Papa Leo XIV: Hotuba Kwa Baraza la Makardinali: Umoja, Ushuhuda Na Sinodi
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mkutano wa Baraza la Makardinali ulioitishwa na Baba Mtakatifu Leo XIV kuanzia tarehe 7 Januari hadi tarehe 8 Januari 2026, hizi zimekuwa ni siku za: Sala, Tafakari na Majadiliano ya kina kadiri ya maisha na utume wa Kanisa mintarafu Kristo Yesu; Mwanga na Nuru ya Mataifa. Mama Kanisa anatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Makardinali wamepata nafasi ya kutafakari kuhusu: Waraka wa Kitume wa Papa Francisko: “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili”, anayetoa kipaumbele cha kwanza kwa furaha ya Injili, kwa kuwaalika waamini kushirikisha furaha yao inayopata chimbuko kutoka katika huruma na upendo wa Mungu kwa wanadamu. Katika mwono huu, Kristo ni kiini cha Injili na kwamba, Kanisa linaalikwa kufanya mageuzi makubwa kama sehemu ya Uinjilishaji Mpya. Waraka wa “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu”, hii ilikuwa ni mada ya pili. Waraka huu wa kitume unachota utajiri wake katika mapendekezo yaliyotolewa na Mababa wa Sinodi juu ya Uinjilishaji Mpya kama njia ya kutangaza na kushuhudia Imani ya Kikristo katika ulimwengu mamboleo. Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, Liturujia chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Makundi 9 ya Makardinali kutoka katika Makanisa mahalia yametoa ushauri kwa Baba Mtakatifu na kwamba, ameonesha utayari kusikiliza ushauri wao, ili kupenda na kuhudumia, tayari kujikita katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Utamaduni wa kusikilizana, kutembea na kufanya kazi kwa pamoja kwa kujikita katika udugu wa kibinadamu na urafiki wa kweli ni mambo yanayoweza kupyaisha maisha na utume wa Kanisa kwa sasa na kwa siku zijazo.
Baba Mtakatifu Leo XIV katika mahubiri yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu aliyoadhimisha pamoja na Baraza la Makardinali, tarehe 8 Januari 2026 kwenye Kanisa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amekazia kuhusu: Umuhimu wa mkutano huu unaowawezesha Makardinali kufanya mang’amuzi ya pamoja, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu, yanayopata chimbuko lake kutoka kwa Kristo Yesu. Baraza la Makardinali, kimsingi ni kielelezo cha Jumuiya ya Sala, ambayo kila Kardinali anachangia kadiri ya uwezo wake ili kupata matunda bora zaidi. Upendo wa Mungu ni ule unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, changamoto na mwaliko kwa wafuasi na mitume wa Kristo Yesu, chimbuko la ushirika ambao Mchumba wa Kristo Yesu anauishi na anataka kuwa ni nyumba na shule kwa jirani zake. Baba Mtakatifu Leo XIV katika hotuba yake ya kuhitimisha Mkutano wa Baraza la Makardinali Alhamisi tarehe 8 Januari 2026 alikazia pamoja na mambo mengine kuhusu: Ukaribu wa Baba Mtakatifu na Baraza la Makardinali kama fursa ya kukutana mubashara na kufahamiana: Kristo Yesu ndiye kiini cha maisha na utume wa Kanisa, changamoto na mwaliko wa kumtangaza na kumshuhudia kwa watu wa Mataifa; Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi unaosimikwa ushirika na utume; Waraka wa “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu.” Katika muktadha huu, Kanisa linapaswa kujikita katika: Toba na wongofu wa kimisionari na kichungaji kwa kuwa ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu. Kanisa lijitambulishe na kueleweka kuwa ni Fumbo la Ushirika unaomwilishwa katika dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa.
Makardinali kimsingi ndio washauri wakuu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro ili kukoleza juhudi za toba, haki, amani na maridhiano; kwa kukuza na kudumisha utu na heshima ya binadamu, ili watu waweze kuishi katika mazingira bora zaidi. Wanaitwa kuwa ni mashuhuda wasio na woga kwa Kristo Yesu na Injili yake na katika mji wa Roma na sehemu mbalimbali za dunia. Mkutano wa Baraza la Makardinali imekuwa ni fursa ya kutangaza na kushuhudia ushirika na umoja wa Kanisa sanjari na karama na mapaji mbalimbali ya Roho Mtakatifu kwa ajili ya huduma ya ushauri kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro na kwamba, Baba Mtakatifu Leo XIV yuko karibu na Makardinali wote. Hii imekuwa ni fursa ya kukutana mubashara, kufahamiana na kujadiliana katika ukweli na uwazi; kama sehemu ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, ili kujenga na kudumisha utamaduni wa kujadiliana na kusikilizana kwa makini. Makardinali watambue kwamba, Kristo Yesu ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa, na kwamba, wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayopata chimbuko lake katika ukweli wa maisha, kama ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa Ulimwengu mamboleo. Tema mbalimbali zilizoibuliwa na Makardinali kwenye mkutano huu zinapata chimbuko lake kutoka katika Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican unaofumbatwa katika hija ya maisha na utume wa Kanisa; Toba na wongofu wa ndani sanjari na upyaisho wa utume na maisha ya Kanisa. Kuna uhusiano wa karibu sana kati ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu. Hii ni sehemu ya maandalizi ya Mkutano Mkuu wa Sinodi ya Maaskofu utakaoadhimishwa mwaka 2028.
Hii ni hija ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi inayokita mizizi yake katika umoja na utume; ushirika kati ya Baba Mtakatifu na Makanisa mahalia sanjari na Mabaraza ya Maaskofu kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Maisha na utume wa Kanisa lazima kutekelezwa mintarafu: Waraka wa Kitume wa Papa Francisko: “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” sanjari na Waraka wa “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu” lengo ni kukazia mchakato wa Uinjilishaji mpya unaokita mizizi yake katika ushuhuda, ili hatimaye, kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo mintarafu: Malezi na makuzi ya utamaduni wa kusikilizana hasa seminarini na kati ya Maaskofu. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ndani ya Kanisa ni kashfa ambayo imechafua maisha na utume wa Kanisa kiasi kwamba, haiwezi kamwe kufichwa, kuikataa wala kuibeza kwani ni ukweli usioweza kufumbiwa macho. Ukweli huu unapaswa kupokelewa na hatimaye, kumwilishwa katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani, wema na utakatifu wa maisha; kwa kuganga na kutibu madonda ya kashfa ya nyanyaso za kijinsia, tayari kuambata upendo na huruma ya Mungu, ili kuanza upya kwa kuchuchumilia: kanuni maadili, utu wema na utakatifu wa maisha. Lengo kuu ni kuzuia kashfa ya nyanyaso za kijinsia isijitokeze tena ndani ya Kanisa. Huu ni ukweli ambao Maaskofu wanapaswa kushirikishana katika maisha na utume wao; waathirika wapokelewe na kusikilizwa na kamwe wasipewe kisogo; wasaidiwe kwa sera na mikakati ya shughuli za kichungaji.
Mkazo ni malezi na makuzi yapewe kipaumbele katika sehemu mbalimbali za shughuli za kichungaji, kama sehemu ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Maaskofu wajiandae kwa ajili ya Maadhimisho ya Mkutano wa Sinodi ya Maaskofu utakaofanyika Mwaka 2028, hii ni hija ya maisha, utume na huduma katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Baba Mtakatifu amewahakikishia Makardinali kwamba, atajipatia muda wa kusoma na kutafakari mchango wao na baadaye atawapatia mrejesho, kama sehemu ya mchakato wa mwendelezo wa majadiliano. Baba Mtakatifu Leo XIV amesema, Mkutano wa Awamu ya Pili ya Baraza la Makardinali utafanyika karibia na maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Miamba wa Imani. Na kwamba, wakati huu, mkutano utachukua muda mrefu kidogo. Ni wakati wa kuonesha mshikamano wa udugu wa kibinadamu, tayari kutangaza Injili ya matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, Mwanga na Nuru ya Mataifa, aliyejifunua kwa watu wa Mataifa, ili kushirikishana: Uchungu na fadhaa ya wanadamu wa nyakati hizi, hasa ya maskini na ya wale wote wanaoteswa, yote ni furaha na matumaini, uchungu na fadhaa ya wafuasi wa Kristo pia. Rej. LG 1.
Mikutano hii inalenga kuonesha ukaribu wa Kanisa la Kiulimwengu kwa watu wanaoteseka, tayari kuwatangazia Injili ya matumaini. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, haya ni matumaini wanayopaswa kushirikishwa vijana, kama ambavyo imebainishwa katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo! Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Makanisa yamefunga tayari Malango ya Jubilei ya Matumaini, kama hitimisho la Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo. Lakini Kristo Yesu ni Lango la: Huruma, Upendo na Matumaini kwa waja wake, ataendelea kubaki akiwa anaambatana na watu wake, kwani ni Lango linalowapeleka watu wa Mungu katika maisha ya Kimungu. Mtoto aliyezaliwa ni Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, anayekuja kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko uletao maisha na uzima wa milele. Kristo Yesu anakuja kuganga na kuponya madonda yanayo mwandama mwanadamu na kwa wale waliovunjika na kupondeka nyoyo wanapata amani na utulivu wa ndani. Baba Mtakatifu Leo XIV amewaalika Makardinali kuombeana wao kwa wao, ili Mwenyezi Mungu awakirimie neema yake ili yale ambayo udhaifu wa kibinadamu hauwezi kuyafikia, watumishi wako hawa wakiendelea kulijenga Kanisa lake, wanga’e kwa uadilifu wa imani na usafi wa moyo. Mtakatifu Petro, Mtume awaombee, ili waendelee kukuza na kudumisha roho ya: umoja na ushirika, huku wakiendelea kuweka nia ya kuutumikia Mtumbwi wake.
