Papa Leo XIV,Ujumbe wa Siku ya Kimisionari 2026:Mmoja katika Kristo,ameungana katika utume
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV amechapisha jumbe wa Siku ya 100 ya Kisimisionari Ulimwenguni 2026, tarehe 26 Januari, katika Dominika ya Tatu ya Kipindi cha Kawaida cha mwaka na sanjari na, Siku kuu ya Uongofu wa Mtakatifu Paulo. Katika Ujumbe huo, Papa anabainisha kuwa, "Katika Siku ya Umisionari Ulimwenguni 2026, ambayo inaadhimisha miaka mia moja ya maadhimisho, iliyoanzishwa na Pio XI ambayo ni ya thamani sana kwa Kanisa, nimechagua mada: "Mmoja katika Kristo, ameungana katika utume." Akiendelea anabainisha kuwa kufuatia Mwaka wa Jubilei, ningependa kuhimiza Kanisa lote kuendelea na safari yake ya umisionari kwa furaha na bidii katika Roho Mtakatifu. Hii inahitaji mioyo iliyoungana katika Kristo, jumuiya zilizopatanishwa na, kwa kila mtu, nia ya kushirikiana kwa ukarimu na uaminifu. Tunapotafakari kuwa wamoja katika Kristo na umoja katika utume, hebu tujiruhusu kuongozwa na kuhuishwa na neema ya Mungu, "kupyaishwa ndani yetu moto wa wito wetu wa umisionari" na kusonga mbele pamoja katika kujitolea kwa uinjilishaji, katika "enzi hii mpya ya umisionari" katika historia ya Kanisa (Mahubiri ya Jubilei ya Ulimwengu wa Umisionari na ya Wahamiaji, 5 Oktoba 2025). Baba Mtakatifu Leo ameganywa Ujumbe huu katika vifungu vitatu:
Mmoja katika Kristo – Wanafunzi wa kimisionari wameungana ndani yake na pamoja na kaka na dada zetu
Fumbo la muungano na Kristo liko katikati ya utume. Kabla ya mateso yake, Yesu alimwomba Baba, “ili wote wawe wamoja. Kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami nilivyo ndani yako, hao nao wawe ndani yetu” (Yh 17:21). Maneno haya yanaonesha hamu kubwa ya Yesu, pamoja na utambulisho wa Kanisa kama Jumuiya ya wanafunzi wake. Huo ni, ushirika unaotokana na Utatu, na unaendelea kudumishwa na Utatu. Ushirika katika huduma ya udugu kati ya wanadamu wote na maelewano na viumbe vyote. Kuwa Mkristo hasa, si kuhusu mazoea au mawazo; ni maisha katika muungano na Kristo, ambapo tunashiriki uhusiano wake wa kifamilia na Baba katika Roho Mtakatifu. Inamaanisha kukaa ndani ya Kristo, kama matawi kwenye mzabibu (taz. Yh 15:4), tukizama katika maisha ya Utatu. Muungano huu hutoa muungano wa pamoja miongoni mwa waamini na ndiyo chanzo cha matunda yote ya kimisionari. Hakika, kama vile Mtakatifu Yohane Paulo II alivyofundisha, "ushirika unawakilisha chanzo na tunda la utume" (Wosia wa Kitume Christifideles Laici, 32). Katika muktadha huo, jukumu kuu la umisionari la Kanisa ni kufufua na kudumisha umoja wa kiroho na kidugu miongoni mwa washiriki wake. Katika hali nyingi, tunakumbana na migogoro, mgawanyiko, kutoelewana na ukosefu wa uaminifu wa pamoja. Hili linapotokea hata ndani ya jumuiya zetu, linadhoofisha ushuhuda wetu. Utume wa uinjilishaji ambao Kristo aliwakabidhi wanafunzi wake unahitaji, zaidi ya yote, mioyo iliyopatanishwa na yenye hamu ya ushirika.
Kwa hivyo, ni muhimu kuongeza juhudi za kiekumeni na Makanisa yote ya Kikristo, tukijenga juu ya fursa zinazotokana na sherehe ya pamoja ya maadhimisho ya miaka 1700 ya Mtaguso wa Nicaea. Mwisho kabisa, kuwa "mmoja katika Kristo" tunaitwa tumkazie macho Bwana, ili aweze kuwa kitovu cha maisha yetu na jumuiya zetu, kitovu cha kila neno, kitendo na uhusiano wa kibinadamu, na kutuongoza kusema kwa mshangao: "Si mimi tena ninayeishi, bali ni Kristo anayeishi ndani yangu"(Gal 2:20). Kwa kusikiliza neno lake kila mara na kupata neema ya Sakramenti, itawezekana kwetu kuwa mawe yaliyo hai katika Kanisa. Leo hii, Kanisa limeitwa kuchukua mada za msingi za Mtaguso wa Pili wa Vatican na Majisterio ya Papa yaliyofuata, hasa yale ya Papa Francisko. Kiukweli, kama Mtakatifu Paulo asemavyo, "hatujitangazi wenyewe; tunamtangaza Yesu Kristo kuwa Bwana"(2 Kor 4:5). Kwa sababu hiyo, ninarudia maneno ya Mtakatifu Paulo VI: “Hakuna uinjilishaji wa kweli ikiwa jina, mafundisho, uzima, ahadi, ufalme na fumbo la Yesu wa Nazareti, Mwana wa Mungu, havitatangazwa” (Wosi awa Kitume Evangelii Nuntiandi, 22). Mchakato huu wa uinjilishaji wa kweli huanza katika moyo wa kila Mkristo ili kuwafikia wanadamu wote. Kwa hivyo, kadiri tunavyoungana zaidi katika Kristo, ndivyo tutakavyoweza zaidi kutekeleza pamoja utume aliotukabidhi.
Umoja katika utume: Ili ulimwengu uweze kumwamini Kristo Bwana
Umoja wa wanafunzi siyo mwisho wenyewe; bali unaelekezwa kwenye utume. Yesu anasema hili waziwazi: “Ili ulimwengu upate kusadiki kwamba Wewe ndiye uliyenituma” (Yh 17:21). Ni kupitia ushuhuda wa jumuiya iliyopatanishwa, ya kidugu na iliyoungana ndipo kutangaza Injili kunapata nguvu yake kamili ya mawasiliano. Kwa mtazamo huo, inafaa kukumbuka kauli mbiu ya Mwenyeheri Paolo Manna, “Makanisa Yote Yameungana kwa ajili ya uongofu wa ulimwengu wote,” ambayo kwa ufupi inaonesha wazo lililochochea kuanzishwa kwa Umoja wa Kimisionari wa Kipapa mwaka 1916. Katika maadhimisho ya miaka 110, ninatoa shukrani zangu na baraka zangu kwa kujitolea kwake kuhamasisha na kuunda roho ya umisionari ya mapadre, watu waliowekwa wakfu na waamini walei, wakiendeleza umoja wa juhudi zote za uinjilishaji. Kiukweli, hakuna mtu aliyebatizwa ambaye ni mgeni au kutojali utume: kila mtu, kila mmoja kulingana na wito wake na hali yake ya maisha, anashiriki katika kazi kubwa ambayo Kristo ameikabidhi Kanisa lake. Kama Papa Francisko alivyotukumbusha mara kwa mara, kutangaza Injili ni kitendo ambacho kila wakati huwa na upatanisho, cha kijumuiya na cha kisinodi.
Kwa sababu hiyo, umoja katika utume unamaanisha kulinda na kukuza hali ya kiroho ya ushirika na ushirikiano wa kimisionari. Kwa kukuza mtazamo huu kila siku, neema ya Mungu hutufundisha polepole kuwaona kaka na dada zetu kupitia mitazamo ya imani. Pia tunajifunza kutambua kwa furaha mema ambayo Roho huvuvia ndani ya kila mtu, kukumbatia utofauti kama hazina, kubeba mizigo ya kila mmoja na kutafuta kila wakati umoja unaotoka juu. Hakika, sote tunashiriki utume mmoja katika "Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja, Mungu mmoja na Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote" (Efe 4:5-6). Kiroho, hiki kinaunda usemi wa kila siku wa wanafunzi wa kimisionari. Hutusaidia kurejesha maono ya Ulimwengu mzima ya utume wa Kanisa wa kuinjilisha, na kushinda ukosefu wa juhudi zilizoratibiwa na kuundwa kwa vikundi miongoni mwa wafuasi wa Bwana mmoja - kama vile "Mimi ni wa Paulo," "Mimi ni wa Apolo" (taz. 1 Kor 1:10-12).
Bila shaka, umoja wa kimisionari haupaswi kueleweka kama umoja tu, bali kama muunganiko wa karama tofauti kwa kusudi moja, yaani kufanya upendo wa Kristo uonekane na kuwaalika kila mtu kukutana naye. Uinjilishaji unapatikana wakati jumuiya mahalia zinaposhirikiana na wakati tofauti za kiutamaduni, kiroho na kiliturujia zinaoneshwa kikamilifu na kwa usawa katika imani moja. Kwa hivyo ninahimiza taasisi zote katika Kanisa kuimarisha hisia zao za ushirika wa kikanisa wa kimisionari na kukuza njia bunifu na thabiti za kushirikiana kwa ajili na katika utume. Katika suala hili, ningependa kushukuru Vyama vya Kipapa vya Utume kwa huduma yao kwa ushirikiano wa kimisionari, ambayo nilifanya uzoefu kwa shukrani wakati wa huduma yangu huko Peru. Vyama hivi kama vile vya Uenezaji wa Imani, Utoto Mtakatifu, Mtakatifu Petro Mtume na Umoja wa Kipapa wa Kimisionari, vinaendelea kukuza na kuunda ufahamu wa kimisionari kwa waamini wa rika zote, na kukuza mtandao wa sala na upendo unaounganisha jamii ulimwenguni kote.
Hapa, inafaa kuzingatia kwamba mwanzilishi wa Jumuiya ya Uenezaji wa Imani, Mwenyeheri Pauline Marie Jaricot, alianzisha Rozari Hai miaka mia mbili iliyopita. Hata leo hii inaendelea kuwaleta pamoja waamini wengi ulimwenguni kote ili kuombea kila hitaji la kiroho na kimisionari. Pia inafaa kukumbuka kwamba, kufuatia pendekezo kutoka Jumuiya ya Uenezaji wa Imani, Papa Pio XI alianzisha Siku ya Kimisionari Ulimwenguni mnamo 1926. Sadaka za kila mwaka zinazokusanywa siku hiyo zinasambazwa na Jumuiya, kwa niaba ya Papa, ili kusaidia mahitaji mbalimbali ya utume wa Kanisa. Kwa hivyo, Jumuiya nne, kwa ujumla na kila moja katika upekee wake, bado zina jukumu muhimu kwa Kanisa lote. Ni ishara hai ya umoja na ushirika wa kimisionari wa Kanisa. Ninawaalika kila mtu kufanya kazi nao kwa roho ya shukrani.
Utume wa kupenda: Kutangaza, kuishi na kushiriki upendo mwaminifu wa Mungu
Ikiwa umoja ndio sharti la utume, upendo ndio kiini chake. Habari Njema ambayo tumetumwa kuitangaza kwa ulimwengu si wazo la kufikirika; ni Injili ya upendo mwaminifu wa Mungu, ambao ulifanyika mwili katika uso na maisha ya Yesu Kristo. Utume wa wanafunzi na Kanisa kwa ujumla ni kuendeleza utume wa Kristo katika Roho Mtakatifu: utume uliozaliwa kwa upendo, ulioishi katika upendo, na unaoongoza kwenye upendo. Kiukweli, Bwana mwenyewe, katika sala yake kuu kwa Baba kabla ya mateso yake, baada ya kuomba umoja miongoni mwa wanafunzi wake, anahitimisha akisema: "ili upendo ulionipenda nao uwe ndani yao, nami ndani yao" (Yh 17:26). Wakisukumwa na upendo wa Kristo, Mitume walitoka kwenda kuinjilisha kwa ajili ya Kristo (taz. 2 Kor 5:14). Vile vile, katika karne nyingi, Wakristo wengi, mashahidi, watafakuri wa ndani na wamisionari, wamejitolea maisha yao ili kujulisha upendo huu wa kimungu kwa ulimwengu. Hivyo, wakiongozwa na Roho Mtakatifu, Roho wa upendo, utume wa Kanisa wa uinjilishaji utaendelea hadi mwisho wa wakati.
Ningependa kutoa shukrani zangu za kipekee kwa wamisionari wa ad gentes wa leo. Kama Mtakatifu Francis Xavier, wameacha nchi yao, familia zao na hisia zote za usalama ili kutangaza Injili na kumpeleka Kristo na upendo wake katika maeneo ambayo mara nyingi huwa na changamoto, maskini, yaliyojaa migogoro au mbali na utamaduni. Licha ya shida na mapungufu ya kibinadamu, wanaendelea kujitolea kwa furaha, kwa sababu wanajua kwamba Kristo mwenyewe, na Injili yake, ndiyo hazina kubwa zaidi tunayoweza kutoa. Kupitia uvumilivu wao, wanaonesha kwamba upendo wa Mungu unapita vizuizi vyote. Ulimwengu bado unahitaji mashuhuda hawa jasiri wa Kristo, na jumuiya za kikanisa bado zinahitaji miito mipya ya kimisionari. Tunapaswa kuwaweka karibu na mioyo yetu kila wakati na kuwaombea kwa Baba kila mara. Atupe zawadi ya vijana na watu wazima ambao wako tayari kuacha kila kitu nyuma ili kumfuata Kristo katika njia ya uinjilishaji hata miisho ya dunia!
Nikiwa nimejawa na pongezi kwa wamisionari wanaume na wanawake, ninatoa wito maalum kwa Kanisa lote ili kuungana nao katika utume wa Uinjilishaji, kupitia ushuhuda wa maisha yetu katika Kristo, kupitia sala na kupitia michango yetu kwa ajili ya utume. Kama Mtakatifu Francis wa Assisi alivyosema, "Upendo haujapendwa," na tunamtazama kwa njia ya pekee katika kumbukumbu ya miaka mia nane ya kurudi kwake mbinguni. Tupate msukumo katika hamu yake ya kuishi katika upendo wa Bwana na kuusambaza kwa wale walio karibu na walio mbali, kwa sababu, kama alivyosema, "upendo huu, Aliyetupenda sana ni wa kupendwa sana" (Mtakatifu Bonaventure wa Bagnoregio, Maisha ya Mtakatifu Francis, sura ya IX, 1; Fonti Francescane, 1161).
Pia tupate msukumo kutoka bidii ya Mtakatifu Thérèse wa Mtoto Yesu, ambaye alitangaza kwamba angeendelea na utume wake hata baada ya kifo: “Nitatamani mbinguni kitu kile kile ninachotamani duniani sasa: kumpenda Yesu na kumfanya apendwe” (Barua ya 220 kwa Abbé Bellière, 24 Februari 1897). Tukiongozwa na ushuhuda huu, sote tujitoe kuchangia utume mkuu wa uinjilishaji, ambao daima ni kazi ya upendo, kulingana na wito wetu wenyewe na zawadi tulizopokea. Maombi yenu na usaidizi wenu wa vitendo, hasa katika Siku ya Uinjilishaji Ulimwengune, yatakuwa msaada mkubwa katika kupeleka Injili ya upendo wa Mungu kwa kila mtu, hasa maskini na wale walio na uhitaji mkubwa. Kila zawadi, haijalishi ni ndogo kiasi gani, inakuwa kitendo chenye maana cha ushirika wa kimisionari. Ninarudisha shukrani zangu za dhati "kwa kila kitu mtakachofanya kunisaidia kuwasaidia wamisionari ulimwenguni kote" (Ujumbe wa Video wa Siku ya Kimisionari kwa mwaka 2025, tarehe 19 Oktoba 2025). Ili kukuza ushirika wa kiroho, ninawapatia baraka yangu kwa sala hii rahisi:
Baba Mtakatifu, utufanye tuwe wamoja katika Kristo, wenye mizizi katika upendo wake unaounganisha na kupyaishwa. Waamini wote wa Kanisa wawe wamoja katika utume, watiifu kwa Roho Mtakatifu, jasiri katika kutoa ushuhuda wa Injili, kutangaza na kudhihirisha upendo wako mwaminifu kila siku kwa viumbe vyote. Uwabariki wanaume na wanawake wote wa kimisionari, waunge mkono katika juhudi zao, na uwalinde kwa matumaini! Maria, Malkia wa Utume, usindikize kazi yetu ya uinjilishaji katika kila kona ya dunia: utufanye vyombo vya amani, na utujalie kwamba ulimwengu wote uweze kutambua katika Kristo nuru inayookoa. Amina.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku: Just click here
