Tafuta

Juma 59 la Kuombea Umoja wa Wakristo linalonogeshwa na kauli mbiu: “Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu.” Efe 4:4. Juma 59 la Kuombea Umoja wa Wakristo linalonogeshwa na kauli mbiu: “Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu.” Efe 4:4.   (@Vatican Media)

Papa Leo XIV: Juma la 59 La Kuombea Umoja wa Wakristo: Ushuhuda wa Imani

Juma 59 la Kuombea Umoja wa Wakristo: Kauli mbiu: “Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu.” Efe 4:4. Tafakari ya Mwaka 2026 imeandaliwa na Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo pamoja na Kanisa la Armenia linaloendelea kujipambanua kuwa ni nguzo ya imani, umoja na mwendelezo wa Mapokeo ya Kikristo. Baba Mtakatifu Leo XIV anawahamasisha waamini kujibidiisha kusali ili kuuombea umoja huu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Juma 59 la Kuombea Umoja wa Wakristo linalonogeshwa na kauli mbiu: “Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu.” Efe 4:4. Tafakari ya Mwaka 2026 imeandaliwa na Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo pamoja na Kanisa la Kitume la Armenia linaloendelea kujipambanua kuwa ni nguzo ya imani, umoja na mwendelezo wa Mapokeo ya Kikristo. Baba Mtakatifu Leo XIV anawahamasisha waamini wa Kanisa Katoliki kujibidiisha kusali kwa ajili ya kuombea Umoja wa Wakristo, ili umoja kamili na unaoonekana wa Wakristo wote uweze kupatikana. Hii ni dhamana na wajibu unaopaswa kujikita katika kutafuta na kudumisha haki na amani, sehemu mbalimbali za dunia. Fumbo la Pasaka ni sababu na kiini cha imani, furaha na matumaini ya Wakristo hapa duniani, kwani kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake Kristo Yesu amemkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na kumkirimia maisha ya uzima wa milele, mwaliko wa kudumisha upendo. Kwa njia ya huruma na upendo wa Mungu, waamini wamepewa matumaini mapya.

Juma la 59 la Kuombea Umoja wa Wakristo
Juma la 59 la Kuombea Umoja wa Wakristo   (@Vatican Media)

Kristo Yesu katika ile Sala yake ya Kikuhani, aliwaombea wafuasi wake ili wawe wamoja, ili kushinda kishawishi cha kinzani na mapambano ambayo yamesababisha machozi ya watu wengi sana kumwagika! Sala na Ibada ya Misa Takatifu iwe ni ushuhuda unaounganisha mateso na mahangaiko ya watu mahalia, ili hatimaye, kuweza kumtolea Kristo Yesu sala na mahangaiko yao, ili wote wawe wamoja kwa kushinda kishawishi cha mapambano na kinzani. Umoja ambayo Yesu aliwaombea wafuasi wake ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wote wa Mungu, ili kusiwepo tena na mambo yanayochafua na kuharibu zawadi ya Mungu kwa mwanadamu, ili kila mwananchi aweze kuwa ni mdau na mshiriki katika ujenzi wa historia ya Kanisa. Hii ni sehemu ya salam zilizotolewa na Baba Mtakatifu Leo XIV kwa waamini, wageni na mahujaji wakati wa Katekesi yake, Jumtano tarehe 21 Januari 2026 kwenye Ukumbi wa Paulo VI, mjini Vatican.

Papa Leo XIV: Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo: Haki na Amani
Papa Leo XIV: Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo: Haki na Amani   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Kristo Yesu kabla ya kuingia kwenye Fumbo la Pasaka alisali na kuwaombea wafuasi wake ili wawe wamoja. Mama Kanisa anapoendelea kusali kwa ajili ya Kuombea Umoja wa Wakristo, Baba Mtakatifu Leo XIV anaendelea kuwahimiza Wakristo sehemu mbalimbali za dunia, ili waweze kuwa wamoja, ili walimwengu waweze kumwamini Kristo Yesu pamoja na Ufunuo wake. Anawahimiza waamini kuendelea kuombea: haki, amani, utu, heshima na haki msingi za binadamu kwani kwa sasa vita na ghasia vinaonekana kuwa ndio mtindo wa kisasa. Kristo Yesu katika Ufunuo wa Fumbo la Mwili wake, amewafunulia wanadamu, Baba yake wa milele; awasaidie watu wa Mataifa kujizatiti katika njia ya haki na upatanisho. Waamini wajifunze kumtafakari Kristo Yesu aliyezaliwa, akateswa, akafa na kufufuka kwa wafu, ili hatimaye, waweze kumpenda na kutenda kama anavyopenda na kutenda Yeye, kwa kutambua ufunuo wa Uso wa Mungu kwa waja wake, ili hatimaye, waweze kuishi kadiri ya mapenzi ya Mungu, kwa sababu Kristo Yesu ndiye amani na matumaini ya waja wake. Baba Mtakatifu Leo XIV mwishoni mwa tafakari yake amewaalika waamini wa Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo duniani, kumwomba Kristo Yesu, ili waamini wote waondoe migawanyiko, ili hatimaye, waweze kujenga vifungo imara vya umoja wa Wakristo.

Umoja wa Wakristo 2026
21 Januari 2026, 15:06