Tafuta

Shirikisho la Vyombo Vya Habari vya Kikatoliki Nchini Ufaransa “Fédération des Médias Catholiques de France” kuanzia tarehe 21 hadi 23 Januari 2026 vinafanya mkutano wake mkuu wa 29 huko Lourdes, nchini Ufaransa. Shirikisho la Vyombo Vya Habari vya Kikatoliki Nchini Ufaransa “Fédération des Médias Catholiques de France” kuanzia tarehe 21 hadi 23 Januari 2026 vinafanya mkutano wake mkuu wa 29 huko Lourdes, nchini Ufaransa.  (ANSA)

Ujumbe wa Papa Leo XIV Kwa Shirikisho La Vyombo Vya Habari Vya Kikatoliki Ufaransa

Shirikisho la Vyombo Vya Habari vya Kikatoliki Nchini Ufaransa kuanzia tarehe 21 hadi 23 Januari 2026 vinafanya mkutano wake mkuu wa 29 huko Lourdes, ili kusoma alama za nyakati, tayari kuangalia fursa zilizopo sanjari na kujibu changamoto zinazoendelea kuibuliwa katika tasnia ya mawasiliano ya jamii.; Matumizi ya Teknolojia ya Akili Unde, ili kukuza na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kijamii, bila ya kumtenga mtu awaye yote. Hii ni huduma kwa wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV anawashukuru na kuwapongeza wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii kwa mchango wao mkubwa ambao ni neema na baraka kwa Mama Kanisa katika maisha na utume wake. Anakazia umuhimu wa kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano. Aidha ameonesha mshikamano wa Mama Kanisa na waandishi wa habari waliofungwa au kupotea katika mazingira tatanishi akieleza kwamba, waandishi wa habari ni wahudumu wa ukweli; kumbe, kuna umuhimu wa kutumia vyema rasilimali muda kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Pia anakazia umuhimu wa mawasiliano yanayojenga na kudumisha umoja na mshikamano kati ya watu wa Mataifa; Matumizi sahihi ya teknolojia ya akili unde “Artificial Intelligence” na kwamba, Vyombo vya mawasiliano ya jamii visaidie kukuza na kudumisha kiu ya haki, amani, umoja na upendo; ili kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu na kwa namna ya pekee kuna haja ya kusimama kidete kulinda uhuru wa vyombo vya mawasiliano ya jamii. Matumizi ya teknolojia ya Akili Unde “Artificial Intelligence” yanaendelea kuleta mageuzi makubwa katika ulimwengu wa kazi na mahali wanapoishi watu! Mabadiliko haya ni makubwa, kumbe, yanapaswa kuongozwa na kusimamiwa na sheria mpya, kanuni maadili na utu wema. Katika mchakato wa tasnia ya mawasiliano, kuna haja ya kujikita katika: huruma na upendo, udugu wa kibinadamu na mshikamano. Maendeleo ya sayansi na teknolojia yanachangia kwa kiasi kikubwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, lakini hayana budi kufumbatwa katika utu na heshima ya binadamu. Compyuta ni chombo cha huduma ambacho kimetumiwa na watu wengi kwa ajili ya maendeleo, lakini pia, kuna baadhi ya watu wamekitumia vibaya kwa malengo yao binafsi kiasi cha kuleta tafrani ulimwenguni. Sayansi na teknolojia haina budi kujikita katika misingi ya maadili na utu wema; malezi na majiundo kwa ajili ya matumizi sahihi ya nyenzo za mawasiliano ya jamii; ili kujenga uelewa na uwajibikaji wa pamoja.

Maendeleo na matumizi makubwa ya teknolojia ya akili unde yadhibitiwe
Maendeleo na matumizi makubwa ya teknolojia ya akili unde yadhibitiwe   (AFP or licensors)

Matumizi ya Akili Unde yataendelea kusababisha mabadiliko makubwa katika maisha ya watu, kumbe, malezi na majiundo makini ni muhimu sana hasa kwa vijana wa kizazi kipya. Hili ni jukumu la viongozi wa Serikali, wanasiasa, watunga sera na sheria; wafanyabiashara, wasomi na wanazuoni pamoja na viongozi wa dini kushirikiana na kushikamana, ili kuhakikisha kwamba, utu, heshima na haki msingi za binadamu zinalindwa na kudumishwa. Kwa njia hii, wataweza kugundua mapungufu yanayoweza kujitokeza na hivyo kuyafanyia kazi kwa kuangalia mambo msingi yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza. Maendeleo ya sayansi na teknolojia yalenge ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Uwajibikaji wa wote, kanuni maadili na utu wema; utawala wa sheria na haki ni mambo msingi katika kukuza matumizi halali ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii. Baba Mtakatifu Leo XIV anasistizia kuwa wajibu wa kuhakikisha matumizi ya kimaadili ya Teknolojia ya Akili Unde haupaswi kuwa wa wabunifu na waendeshaji wa mifumo pekee, bali hata watumiaji wanahusika. Matumizi ya Teknolojia ya Akili Unde yanahitaji mfumo madhubuti wa kimaadili na wa kisheria, unaotoa kipaumbele cha kwamba, kwa: utu, heshima na haki msingi za binadamu badala ya kulenga faida au ufanisi pekee.

Teknolojia ya Akile Unde isimamiwe na maadili, utu wema na haki msingi
Teknolojia ya Akile Unde isimamiwe na maadili, utu wema na haki msingi   (REUTERS)

Ni katika muktadha huu, Shirikisho la Vyombo Vya Habari vya Kikatoliki Nchini Ufaransa “Fédération des Médias Catholiques de France” kuanzia tarehe 21 hadi 23 Januari 2026 vinafanya mkutano wake mkuu wa 29 huko Lourdes, nchini Ufaransa, ili kusoma alama za nyakati, tayari kuangalia fursa zilizopo sanjari na kujibu changamoto zinazoendelea kuibuliwa katika tasnia ya mawasiliano ya jamii. Hii ikiwa ni pamoja na maendeleo makubwa ya matumizi ya Teknolojia ya Akili Unde, ili kukuza na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kijamii, bila ya kumtenga mtu awaye yote. Hii ni huduma inayoweza kutolewa na vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki, kwa wote hata na kwa wale wasioamini. Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa washiriki wa Mkutano mkuu wa 29 wa Shirikisho la Vyombo Vya Habari vya Kikatoliki Nchini Ufaransa “Fédération des Médias Catholiques de France.”  Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe huu, anawahimiza wadau katika tasnia ya mawasiliano ya jamii kupanda maneno mazuri, kukuza na kudumisha sauti zinazotafuta kwa ujasiri: haki, amani na upatanisho. Katika ulimwengu uliogawanyika na kumeguka kuna umuhimu wa uwepo wa antena zinazokamata na kusambaza uzoefu wa wanyonge, waliotengwa, wale walio peke yao na wanaohitaji kutambua furaha ya kujisikia kupendwa.

Utu, Heshima na Haki msingi ni mambo yanayo paswa kupewa kipaumbele
Utu, Heshima na Haki msingi ni mambo yanayo paswa kupewa kipaumbele

Padre Jacques Hamel ni mfano bora wa kuigwa kwani ni kiongozi na zawadi kubwa kwa wanatasnia ya mawasiliano ya jamii, wanaoendelea kujisadaka ili kukuza, haki, amani na majadiliano ya kidini. Padre Hamel alikuwa ni shuhuda wa imani, hata kifo. Siku zote aliamini katika umuhimu wa majadiliano; utamaduni wa kusikilizana kwa subira pamoja na kuheshimiana; sanjari na kujenga ujirani mwema, bila kuathiriwa na tofauti zao msingi zinazoweza kuwatumbukiza katika ubaguzi. Mfano wake bora wa maisha, uwatie shime wanatasnia ya mawasiliano ya jamii kutafuta ukweli katika upendo, wawe ni madaraja ya kuunganisha kile kilicho vunjika; tayari kuganga na kutibu madonda na majeraha ya mwanadamu. Mwishoni mwa ujumbe wake, Baba Mtakatifu Leo XIV amewaweka wanatasnia wa mawasiliano ya kijamii kutoka nchini Ufaransa chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria pamoja na maombezi ya Mtakatifu Francisko wa Sale, na hatimaye, akawapatia baraka zake za kitume. Mama Kanisa tarehe 28 Desemba 2022 alizindua Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 400 tangu Mtakatifu Francisko wa Sales, Askofu, Mwalimu wa Kanisa na Msimamizi wa Waandishi wa Habari alipofariki dunia. Yeye alizaliwa tarehe 21 Agosti 1567, huko Sales; Thorens-Glières, Ufaransa, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 18 Desemba 1593, na Desemba 1602 akawekwa wakfu kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Geneva, Uswis na hatimaye kufariki dunia tarehe 28 Desemba 1622 huko Lyon. Papa Alexander VII akamtangaza kuwa Mwenyeheri 8 Januari 1662 na hatimaye Mtakatifu tarehe 19 Aprili 1665. Papa Leo wa XIII kunako mwaka 1887 akamtangaza kuwa ni Mwalimu wa Kanisa.

Papa Leo XIV Mawasiliano
22 Januari 2026, 15:41