Tafuta

Tarehe 3 Januari 2026 Askofu mkuu Chaves  ametangaza kuzinduliwa kwa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 800 tangu Kanisa kuu la Jimbo kuu la Toledo lilipozinduliwa kunako mwaka 1226 . Tarehe 3 Januari 2026 Askofu mkuu Chaves ametangaza kuzinduliwa kwa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 800 tangu Kanisa kuu la Jimbo kuu la Toledo lilipozinduliwa kunako mwaka 1226 . 

Papa Leo XIV: Jubilei ya Miaka 800 ya Kanisa Kuu la Toledo, Hispania:1226-2026

Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 800 tangu kuanzishwa kwa Kanisa kuu la Jimbo kuu la Toledo, anasema: ni matumaini yake kwamba, maadhimisho ya Jubilei hii ni muda muafaka wa kukimbilia na kuambata neema; toba, wongofu wa ndani na msamaha wa dhambi, ili kukumbatia huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka. Jiwe la msingi la ujenzi wa Kanisa hili liliwekwa kunako mwaka 1226! Iweni Mawe Hai!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kanisa kuu ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa Katoliki kama Kanisa kuu la Jimbo husika linamo kaa kiti cha Askofu kinachoashiria mamlaka yake ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Hili ni Kanisa linalotumika kama moyo wa maisha ya kiroho; kitovu cha maadhimisho ya Mafumbo makuu ya Kanisa, kama vile Upadrisho au watawa kuwekwa wakfu. Hiki ni kitovu cha maisha ya Kanisa mahalia na yale ya kijamii; ni hazina ya kihistoria ya imani, sanaa, na utamaduni. Hii ni Parokia kuu inayounganisha Parokia zote za Jimbo husika! Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema, Jubilei ni kipindi cha kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini. Ni wakati muafaka wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema na baraka anazowakirimia waja wake hata bila mastahili yao. Ni muda wa kufanya toba na kuomba msamaha kwa mapungufu yote yaliyojitokeza katika maisha na utume, tayari kuomba tena neema na baraka ya kusonga mbele kwa imani mapendo na matumaini zaidi. Askofu mkuu Francisco Cerro Chaves wa Jimbo kuu la Toledo, “Archidioecesis Metropolitae Toletana” lililoko nchini Hispania, tarehe 3 Januari 2026 ametangaza kuzinduliwa kwa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 800 tangu Kanisa kuu la Jimbo kuu la Toledo lilipozinduliwa kunako mwaka 1226 na limekuwa na mchango mkubwa katika historia ya Hispania, Ulaya na Amerika ya Kusini.

Jubilei ya Miaka 800 ya Kanisa Kuu la Toledo, Hispania
Jubilei ya Miaka 800 ya Kanisa Kuu la Toledo, Hispania

Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 800 tangu kuanzishwa kwa Kanisa kuu la Jimbo kuu la Toledo, anasema: ni matumaini yake kwamba, maadhimisho ya Jubilei hii ni muda muafaka wa kukimbilia na kuambata neema; toba, wongofu wa ndani na msamaha wa dhambi, ili kukumbatia huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka.Ilikuwa ni Mwaka 1226, miaka 800 iliyopita Askofu mkuu Rodrigo Jiménez de Rada pamoja na Mfalme Ferdinando III walipoweka Jiwe la msingi la ujenzi wa Kanisa kuu la Jimbo kuu la Toledo, nchini Hispania. Ujenzi wa Kanisa hili umechangia kwa kiasi kikubwa katika mchakato wa uinjilishaji wa dunia mpya, mchango ambao umeacha chapa ya kudumu katika historia na sanaa ya watu wa Mungu nchini Hispania, mintarafu Hekalu hili kuu. Kanisa hili katika Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 800 tangu lilipoanzishwa, ni fursa kwa Mama Kanisa kuadhimisha matukio mbalimbali ya Kiliturujia na kitamaduni; amana na utajiri wa maisha ya kiroho wa Kanisa hili mahalia, chemchemi ya matumaini kwa siku za usoni. Baba Mtakatifu Leo XIV amewakumbusha na kuwashukuru watu wa Mungu nchini Hispania kwa maadhimisho ya Liturujia ya “Hispano-Mozarabic,” inayoadhimishwa kila siku katika Hekalu hili na hivyo kuwafanya kuwa kama “mawe hai.” Katika kipindi chote cha miaka 800 waamini wamesimama kidete kulinda na kudumisha imani na ushirika na Khalifa wa Mtakatifu Petro na kwamba, huu ni ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo na amejifunua kwa walimwengu kwa njia ya Mtoto mchanga, Kristo Yesu aliyelazwa katika hori ya kulia wanyama.

Papa Leo XIV: Kanisa halina budi kuonesha upendeleo kwa maskini.
Papa Leo XIV: Kanisa halina budi kuonesha upendeleo kwa maskini.   (@Vatican Media)

Upendeleo wa Mungu kwa maskini ni kielelezo cha huruma ya Mungu kwa maskini na binadamu dhaifu anayesubiri kufunguliwa kwa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika haki, udugu wa kibinadamu na mshikamano na kwamba, maskini wanayo nafasi ya pekee katika moyo wa Mungu, mwaliko kwa Mama Kanisa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wale wote wanaonyanyaswa na kudhulumiwa. Kimsingi, historia nzima ya ukombozi inasimikwa katika uwepo wa maskini kama inavyojionesha kwenye historia ya Fumbo la Umwilisho na katika maisha.Ni Masiha maskini na kwa ajili ya maskini, aliyetumwa na Baba yake wa mbinguni kuwatangazia maskini Habari Njema. Katika Agano la Kale, umaskini ulifungamanishwa na dhambi binafsi, lakini Kristo Yesu katika Agano Jipya anaonesha kwamba, maskini wana nafasi ya pekee miongoni mwa watu wa Mungu. Kimsingi, huruma kwa maskini imeoneshwa kwa kina katika Maandiko Matakatifu na kwamba, Mungu ni upendo ndiyo maana Mama Kanisa anakazia matendo ya huruma: kiroho na kimwili na kama Kristo Yesu anavyobainisha kwenye Heri za Mlimani, muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu na kwamba, hiki ni kielelezo cha imani tendaji kama Mwinjili Luka anavyosimulia katika Kitabu cha Matendo ya Mitume.

Kanisa hili ni chemchemi ya imani, matumaini na mapendo
Kanisa hili ni chemchemi ya imani, matumaini na mapendo

Upendo kwa maskini ni ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo, mwaliko kwa waamini kuiga mfano huu mzuri, utakao zaa utajiri mkubwa. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika watu wa Mungu Jimbo kuu la Toledo nchini Hispania kusoma alama za nyakati, tayari kutambua mifumo mipya ya umaskini wa hali na kipato na kwamba, katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 800 tangu kuanzishwa kwa Kanisa kuu la Jimbo kuu la Toledo, maskini wa hali na mali wapewe kipaumbele na kwamba, hii ni chemchemi, amana na utajiri wa Kanisa. Mwishoni mwa ujumbe wake, Baba Mtakatifu Leo XIV anawashukuru na kuwapongeza watu wa Mungu jimboni humo, kwa kuendelea kulipyaisha Kanisa linalosafiri na kwamba, anaendelea kuwakumbuka na kuwaombea. Na hatimaye, akawaweka nchini ya ulinzi na maombezi ya Bikira Maria wa Tabernakulo: “Virgen del Sagrario” Msimamizi na mwombezi wao!

Jubilei Miaka 800
05 Januari 2026, 10:20