Papa Leo XIV Kukutana na Makleri Na Kuanza Kutembelea Parokia za Roma
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mama Kanisa anasema, Kipindi cha Kwaresima ni fursa ya kuamsha na kupyaisha ari na mwamko wa kimisionari na shughuli za kichungaji tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Huu ni mwaliko wa kuwakumbuka na kuwaombea wainjilishaji wote, ili waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa kile wanacho amini, kufundisha na kuadhimisha. Iwe ni fursa ya kugundua na kutambua kwamba, wao kama waamini ni Mitume wa Yesu, changamoto na mwaliko wa kutafuta na kuambata mapenzi ya Mungu katika maisha. Kwaresima ni kipindi cha kuimarisha na kuboresha imani, matumaini na mapendo kwa: kufunga na kusali; kwa kufanya toba na malipizi ya dhambi; kwa kushiriki kikamilifu katika Sakramenti za Kanisa; Kwa kusoma, kutafakari na hatimaye, kumwilisha Neno la Mungu katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo makini cha imani tendaji. Lengo ni kujitakasa na kuambata utakatifu wa maisha, ili hatimaye, kushiriki furaha ya Kristo Mfufuka wakati wa Sherehe ya Pasaka ya Bwana, huku wakiwa wamepyaishwa kwa neema ya Roho Mtakatifu.
Waamini watambue kwamba wanaitwa kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao kwa watu wanaowazunguka na wale wote ambao Mwenyezi Mungu anawajalia fursa ya kukutana nao katika hija ya maisha yao, ili waweze kujaliwa mwanga na furaha ya Injili katika maisha yao. Mateso na kifo cha Kristo Msalabani, kiwe ni kikolezo cha toba na wongofu wa ndani kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa anayesema: “Lakini sikujulikana uso wangu na makanisa ya Uyahudi yaliyokuwa katika Kristo; ila wamesikia tu ya kwamba huyo aliyetuudhi hapo kwanza, sasa anaihubiri imani ile aliyoiharibu zamani. Wakamtukuza Mungu kwa ajili yangu.” Gal 1: 22-24. Waamini wajitahidi kuwa na kumbukumbu hai ya kukutana na Kristo Yesu katika maisha na utume wao. Ni wakati wa kuuvua utu wa kale na kuanza kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka.
Kipindi cha Kwaresima kinasimikwa katika nguzo kuu nne: yaani; Sala, Kufunga, Neno la Mungu na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo cha imani tendaji. Kipindi hiki cha Kwaresima ni mwaliko wa kupanda juu Mlimani Tabor ili kupata mang’amuzi ya maisha ya kiroho na kiutu, ili hatimaye kuweza kuzama zaidi katika Fumbo la maisha ya Kristo Yesu kama utimilifu wa Sheria na Unabii. Ni mwaliko wa kumsikiliza Kristo Yesu kwa umakini mkubwa kama mtindo wa maisha ya Kanisa la Kisinodi na Kimisionari. Waamini wapambane na changamoto za maisha na utume wao kwa ari, ujasiri na moyo mkuu, ili kwamba, Fumbo la Msalaba liwasaidie kukuza imani, matumaini na mapendo, ili hatimaye, waweze kuwa ni mashuhuda na wajenzi wa Kanisa la Kimisionari na la Kisinodi.
Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2026, Baba Mtakatifu Leo XIV, Alhamisi tarehe 19 Februari 2026 atakutana na kuzungumza na Makleri wa Jimbo kuu la Roma kwenye Ukumbi wa Paulo VI kuanzia saa 4:00 kwa Saa za Ulaya sawa na Saa 6:00 kwa Saa za Afrika Mashariki na Kati. Kwa mara ya kwanza katika maisha na utume wake kama Kahlifa wa Mtakatifu Petro na Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma, Baba Mtakatifu Leo XIV ataanza kutembelea Parokia tano za Jimbo Kuu la Roma kama ifuatavyo: Parokia ya Bikira Maria Malkia wa Amani huko Ostia Lido, Kusini mwa Roma, itakuwa ni tarehe 14 Februari 2026; Parokia ya Moyo Mtakatifu wa Yesu huko Castro Petrorio, iliyoko kati kati ya mji wa Roma ni hapo tarehe 22 Februari 2026. Parokia ya Kupaa Bwana Mbinguni, iliyoko Mashariki mwa mji wa Roma, itatembelewa na Baba Mtakatifu Leo XIV tarehe Mosi, Mwezi Machi 2026. Parokia ya Bikira Maria Kutolewa Hekaluni ni hapo tarehe 8 Machi 2026 na hatimaye, Parokia ya Moyo Mtakatifu wa Kristo Yesu huko “Ponte Mammolo, Kaskazini mwa Jimbo kuu la Roma ni hapo tarehe 15 Machi 2026.
Kardinali Baldassare Reina, maarufu kama “Baldo”, Makamu Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma anasema, katika hija hizi za kichungaji za Baba Mtakatifu Leo XIV Jimbo kuu la Roma ni nafasi kwa Baba Mtakatifu kukutana na kuzungumza na viongozi wa Kanisa, Vyama vya Kitume, Wahamasishaji wa shughuli za kichungaji pamoja na utume wa vijana wa kizazi kipya huko Parokiani. Hija hizi za kitume Jimbo kuu la Roma ni mwendelezo wa utamaduni na Mapokeo ya watangulizi wake, chemchemi ya furaha, imani na matumaini kwa watu wa Mungu Jimbo kuu la Roma. Ni nafasi muafaka kwa Baba Mtakatifu Leo XIV kufafanua na kuhimiza sera na mpango mkakati wa shughuli za kichungaji Jimbo kuu la Roma.
