Tafuta

Baba Mtakatifu Leo XIV Ijumaa tarehe 9 Januari 2026 amekutana na kuzungumza na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican. Baba Mtakatifu Leo XIV Ijumaa tarehe 9 Januari 2026 amekutana na kuzungumza na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican.   (@VATICAN MEDIA)

Papa Leo XIV Diplomasia ya Vatican: Utu, Heshima, Haki Msingi Na Amani

Papa Leo XIV: Amewakaribisha Mabalozi wapya, Jubilei ya Matumaini; Maboresho ya uhusiano wa kidiplomasia; Hija ya Kitume; Jubilei ya Miaka 1700 ya Mtaguso wa Nicea! Ujenzi wa Mji wa Mungu na Mji wa Duniani; matumizi sahihi ya lugha; haki msingi za binadamu; uhuru wa dhamiri, uhuru wa kidini; Majadiliano ya kidini; Vita; Utu na heshima ya binadamu; Tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; Vita Ukanda wa Gaza; Mgogoro wa Venezuela, Vita Maziwa Makuu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Dhana ya diplomasia ya Vatican inafumbatwa katika amani, kwa kusimama kidete kupambana na baa la njaa na umaskini duniani; kwa kulinda na kutunza mazingira bora nyumba ya wote kwani kuna mamilioni ya watu wanaoathirika kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi na ukosefu wa fursa za ajira na maendeleo fungamani! Mataifa yatambue kwamba, yanategemeana na kukamilishana na kwamba, binadamu ni kiumbe jamii. Kwa njia, hii, Jumuiya ya Kimataifa inaweza kuwa ni alama ya matumaini kwa wale waliopondeka, kuvunjika moyo na waliokata tamaa ya maisha kutokana na sababu mbalimbali. Vatican katika mchakato wa kidiplomasia na uhusiano wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa inakazia kwa namna ya pekee: Mosi, umuhimu wa kushirikiana na kushikamana katika mapambano dhidi ya umaskini unaodhalilisha utu na heshima ya binadamu sehemu mbalimbali za dunia. Jambo la pili, ni uhamasishaji wa familia ya binadamu kujenga na kudumisha madaraja ya watu kukutana na kusaidiana, ili kujenga na kuimarisha: haki, umoja na udugu wa kibinadamu ili kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Vatican inakazia pamoja na mambo mengine: ujenzi wa utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kutatua migogoro ya kivita, mipasuko, kinzani na changamoto mbalimbali zinazoendelea kujitokeza katika uso wa dunia! Lengo la diplomasia ya Vatican ni kukuza na kudumisha mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa amani duniani. Katika sehemu hii, Vatican imekuwa ni sauti ya kinabii na hasa zaidi sauti ya watu wasiokuwa na sauti! Jumuiya ya Kimataifa inahamasishwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu, uhuru wa kuabudu, utu na heshima ya binadamu wote bila ubaguzi.

Diplomasia ya Vatican inasimikwa katika utu, heshima na haki msingi
Diplomasia ya Vatican inasimikwa katika utu, heshima na haki msingi   (@Vatican Media)

Ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa inataka kupata maendeleo ya kweli na endelevu, basi binadamu anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati ya maendeleo fungamani! Kanisa linapenda kudumisha mchakato wa haki, amani, utulivu na maridhiano kwa kuzimisha moto wa machafuko, kinzani na vita kwa maji ya: baraka, majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kuzingatia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni mchakato wa majadiliano ya kidiplomasia unaojikita katika kubainisha mbinu mkakati wa mawasiliano, vikwazo na vizingiziti vinavyoweza kujitokeza pamoja na kuunda mazingira ya kuaminiana na kuthaminiana, ili kuendeleza majadiliano. Diplomasia inayotekelezwa na Vatican sehemu mbali mbali za dunia inajikita kwa namna ya pekee, katika msingi wa haki, amani na maridhiano kati ya watu! Ni diplomasia inayojipambanua kwa kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Ni katika muktadha wa utekelezaji wa diplomasia ya Vatican, Baba Mtakatifu Leo XIV Ijumaa tarehe 9 Januari 2026 amekutana na kuzungumza na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican. Katika hotuba yake: amewakaribisha Mabalozi kutoka Kazakhstan, Burundi na Belarus; Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo; Maboresho ya uhusiano kati ya Italia na Vatican; Hija ya Kitume nchini Uturuki na Lebanon, sanjari na Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 1700 ya Mtaguso wa Nicea! Ujenzi wa Mji wa Mungu na Mji wa Duniani; matumizi sahihi ya lugha na uhuru wa mtu kujieleza; haki msingi za binadamu na uhuru wa dhamiri, uhuru wa kidini; Majadiliano ya kidini; Vita; Utu na heshima ya binadamu; tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; Vita kati ya Israeli na Palestina; Mgogoro wa Venezuela, Vita inayoendelea kwenye Ukanda wa Maziwa Makubwa, Mgogoro wa Myanmar, Azimio la Amani Kati ya Armenia na Azerbaijan na hatimaye, ni maadhimisho ya Jubilei ya miaka 800 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Francisko wa Assisi, mtu wa amani na majadiliano, aliyejitahidi kuishi ukweli katika hali ya unyenyekevu!

Papa Leo XIV akizungumza na Wanadiplomasia Mjini Vatican
Papa Leo XIV akizungumza na Wanadiplomasia Mjini Vatican   (@VATICAN MEDIA)

Baba Mtakatifu Leo XIV katika hotuba yake: amewakaribisha Mabalozi kutoka Kazakhstan, Burundi na Belarus; kielelezo cha mahusiano mazuri ya kidiplomasia kati ya Vatican na nchi hizi. Amewashukuru wanadiplomasia na viongozi mbalimbali wa Serikali waliohudhuria mazishi ya Baba Mtakatifu Francisko, aliyeheshimika na wengi kama Baba na kiongozi mahiri wa watu wa Mungu, aliyejisadaka kwa ajili ya shughuli za kichungaji zilizosimikwa katika upendo. Lango la Jubilei ya Matumaini limefungwa lakini amana na utajiri wa Mama Kanisa unaobubujika kutoka katika huruma na upendo wa Mungu bado unaendelea kubaki wazi. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kadiri ya takwimu zilizotolewa, kuna waamini zaidi ya milioni 33.5 kutoka katika nchi 185 wamepitia Lango hili. Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo yalizinduliwa na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 24 Desemba 2024. Kwa hakika mahujaji wa matumaini kutoka sehemu mbalimbali za dunia wamepitia katika Lango hili, ambalo litaendelea kubaki wazi katika maisha ya kiroho kwa wale ambao bado wametia nia ya kuhatarisha maisha yao, wanaosikia hamu ya kuondoka na kutafuta ukweli wa maisha katika Kristo Yesu, Mwana wa Mungu anayejifunua kwa walimwengu na mganga wa maisha ya kiroho kwa waja wake. Hii imekuwa ni fursa kwa waamini kujenga na kuimarisha mahusiano na mafungamano yao na Kristo Yesu, kwa kupata faraja pamoja na kupyaisha imani na matumaini. Mji wa Roma, umeonesha ukarimu mkubwa kwa mahujaji na watalii kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuishukuru Serikali ya Italia, vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuhakikisha kwamba, Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo yanafanikiwa kwa ufanisi mkubwa na kama ilivyotokea hata katika kifo na hatimaye, mazishi ya Baba Mtakatifu Francisko.

Jubilei ya matumaini kimekuwa ni kipindi cha neema na baraka
Jubilei ya matumaini kimekuwa ni kipindi cha neema na baraka   (@VATICAN MEDIA)

Kumekuwepo na maboresho makubwa ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Italia na kwamba, Mwaka 2026: “Makubaliano ya Huduma ya Kiroho kwa Wanajeshi wa Vikosi Vya Ulinzi na Usalama nchini Italia” yanaanza kutumika rasmi. Makubaliano yaliyotiwa saini kati ya Italia na Vatican kwa kujenga Kituo cha kuzalisha umeme wa jua huko “Santa Maria di Galeria” kitaruhusu usambazaji wa umeme kwa ajili ya mji wa Vatican kwa kutumia vyanzo mbadala na hii inathibitisha dhamiri ya kuendelea kujikita katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Katika kipindi cha uongozi wake, Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, amebahatika kukutana na kuzungumza na viongozi mbalimbali wa Italia na kwa namna ya pekee anamshukuru Rais Sergio Mattarella. Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Leo XIV nchini Uturuki kuanzia tarehe 27 hadi tarehe 30 Novemba 2025 ilinogeshwa na kauli mbiu: “Bwana mmoja, Imani na Ubatizo Mmoja.” Baba Mtakatifu Leo XIV katika hija hii ya kitume amekazia pamoja na mambo mengine: Umuhimu wa uinjilishaji, Utangazaji na ushuhuda wa Injili yaani “Kerygma” kuhusu: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, chemchemi ya wokovu. Utengano kati ya Wakristo ni kikwazo cha ushuhuda wa Injili ya Kristo Yesu. Huu ni mwaliko kwa Wakristo kutembea kwa pamoja katika hija ya maisha ya kiroho kuelekea Maadhimisho ya Mwaka wa Ukombozi, yaani miaka 2033 ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, huko mjini Yerusalemu.

Jubilei ya Miaka 1700 ya Mtaguso wa NICEA
Jubilei ya Miaka 1700 ya Mtaguso wa NICEA   (ANSA)

Baba Mtakatifu Leo XIV amewashukuru viongozi wote walioshiriki katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 1700 ya Mtaguso Mkuu wa Nicea uliofanyika Asia Ndogo kunako Mwaka 325. Huu ulikuwa ni Mtaguso wa kwanza wa Kiekumene kufanyika katika historia ya Kanisa na hivyo ukaibua imani ambayo ilikamilishwa na Mtaguso wa Kwanza wa Costantinopol ulioadhimishwa Mwaka 381 na hivyo kutoa dira na mwongozo wa imani ya Kanisa kwa Kristo Yesu. Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Leo XIV nchini Lebanon kuanzia tarehe 30 Novemba hadi tarehe 2 Desemba 2025 ilinogeshwa na kauli mbiu “Heri wapatanishi; Maana hao wataitwa wana wa Mungu.” Mt. 5:9. Baba Mtakatifu amewataka watu wa Mungu nchini Lebanon kujikita kikamilifu katika kutafuta na kudumisha haki na amani hata katikati ya mtutu wa bunduki na kwamba, hii ni changamoto endelevu dhidi ya: chuki, kiburi, utawala wa mabavu, utengano na uhasama!Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, alikutana na watu wa Mungu waliosheheni: Imani, matumaini na mapendo, wanaotamani kuona jamii inasimikwa katika haki na mafungamano ya kijamii, changamoto na mwaliko wa kujenga utamaduni wa mshikamano! Mtakatifu Augostino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa alikazia ujenzi wa Mji wa Mungu yaani Yerusalemu ya Mbinguni, au Kanisa na Mji wa Duniani unaosimikwa katika taratibu, sheria na kanuni za kisiasa. Roma, “Caput Mundi” yaani Mji mkuu wa Ulimwengu, ambao nguvu na utukufu wake ulishushwa chini kunako mwaka 410 BK. Huu ni mji uliosimikwa katika kiburi cha kujipenda “Amor sui” uchu wa mali na madaraka, kiasi cha kulumbana na Kanisa, lakini Wakristo walikuwa wanaishi katika mji wa dunia, huku macho yao wakiyaelekeza mbinguni; kwa kujikita katika msingi ya haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi.

Mkataba wa Huduma ya Maisha ya Kiroho kwa Vikosi Vya Ulinzi na Usalama
Mkataba wa Huduma ya Maisha ya Kiroho kwa Vikosi Vya Ulinzi na Usalama   (Vatican Media)

Hii ni changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi; haki, amani na maridhiano; Kwa kukazia utawala wa sheria na Sheria za Kimataifa, unaowawezesha raia wote kuishi kwa amani na utulivu. Umoja wa Mataifa ni matunda ya kiu ya amani kutoka sehemu mbalimbali za dunia; umoja, na mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa; ili kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu! Kumbe kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika umuhimu wa sheria za kimataifa za kibinadamu ili kuziwezesha Serikali kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu msingi wa uhuru, kwa kukuza majadiliano na hivyo kujenga jamii inayosimikwa katika haki na umoja wa familia ya binadamu badala ya kukumbatia sera zinazowagawa walimwengu na matokeo yake ni vita. Kumbe, kuna haja ya kutumia vyema lugha kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu Leo XIV katika hotuba yake amekazia kuhusu haki msingi za binadamu; uhuru wa dhamiri, uhuru wa kidini. Akili ya mwanadamu inatambua uhuru wa dini kama sehemu ya haki msingi za binadamu, inayofumbata, utu na heshima yake. Uhuru wa kidini unapaswa kushuhudiwa katika maisha ya faragha na yale ya hadharani. Hii ni changamoto kubwa katika ulimwengu wa utandawazi, maendeleo ya sayansi na teknolojia. Uhuru wa dini ni nguzo ya haki msingi za binadamu; ni kiiini cha Habari Njema ya Wokovu na ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya binadamu. Uhuru wa kuabudu na kidini unaweza kusaidia kukuza na kudumisha umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu. Hii ni chachu ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa na kwamba, ukweli na uwazi ni kanuni msingi katika majadiliano ya kidini na kiekumene.

Majadiliano ya kidini ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa
Majadiliano ya kidini ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa   (Vatican Media)

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, takribani miaka 60 iliyopita walitoa tamko kuhusu majadiliano ya kidini kwa watu wa nyakati hizi linalojulikana kama “Nostra Aetate." Hili ni tamko linalokazia pamoja na mambo mengine: Dhamana ya Kanisa katika kuhamasisha umoja na upendo kati ya watu wa Mataifa; kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, ili kusimama kidete kutangaza na kushuhudia pamoja utu na heshima ya binadamu. Kanisa Katoliki linatambua mambo ya kweli na matakatifu katika dini mbalimbali, lina heshimu na kuthamini namna yao ya kutenda na kuishi; sheria na mafundisho yao. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanakaza kusema, Kanisa litaendelea kutangaza kwamba: Kristo Yesu ni njia, ukweli na uzima na ambaye ndani mwake mwanadamu anapata utimilifu wa maisha ya utauwa na upatanisho kati yake na Mwenyezi Mungu. Mama Kanisa anawahamasisha watoto wake kuendelea kujikita katika majadiliano ya kidini, ili kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu; ustawi na mafao ya wengi. Kanisa linatambua kwamba, bado kuna changamoto nyingi na vikwazo vya kufanyiwa kazi, lakini hadi hapa linapenda kumshukuru Mungu kwa jiitihada zilizofikiwa. Baba Mtakatifu Leo XIV anasikitika kusema kwamba, Wakristo sehemu mbalimbali za dunia wanaendelea kunyanyaswa na kudhulumiwa kama ilivyo huko Bangladesh, Ukanda wa Sahel, Nigeria na Cabo Delgado, huko Msumbiji.

Wakristo sehemu mbalimbali za dunia wananyanyaswa na kudhulumiwa
Wakristo sehemu mbalimbali za dunia wananyanyaswa na kudhulumiwa   (AFP or licensors)

Kuna haja ya kusimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu. Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, (IOM) kwa mwaka 2026 linaadhimisha kumbukizi ya Miaka 75 tangu kuanzishwa kwake. Sababu nzito zinazopelekea watu kujikuta wanatumbukizwa kwenye biashara haramu ya binadamu na viungo vyake sanjari na mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo ni umaskini wa hali na kipato, unaowawadanganya watu hawa kwamba, watapata fursa za ajira na hivyo kuondokana na hali yao duni. Lakini ukweli wa mambo, wanapofika huko wanakopelekwa, wanajikuta wakiwa wametumbukizwa kwenye biashara ya binadamu na viungo vyake sanjari na utumwa mamboleo kiasi kwamba, hawana tena uwezo wa kurejea nchini mwao. Ni watu wanaotoka katika maeneo ya vita, njaa na magonjwa; watu walioathirika kutokana na mipasuko ya: kiuchumi, kidini, kijamii, hali ngumu ya maisha pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi. Lakini, sababu kubwa zaidi ni watu kufilisika kimaadili na kiutu, kutokana na kuelemewa na uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka na madaraka! Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, utu, heshima na haki msingi za wakimbizi na wahamiaji ni muhimu zikatambuliwa na kuheshimiwa.

Papa Leo XIV: Tunu msingi za maisha ya ndoa na familia zidumishwe
Papa Leo XIV: Tunu msingi za maisha ya ndoa na familia zidumishwe   (@VATICAN MEDIA)

Mama Kanisa katika maisha na utume wake, anapenda kuwahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanakuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na familia, kwa kutangaza na kushuhudia: ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia katika jamii inayotaka kugeuzia kisogo utakatifu wa maisha ya ndoa. Mama Kanisa anatambua kwamba, familia ni Kanisa dogo la nyumbani, ni shule ya utakatifu haki na amani; ni mahali pa kujifunzia fadhila mbalimbali za Kikristo, kiutu na kijamii! Kwa hakika kuna haja ya kuwa na mashuhuda wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, anasema Baba Mtakatifu Leo XIV ili waweze kulielewa na hatimaye, kulipokea pendo la Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Hii ni nguvu inayounganisha, kupatanisha na kuimarisha umoja na mshikamano. Ndoa ya Kikristo inasimikwa katika upendo kati ya Bwana na Bibi, tayari kupokea na kuendeleza zawadi ya maisha; malezi na makuzi ya watoto ambao kimsingi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mungu. Baba Mtakatifu Leo XIV amekemea sana utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera na mikakati ya utoaji mimba pamoja na uzalishaji wa binadamu kwa njia ya chupa “Surrogacy” vitendo vinavyokiuka utu, heshima na haki msingi za watoto kwa kuwageuza kuwa kama “bidhaa.” Kumbe kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika kulinda na kudumisha haki, amani ustawi na maendeleo ya wengi. Amesikitishwa na vita inayoendelea Ukanda wa Gaza kati ya Israeli na Palestina; changamoto ya amani inayoendelea kufuka moshi huko Amerika ya Kusini. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema: Utu, heshima na haki msingi za watu wa Mungu nchini Venezuela zinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, ili hatimaye, kushinda vurugu na kuanza safari ya majadiliano katika: Ukweli, haki na amani; kwa kuheshimu uhuru wa nchi ya Venezuela, Sheria za Kimataifa sanjari na kuhakikisha utawala wa sheria uliowekwa katika Katiba, kuheshimu haki za binadamu na za kiraia za kila mtu, na kufanya kazi kwa umoja, ili hatimaye kuweza kujenga mustakabali tulivu wa ushirikiano kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini wanaoendelea kuteseka kutokana na hali mbaya ya kiuchumi.

Utu, heshima na haki msingi za watu wa Venezuela zilindwe na kuheshimiwa
Utu, heshima na haki msingi za watu wa Venezuela zilindwe na kuheshimiwa   (ANSA)

Mwishoni mwa tamko lake, Baba Mtakatifu Leo XIV aliwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali na kuyakabidhi maombi yao chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria wa Coromoto na ya Watakatifu José Gregorio Hernández na Sr. Carmen Rendiles. Migogoro ya kivita huko Sudan Kongwe na Sudan ya Kusini, Asia ya Mashari, Myanmar na Ukanda wa Maziwa Makuu, ni maeneo yanayohitaji ujasiri wa kutafuta na kukuza Injili ya amani kwa kujikita katika majadiliano katika ukweli na uwazi; Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia, kuishi katika unyenyekevu na ukweli, tayari kuwa na ujasiri wa kusamehe na kusahau. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Leo XIV kwamba, Tamko la Amani kati ya Armenia na Azerbaijan lililotiwa saini mwezi Agosti 2025 litaanza kutekelezwa ili kujenga na kudumisha haki na amani inayodumu. Baba Mtakatifu ameipongeza Vietnam ambayo inaendelea kuboresha mahusiano ya kidiplomasia na Vatican, ili kuliwezesha Kanisa kutekeleza dhamana na utume wake barabara nchini Vietnam. Hatimaye, Baba Mtakatifu amehitimisha hotuba yake kwa kufanya rejea katika Maadhimisho ya Jubilei ya miaka 800 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Francisko wa Assisi, mtu wa amani na majadiliano, aliyejitahidi kuishi ukweli katika hali ya unyenyekevu! Maisha yake yanang'aa kwa mwanga angavu, kwa kuwa yalitiwa msukumo na ujasiri wa kuishi katika ukweli, na ufahamu kwamba ulimwengu wa amani unajengwa kuanzia na mioyo ya unyenyekevu iliyoelekezwa kuelekea mji wa mbinguni.  Moyo mnyenyekevu na wa kupenda amani ndio ambao Baba Mtakatifu Leo XIV anatamani kuuona kwa kila mmoja wao na kwa watu wote wa Mungu; sehemu mbalimbali za dunia mwanzoni mwa Mwaka mpya wa 2026.

Papa Leo XIV Diplomasia ya Vatican

 

09 Januari 2026, 15:52