Tafuta

Hadi kufikia tarehe 9 Januari 2026 takwimu zinaonesha kwamba, Vatican ina uhusiano wa Kidiplomasia na nchi 184 na Mashirika ya Kimataifa ni 9, Jumla ni Nchi na Mashirika ya Kimataifa 93 Hadi kufikia tarehe 9 Januari 2026 takwimu zinaonesha kwamba, Vatican ina uhusiano wa Kidiplomasia na nchi 184 na Mashirika ya Kimataifa ni 9, Jumla ni Nchi na Mashirika ya Kimataifa 93  (Vatican Media)

Vatican Ina Uhusiano wa Kidiplomasia na Nchi 184 Na Mashirika ya Kimataifa ni 93

Takwimu zinaonesha kwamba, Vatican ina uhusiano wa kidiplomasia na nchi 184 duniani hadi kufikia mwaka 2026. Mabalozi wakazi wanaoishi mjini Roma kwa sasa ni 89, wengine, ni mabalozi wanaowakilisha nchi zao wakiwa wanatoka nje ya Roma. Kuna Mashirika ya Kimataifa kama vile, Shirikisho la Nchi za Kiarabu pamoja na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR yote haya yanafanya idadi yake ifikie 93. Diplomasia: Ujenzi: haki, amani na maridhiano.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV anabeba ndani mwake tasaufi ya Mtakatifu Agostino anayetoa ufunguo wa jinsi ya kutafuta amani, mintarafu diplomasia kwa kujikita katika amani “Ukipenda amani, katika hali yoyote uliyo nayo; wahurumie wale ambao hawapendi kile unachopenda; wahurumie kwa kukosa kile ambacho unacho wewe.” Ni maneno kuntu kutoka kwa Mtakatifu Augostino, mwaliko na changamoto ya watu kuvuka tofauti zao msingi, ili hatimaye kujenga msingi wa majadiliano kati ya watu wa Mataifa, Majadiliano ya kidini na majadiliano kati ya watu wenyewe. Watu wa Mungu wanapaswa kushukuru kwa maendeleo makubwa sayansi na teknolojia ambayo inaonesha matunda mengi, lakini pia dunia imeendelea kushuhudia kinzani, migogoro, mipasuko na vita; ukosefu wa usawa unaendelea kupanuka kila kukicha, hali inayoongesha choyo na ubinafsi, changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa. Katika hali na mazingira kama haya, uzoefu na mang’amuzi ya Mama Kanisa ni msaada mkubwa sana kwa Jumuiya ya Kimataifa.

Diplomasia ya Vatican inajikita katika utu, heshima, haki na amani
Diplomasia ya Vatican inajikita katika utu, heshima, haki na amani   (@VATICAN MEDIA)

Takwimu zinaonesha kwamba, Vatican ina uhusiano wa kidiplomasia na nchi 184 duniani hadi kufikia Januari 9, mwaka 2026. Mabalozi wakazi wanaoishi mjini Roma kwa sasa ni 89, wengine, ni mabalozi wanaowakilisha nchi zao wakiwa wanatoka nje ya Roma. Kuna Mashirika ya Kimataifa kama vile, Shirikisho la Nchi za Kiarabu pamoja na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR yote haya yanafanya idadi yake ifikie 93. Diplomasia ya Kimataifa inajielekeza zaidi katika ujenzi wa haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Hii ni sehemu ya utangulizi uliotolewa na Balozi George Poulides kutoka Cyprus, ambaye ni Dekano wa Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican, Ijumaa tarehe 9 Januari 2026 wakati Baba Mtakatifu Leo XIV alipokutana na kuzungumza na Mabalozi hawa kwa mara ya pili mesema, Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kumkumbuka na kumwombea Hayati Baba Mtakatifu Francisko ambaye ni kiongozi aliyesimama kidete kupambania amani pamoja na changamoto mbalimbali za Jumuiya ya Kimataifa. Bado anayo kumbukumbu hai, ya bahari ya watu waliofurika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro na viunga vyake siku ile ya tarehe 8 Mei 2025 alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki akiwa ni Papa 267 na kwamba, salam zake za kwanza ni “Amani ya Kristo Mfufuka Iwe Nanyi Nyote.”

Vatican ina uhusiano wa kidiplomasia na nchi 184 na Mashirika 93
Vatican ina uhusiano wa kidiplomasia na nchi 184 na Mashirika 93   (@VATICAN MEDIA)

Ujumbe Baba Mtakatifu kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya Kuombea Amani Duniani hutumwa kwa wakuu wa nchi na Jumuiya ya Kimataifa. Ujumbe huu huonesha dira na mwelekeo wa utendaji wa shughuli za kidiplomasia zitakazotekelezwa na Vatican katika kipindi cha Mwaka mzima. Amani kama tunda la haki, linamtazama mwanadamu katika ujumla wake, kiroho, kimwili, kisiasa, kiuchumi na hata kiutamaduni. Na kwamba, mwanadamu anapaswa kupata haki yake ya msingi katika hayo, ile haki ya kuzaliwa nayo, kinyume cha hapo tayari mwanadamu anakosa haki yake ya msingi, na ndio chanzo cha vurugu na kukosekana kwa amani katika jamii. Balozi George Poulides amegusia hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Leo XIV nchini Uturuki na Lebanoni, Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 1700 ya Mtaguso wa NICEA, mkazo ukiwa ni katika ujenzi wa haki na amani, kwa kujikita katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi. Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo na kwamba, maadhimisho haya yamekoleza moyo wa upendo, na udugu wa kibinadamu; haki na amani na kwamba, kuna uwezekano mkubwa wa watu kutoka katika tamaduni mbalimbali kuishi kwa amani na upendo. Anasema, binadamu yupo katika njia panda, akikabiliana na mapinduzi ya kidijitali yanayoletwa na Akili Unde (AI) ambayo imekuwa na athari kubwa katika nyanja mbalimbali kama elimu, ajira, sanaa, afya, utawala, mawasiliano, na hata masuala mbalimbali ya kijeshi. Hali hii inahitaji uwajibikaji na busara ili kuhakikisha kwamba maendeleo ya Teknolojia ya Akili Unde yanafanyika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi vinginevyo ni hatari kwa utu wa binadamu. Amewakumbuka vijana walipoteza maisha huko Crans-Montana, amewakumbuka na kuwaombea watu wa Mungu nchini Venezuela wanaokabiliana na hali tete ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Mwishoni wa hotuba yake amemtakia Baba Mtakatifu Leo XIV heri na baraka kwa Mwaka 2026.

Dekano
09 Januari 2026, 15:13