Papa Leo XIV Anafuatilia Kwa Umakini Hali Tete Nchini Venezuela
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Rais wa Venezuela, Nicolás Maduro, na mkewe, Cilia Flores, Jumamosi tarehe 3 Januari 2026 wamekamatwa na Marekani baada ya shambulio kubwa la kijeshi nchini humo. Rais Donald Trump wa Marekani amesema kuwa operesheni hii ilifanywa kwa ushirikiano na vyombo vya sheria vya Marekani na kwamba, Maduro na mke wake wamehamishiwa nchini Marekani ili kujibu tuhuma zinazowakabili. Waziri wa Ulinzi wa Venezuela Vladimir Padrino López, amesema shambulio hilo limeyakumba maeneo ya raia na kwamba Serikali inaendelea kukusanya taarifa kuhusu waliopoteza maisha na waliojeruhiwa. Serikali pia imetangaza hali ya hatari Kitaifa na kudai shambulio hilo ni jaribio la Marekani kudhoofisha uhuru wa kisiasa wa Venezuela na kudhibiti rasilimali zake, hasa nishati ya mafuta na madini. Taarifa za awali zinaonesha kwamba, katika shambulizi hili walau kuna watu 40 wamepoteza maisha.
Ni katika muktadha wa shambulio kubwa la jeshi la Marekani nchini Venezuela, Baba Mtakatifu Leo XIV baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Dominika tarehe 4 Januari 2026 alisema kwamba, anafuatilia kwa karibu sana yale yanayoendelea kujiri nchini Venezuela. Anasema: Utu, heshima na haki msingi za watu wa Mungu nchini Venezuela zinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, ili hatimaye, kushinda vurugu na kuanza safari ya majadiliano katika haki na amani; kwa kuheshimu uhuru wa nchi ya Venezuela, kuhakikisha utawala wa sheria uliowekwa katika Katiba, kuheshimu haki za binadamu na za kiraia za kila mtu, na kufanya kazi kwa umoja, ili hatimaye kuweza kujenga mustakabali tulivu wa ushirikiano kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini wanaoendelea kuteseka kutokana na hali mbaya ya kiuchumi. Mwishoni mwa tamko lake, Baba Mtakatifu Leo XIV aliwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali na kuyakabidhi maombi yao chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria wa Coromoto na ya Watakatifu José Gregorio Hernández na Sr. Carmen Rendiles. Mwishoni, Baba Mtakatifu Leo XIV amewaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema wawe na imani kwa Mungu wa imani; watu waoneshe mshikamano wa kidugu na watu wanaoteseka kutoka na vita, kinzani na mipasuko ya kijamii.
Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Venezuela (CEV) ni chombo cha kudumu cha Maaskofu Katoliki nchini Venezuela kilichoundwa kutekeleza majukumu ya shughuli za kichungaji kwa ushirikiano, kuendeleza utume wa Kanisa, na kushughulikia masuala ya kitaifa, mara nyingi wakijikita katika kusimamia: haki msingi za binadamu, mgogoro wa kijamii, majadiliano, kinzani na migogoro ya kisiasa. Baraza la Maaskofu wa Venezuela (CEV) “The Venezuelan Episcopal Conference (CEV)” katika kipindi hiki kigumu cha maisha na historia ya nchi yao, wanawaomba watu wa Mungu nchini humo kuwa na utulivu, hekima na nguvu ya kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo. Wanawaomba wananchi wa Venezuela kuonesha mshikamano wa udugu wa kibinadamu na wale wote walioathirika pamoja na wale ambao wamewapoteza ndugu zao na kwamba, waendelee kusali kwa ajili ya umoja wa watu wa Mungu nchini Venezuela. Wanawaomba wazidi kusali kwa ajili ya amani inayopata chimbuko lake kutoka katika undani wa nyoyo zao, wakatae vurugu; Watu wajitahidi kukutana na kusaidiana kwa hali na mali na kwamba, maamuzi yatakayofanywa, yafanywe kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Venezuela. Bikira Maria wa Coromoto, Mwombezi na Msimamizi wa Venezuela, awasindikize katika hija ya maisha yao katika kipindi hiki kigumu!
Serikali ya Marekani inamshutumu Rais Maduro kwa kuhusika katika usafirishaji wa dawa za kulevya nchini humo, haswa “fentanyl na kokeni” na kumtuhumu kuwa kiongozi na mshirika mkubwa wa watuhumiwa wakubwa wa dawa za kulevya nchini humo, “Cartel de los Soles.” Aidha Rais Trump amemshutumu Maduro kwa kuhusika na kuingiza maelfu ya wakimbizi wa Venezuela nchini Marekani, ambao kwa sasa ni zaidi ya watu milioni nane, tangu mwaka 2013 Maduro alipoingia madarakani. Rais Maduro amepinga vikali tuhuma hizi, akisema Marekani inatumia "vita dhidi ya dawa za kulevya" kama kisingizio cha kumng'oa madarakani, ili kudhibiti rasilimali kubwa ya nishati ya mafuta kutoka Venezuela.
