Tafuta

Mfuko wa “Centesimus Annus Pro Pontefice” kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro, CAPP, ulianzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II, tarehe 5 Juni 1993. Mfuko wa “Centesimus Annus Pro Pontefice” kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro, CAPP, ulianzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II, tarehe 5 Juni 1993.   (@Vatican Media)

Papa Leo XIV: Umuhimu wa Mafundisho Jamii Ya Kanisa Katika Kudumisha Haki Na Amani

Mfuko wa “Centesimus Annus Pro Pontefice” kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro, tarehe 23 Januari 2026, ulifanya mkutano wake huko mjini Luxembourg na kauli mbiu: “Ujenzi wa Amani Barani Ulaya: Ni Wajibu Gani wa Mafundisho Jamii ya Kanisa Katoliki na Maadili ya Kiulimwengu? Papa Leo XIV anakazia: Mchango muhimu unaotolewa na dini mbalimbali duniani kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi: Umuhimu wa Mafundisho Jamii ya Kanisa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mafundisho Jamii ya Kanisa yanapata chimbuko lake mintarafu kanuni na muundo wa elimu fahamu, taalimungu, hususan taalimungu maadili ambayo ni dira na mwongozo wa maisha ya watu. Yanachota amana na utajiri wake kutoka katika Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa na imani thabiti ambayo inamwilisha Neno la Mungu katika matendo, kielelezo cha imani tendaji. Mambo msingi katika mchakato wa kudumisha haki msingi za binadamu: Amani katika ukweli, haki, upendo na uhuru. Hizi ni tunu ambazo ni urithi mkubwa kwa binadamu wote kwani zinabubujika kutoka katika asili ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu hivyo zinapaswa kulindwa, kutetewa na kuheshimiwa na wote; kwa kuzingatia kwamba, haki inakwenda sanjari na wajibu; hakuna haki pasi na wajibu. Hii ni haki ya kuishi, kupata huduma bora ya makazi, afya, elimu, kuabudu, uhuru wa dhamiri, uhuru wa kuchagua mfumo wa maisha; haki za kiuchumi na kisiasa pamoja na uhuru wa kwenda unakotaka kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo. Kanisa Katoliki lina amana na utajiri mkubwa wa Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayopata chimbuko lake katika Waraka wa Kichungaji wa Baba Mtakatifu Leo XIII; Mambo Mapya; “Rerum Novarum.” Alisema, kazi ni utimilifu wa utu na heshima ya binadamu, ina thamani na heshima yake ya asili. Aligusia haki msingi za wafanyakazi, mshahara na wajibu wa wafanyakazi; Umiliki wa binafsi wa mali; wajibu wa Serikali, sanjari na kuwalinda wanyonge ndani ya jamii; Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Mafundisho Jamii ya Kanisa ni muhimu katika kudumisha haki na amani
Mafundisho Jamii ya Kanisa ni muhimu katika kudumisha haki na amani   (AFP or licensors)

Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, katika Waraka wake kuhusu Masuala ya Kijamii “Centesimus Annus” alifafanua kwa kina kuhusu asili ya haki msingi za binadamu; umuhimu wa kukuza na kudumisha upendo na mshikamano miongoni mwa Jumuiya ya Kimataifa, kama inavyojidhihirisha katika Waraka wake wa “Sollicitudo Rei Socialis” cheche ya uanzishaji wa vyama vya kitume kijamii vilivyokuwa vinapania kulinda na kutetea uhuru, utu na haki msingi za binadamu.Itakumbukwa kwamba, uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu ni muhtasari wa haki zote za binadamu. Dini zisaidie kujenga amani, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu na kamwe zisiwe ni chanzo cha vurugu, kinzani na vita. Kanuni maadili na utu wema ni sehemu muhimu sana katika maisha ya mwanadamu zinazopaswa kuheshimiwa ili amani na utulivu viweze kushika kasi, bila kusahau nafasi na dhamana ya uwepo wa Mungu katika maisha ya mwanadamu. Waamini wanapaswa kufahamu vyema kweli za imani yao ili wasiyumbishwe, bali wasimame kidete kuilinda na kuitetea kwa ajili ya ustawi, mafao ya maendeleo ya wengi. Baba Mtakatifu Leo XIV ambaye anaongozwa na kauli mbiu yake ya Kiaskofu “In Illo unum uno” Yaani “Ingawa sisi Wakristo ni wengi, katika Kristo mmoja sisi ni wamoja.” Huu ni ufafanuzi uliotolewa na Mtakatifu Augustino mintarafu Zaburi ya 127.

Papa Leo XIV akizungumza na viongozi kutoka Luxembourg
Papa Leo XIV akizungumza na viongozi kutoka Luxembourg   (ANSA)

Katika salam zake kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, “Urbi et Orbi”, Alhamisi tarehe 8 Mei 2025 alikazia pamoja na mambo mengine: Umuhimu wa ujenzi wa amani inayobubujika kutoka kwa Kristo Mfufuka; Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na upendo kwa waja wake wote na kwamba, kamwe ubaya hauwezi kushinda. Kuna haja ya kuwa vyombo na wajenzi wa haki na amani; waaminifu kwa Kristo Yesu, tayari kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo, huku wakijitahidi kuwa ni wamisionari. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kati ya waamini yeye ni Mkristo na kwao yeye ni Askofu. Hii ni changamoto kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanajenga Kanisa la: Kisinodi na kimisionari, kwa kujikita katika Injili ya upendo hasa kwa maskini na wahitaji sanjari na majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni, ili kujenga madaraja ya kuwakutanisha watu.Mfuko wa “Centesimus Annus Pro Pontefice” kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro, CAPP, ulianzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II, tarehe 5 Juni 1993. Hii ni kumbukumbu endelevu tangu Papa Leo XIII alipochapisha Waraka wake wa Kitume “Rerum Novarum” yaani “Mambo Mapya” msingi wa Mafundisho Jamii ya Kanisa. Lengo la mfuko huu ni kufanya upembuzi yakinifu, kufafanua na kumwilisha Mafundisho Jamii ya Kanisa katika uhalisia wa maisha ya watu, kwa kuwasaidia: wafanyabiashara na wataalam katika medani mbalimbali za maisha; kufahamu shughuli zinazotekelezwa na Vatican katika kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mfuko huu umeendelea kuwa nyenzo muhimu sana ya ushuhuda wa uwepo fungamani wa Kanisa katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu. Mfuko unawajumuisha viongozi wa Kanisa Katoliki, wasomi na wataalamu kutoka katika nyanja mbalimbali.

Papa Leo XIV akizungumza na baadhi ya wajumbe wa CAPP.
Papa Leo XIV akizungumza na baadhi ya wajumbe wa CAPP.   (ANSA)

Mfuko wa “Centesimus Annus Pro Pontefice” kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro, CAPP, Ijumaa tarehe 23 Januari 2026, ulifanya mkutano wake huko mjini Luxembourg kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Ujenzi wa Amani Barani Ulaya: Ni Wajibu Gani wa Mafundisho Jamii ya Kanisa Katoliki na Maadili ya Kiulimwengu? Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa washiriki wa mkutano huu anakazia: Mchango muhimu unaotolewa na dini mbalimbali duniani kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Shida kubwa inayojitokeza ni kwa baadhi ya watu kutaka kuufanya ukweli kuwa ni mawazo binafsi. Haki na amani vinaweza kustawi katika jamii inayozingatia na kuheshimu ukweli pamoja na tunu msingi za kimaadili na utu wema, kwa kutambua kwamba, mwanadamu ameumbwa kw asura na mfano wa Mungu. Mtakatifu Yohane Paulo II anakaza kusema, hakuna maendeleo ya kweli bila kuheshimu na kuzingatia na kumwilisha msingi wa ukweli katika uhalisia wa maisha. Baba Mtakatifu Leo XIV anakaza kusema, Mafundisho Jamii ya Kanisa yanachota amana na utajiri wake kutoka kwa Kristo Yesu ambaye anasema: “Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.” Yn 14:6. Mafundisho Jamii ya Kanisa ni msingi unaowezesha haki, amani na maridhiano kuweza kutawala kati ya Jumuiya ya watu wa Mataifa. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Leo XIV kwa Bara la Ulaya litaendelea kuzamisha mizizi yake katika tunu msingi za maisha ya Kikristo na kwamba, Kanisa litaendelea kuchangia tunu msingi ili kweli Bara la Ulaya liweze kusimikwa katika msingi wa haki.

Mafunndisho Jamii ya Kanisa

 

24 Januari 2026, 17:03