Tafuta

Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwaombea waathirika wa mafuriko Kusini mwa Afrika na amekumbushia pia madhila makubwa wanayopitia wananchi walioko Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC. Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwaombea waathirika wa mafuriko Kusini mwa Afrika na amekumbushia pia madhila makubwa wanayopitia wananchi walioko Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC. 

Papa Leo XIV Awakumbuka Waathirika wa Mafuriko Kusini Mwa Afrika

Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwaombea waathirika wa mafuriko Kusini mwa Afrika na amekumbushia pia madhila makubwa wanayopitia wananchi walioko Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC wanaolazimika kuikimbia nchi yao na hivyo kujitafutia: hifadhi na usalama nchini Burundi kutokana na ghasia na vita inayoendelea nchini humo na kwamba, hili ni janga kubwa la kibinadamu. Papa anakazia: Majadiliano, Upatanisho na Amani ya Kudumu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mafuriko Kusini mwa Afrika yamesababisha: vifo, uharibifu wa miundombinu, kukatika kwa mawasiliano, kufungwa kwa vivutio vya kitalii kama Hifadhi ya Kruger, na uhamisho wa watu, huku serikali zikihamasisha uokoaji na ukarabati wa huduma za jamii, na mamlaka za hali ya hewa zikitoa tahadhari. Athari hizi ni pamoja na adha ya usafiri, hasara za kiuchumi, na mahitaji ya haraka ya huduma za dharura. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Leo XIV mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 18 Januari 2026, aliwakumbuka na kuwaombea waathirika wa mafuriko Kusini mwa Afrika. Baba Mtakatifu Leo XIV amekumbushia pia madhila makubwa wanayopitia wananchi walioko Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC wanaolazimika kuikimbia nchi yao na hivyo kujitafutia: hifadhi na usalama nchini Burundi kutokana na ghasia na vita inayoendelea nchini humo na kwamba, hili ni janga kubwa la kibinadamu. Baba Mtakatifu anakazia pamoja na mambo mengine, umuhimu wa pande zote zinazohusika kujikita katika majadiliano, upatanisho na amani ya kweli na ya kudumu.

Papa Leo XIV amewakumbuka na kuwaombea waathirika wa Mafuriko
Papa Leo XIV amewakumbuka na kuwaombea waathirika wa Mafuriko

Wakati huo huo, Askofu mkuu João Carlos Hatoa Nunes wa Jimbo kuu la Maputo nchini Msumbiji anasema, mafuriko yaliyotokea hivi karibuni nchini Msumbiji yamesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Kuna watu ambao wamewapoteza wapendwa wao. Wote hawa anapenda kuwakabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa matumaini na faraja, ili aweze kuwafariji wale wanaomboleza, kuwatia shime wale waliopoteza mali zao na aendelee kuwategemeza waathirika. Kimsingi mafuriko ni jambo la kawaida, lakini linatoa changamoto kwa mtu binafsi, jumuiya na jamii katika ujumla wake, kuhakikisha kwamba, kila mtu anawajibika katika kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Mwenyezi Mungu anaendelea kuzungumza na waja wake kupitia kilio cha Maskini na Dunia Mama na kwamba, kupuuza sauti hii kuna madhara yake makubwa katika maisha ya watu.

Waathirika wa Mafuriko Kusini mwa Afrika
Waathirika wa Mafuriko Kusini mwa Afrika   (ANSA)

Askofu mkuu João Carlos Hatoa Nunes anasema, huu si wakati wa kunyoosheana vidole, kwa kutupiana shutuma na lawama, bali ni wakati muafaka wa kuhakikisha kwamba, imani inamwilishwa katika matendo ya huruma, kama kielelezo halisi cha upendo na mshikamano wa kibinadamu. Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Jimbo kuu la Maputo, Caritas Maputo, linaendelea kukusanya misaada ili hatimaye, kuwagawia waathirika, ili kupunguza makali ya maisha. Kila mtu anaweza kuchangia hata kama ni kidogo, kwani haba na haba hujaza kibaba. Huu ni wakati wa kujenga upya makazi, lakini zaidi ni wakati muafaka wa kupyaisha mahusiano, mafungamano na majukumu kwa kuwa tayari kusikiliza kwa makini na hivyo kuunga mkono jitihada hizi zinazopania kuleta nafauu kwa waathirika. Askofu mkuu João Carlos Hatoa Nunes anasema, huu ni wakati muafaka wa kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya udugu wa kibinadamu, kwa kujizatiti katika ulinzi na utunzaji wa mazingira nyumba ya wote.

Papa Maafa Kusini Mwa Afrika
20 Januari 2026, 15:09