Mwenyeheri Giovanni Merlini: Wito, Maisha na Utume Wake!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Katika Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana, Mtumishi wa Mungu Giovanni Merlini, Dominika tarehe 12 Januari 2025 akatangazwa kuwa ni Mwenyeheri. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume wa kumtangaza Mtumishi wa Mungu Giovanni Merlini kuwa ni Mwenyeheri anasema, kwa hakika alikuwa ni Mtume mwenye ari na mwamko wa Fumbo la Pasaka ya Kristo linaloleta wokovu, shuhuda amini wa Injili na mshauri mwenye busara. Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe 12 Januari. Mwenyeheri Giovanni Merlini, Padre Mmisionari wa Shirika la Damu Azizi ya Yesu, C.PP.S., alijisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya utume kwa watu wa Mungu, akawa mshauri mwenye busara kwa roho nyingi na mjumbe wa amani. Kardinali Angelo De Donatis Mhudumu mkuu wa Baraza la Kipapa la Toba ya Kitume pamoja na Kardinali Lazzaro You Heung Sik, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makleri, ni viongozi walionogesha kumbukizi ya mwaka mmoja tangu Mtumishi wa Mungu Giovanni Merlini alipotangazwa kuwa ni Mwenyeheri, kuanzia tarehe 9 hadi 13 Januari 2026. Hizi zimekuwa ni siku za sala, tafakari na shuhuda mbalimbali mintarafu wito, maisha na utume wa Mwenyeheri Giovanni Merlini. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Leo XIV tarehe 18 Septemba 2025 alikutana na kuzungumza na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa 22 wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, C.PP.S., uliongozwa na kauli mbiu: “Damu ya Kristo, Tumaini la Ulimwengu” na kuwapongeza waasisi wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, waliokuwa wazi kwa utendaji wa Roho Mtakatifu, wakaweza kusoma na kufasiri alama za nyakati na hatimaye kujibu kwa njia yenye mwanga kwa mahitaji ambayo yalijitokeza hatua kwa hatua. Baba Mtakatifu Leo XIV pamoja na mambo mengine alikazia kuhusu wito wa maisha ya kitawa yanayosimikwa katika ujenzi wa jumuiya, kama mahali patakatifu na chemchemi ya maongozi; ushuhuda na nguvu katika utume; ili katika ushirika, wema uweze kuongezeka na kukua.
Pili ni Utii kama kielelezo cha upendo, ili hatimaye, kutafuta na kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha na utume wao. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Utii, katika maana yake ya ndani kabisa inakita mizizi yake katika dhana ya kuwasikiliza wengine kwa bidii na ukarimu; Utii ni tendo kuu la upendo linalosimikwa katika imani, sadaka na ujenzi wa mahusiano ya kudumu; maisha ya pamoja na hivyo kuimarishwa katika uaminifu. Utii ni shule ya uhuru katika upendo. Mtakatifu Gaspari alisoma alama za nyakati. Alikuwa na uwezo wa: kutazama, kutathmini, kupenda na kisha kuyamwilisha yote haya katika matendo, tayari kuwahudumia watu katika mahitaji yao msingi, huku wakiitambua sauti ya Mungu katika umaskini wa jirani zao. Hii ni changamoto kwa wanashirika katika ulimwengu mamboleo kujikita katika maadili, ili kusonga mbele! Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana, Kardinali Marcello Semeraro, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 12 Januari 2025 alimtangaza Mtumishi wa Mungu Giovanni Merlini, kuwa ni Mwenyeheri. Yeye alizaliwa tarehe 28 Agosti 1795 huko Spoleto, Perugia nchini Italia. Akapewa daraja Takatifu ya Upadre tarehe 19 Desemba 1818. Tarehe 15 Agosti 1820 akajiunga na Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, lililokuwa limeanzishwa na Mtakatifu Gaspari del Bufalo tarehe 15 Agosti 1815. Alijiunga na Shirika baada ya kuvutiwa sana na mahubiri yaliyotolewa na Mtakatifu Gaspari, kuhusu Fumbo la Ukombozi chemchemi ya upendo wa kimisionari.
Kumbe, Tasaufi ya Damu Azizi ya Yesu ni msaada kwa kila Mkristo kwa kuwa Damu ya Kristo ndiyo ni msingi wa ukombozi wa mwanadamu na ni kielelezo cha juu kabisa cha upendo wa Mungu kwa watu wote. Tasaufi hii ina msingi wake katika na Neno la Mungu na katika Fumbo la Ekaristi Takatifu ambalo ndilo chanzo na kilele cha maisha ya kila siku ya Kanisa na maisha ya Mkristo kwa jumla. Tena Ekaristi Takatifu ni ujumuisho mzima wa imani ya Kikristo na ni msingi wa mitazamo sahihi ya Kikristo. Rej KKK 1324 na 1327.Tasaufi ya Damu Azizi ya Yesu, Agano Jipya na la Milele, ikawa ni msingi wa maisha na sadaka, kwa bidii ya kutafakari na shauku ya kitume “cum ardore contemplativo et passione apostolica.” Mwenyeheri Giovanni Merlini aliishi nyakati za Mapinduzi ya Napoleone, wakati wa mchakato wa mafundisho tanzu ya Kanisa. Papa Pio IX kunako tarehe 8 Desemba 1854 akatangaza rasmi kwamba, Mwenyeheri kabisa Bikira Maria, tangu nukta ya kutungwa kwake mimba, kwa neema na upendeleo wa pekee wa Mwenyezi Mungu, kwa kutazamia mastahili ya Kristo Yesu, Mwokozi wa wanadamu wote, alikingiwa na kila doa la dhambi ya asili. Mwenyeheri Giovanni Merlini akatangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili katika maisha ya kila siku kwa kutambua mbegu za Ufalme wa Mungu na hivyo akajipambanua kuwa ni chombo cha huruma ya Mungu na amani; na shuhuda wa matumaini yasiyotahalisha. “Spes non confundit.”
Kati ya Mwaka 1847 hadi 1873 aliteuliwa kuwa ni Mkuu wa tatu wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu. Kama kiongozi akaonesha utakatifu wa maisha, udugu, ari na mwamko wa kimisionari; ukaribu na majadiliano katika ukweli na uwazi; kupima mang’amuzi ya maisha na utume wa kimisionari mbele ya Msalaba. Ni katika wakati wa uongozi wake, Shirika likapanuka na kuenea nje ya mipaka ya Italia hadi Kaskazini mwa Ulaya na nchini Marekani. Katika maisha na utume wake alibahatika kuwa ni kiongozi wa maisha ya kiroho kwa Mtakatifu Maria De Mattias, utume alioutekeleza kwa kipindi cha miaka arobaini na mbili. Akasaidia kujenga na kuwaimarisha Masista Waabuduo Damu Takatifu ya Yesu, ASC. Katika mashauri yake alikazia: majadiliano katika utu, heshima na ukuaji wa maisha ya kiroho, daima wakitafuta kutekeleza mapenzi ya Mungu. Mwenyeheri Giovanni Merlini, alisaidiana na Mtakatifu Gaspari del Bufalo kupyaisha maisha ya waamini na makleri kwa namna ya pekee kama yaliyoasisiwa na Papa Pio VII na Pio 1X kwa njia ya mahubiri, mafungo na hata wakati mwingine akahatarisha maisha yake kwa kutangaza Injili miongoni mwa majangili, kielelezo cha mtume wa msamaha unaobubujika kutoka katika Damu Azizi ya Kristo. Fumbo la Pasaka ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa na kwamba Waraka wa Kitume wa “Amantissimus human” wa Mwaka 1862 ulionesha umuhimu wa Tasaufi ya Damu Azizi ya Kristo na kunako mwaka 1849 katika Waraka wa Kitume wa “Redempti sumus” Sikukuu ya Damu Azizi ya Yesu, ikatangazwa kuwa ni Sikukuu kwa Kanisa zima. Mwenyeheri Giovanni Merlini akaitupa mkono dunia tarehe 12 Januari 1873 kwa ajali.
Tarehe 10 Mei 1973 Baraza la Kipapa la Kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu likamtangaza kuwa ni Mtumishi wa Mungu. Tarehe 23 Mei 2024 Baba Mtakatifu Francisko akaruhusu atangazwe kuwa ni Mwenyeheri. Kwa upande wake, Kardinali Marcello Semeraro, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu amesema kwa ufupi kabisa kwamba, Mwenyeheri Giovanni Merlini ni kiongozi aliyeweza kuunganisha tafakari na kuimwilisha katika matendo ya huruma na adili; ni mtu wa Mungu aliyesimika maisha yake katika sala, mahiri katika mahubiri, tajiri wa karama ya busara aliyethubutu kusoma alama za nyakati, akatafuta ushauri wa kina na kujibu changamoto zilizokuwa mbele yake kwa upendo mkamilifu. Ni kiongozi aliyethubutu kumwilisha tafakari katika matendo, bila ya kujibakiza kwa wale waliohitaji msaada wake. Ni kiongozi aliyejenga na kudumisha urafiki kati ya watakatifu Gaspari del Bufalo na Maria De Mattias, hawa wakapendana na kushikamana katika umoja na upendo “Ubi est charitas et delectio, ibi est sanctorum congregatio.” Huu ni umoja na upendo unaounda watakatifu ndani ya Kanisa. Mwenyeheri Giovanni Merlini alikuwa ni chemchemi ya matumaini, shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu na imani inayomwilishwa katika furaha. Ni matumaini ya Mama Kanisa katika maadhimisho ya Mwaka wa Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, waamini wataendelea kuwa ni mashuhuda wa imani yenye furaha, ari na mwamko wa upendo, ili kuwakarimia jirani zao walau uso wa tabasamu na furaha ya kweli; mwono wa udugu wa kibinadamu; usikivu wa kweli na huduma makini kwa kutambua kwamba, katika Roho wa Kristo Yesu kila jambo linaweza kuwa ni mbegu ya matumaini.
