Tafuta

Papa anajibu swali. Papa anajibu swali.  (@Vatican Media)

Papa:Katika Kanisa,tatizo si idadi bali ni kuhisi Kanisa

Katika jarida la mwezi Januari la "Piazza San Pietro,"Papa Leo XIV anajibu barua kutoka kwa Katekista wa Uswiss ambaye anaandika:"Ninapanda,lakini miche inajitahidi kukua.Watoto na familia wanapendelea michezo na sherehe."Papa alijibu:"Saa zilizotengwa kwa katekista hazipotezwi kamwe hata kama washiriki ni wachache sana.Tatizo ni ukosefu wa ufahamu katika kujihisi Kanisa."

Vatican News

Toleo la Januari 2026 la Jarida la 'Piazza San Pietro,' yaani la 'Uwanja wa Mtakatifu Petro' lililojitolea kikamilifu kwa mada ya amani, linaanza, kama kawaida, kwa hotuba ya Papa Leo XIV. Mwezi wa Januari, Papa anamjibu msomaji: Nunzia, Katekista wa Uswiss anayeishi Laufenburg, mji mdogo wenye wakazi 620. "Mimi hupanda, lakini miche inajitahidi kukua. Watoto na familia wanapendelea michezo na sherehe," anaandika mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 50, akisimulia kwa shauku kujitolea kwake kwa miongo kadhaa kwa Katekista, kuanzia Komunio ya Kwanza hadi Kipaimara.

Katika barua yake, lakini analaani ukweli mgumu: "Hapa Uswiss, ni vigumu kuwafanya wazazi na, wakati mwingine, hata watoto na vijana wamtegemee Mungu." Familia hazipo mara nyingi na mara nyingi hazijali desturi za kidini; Watoto wanavutiwa na michezo, muziki, simu ya mikononi na sherehe, badala ya imani; Dominika  zenye makanisa yasiyo na watu wengi, yanayohudhuriwa hasa na wazee; mapambano ya kila siku ya "kupanda" katika wakati ardhi inaonekana tasa: hii ndiyo picha iliyochorwa na Katekista wa Uswiss. Akiwa amevunjika moyo, anarudia ahadi yake: "Ninajaribu kupanda, na  miche inajitahidi kukua." Na anamwomba Papa awaombee vijana waliokabidhiwa uangalizi wake na kwa ajili yake mwenyewe, ili asipoteze ujasiri wa kuendelea.

Jibu la Papa Leo XIV

Kutoka kwenye kurasa za Uwanja wa Mtakatifu Petro, zinazoratibiwa  na Padre Enzo Fortunato, Papa Leo XIV anashughulikia wasiwasi wa Nunzia na kuuweka ndani ya muktadha wa Ulaya: "Hali unayoishi si tofauti na ile ya nchi zingine za Kikristo za kale." Papa Leo XIV anatualika tuangalie zaidi ya takwimu za ushiriki: "Saa zilizotengwa kwa ajili ya Katekesi  hazipotezwi kamwe, hata kama washiriki ni wachache sana." Na anaibua changamoto ya kikanisa: "Tatizo si namba, ambazo, hakika, hutoa utulivu, bali ni ukosefu unaozidi kuonekana wa ufahamu wa hisia zetu za kuwa Kanisa, yaani, viungo hai vya Mwili wa Kristo, vyote vikiwa na karama na majukumu ya kipekee, na si wapokeaji wa sakramenti takatifu, labda kutokana na mazoea tu."

Kwa Nunzia na kwa wale wanaopitia magumu yaleyale Papa anaonesha njia: "Kama Wakristo, tunahitaji uongofu kila wakati. Na lazima tuutafute pamoja." Na anakumbusha kwamba mlango wa kweli wa imani "ni Moyo wa Kristo, ambao daima uko wazi." Wito wa mwisho wa Papa umejikita katika urithi wa Papa Paulo VI kuwa: "Tunachoweza kufanya ni kushuhudia furaha ya Injili ya Kristo, furaha ya kuzaliwa upya na ufufuko."

Jarida Piazza San Pietro
14 Januari 2026, 10:03