Baraza La Makardinali: Vipaumbele: Uinjilishaji, Utume, Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Liturujia
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kutangaza na kushuhudia Injili ni dhamana na utume ambao Kristo Yesu amewakabidhi Mitume wake. Huu ni utume wa kwanza unaopaswa kutekelezwa na Mama Kanisa kwa kila mtu na kwa ulimwengu mzima. Utume huu unatekelezwa kikamilifu na Mama Kanisa anapotangaza na kushuhudia Injili ya upendo inayomwilishwa katika huduma makini kwa binadamu wote: kiroho na kimwili. Upendeleo wa pekee ni kwa maskini, wagonjwa na wadhaifu ndani ya jamii. Katika muktadha huu, Kanisa linapaswa kujikita katika: Toba na wongofu wa kimisionari na kichungaji kwa kuwa ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu. Kanisa lijitambulishe na kueleweka kuwa ni Fumbo la Ushirika unaomwilishwa katika dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Makardinali kimsingi ndio washauri wakuu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro ili kukoleza juhudi za toba, haki, amani na maridhiano; kwa kukuza na kudumisha utu na heshima ya binadamu, ili watu waweze kuishi katika mazingira bora zaidi. Ukardinali umegawanyika katika ngazi kuu tatu: Kardinali Askofu, Kardinali Padre na Kardinali Shemasi. Makardinali wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu, kwa kuhakikisha kwamba, imani inamwilishwa katika matendo; daima wakijielekeza zaidi katika huduma kwa watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia. Makardinali wanaojitambulisha kwa mavazi mekundu, wanaitwa kusadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake, tayari kuwashirikisha watu wa Mataifa, ile furaha ya Injili. Ni mwaliko wa huduma makini kwa watu wa Mungu. Makardinali hawa ni wawakilishi wa Mama Kanisa kutoka sehemu mbalimbali za dunia ili hatimaye kushuhudia: Kanisa moja, takatifu, katoliki na la Mitume; kuendeleza umoja wa Kanisa na Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na Makanisa mahalia.
Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanabainisha kwamba kusudi uaskofu uwe na umoja usiogawanyika, Kristo Yesu alimweka Mtakatifu Petro, juu ya mitume wengine, na katika yeye akatia chanzo na msingi unaodumu na unaoonekana wa umoja wa imani na ushirika wa Kanisa. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, kwa nguvu ya Ukatoliki (Catholicitatis) huu kila sehemu huvipeleka vipaji vyake yenyewe kwa sehemu nyingine na kwa Kanisa lote, hivi kwamba sehemu zote pamoja, na kila moja pia, hukithiri kwa kushirikiana zenyewe kwa zenyewe na kufanya juhudi ili kupata ukamilifu katika umoja. Mamlaka kuu ya Kiti cha Mtakatifu Petro imepewa dhamana ya kusimamia ushirika wote wa mapendo, hulinda tofauti za haki zilizopo kwa kukazia ushirika katika mema na huduma makini kwa watu wa Mungu. Rej. Lumen gentium, 13.
Baba Mtakatifu Leo XIV anabeba ndani mwake tasaufi ya Mtakatifu Agostino anayetoa ufunguo wa jinsi ya kutafuta amani, mintarafu diplomasia kwa kujikita katika amani “Ukipenda amani, katika hali yoyote uliyo nayo; wahurumie wale ambao hawapendi kile unachopenda; wahurumie kwa kukosa kile ambacho unacho wewe.” Ni maneno kuntu kutoka kwa Mtakatifu Augostino, mwaliko na changamoto ya watu kuvuka tofauti zao msingi, ili hatimaye kujenga msingi wa majadiliano kati ya watu wa Mataifa, Majadiliano ya kidini na majadiliano kati ya watu wenyewe. Watu wa Mungu wanapaswa kushukuru kwa sayansi ya ugunduzi ambayo inaonesha matunda mengi, lakini pia dunia imeendelea kushuhudia kinzani, migogoro, mipasuko na vita; ukosefu wa usawa unaendelea kupanuka kila kukicha, hali inayoongesha choyo na ubinafsi, changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa. Katika hali na mazingira kama haya, uzoefu na mang’amuzi ya Mama Kanisa ni msaada mkubwa sana kwa Jumuiya ya Kimataifa.
Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Leo XIV ameitisha mkutano wa siku mbili kwa ajili ya Makardinali, yaani kuanzia tarehe 7 Januari hadi tarehe 8 Januari 2026, hizi zimekuwa ni siku za: Sala, Tafakari na Majadiliano ya kina kadiri ya maisha na utume wa Kanisa mintarafu Kristo Yesu; Mwanga na Nuru ya Mataifa. Mama Kanisa anatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Baba Mtakatifu Leo XIV katika hotuba yake ya utangulizi wa Mkutano wa Baraza la Makardinali, Jumatano tarehe 7 Januari 2025 amesema kwamba, Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, katika Kristo Kanisa ni kama Sakramenti au ishara na chombo cha kuwaunganisha watu kiundani na Mungu na kuleta umoja kati ya wanadamu wote. Kumbe Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ulidhamiria kuwaelezea walimwengu maumbile yake na utume ambao ni kwa ajili ya watu wote. Mazingira ya nyakati hizi yanafanya wajibu huu wa Kanisa uwe wa sharti zaidi sasa hivi, ili watu wote wanaozidi kuunganika siku ya leo kwa vifungo vya kijamii, kiteknolojia na kiutamaduni, wapate kuufikia pia umoja kamili ndani ya Kristo Yesu. Rej Lumen gentium, 1.
Kwa hakika Kristo Yesu ni Mwanga na Nuru ya Mataifa, unaowawezesha watu wa Mungu kutembea katika mwanga. Watakatifu Paulo VI na Yohane Paulo II walijisadaka sana katika mchakato wa Uinjilishaji sehemu mbalimbali za dunia, kama tukio muhimu sana la historia ya wokovu. Mababa watakatifu Benedikto XVI na Francisko walikazia kuhusu nguvu ya Kristo inayowavuta watu kumfuata. Hii ni nguvu inayosimikwa katika upendo uliopata hitimisho lake katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu. Nguvu ya upendo wa Mungu imemwilishwa katika maisha na utume wa Kristo Yesu na katika Roho Mtakatifu, zawadi ya Mungu kwa Kanisa, kwa ajili ya kulitakatifuza Kanisa na hivyo kutangaza Habari Njema ya Wokovu. Papa Francisko katika Waraka wake wa Kitume: "Dilexit nos” yaani “Alitupenda” “Juu ya upendo wa kibinadamu na wa Kimungu wa Moyo Mtakatifu wa Yesu Kristo anasema, KristoYesu aliwapenda waja wake upeo na kuwataka kutambua kuwa, hakuna jambo lolote linaloweza kuwatenga na upendo wake, kiasi kwamba aliwaita rafiki zake. Yesu anapenda kuwapatia waja wake upendo na urafiki na kwamba, “alitupenda sisi kwanza na kwamba, upendo wa Kristo Yesu unawawajibisha “Caritas Christi Urget Nos” 2Kor 5:14 na akiisha inuliwa juu ya nchi atawavuta wote kwake. Rej Yn 12:32. Kwa hakika upendo ni kiini cha imani, changamoto na mwaliko kwa Kanisa kujenga na kudumisha umoja unaovutia, tayari kutangaza na kushuhudia nguvu ya upendo wa Kristo Yesu wenye mvuto na unaomwilishwa katika Amri kuu ya Upendo, ushuhuda wa upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu. Kama Makardinali wanaitwa na kutumwa kusimika maisha yao katika majadiliano, ili waweze kufanya kazi kwa pamoja kwa ajili ya huduma kwa Kanisa, huku wakiendelea kukua na kukomaa katika ushirika, kama mfano bora wa ujenzi wa urika wa Maaskofu. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, tayari amekwisha kutana na kuzungumza na baadhi yao ili kupata ushauri unaomwezesha kutekeleza dhamana na wajibu wake wa: kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu.
Makardinali wanaendelea kutafakari kuhusu: Waraka wa Kitume wa Papa Francisko: “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili”, anayetoa kipaumbele cha kwanza kwa furaha ya Injili, kwa kuwaalika waamini kushirikisha furaha yao inayopata chimbuko kutoka katika huruma na upendo wa Mungu kwa wanadamu. Katika mwono huu, Kristo ni kiini cha Injili na kwamba, Kanisa linaalikwa kufanya mageuzi makubwa kama sehemu ya Uinjilishaji Mpya. Waraka wa “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu.” Waraka huu wa kitume unachota utajiri wake katika mapendekezo yaliyotolewa na Mababa wa Sinodi juu ya Uinjilishaji Mpya kama njia ya kutangaza na kushuhudia Imani ya Kikristo katika ulimwengu mamboleo. Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, Liturujia chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Makundi 9 ya Makardinali kutoka katika Makanisa mahalia yatatoa ushauri kwa Baba Mtakatifu na kwamba, yuko tayari kusikiliza ushauri wao, ili kupenda na kuhudumia, tayari kujikita katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Utamaduni wa kusikilizana, kutembea na kufanya kazi kwa pamoja kwa kujikita katika udugu wa kibinadamu na urafiki wa kweli ni mambo yanayoweza kupyaisha maisha na utume wa Kanisa kwa sasa na kwa siku zijazo.
Baba Mtakatifu Leo XIV katika mahubiri yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu aliyoadhimisha pamoja na Baraza la Makardinali, tarehe 8 Januari 2025 kwenye Kanisa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amekazia kuhusu: Umuhimu wa mkutano huu unaowawezesha Makardinali waweze kufanya mang’amuzi ya pamoja, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu, yanayopata chimbuko lake kutoka kwa Kristo Yesu. Baraza la Makardinali, kimsingi ni kielelezo cha Jumuiya ya Sala, ambayo kila Kardinali anachangia kadiri ya uwezo wake ili kupata matunda bora zaidi. Upendo wa Mungu ni ule unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, changamoto na mwaliko kwa wafuasi na mitume wa Kristo Yesu, chimbuko la ushirika ambao Mchumba wa Kristo Yesu anauishi na anataka kuwa ni nyumba na shule kwa jirani zake. Baba Mtakatifu anawaalika Makardinali katika kipindi hiki kujikita katika upendo wa mungu, Kanisa na watu wenye mapenzi mema. Makardinali wahakikishe kwamba, wanazama katika Sala na ukimya; waangaliane na kujadiliana, wakijitahidi kuishi katika hali ya unyenyekevu, ukarimu na kwamba, ni kwa neema ya Mungu wako hapo. Karam ana zawadi mbalimbali walizokirimiwa na Mwenyezi Mungu zinapaswa kuwekezwa kwa tahadhari na ujasiri katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Hii ndiyo ari ambayo Makardinali wanapaswa kuifanyia kazi kwa kushirikiana na wote kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa; chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Mama Kanisa katika maisha na utume wake katika kipindi cha Milenia mbili amejumuisha Fumbo hili katika uzuri wake wenye sura nyingi, ushuhuda unaotolewa na Mkutano wa Makardinali katika asili, zama hizi; katika umoja wa neema na imani, uliowakusanya pamoja na kuwaunganisha kama ndugu wamoja. Binadamu katika ulimwengu mamboleo ana kiu na njaa ya haki na amani; anakabiliwa na majanga mbalimbali; amejikatia tamaa na kwamba, kama Kanisa halina majibu ya moja kwa moja, changamoto na mwaliko kwa Makardinali kushirikiana na kushikamana na Khalifa wa Mtakatifu Petro ili kupata mahitaji msingi ili kuwakirimia wale wanaoomba msaada; kwa kupata baraka ya Mungu, neema na upendo kwa wote, ili kamwe asiwepo mtu anayekosa mahitaji yake msingi. Huduma kwa Kanisa la Kiulimwengu ni zawadi kubwa na kito cha thamani kwa kila Kardinali katika ngazi mbalimbali na kwamba, Baba Mtakatifu Leo XIV ametumia nafasi hii kuwapongeza na kuwashukuru kila mmoja katika utume wao na kwa namna ya pekee katika jukumu la Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu Leo XIV amehitimisha mahubiri yake kwa Baraza la Makardinali kwa mneno ya Mtakatifu Augustino: "Neema nyingi unazotupatia kwa maombi yetu; hata zile tulizopokea kabla ya kuomba ni zawadi kutoka kwako, na hata kukiri kwao baada ya kuzipokea ni zawadi kutoka kwako. Kumbuka, Bwana, kwamba sisi ni mwanadamu; Kwa hivyo tunakuambia: "Toa unachoamuru, na uamuru utakalo.”
Wakati huo huo, Kardinali Timothy Radcliffe, O.P. katika tafakari yake, Jumatano tarehe 7 Januari 2026 amegusia kuhusu muujiza wa Yesu kutembea juu ya maji na jinsi Mitume walivyoshikwa na woga na hatimaye kutulizwa na Kristo Yesu. Rej Mk 6:45-52. Huu ni mwaliko kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro kushirikiana na Kristo Yesu katika kukabiliana na changamoto za dhoruba; Makardinali wanapaswa kubaki ndani ya mashua pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro ili kukabiliana na dhoruba za nyakati hizi na kwamba, Mwenyezi Mungu daima yuko pamoja na kati ya waja wake, hata pale anapoonekana kwamba, hayupo wala haonekani. Makardinali wanapaswa kuanzisha mahusiano ya karibu zaidi na Kristo Yesu, katika maisha na utume wao. Ulimwengu mamboleo una changamoto zake: Vita kuu ya Tatu ya Dunia inayopiganwa vipande vipande; umaskini wa kutupwa, wasiwasi wa maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia na hasa matumizi makubwa ya teknolojia ya akili unde “Artificial Intelligence, AI.” Na kwa upande wa Kanisa: Nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo; migawanyiko ya kiitikadi na kisiasa; mambo yanayohitaji Makardinali kukutana na Kristo Yesu katika maisha na utume wao! Wanahitaji kupata uzoefu na mang’amuzi ya kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka katika maadhimisho ya Mwaka wa liturujia wa Kanisa! Kila mtu anapaswa kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu alivyowalisha watu elfu tano kwa mikate mitano na samaki wawili. Re. Mk 6: 36-44. Kwa njia ya neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu wanaweza kuchangia katika mchakato wa kukabiliana na changamoto mamboleo, jambo la msingi ni kutoifanya mioyo yao kuwa mizito. Rej Mk 6: 52. Wajitahidi kufungua mioyo yao ili kupokea zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu; wajitahidi kufungua mikono yao na masikio yao kwa Mungu na kwa jirani zao!
