Papa Leo XIV Akutana na Ujumbe wa Kiekumene Kutoka Finland: Ubatizo Mmoja!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mama Kanisa anasema uekumene wa damu unajikita katika: Vita, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo sehemu mbalimbali za dunia. Lakini, ikumbukwe kwamba, damu ya mashuhuda hawa wa imani ni chachu na mbegu ya Ukristo. Uekumene wa maisha ya kiroho na utakatifu wa maisha unafumbatwa katika toba na wongofu wa ndani; kwa kujikana na kujivika fadhila ya unyenyekevu; moyo wa ukarimu na udugu wa kibinadamu; upole, uvumilivu na kutumikia bila ya kujibakiza. Wakristo wanakumbushwa kwamba, kadiri wanavyojitahidi kuishi maisha matakatifu mintarafu tunu msingi za Kiinjili, ni kwa kadiri ileile watahamasishana kutekeleza umoja wa Wakristo na udugu wa kibinadamu kati yao. Uekumene wa huduma unatekelezwa kwa njia ya sera na mikakati ya shughuli za kichungaji sanjari na maisha ya kitume. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Leo XIV Jumatatu tarehe 19 Januari 2026 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa kiekumene kutoka nchini Finland wanaohiji mjini Roma, kama sehemu ya maadhimisho ya Sikukuu ya Mtakatifu Henric, Msimamizi na Mwombezi wa Finland inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 19 Januari. Ujumbe wa kiekumene kutoka Finland umeongozwa na Askofu mkuu Tapio Luoma wa Jimbo kuu la Turku, linaloadhimisha Kumbukizi ya Miaka 750 tangu kuanzishwa kwake. Mtakatifu Enric, Msimamizi na Mwombezi wa Finland ni mjumbe na chombo cha amani, aliyekazia umuhimu wa kuombea amani duniani; ni kielelezo cha ushirika, zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, maadhimisho ya sikukuu yake, yawe ni kikolezo cha umoja na ushirika wa Wakristo wote, ili kwa pamoja waweze kumtukuza Mwenyezi Mungu.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema: Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo kwa Mwaka 2026 linalonogeshwa na kauli mbiu: “Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu.” Efe 4:4. Mama Kanisa anakiri na kuungama juu ya: “Ubatizo mmoja kwa maondoleo ya dhambi.” Kanuni ya Imani ya Nicea-Constantinopoli ni formula rasmi ambayo ilipitishwa na Mababa wa Mtaguso wa Kwanza wa Nicea (325) ikakamilishwa na Mtaguso wa kwanza wa Konstantinopoli (381) ili kubainisha imani sahihi ya Kanisa Katoliki dhidi ya uzushi, hasa wa Ario na wafuasi wake. Katika mazingira hayo, lengo kuu lilikuwa kwanza kabisa ni kumkiri Kristo Yesu “Mungu kweli kwa Mungu kweli” yaani Mungu kweli sawa na Baba, halafu kwamba: Roho Mtakatifu anastahili kuabudiwa pamoja na Baba na Mwana (Utatu Mtakatifu). Wakristo wanataka kutembea pamoja na Kristo Yesu ambaye ni njia, ukweli na uzima. Hiki ni kielelezo cha imani na ukweli ambao ni Kristo Yesu mwenyewe. Huu ni ukweli uliofanyika mwili.
Na Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kiri hii ya imani ni kiini cha umoja na udugu wa Kikristo! Wakristo wanahimizwa kuwa ni vyombo na wajumbe wa Injili ya matumaini; na mwanga wa Mataifa, ili kufukuza giza sehemu mbalimbali za dunia. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Makanisa yamefunga tayari Malango ya Jubilei ya Matumaini, kama hitimisho la Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo. Lakini Kristo Yesu ni Lango la Matumaini kwa waja wake, ataendelea kubaki akiwa anaambatana na watu wake; ni Lango linalowapeleka watu wa Mungu katika maisha ya Kimungu. Matumaini ya Kikristo hayana ukomo. Kwa kukutana na kuimarishwa na neema na baraka kutoka kwa Kristo Yesu, Wakristo wanaitwa na kutumwa kuwa ni mashuhuda wa ukweli unaookoa na maneno yanayojenga kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu anawapongeza Wakristo kutoka Finland, nchi ambayo ni mfano bora wa kuigwa katika majadiliano ya kiekumene, kwani Makanisa nchini humo yanajipambanua kwa kuragibisha utamaduni wa: matumaini, utu wa binadamu na huruma.
Itakumbukwa kwamba, Huduma Shufaa (Palliative Care) ni huduma zinazotolewa kwa watu wanaougua magonjwa mazito, kwa lengo la kutoa unafuu kutokana na maumivu na matatizo mengine, na hivyo kuongeza ubora wa maisha kwa mgonjwa na familia yake, kwa kujikita katika Injili ya: Upendo, huruma, na heshima kwa utu wa binadamu. Hizi ni huduma za kimatibabu, kisaikolojia, kijamii, na maisha ya kiroho, zinazotolewa kuanzia utambuzi wa ugonjwa hadi mwisho wa maisha, na huleta matumaini na faraja kwa mgonjwa na familia yake. Baba Mtakatifu Leo XIV anayapongeza Makanisa nchini Finland kwa hatua kubwa ya kiekumene, inayolenga pamoja na mambo mengine: kuadhimisha pamoja Sikukuu ya Mtakatifu Enric, Msimamizi na Mwombezi wa Finland, sanjari na kukoleza utekelezaji wa Majadiliano ya Kiekumene kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiinjili la Kiluteri nchini Finland na kwamba, Kanisa Katoliki litaweza kushirikisha uzoefu na mang’amuzi yake katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Baba Mtakatifu Leo XIV anawataka Wakristo kutoka Finland kuwa ni mashuhuda wa matumaini na kwamba, waendelee kuimarishwa kwa maombezi ya Watakatifu Petro, Paul na Mtakatifu Enric. Mwishoni, amewapatia baraka zake za kitume na kwa pamoja wakasali Sala ya Baba Yetu.
Wakati huo huo, Askofu Tapio Luoma, wa Jimbo Katoliki Turku amemwelezea Baba Mtakatifu Leo XIV kwamba, Jimbo lake, linaadhimisha Jubilei ya Miaka 750 tangu kuanzishwa kwake; umuhimu wa uongozi katika kulinda na kutunza mali ya Kanisa pamoja na kusimamia kwa uaminifu uteuzi wa Maaskofu mahalia. Hili ni Jimbo ambalo limekuwa ni kitovu cha elimu na utamaduni nchini Finland na kwamba, limesaidia sana katika mchakato wa kutamadunisha Injili ili kuinjilisha tamaduni mintarafu tunu msingi za Kiinjili. Juhudi zote hizi hazina budi kwenda sanjari na majadiliano ya kidini na kiekumene kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji yam tu mzima kiroho na kimwili. Kama Kanisa mahalia lina dhamana na wajibu wa kutafuta na kudumisha amani na majadiliano na mwishoni, wametumia fursa hii, kumkaribisha Baba Mtakatifu Leo XIV nchini Finland, panapo majaliwa.
