna haja ya kutumia nyenzo zitakazo saidia kusitisha matumizi mabaya ya madaraka na hivyo kujikita katika utawala wa haki na sheria. Tunu msingi za michezo katika majiundo ili kuweza kuwa na maisha tele pamoja na utimilifu wake. Rej. Yn 10:10.

Wazee ni amana na utajiri wa Jumuiya
Wazee ni amana na utajiri wa Jumuiya   (@VATICAN MEDIA)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, michezo ni shule ya maisha: inawafunda watu kuwa ndugu wamoja wanaoshirikiana na kushikamana; kwa kutambua na kuthamini umoja na tofauti zao msingi. Uwepo wa wagonjwa ni ushuhuda wenye mvuto na mashiko na kwamba, kila mtu analo jambo ambalo anaweza kuchangia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu na kwamba, maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, sala za watu wa Mungu daima zinawasindikiza katika maisha yao na kwamba, kwa msaada wa Roho Mtakatifu waendelee kuwa ni mashuhuda wa imani na matumaini. Baba Mtakatifu Leo XIV amewakumbusha kwamba, hii ni Parokia yake ya kwanza kuitembelea tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki na kwamba hapa kuna mizizi ya maisha na utume wa Mtakatifu Augostino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa. Mwishoni mwa ziara yake ya kichungaji kwenye Parokia ya Bikira Maria Malkia wa Amani huko Ostia Lido, Kusini mwa Roma, Baba Mtakatifu Leo XIV amewataka waamini kuwa ni nuru ya ulimwengu na hatimaye, akawapatia baraka zake za kitume!

Papa Leo XIV Hija ya Kitume
16 Februari 2026, 10:30