Tafuta

Baba Mtakatifu Leo XIV mwanzoni mwa mwaka mpya hukutana na kuzungumza na vikosi vya ulinzi na usalama mjini Vatican. Baba Mtakatifu Leo XIV mwanzoni mwa mwaka mpya hukutana na kuzungumza na vikosi vya ulinzi na usalama mjini Vatican.   (@Vatican Media)

Papa Leo XIV: Hotuba Kwa Vikosi Vya Ulinzi na Usalama Mjini Vatican

Mwanzoni mwa mwaka mpya Papa kukutana na kuzungumza na vikosi vya ulinzi na usalama mjini Vatican. Lengo ni kusalimiana, kutoa shukrani kwa huduma makinii ili kuhakikisha kunakuwepo ulinzi na usalama kwa Baba Mtakatifu na wasaidizi wake wa karibu, watalii na waamini katika ujumla wake wanaotembelea Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican sanjari na kuwatakia heri na baraka za Mwaka Mpya wa 2026. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kumekuwepo na utamaduni wa Khalifa wa Mtakatifu Petro na kwa sasa katika nafsi ya Baba Mtakatifu Leo XIV mwanzoni mwa mwaka mpya kukutana na kuzungumza na vikosi vya ulinzi na usalama mjini Vatican. Lengo ni kusalimiana, Baba Mtakatifu kutoa shukrani kwa huduma makini zinazotolewa, ili kuhakikisha kunakuwepo ulinzi na usalama kwa Baba Mtakatifu mwenyewe, wasaidizi wake wa karibu, watalii na waamini katika ujumla wake wanaotembelea Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican sanjari na kuwatakia heri na baraka za Mwaka Mpya wa 2026. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru kwa huduma makini iliyoliwezesha Kanisa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kadiri ya takwimu zilizotolewa, kuna waamini zaidi ya milioni 33.5 kutoka katika nchi 185 wamepitia Lango hili. Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo yaliyozinduliwa na Hayati Baba Mtakatifu Francisko tarehe 24 Desemba 2024. Kwa hakika mahujaji wa matumaini kutoka sehemu mbalimbali za dunia wamepitia katika Lango hili, ambalo litaendelea kubaki wazi katika maisha ya kiroho kwa wale ambao bado wametia nia ya kuhatarisha maisha yao, wanaosikia hamu ya kuondoka na kuutafuta ukweli wa maisha katika Kristo Yesu. Wanajeshi hawa wametekeleza dhamana na wajibu wao kwa ari na moyo mkuu na kwamba, shukrani za pekee zinaziendea familia, ndugu na jamaa zao, waliopokea sadaka na majitoleo yao, walipokuwa wakifanya kazi.

Papa Leo XIV anavishukuru na kuvipongeza vyombo vya ulinzi na usalama
Papa Leo XIV anavishukuru na kuvipongeza vyombo vya ulinzi na usalama   (@VATICAN MEDIA)

Papa Francisko alifariki dunia tarehe 21 Aprili 2025 na kuzikwa tarehe 26 Aprili 2025 katika Ibada iliyoongozwa na Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali. Mara baada ya Misa Takatifu Maandamano yalianza kutoka katika Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican hadi kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, ili kupumzishwa kwenye usingizi wa amani, Ibada iliyoongozwa kwa faragha na Kardinali Kevin Joseph Farrel, “Camerlengo” mkuu wa Kanisa Katoliki. Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali, Jumatano tarehe 7 Mei 2025 aliongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro: “Pro eligendo Romano Pontifice.” Mama Kanisa akasali na kuomba: Umoja na ushirika; Ujenzi wa udugu wa kibinadamu; Umoja kati ya Wakristo, Urika wa Maaskofu na Khalifa wa Mtakatifu Petro, ili kweli Kanisa liweze kuwa ni “nyumba na shule ya ushirika” kwa kuendelea kuwa aminifu kwa tunu msingi za Kiinjili.

Papa Leo XIV anavishukuru vyombo vya ulinzi na usalama mjini Vatican
Papa Leo XIV anavishukuru vyombo vya ulinzi na usalama mjini Vatican   (@VATICAN MEDIA)

Mwadhama Kardinali Robert Francis Prevost, wa Shirika la Mtakatifu Augustino, O.S.A. ndiye Baba Mtakatifu, wa 267 aliyechaguliwa na Baraza la Makardinali katika mkutano wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, Askofu mkuu wa Roma, kama alivyotangazwa na Kardinali Shemasi Dominique Mamberti, Alhamisi tarehe 8 Mei 2025 na amechagua jina la Leo wa XIV. Kwa hakika anasema, Baba Mtakatifu Leo XIV matukio yote haya yaliacha changamoto kubwa katika shughuli za ulinzi na usalama mjini Vatican, lakini wao wakaonesha moyo wa sadaka na majitoleo; weledi, taaluma na busara kwa kuhakikisha kuwa kila kitu kinafanyika kwa utaratibu, kanuni na sheria za Kanisa. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, utaratibu na usalama ni zawadi ambazo zinahitaji sadaka kubwa kutoka kwa wale wanaosimamia, lakini zinachangia kwa kiasi kikubwa kwa manufaa ya wote: Kufuata kanuni, lakini pia kwa utekelezaji wake katika mazingira ya haki na amani. Mazingira salama kwa hakika ni msaada mkubwa kwa maisha ya sala, kwa wageni na mahujaji wanaofika mjini Roma, ambao kimsingi wameweza kupata uzoefu huu, baada ya kufanya safari ndefu pamoja na sadaka ya kimwili na kiuchumi katika kipindi cha miezi michache iliyopita, zote hizi ni shukrani zinazopaswa kuwaendea wanajeshi wa vikosi vya ulinzi na usalama mjini Vatican.

Wanajeshi na walinzi wa Vatican wamejitosa bila ya kujibakiza
Wanajeshi na walinzi wa Vatican wamejitosa bila ya kujibakiza   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Malaika Mkuu Mikaeli ndiye Msimamizi na Mwombezi wa Jeshi la Polisi nchini Italia. Amemwomba msaada wa ulinzi na usimamizi, ili aweze kuwahakikishia raia: amani, utulivu na uaminifu; ili waweze kuheshimu sheria na kanuni pasi na shuruti, mintarafu ari na moyo wa udugu wa kibinadamu. Lengo ni kukazia uaminifu na utulivu; utu, heshima na haki msingi za binadamu, kama msingi wa huduma na mchakato wa ukuaji wa mtu binafsi na ule wa kijumuiya. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Leo XIV kwamba, katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo wameweza kujichotea neema na baraka. Mwishoni mwa hotuba yake, amewatakia amani na utulivu wa ndani kama mambo msingi katika ujenzi wa maisha ya kijamii yanayosimikwa katika amani. Uwepo wao uwe ni hakikisho la ufanisi zaidi, utaratibu mwema na utulivu ambao ni muhimu sana katika mchakato wa ujenzi wa maisha ya kijamii yanayosimikwa katika amani na utulivu na katika tunu msingi za Kiinjili. Mwishoni, mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Leo XIV amewakabidhi wanajenzi wa vikosi vya ulinzi na usalama vya Vatican chini ya Ulinzi na maombezi ya Bikira Maria na ya Mtakatifu Mikaeli Malaika Mkuu na kwamba, anawahakikishia sala zake katika maisha na utume wao.

Usalama 2026
19 Januari 2026, 15:25