Tafuta

Baba Mtakatifu Leo XIV ameitisha Baraza la Makardinali. Ambalo limeanza mkutano wake Jumatano tarehe 7 Januari na unahitimishwa tarehe 8 Januari 2026 Baba Mtakatifu Leo XIV ameitisha Baraza la Makardinali. Ambalo limeanza mkutano wake Jumatano tarehe 7 Januari na unahitimishwa tarehe 8 Januari 2026   (@Vatican Media)

Papa Leo XIV: Baraza la Makardinali Laanza Mkutano Wake Mjini Vatican

Kimsingi, Makardinali katika siku hizi mbili za: Sala, Tafakari, Majadiliano kama sehemu ya ujenzi wa urika wa Maaskofu, zinalenga pamoja na mambo mengine zinalenga kukuza na kudumisha umoja na ushirika, Makardinali wanajadili pamoja na mambo mengine: Kanisa la Kimisionari na Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi; Dhamana na wajibu wa Sekretarieti kuu ya Vatican kwa Makanisa mahalia sanjari na umuhimu wa Liturujia katika maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanabainisha kwamba kusudi uaskofu uwe na umoja usiogawanyika, Kristo Yesu alimweka Mtakatifu Petro, juu ya Mitume wengine, na katika yeye akatia chanzo na msingi unaodumu na unaoonekana wa umoja wa imani na ushirika wa Kanisa. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, kwa nguvu ya Ukatoliki (Catholicitatis) huu kila sehemu huvipeleka vipaji vyake yenyewe kwa sehemu nyingine na kwa Kanisa lote, hivi kwamba, sehemu zote pamoja, na kila moja pia, hukithiri kwa kushirikiana zenyewe kwa zenyewe na kufanya juhudi ili kupata ukamilifu katika umoja. Mamlaka kuu ya Kiti cha Mtakatifu Petro imepewa dhamana ya kusimamia ushirika wote wa mapendo, hulinda tofauti za haki zilizopo kwa kukazia ushirika katika mema na huduma makini kwa watu wa Mungu. Rej. Lumen gentium, 13. Urika wa Maaskofu hauwezi kuwa na mamlaka usipounganika na Baba Mtakatifu, aliye Mwandamizi wa Petro, Mtakatifu na Mtume; kwa nguvu ya wadhifa wake kama Wakili wa Kristo na Mchungaji wa Kanisa lote, ana mamlaka katika Kanisa, iliyo kamili, ya juu kabisa na iwahusuyo wote (plenam, supremama et universalem potestatem) ambayo anaweza kuyatimiza kwa uhuru. Urika wa Maaskofu ni urithi wa urika wa Mitume katika kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Rej. Lumen gentium, 22-27. Baba Mtakatifu Leo XIV ameitisha Baraza la Makardinali, ambalo limeanza mkutano wake Jumatano tarehe 7 Januari na unahitimishwa tarehe 8 Januari 2026 kwa Ibada ya Misa Takatifu. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna Makardinali 245 kutoka sehemu mbalimbali za dunia na kati yao kuna Makardinali 122 wenye haki ya kupiga na kupigiwa kura na wengine 123 hawana haki tena ya kupiga wala kupigiwa kura wakati wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Baraza la Makardinali limeanza mkutano wake wa kawaida
Baraza la Makardinali limeanza mkutano wake wa kawaida   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wa Kitume “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili”, anatoa kipaumbele cha kwanza kwa furaha ya Injili, kwa kuwaalika waamini kushirikisha furaha yao inayopata chimbuko kutoka katika huruma na upendo wa Mungu kwa wanadamu. Katika mwono huu, Kristo ni kiini cha Injili na kwamba, Kanisa linaalikwa kufanya mageuzi makubwa kama sehemu ya Uinjilishaji Mpya. Waraka huu ni ramani inayotoa dira na mwongozo thabiti wa shughuli za kichungaji unaopaswa kutekelezwa na Mama Kanisa kwa sasa na kwa siku za usoni kwa kuwa na mwono wa kinabii na mwelekeo chanya, licha ya vikwazo na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika maisha na utume wa Kanisa, ili Kristo Mfufuka aendelee kupeperusha bendera ya ushindi. Kutangaza na kushuhudia Injili ni dhamana na utume ambao Kristo Yesu amewakabidhi Mitume wake. Huu ni utume wa kwanza unaopaswa kutekelezwa na Mama Kanisa kwa kila mtu na kwa ulimwengu mzima. Utume huu unatekelezwa kikamilifu na Mama Kanisa anapotangaza na kushuhudia Injili ya upendo inayomwilishwa katika huduma makini kwa binadamu wote: kiroho na kimwili. Upendeleo wa pekee ni kwa maskini, wagonjwa na wadhaifu ndani ya jamii. Katika muktadha huu, Kanisa linapaswa kujikita katika wongofu wa kimisionari, kwa kuwa ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu. Kanisa lijitambulishe na kueleweka kuwa ni Fumbo la Ushirika unaomwilishwa katika dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa.

Baraza la Makardinali ni chombo kikuu cha ushauri kwa Khalifa wa Mt. Petro
Baraza la Makardinali ni chombo kikuu cha ushauri kwa Khalifa wa Mt. Petro   (Vatican Media)

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 19 Machi 2022, Sherehe ya Mtakatifu Yosefu Mume wake Bikira Maria, aliridhia kuchapishwa kwa Katiba mpya ya Kitume inayojulikana kama “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu.” Waraka huu wa kitume unachota utajiri wake katika mapendekezo yaliyotolewa na Mababa wa Sinodi juu ya Uinjilishaji Mpya kama njia ya kutangaza na kushuhudia Imani ya Kikristo katika ulimwengu mamboleo. Kimsingi, Makardinali katika siku hizi mbili za: Sala, Tafakari, Majadiliano kama sehemu ya ujenzi wa urika wa Maaskofu, ili kukuza na kudumisha umoja na ushirika, Makardinali wanajadili pamoja na mambo mengine: Kanisa la Kimisionari na Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi; Dhamana na wajibu wa Sekretarieti kuu ya Vatican kwa Makanisa mahalia sanjari na umuhimu wa Liturujia katika maisha na utume wa Kanisa.Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanafafanua nafasi ya Liturujia katika fumbo la Kanisa kwa kusema kwamba, maana kwa njia ya Liturujia, hasa Sadaka takatifu ya Ekaristi, “latimizwa tendo la ukombozi wetu.”

Umuhimu wa liturujia Katika Maisha na Utume wa Kanisa
Umuhimu wa liturujia Katika Maisha na Utume wa Kanisa   (@Vatican Media)

Liturujia inasaidia kikamilifu waamini waoneshe katika maisha yao na kuwadhihirishia wengine fumbo la Kristo na pia maumbile halisi ya Kanisa la kweli. Kanisa kwa undani kabisa ni la kibinadamu na pia la kimungu, linaloonekana lakini lenye mambo yasiyoonekana ndani yake, lenye bidii kubwa katika matendo na uradhi katika kutafakari, lililopo ulimwenguni lakini kama mwenye kuhiji. Hayo yote yamo ili yale ya kibinadamu ndani yake yaelekezwe kwa yale ya kimungu, yaonekanayo kwa yasiyoonekana, matendo kwenye kutafakari, yaliyopo yaelekee mji ujao tunakoelekea. Hivyo Liturujia kila siku inawajenga wale waliomo katika Kanisa wawe hekalu takatifu la Bwana, makao ya Mungu katika Roho, mpaka kuufikia utimilifu wa Kristo.  Wakati huohuo kwa namna ya ajabu Liturujia inaimarisha nguvu za waamini kumhubiri na kumshuhudia Kristo Yesu; na kwa njia hiyo inawaonesha wale walio nje [nalo,] Kanisa lililo ishara iliyoinuliwa juu kati ya mataifa, ambayo chini yake watoto wa Mungu waliotawanyika wakusanyika katika umoja mpaka liwepo zizi moja chini ya mchungaji mmoja. Rej. SC, 2.

Baraza la Makardinali
07 Januari 2026, 17:08