Tafuta

Papa Leo XIV kwa SEEK26:Mkihisi Bwana anawaita,msiogope!

Papa Leo XIV alituma ujumbe wake kwa washiriki wa Mkutano SEEK26 ambao unafanyika kwa wakati mmoja huko Ohio,Texas na Colorado.Akihutubia vijana hao,aliwakumbusha kwamba"bidii ya umisionari huzaliwa kutokana na kukutana kweli na Kristo na kupata furaha ambayo huwezi kutoishirikisha.Hakuna hofu ikiwa Bwana anawaita kwa sababu katika Yeye mioyo hupata amani."

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Katika mpango ulioanza Alhamisi, tarehe 1 Januari 2026, na utakamilika Jumatatu tarehe 5 Januari 2026, ukifanyika kwa wakati mmoja huko Columbus, Ohio, Fort Worth, Texas, na Denver, Colorado. Baba Mtakatifu Leo XIV aliwatumia ujumbe kwa njia ya video. Ni katika tukio linalowakutanisha maelfu ya Wakatoliki na linaadhimishwa kwa nia ya sala, ibada, mikutano, na sherehe. Katika ujumbe huo kwa lugha ya kiingereza. Ufuatao ni ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV:

Ni furaha kwangu kuwasalimu nyote mnaohudhuria Mikutano ya SEEK26 inayofanyika Columbus, Denver, na Fort Worth. Mmekusanyika wakati wa Noeli, wakati baadhi ya masomo ya Injili kwa ajili ya Misa yanachukuliwa kutoka sura ya kwanza ya Injili ya Yohane. Kuelekea mwisho wa sura hii, tunaambiwa jambo fulani kuhusu wanafunzi wawili wa kwanza wa Yesu, mmoja wao akiwa Andrea. Walikuwa wanafunzi wa Yohana Mbatizaji, na Yohana alipomtaja Yesu kama Mwana-Kondoo wa Mungu, walianza kumfuata Yesu mara moja (Yh 1, 36). Yesu alipowaona, aligeuka na kutamka maneno ya kwanza yaliyoandikwa katika Injili ya Yohana: "Mnatafuta nini?"(Yh 1, 38). Yesu anawauliza wanafunzi swali hili kwa sababu anajua mioyo yao. Hawakuwa na utulivu, kwa njia nzuri. Hawakutaka kuridhika na utaratibu wa kawaida wa maisha. Walikuwa wazi kwa Mungu na walitamani kupata maana. Leo, Yesu anawauliza kila mmoja wenu swali lile lile. Wapendwa vijana, mnatafuta nini? Kwa nini mko hapa kwenye mkutano huu? Labda mioyo yenu haina utulivu, inatafuta maana na utimilifu, mwelekeo maishani.

Jibu linapatikana ndani ya mtu. Bwana Yesu pekee ndiye anayetuletea amani na furaha ya kweli na kutimiza kila moja ya matamanio yetu ya ndani kabisa. Wanafunzi wanajibu kwa kumuuliza anaishi wapi. Haikutosha kwa mtu mwingine kuwaambia kwamba Yesu alikuwa Mwana-Kondoo wa Mungu; walitaka kumjua yeye binafsi kwa kutumia muda pamoja naye. Wakati wa mkutano huu, ninyi pia mtapata fursa ya kutumia muda na Bwana. Kama Andrea labda kwa baadhi yenu hii inaweza kuwa mkutano wenu wa kwanza wa kweli na Kristo. Kwa wengine, mwisho wa juma hili, itakuwa fursa ya kuimarisha uhusiano wenu naye pamoja na uelewa wenu wa imani ya Kikatoliki. Kuweni wazi kwa kile ambacho Bwana amewaandalia! Wanafunzi hao wawili mwanzoni walikaa na Yesu kwa saa chache tu, lakini mkutano huo ulibadilisha maisha yao milele. Jambo la kwanza ambalo Andrea alifanya ni kwenda kumwambia ndugu yake Simoni, "Tumemwona Masiha" (Yh 1, 41); kwa maneno mengine, "Tumemwona yule tuliyemtafuta!"

Hili ndilo jibu tunaloweza kutoa sote mara tu tunapomjua Bwana. Kwa hivyo, kifungu hiki kinatuambia maana ya kuwa wamisionari. Baada ya kukutana na Yesu, Andrea hakuweza kujizuia kushirikisha na ndugu yake kile alichokipata. Hakika, bidii ya umisionari huzaliwa kutokana na kukutana na Kristo. Tunatamani kushirikisha na wengine kile tulichopokea, ili wao pia wajue utimilifu wa upendo na ukweli unaopatikana ndani Yake pekee. Ninaomba kwamba, mtapoondoka kwenye mkutano huo, nyote mtasukumwa na bidii hii hii ya umisionari kushirikishana na wale walio karibu nanyi furaha mliyopokea kutokana na kukutana na Bwana kweli.

Wapendwa vijana, mnapomkaribia Yesu katika mwisho wa juma hili, kupitia urafiki, sakramenti, na Ibada ya Ekaristi, msiogope kumuomba anawaitia  nini. Baadhi yenu, kama Andrea na Simoni Petro, mnaweza kuitwa kwenye ukuhani, kuwatumikia watu wa Mungu kupitia ibada za sakramenti, kupitia kuhubiri Neno la Mungu, kutembea na watu wa Mungu. Wengine wanaweza kuitwa kwenye maisha ya kitawa, kujitoa kikamilifu kwa Mungu; wengine wanaweza kuitwa kwenye ndoa na maisha ya familia. Mkihisi Bwana anawaita, msiogope. Kwa mara nyingine tena, acheni nisisitize kwamba ni Yeye tu anayejua matamanio ya ndani kabisa, labda yaliyofichwa, ya moyo weni na njia itakayowaongoza kwenye utimilifu wa kweli.

Mwachie awaongoze na kuwasindikiza! Mkutano huu unapoanza na Sherehe ya Maria Mtakatifu, Mama wa Mungu, tumwombe atuongoze kwa Yesu Kristo, Mwanawe, ili tuweze kumjua kweli, tujue upendo wake kwetu na mpango mzuri alio nao kwa kila mmoja wetu. Kwa njia hyo, mioyo yetu itapata amani kweli katika Yule tunayemtafuta. Kwa kuwapatia kila mmoja wenu, na  kwa maombezi ya Mama Yetu, ninawaombea ninyi kwa hiari  na familia zenu Baraka za kimungu ya kipindi hiki cha Noeli  na Mungu Mwenyezi awabariki nyote, Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu. Amina."

02 Januari 2026, 10:28