Papa Leo XIV Asikitishwa na Ajali ya Treni Nchini Hispania: 41 Wamefariki Dunia
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Oscar Puente, Waziri wa Uchukuzi wa Hispania, zaidi ya watu 41 wamefariki dunia na wengine zaidi 152 wamejeruhiwa na kwamba watu 24 wana hali mbaya zaidi. Wengine wanaendelea kupatia tiba. Ajali hiyo ilitokea Dominika 18 Januari 2026 karibu na mji wa Adamuz, eneo ambalo liko karibu na Jiji la Cordoba, nchini Hispania wakati treni ya mwendokasi iliyokuwa ikisafiri kutoka Malaga kuelekea Madrid, ikiwa na abiria 317 ilipoacha njia na kuvuka upande wa pili wa reli na hivyo kugongana uso kwa uso na treni nyingine iliyokuwa imebeba abiria 200. Taarifa zinaonesha kwamba, hadi kufikia Jumanne tarehe 20 Januari 2026 watu 43 walikuwa hawajulikani mahali walipo! Hispania imetangaza siku tatu za maombolezo.
Baba Mtakatifu Leo XIV katika salam zake za rambirambi zilizoandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, kwenda kwa Askofu mkuu Luis Javier Argüello García, wa Jimbo kuu la Valladolid ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania anasema, amesikitishwa sana na taarifa ya ajali ya treni iliyotokea Dominika tarehe 18 Januari 2026. Anawaombea marehemu wote waweze kupata pumziko la milele; majeruhi wafarijike na kupona mapema, ili waweze kuendelea na shughuli zao za kila siku. Kikosi cha uokoaji kiendelee kutoa huduma na msaada kwa waathirika. Mwishoni, Baba Mtakatifu Leo XIV akawapatia baraka zake za kitume.
