Tafuta

Papa Leo XIV: Lango la Jubilei ya Matumaini limefungwa lakini amana na utajiri wa Mama Kanisa unaobubujika kutoka katika huruma na upendo wa Mungu bado unaendelea kubaki wazi. Papa Leo XIV: Lango la Jubilei ya Matumaini limefungwa lakini amana na utajiri wa Mama Kanisa unaobubujika kutoka katika huruma na upendo wa Mungu bado unaendelea kubaki wazi.   (@Vatican Media)

Papa Leo XIV: Epifania ya Bwana: Lango la Jubilei ya Matumaini; Furaha ya Injili

Lango la Jubilei ya Matumaini limefungwa lakini amana na utajiri wa Mama Kanisa unaobubujika kutoka katika huruma na upendo wa Mungu bado unaendelea kubaki wazi. Baba Mtakatifu amepiga magoti, akasali katika ukimya na baadaye akafunga Lango la Jubilei, ambalo kadiri ya takwimu zilizotolewa, waamini zaidi ya milioni 33.5 kutoka katika nchi 185 wamepitia Lango hili. Jubilei hii ilizinduliwa na Papa Francisko tarehe 24 Desemba 2024: Lango la Matumaini liko wazi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hayati Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Admirabile signum” yaani “Ishara ya Kushangaza”: Maana na Umuhimu wa Pango la Noeli” uliotolewa tarehe 1 Desemba 2019 anasema, inapokaribia Sherehe ya Tokeo la Bwana, au Epifania, Sanamu za Mamajusi watatu kutoka Mashariki zinawekwa kwenye Pango la Noeli. Hawa ni wataalam wa nyota kutoka Mashariki waliojitaabisha kumtafuta Mtoto Yesu na hatimaye walipomwona wakamzawadia: Ubani unaonesha Umungu wa Kristo Yesu; Manemane ni ushuhuda wa ubinadamu wa Kristo Yesu utakaokabiliwa na mateso, kifo na ufufuko kwa wafu. Dhahabu ni kielelezo cha Ufalme wa Kristo Yesu, yaani; Ufalme wa kweli na uzima; Utakatifu na neema; haki, upendo na amani. Kila mwamini anahimizwa kuwa kweli ni shuhuda na chombo cha matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama chemchemi ya furaha na amani inayobubujika kutoka kwa Mtoto Yesu. Katika Sherehe ya Epifania yaani Tokeo la Bwana, inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 6 Januari, Mama Kanisa pia anaadhimisha Siku ya Utoto Mtakatifu, iliyoanzishwa na Papa Pius XII, kunako mwaka 1950, aliyetaka waamini kutoa kipaumbele cha kwanza kwa malezi na makuzi ya watoto wao kama Kristo Yesu, alivyowapatia nafasi ya pekee, katika maisha na utume wake. Tokeo la Bwana ni sherehe ya sala na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, huruma na mapendo. Ni Siku ya kutangaza pamoja Injili ya upendo; Kusali kwa pamoja kama ndugu; kucheza pamoja, kielelezo makini cha ujenzi wa udugu wa kibinadamu, tayari kutembea pamoja kama mahujaji wa imani na matumaini, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watoto wanaoteseka sehemu mbalimbali za dunia kama anavyosema Baba Mtakatifu Leo XIV kwamba, hawa ni watoto ambao wamepokwa: utu, heshima na haki zao msingi. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Makanisa yamefunga tayari Malango ya Jubilei ya Matumaini, kama hitimisho la Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo.

Lango la Jubilei limefungwa, lango la matumaini liko wazi!
Lango la Jubilei limefungwa, lango la matumaini liko wazi!

Lakini Kristo Yesu ni Lango la Matumaini kwa waja wake, ataendelea kubaki akiwa anaambatana na watu wake, ni Lango linalowapeleka watu wa Mungu katika maisha ya Kimungu. Mtoto aliyezaliwa ni Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, anayekuja kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko uletao maisha na uzima wa milele. Kristo Yesu anakuja kuganga na kuponya madonda yanayo mwandama mwanadamu na kwa wale waliovunjika na kupondeka nyoyo wanapata amani na utulivu wa ndani. Katika maadhimisho ya Sherehe ya Tokeo la Bwana, tarehe 6 Januari 2026 Baba Mtakatifu ameanza Ibada ya Misa Takatifu kwa kufunga Lango la Jubilei ya Matumaini kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa kufuata madhehebu yaliyowekwa tangu mwaka 1975, yakafanyiwa marekebisho na Mtakatifu Yohane Paulo II katika Maadhimisho ya Jubilei Kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo. Lango la Jubilei ya Matumaini limefungwa lakini amana na utajiri wa Mama Kanisa unaobubujika kutoka katika huruma na upendo wa Mungu bado unaendelea kubaki wazi. Baba Mtakatifu amepiga magoti, akasali katika ukimya na baadaye akafunga Lango la Jubilei, ambalo kadiri ya takwimu zilizotolewa, waamini zaidi ya milioni 33.5 kutoka katika nchi 185 wamepitia Lango hili. Tendo hili ni ishara ya kufungwa rasmi kwa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo; Jubilei iliyozinduliwa na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 24 Desemba 2024. Kwa hakika mahujaji wa matumaini kutoka sehemu mbalimbali za dunia wamepitia katika Lango hili, ambalo litaendelea kubaki wazi katika maisha ya kiroho kwa wale ambao bado wametia nia ya kuhatarisha maisha yao, wanaosikia hamu ya kuondoka na kutafuta ukweli wa maisha katika Kristo Yesu, Mwana wa Mungu anayejifunua kwa walimwengu.

Maandamano ya Sherehe ya Epifania kwenye Viunga vya Vatican
Maandamano ya Sherehe ya Epifania kwenye Viunga vya Vatican   (ANSA)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Mwinjili Mathayo 2:1-12 anaelezea ile furaha ya Mamajusi kutoka Mashariki walipomwona Mtoto Yesu, kielelezo cha Ufunuo wa Mungu kwa watu wa Mataifa. Lakini pia Ufunuo huu wa Mungu unakumbana na furaha na wasi wasi wa ndani; upinzani na utii; woga na kiu ya kutaka kuonana na Mungu anayejifunua kwa waja wake, chemchemi ya Injili ya matumaini, mabadiliko na mwanzo mpya kama anavyosema Nabii Isaya: “Ondoka, uangaze; kwa kuwa nuru yako imekuja, Na utukufu wa BWANA umekuzukia.” Isa 60:1. Lakini ufunuo wa Mungu kwa Mataifa ulimfadhaisha sana Mfalme Herode na Yerusalemu pia pamoja naye kwa kuwaona Mamajusi kutoka Mashariki. Mama Kanisa anachangamotishwa na muktadha huu, kuwa ni chombo cha furaha na matumaini, kwa kutambua kwamba, hata leo hii, bado kuna Mamajusi wa furaha na matumaini, kwa sababu mwanadamu ni msafiri “Homo viator” kama wanavyosema wahenga; ni msafiri wa matumaini kumwendea Mwenyezi Mungu; matumaini kama ambayo Bikira Maria alikuwa ameyabeba mikononi mwake, yaani Mtoto Yesu na Mamajusi wakaanguka na kumsujudia na wala si kama zawadi ya: Dhahabu, Uvumba na Manemane walizokuwa wamebeba vibindoni mwao. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Maeneo Matakatifu kama vile: Makanisa makuu na Madhabahu yameibukia kuwa ni maeneo ya hija ya Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo na kwamba, sasa ni wakati wa maeneo haya kusambaza harufu ya maisha kwamba, huu ni mwanzo wa dunia mpya! Huu ni mwaliko kwa waamini kujiuliza maswali msingi! Je, ndani ya Kanisa letu kuna maisha, kuna nafasi ya kile kinachozaliwa leo! Je, wanapenda kuwa ni vyombo, watangazaji na mashuhuda wa Habari Njema ya Wokovu, tayari kutumwa na Mwenyezi Mungu. Maandiko Matakatifu yanamwonesha Mfalme Herode akifadhaika na Yerusalemu pamoja naye, na akataka kutumia utafiti wa Mamajusi kwa ajili ya ustawi na mafao yake binafsi, akaelemewa sana na woga, uliomfanya kuwa kipofu. Baba Mtakatifu Leo XIV anakaza kusema, furaha ya Injili ni chemchemi ya huru wa ndani, inamwezesha mwamini kuwa na hekima na busara! Wasikivu na wabunifu na kwamba, inapendekeza njia tofauti na zile ambazo zimekwisha kutumiwa!

Mtoto Yesu aliyezaliwa ni chemchemi ya matumaini mapya
Mtoto Yesu aliyezaliwa ni chemchemi ya matumaini mapya   (@Vatican Media)

Mtoto Yesu aliyezaliwa ni chemchemi ya matumaini na kiungo muhimu cha Jumuiya inayopata chimbuko lake kutoka katika Injili ya Matumaini inayokita mizizi yake katika maisha ya watu. Maadhimisho ya Jubilei ni kumbukumbu kwamba, kila kitu kinaweza kupyaishwa na kwamba, Mwenyezi Mungu anapenda kuendelea kukua pamoja na waje wake, ili hatimaye, aweze kuwa ni “Mungu pamoja nasi.” Ni Mungu anayetaka kumkomboa mwanadamu kutoka katika utumwa wa kale na huu mpya. Huyu ni Mungu anayewahusisha na kuwashirikisha vijana wa kizazi kipya, maskini na matajiri, watakatifu na wadhambi katika kazi yake ya huruma inayokita mizizi yake katika haki na kwamba, huu ni: Ufalme wa ukweli na uzima, ufalme wa haki na amani, ufalme wa mapendo na ufalme ambao Mungu anatawala katika mioyo ya watu wake na kuendelea kuchipua na kukua sehemu mbalimbali za dunia. Lakini huu ni Ufalme ambao: “Tangu siku za Yohana Mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu wauteka.” Mt 11:12. Hii ni changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba: Kupenda na kutafuta amani, kuna maanisha kulinda kile ambacho ni kichanga, kidogo na dhaifu kama Mtoto mdogo, mambo ambayo kimsingi yanatumiwa sana kiuchumi na katika muktadha wa kukoleza biashara. Baba Mtakatifu anawauliza waamini, Je, maadhimisho ya Jubilei ya Matumaini yamewasaidia kukimbia aina hiyo ya ufanisi unaogeuza kila kitu kuwa ni biadhaa na binadamu kuwa ni mtaji? Katika muktadha huu, Je, waamini wanaweza kuwatambua wageni kama wasafiri, watafutaji, jirani au kama msafiri au mwandani wa safari? Huu ni wajibu wa kudumu wa Mama Kanisa kuchunguza na kusoma alama za nyakati na hivyo kuzifafanua katika mwanga wa Injili. Rej Gaudium et spes, 4.

Kanisa lisome alama za nyakati na kuzifafanua kwa mwanga wa Injili
Kanisa lisome alama za nyakati na kuzifafanua kwa mwanga wa Injili

Katika Ulimwengu mamboleo, miji mingi na jumuiya nyingi zinatamani kusikia: “Nawe Bethlehemu, katika nchi ya Yuda, Hu mdogo kamwe katika majumbe wa Yuda; Kwa kuwa kwako atatoka mtawala Atakayewachunga watu wangu Israeli.” Mt 2: 6. Bado Mwenyezi Mungu anaendelea kuwashangaza Walimwengu kwa kuwaonesha njia zake na kwamba, wanaotumia mabavu hawajafanikiwa kuutawala Ulimwengu na wenye nguvu hawawezi kuudhibiti. Mamajusi walikuwa na furaha kubwa walipoiona Nyota, changamoto na mwaliko kwa waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kuendelea kuwa ni mahujaji wa matumaini; waminifu kwa Mungu. Huu ni mwaliko kwa waamini kupyaisha Makanisa yao, Jumuiya zao kwa kushikamana na kwa njia hii watakuwa ni Jumuiya za mapambazuko mapya. Bikira Maria Nyota ya Asubuhi ataendelea kuwaongoza waamini na watu wenye mapenzi mema, mbele ya Mwanaye mpendwa Kristo Yesu, ili kutafakari na kumhudumia mwanadamu aliyegeuzwa kwa upendo wa  Neno wa Mungu aliyefanyika Mwili!

Papa Leo XIV Epifania ya Bwana 2026
06 Januari 2026, 15:35