Papa Leo XIV:Tuombee amani Ukraine na sehemu zenye migogoro
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Mara baada ya Tafakari na Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 25 Januari 2026, Baba Mtakatifu Leo XIV aligeukia umati wa mahujaji na waamini waliokuwa chini ya anga la Blu na mawingu meupe kwa neema ya Mungu baada ya mvua katika Uwanja wa Mtakatifu Petro na kusema: “Dominika hii, ya tatu ya Kipindi cha Kawaida, ni Dominika ya Neno la Mungu. Papa Francisko aliianzisha miaka saba iliyopita ili kuhamasisha maarifa ya Maandiko Matakatifu katika Kanisa na kuzingatia Neno la Mungu, katika liturujia na katika maisha ya jumuiya. Ninawashukuru na kuwatia moyo wote wanaojitolea kwa imani na upendo kwa lengo hili kuu.”
Ukraine: “kuongeza juhudi za kukomesha vita”
Papa Leo XIV aliendelea kusema kuwa “Hata siku hizi, Ukraine inakumbwa na mashambulizi yanayoendelea, na kuacha idadi nzima ya watu wakiwa wazi kwa baridi kali. Ninafuatilia kinachoendelea kwa huzuni, na niko karibu na kuwaombea wale wanaoteseka. Mwendelezo wa uhasama, wenye matokeo mabaya zaidi kwa raia, unapanua mpasuko kati ya watu na kuweka mbali amani ya haki na ya kudumu. Ninawaomba kila mtu kuongeza juhudi za kukomesha vita hivi.
Siku ya Ukoma duniani
Leo ni Siku ya Ukoma Duniani. Ninaelezea ukaribu wangu na wote walioathiriwa na ugonjwa huu. Ninawtia moyo Chama cha Marafiki wa Italia cha Raoul Follereau na wote wanaowajali wenye ukoma, wakijitolee kulinda heshima yao.
Mahujaji kutoka sehemu mbalimbali
Ninawakaribisha nyote, waamini wa Roma na mahujaji kutoka nchi mbalimbali!, hasa, ninawasalimu kwaya ya Parokia ya Rakovski nchini Bulgaria, kundi la Quinceañeras ya Panama, wanafunzi wa Taasisi ya Zurbarán ya Badajoz, Hispania; pamoja na wanakipaimara wa Parokia ya Marko Marco Vecchio huko lirenze, Jumuiya ya shule ya Taasisi ya Erodoto ya Corigliano-Rossano, na chama cha kujitolea cha "Cuori Aperti" cha Lecce.
Salamu kwa Chama cha matendo ya vijana Katoliki Italia
Ninawasalimu vijana wa Chama cha Matendo Kikatoliki wa Roma, pamoja na wazazi wao, walimu, na mapadre, ambao wamekuwa kwenye Msafara hai wa Amani . “Wapendwa watoto na vijana, ninawashukuru kwa kutusaidia sisi watu wazima kuona ulimwengu kutokana na mtazamo tofauti: ule wa ushirikiano kati ya watu na watu tofauti. Asante! Muwe wapatanishi nyumbani, shuleni, katika michezo, kila mahali. Msiwe wajeuri kamwe, si kwa maneno wala vitendo. Kamwe! Uovu hushindwa tu kwa wema. Pamoja na vijana hawa, tuombe amani: huko Ukraine, Mashariki ya Kati, na katika kila eneo ambapo, kwa bahati mbaya, mapigano hufanyika kwa maslahi mengine isipokuwa yale ya watu. Amani hujengwa kupitia heshima kwa watu!
Hitimisho la Juma la Kuombea Umoja wa Kikristo
Papa Leo XIV alihitimisha kwa muktadha wa Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo: “ Mchana, kama ilivyo desturi, nitasali Masifu ya Jioni katika Basilika ya Mtakatifu Paulo Nje ya Ukuta pamoja na wawakilishi wa madhehebu mengine ya Kikristo.” Papa aliongeza “ Ninawashukuru wote watakaoshiriki, ikiwa ni pamoja na wale wanaoshiriki kupitia vyombo vya habari, na ninawatakia nyote Dominika njema.”
