Tafuta

Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo linalonogeshwa na kauli mbiu: “Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu.” Efe 4:4. Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo linalonogeshwa na kauli mbiu: “Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu.” Efe 4:4.  

Papa Leo XIV: Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo: Haki Na Amani

Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo linalonogeshwa na kauli mbiu: “Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu.” Efe 4:4. Tafakari ya Mwaka 2026 imeandaliwa na Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo pamoja na Kanisa la Kitume la Armenia linaloendelea kujitambulisha kuwa ni nguzo ya imani, umoja na mwendelezo wa Mapokeo ya Kikristo. Wakristo pia wanapaswa kujibidiisha kutafuta haki na amani duniani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo lilianza kunako mwaka 1908 kama Oktava ya Umoja wa Kikristo, na ililenga katika maombi kwa ajili ya umoja wa kanisa. Tarehe za Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo zilipendekezwa na Padre Paul Wattson, mwanzilishi mwenza wa “Graymoor Franciscan Friars.” Takribani miaka mia moja iliyopita, Papa Leo XIII (1810-1910) katika maisha na utume wake kama Askofu wa 256 wa Roma, alipenda kuwahimiza Wakristo kujibidiisha kusali kwa ajili ya kuombea Umoja wa Wakristo. Baba Mtakatifu Leo XIV mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, Dominika tarehe 18 Januari 2026 amesema Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo linalonogeshwa na kauli mbiu: “Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu.” Efe 4:4. Tafakari ya Mwaka 2026 imeandaliwa na Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo pamoja na Kanisa la Kitume la Armenia linaloendelea kujitambulisha kuwa ni nguzo ya imani, umoja na mwendelezo wa Mapokeo ya Kikristo. Baba Mtakatifu Leo XIV anawahamasisha waamini wa Kanisa Katoliki kujibidiisha kusali kwa ajili ya kuombea Umoja wa Wakristo, ili umoja kamili na unaoonekana wa Wakristo wote uweze kupatikana. Hii ni dhamana na wajibu unaopaswa kujikita katika kutafuta na kudumisha haki na amani, sehemu mbalimbali za dunia.

Jubilei ya Miaka 1700 ya Mtaguso wa NICEA
Jubilei ya Miaka 1700 ya Mtaguso wa NICEA   (ANSA)

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, utengano kati ya Wakristo hupingana wazi na mapenzi ya Kristo Yesu na ni kikwazo kwa ulimwengu na hudhuru tendo takatifu la kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Mtakatifu Yohane Paulo II alitaka kuona kwamba, Kanisa Katoliki linaendeleza majadiliano ya kiekumene na Wakristo wa Makanisa na Madhehebu mbalimbali, ili siku moja wote wawe wamoja chini ya Kristo Yesu, Mchungaji mkuu. Mama Kanisa anaendelea kukazia: Uekumene wa: damu, maisha ya kiroho, sala na huduma, kwani uekumene wa damu na ule wa utakatifu wa maisha ni mambo msingi yanayoshuhudiwa na Wakristo sehemu mbalimbali za dunia katika umoja, udugu na upendo kama kikolezo cha ujenzi wa Ufalme wa Mungu na Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Uekumene wa damu unajikita katika: Vita, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo. Lakini, ikumbukwe kwamba, damu ya mashuhuda hawa wa imani ni chachu ya Ukristo. Uekumene wa maisha ya kiroho na utakatifu wa maisha unafumbatwa katika toba na wongofu wa ndani; kwa kujikana na kujivika fadhila ya unyenyekevu; moyo wa ukarimu na udugu wa kibinadamu; upole, uvumilivu na kutumikia bila ya kujibakiza. Wakristo wanakumbushwa kwamba, kadiri wanavyojitahidi kuishi maisha matakatifu mintarafu tunu msingi za Kiinjili, ni kwa kadiri ileile watahamasisha na kutekeleza umoja wa Wakristo na udugu wa kibinadamu kati yao. Uekumene wa huduma unatekelezwa kwa njia ya sera na mikakati ya shughuli za kichungaji sanjari na maisha ya kitume.

Majadiliano ya kiekumene ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume
Majadiliano ya kiekumene ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Tafakari ya Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo kila mwaka inaandaliwa kwa ushirikiano kati ya Baraza la Makanisa Ulimwenguni; WCC na Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo. Mama Kanisa kuanzia tarehe 18 Januari hadi tarehe 25 Januari 2026 Sikukuu ya Kuongoka kwa Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa, anaanza Maadhimisho ya Juma la 59 la Kuombea Umoja wa Wakristo linalonogeshwa na kauli mbiu: “Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu.” Efe 4:4. Tafakari ya Mwaka 2026 imeandaliwa na Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo pamoja na Kanisa la Kitume la Armenia linaloendelea kujitambulisha kuwa ni nguzo ya imani, umoja na mwendelezo wa Mapokeo ya Kikristo. Wito wa umoja wa Wakristo ni kielelezo cha ushuhuda wa imani unaowataka Wakristo kuhakikisha kwamba wanakuwa kweli ni mashuhuda wa upendo na nguvu ya Kristo Yesu katika mchakato wa kumwilisha Mafundisho msingi ya Kristo Yesu. Utengano miongoni mwa Wakristo si jambo la kawaida, linahitaji kufanyiwa marekebisho ya kina, kwani utengano kati ya Wakristo una madhara makubwa katika Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Unahatarisha ushuhuda unaopaswa kutolewa na Wakristo duniani. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Kristo ndiye msingi wa Kanisa na urithi wa wakristo wote. Lakini inasikitisha kuona kwamba, bado Wakristo wenyewe wamegawanyika kinyume kabisa cha utashi wa Kristo Yesu mwenyewe na utengano huu unaendelea kuwa ni kielelezo cha kashfa ya ushuhuda wa utangazaji wa Injili duniani. Baba Mtakatifu Leo XIV anawatia shime Wakristo kufanya hija pamoja na kutegemezana ili kujenga na kuimarisha umoja miongoni mwa Wakristo.

Kauli Mbiu! Mwili mmoja, na Roho Mmoja na wito mmoja
Kauli Mbiu! Mwili mmoja, na Roho Mmoja na wito mmoja   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Maadhimisho ya Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo ni muda muafaka kwa Wakristo kujisomea na kutafakari Maandiko Matakatifu; Kusali pamoja na Kushirikishana amana na utajiri wa Kanisa. Sala na Tafakari hizi ziwe ni chemchemi ya matumaini mapya, tayari kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili. Baba Mtakatifu Leo XIV katika maisha na utume wake, anaendelea kutoa kipaumbele cha pekee kwa majadiliano ya kiekumene, ili Makanisa yaweze kutembea yakiwa yameshikamana; yanasali na kushirikiana katika huduma makini kwa watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia. Majadiliano ya kiekumene hayana budi kujikita katika utakatifu wa maisha, ushuhuda wa uinjilishaji unaowawezesha wakristo kupambana na changamoto mbalimbali za maisha pamoja na utamadunisho ili kweli Injili ya Kristo iweze kuenea miongoni mwa watu wa Mataifa. Baba Mtakatifu Leo XIV anawataka Wakristo kuwa ni vyombo na mashuhuda wa upendo wa kiinjili kati yao na kati ya watu wa Mataifa, ili kujenga na kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu, alama yenye mvuto na mashiko kwa Kanisa na jamii katika ujumla wake, na kama sehemu muhimu sana ya mapambano dhidi ya changamoto mamboleo. Wakristo kama ilivyokuwa kwa nyakati za Mtakatifu Paulo wanapaswa kujitahidi kuungana pamoja kwa njia ya mawazo na maneno na kwamba, umoja huu si mkakati wa kibinadamu bali ni changamoto kutoka kwa Kristo Yesu mwenyewe, anayewavuta wafuasi wake kuungana sanjari na kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu, ili aweze kutenda kadiri ya mapenzi yake yanayojikita katika upendo kwa mwanadamu. Mwenyezi Mungu ndiye kiini, sababu na kikolezo cha umoja miongoni mwa Wakristo.

Juma la Kuombea Umoja
19 Januari 2026, 16:15