Tafuta

Papa alikutana na  Lazzarini, Kamishna Mkuu wa UNRWA. Papa alikutana na Lazzarini, Kamishna Mkuu wa UNRWA.  (ANSA)

Kamishna wa UNRWA kuhusu Gaza:Tunahitaji kujenga Mustakabali wa Palestina!

Kamishna Mkuu wa UNRWA,Philippe Lazzarini,alizungumza na Vatican News kuhusu mkutano wake na Papa Leo XIV,Januari 12 na mgogoro wa kibinadamu unaozidi kuwa mbaya nchini Palestina."Zaidi ya miaka miwili baada ya vita,hakuna waandishi wa habari wa Kimataifa walioruhusiwa kuingia Gaza.Hili lazima libadilike.Waandishi wa habari wa ndani wamelipa gharama kubwa sana,na wanahitaji kuungwa mkono na waandishi wa habari wa kimataifa,"alisema.

Na Francesca Merlo – Vatican.

"Tulijadili kile ambacho UNRWA inafanya, lakini pia kile ambacho kingetokea ikiwa ingezuiwa kufanya hivyo".  Haya yalisemwa na Philippe Lazzarini, Kamishna Mkuu wa Shirika la Misaada na Kazi la Umoja wa Mataifa kwa Wakimbizi wa Palestina (UNRWA), aliyekutana na Baba Mtakatifu Leo XIV tarehe 12 Januari 2026 mjini Vatican. Baada ya Mkutano huo alizungumza na Vatican News kuhusu mkutano huo, pamoja na mgogoro wa kibinadamu nchini Palestina na jukumu la kimaadili la ulimwengu unaojaribiwa kutazama pembeni.

Mkutano wa Papa na Kamishna Mkuu wa UNRWA
Mkutano wa Papa na Kamishna Mkuu wa UNRWA   (@Vatican Media)

Kukutana na Papa Leo XIV

Wakati wa Mkutano na Baba Mtakatifu, Lazzarini alielezea, mazungumzo hayo kuwa yalilenga hali inayozidi kuzorota kwa kasi huko Gaza, Ukingo wa Magharibi, na Yerusalemu Mashariki, na pia matokeo mapana ya kikanda ya mzozo ambao hauoneshi dalili yoyote ya utatuzi. Katikati ya mazungumzo hayo, aliongeza, ilikuwa jukumu la UNRWA katika eneo hilo. "Tulizungumzia kuhusu maana yake ikiwa Shirika hilo lingezuiwa ghafla kufanya kazi Gaza au Ukingo wa Magharibi bila kuwa na njia mbadala inayofaa," Lazzarini alisema, kwamba njia mbadala kama hiyo inaweza kuchukua umbo la taasisi za Palestina tu "zenye uwezo na mamlaka".

Chimbuko la UNRWA: 'Hatua ya muda na daraja la kibinadamu'

UNRWA iliundwa zaidi ya miaka sabini iliyopita kama hatua ya muda, daraja la kibinadamu lililokusudiwa kudumu hadi suluhisho la kisiasa litakapopatikana. Kuendelea kwake kuwepo, si ushahidi wa kushindwa kwa taasisi, bali ni kutokuwepo kisiasa. Kulikuwa na imani miongoni mwa Nchi Wanachama kwamba wangehitaji miaka michache tu kutatua mgogoro huo,” alielezea. “Ikiwa UNRWA bado ipo leo kama shirika la muda lakini la kudumu, ni kwa sababu, kwa zaidi ya miongo saba, jumuiya ya kimataifa haijaweza kupata suluhisho la kudumu la kisiasa kwa shida ya watu wa Palestina na mgogoro wa Israeli na Palestina.” Kwa muda, mamlaka ya Shirika hilo yamebadilika. “Kwa miongo michache iliyopita,” Lazzarini anaelezea, “UNRWA imekuwa shirika la maendeleo ya binadamu, linalotoa kile ambacho serikali ingeweza kutoa kwa wakazi wake yaani elimu na huduma ya afya ya msingi.”

Kiburi katika mfumo unaofanya kazi

Alielezea UNRWA, imejaribu kutoa hisia ya kawaida, hata pale ambapo haki na fursa zimezuiwa. "Kulingana na mahali wakimbizi wa Palestina wanapoishi, huenda wamezuiwa kupata riziki," alibainisha, akitaja vikwazo vya muda mrefu nchini Lebanon, na kizuizi kilichowekwa Gaza. Hili limeongeza utegemezi, hasa kadiri mgogoro wa kibinadamu unavyoendelea, Lazzarini alisema, na utegemezi huu huathiri hisia ya utu wa mtu. Lakini wakati huo huo, aliongeza kusema kuwa, wakimbizi wengi wa Palestina wanajivunia sana mfumo wa elimu ambao UNRWA imeutoa. Kwa mujibu wa Lazzarini alielezea kuwa Elimu imebaki kuwa isiyoweza kuguswa. "Ardhi imechukuliwa. Nyumba zimechukuliwa. Lakini elimu haijawahi kuchukuliwa," alisisitiza. "Siku zote imekuwa kiburi, na matumaini ya mustakabali bora."

Kufundisha 'hali ya kawaida'

Tumaini hilo sasa linajaribiwa kuliko hapo awali, na alikubali kwamba kufundisha hali ya kawaida na matumaini kwa vizazi vinavyokua chini ya mashambulizi ya mabomu, kuhamishwa, na kupotea kunaonekana kuwa changamoto kubwa. Watoto huko Gaza wamepitia karibu miaka miwili ya uharibifu mkubwa wa kila siku, Lazzarini alisema. "Wote wamepoteza jamaa, wengi wamejeruhiwa, na baadhi wamepoteza marafiki." Hawa ni watoto, ambao walifundishwa kwa miongo kadhaa umuhimu wa haki za binadamu kwa ujumla  lakini wakashuhudia haki hizo zikipuuzwa waziwazi zinapowafikia. Lazima niseme, ni changamoto kubwa sana", alisema. Na bado, aliendelea, "hatuwezi kukata tamaa. Hivi sasa, tuna mamia ya maelfu ya wasichana na wavulana wanaoishi kwenye vifusi, wameumia sana, na ambao wanahitaji kurudi kwenye mazingira ya kujifunza." Mkuu huyo wa UNRWA aidha alionya kwamba kusubiri ujenzi upya kutakuwa janga kubwa. "Tunapaswa kutafuta njia za kuanza tena kujifunza sasa, vinginevyo, tutakuwa na kizazi kilichopotea, na matokeo yake yangeenea zaidi ya Gaza. Tukipoteza kizazi hiki, tutakuwa tunapanda mbegu za itikadi kali zaidi katika siku zijazo," alisisitiza.

Mwandishi wa habari wa Vatican akihojiana na Kamishna Mkuu wa UNRWA
Mwandishi wa habari wa Vatican akihojiana na Kamishna Mkuu wa UNRWA

Ufadhili kwa UNRWA

Hata hivyo, uharaka huu upo katika hali ya wasiwasi pamoja na maamuzi ya baadhi ya mataifa wafadhili. Baadhi  mataifa yanaonesha wasiwasi mkubwa kwa maisha ya raia  wakati huo huo wakisimamisha au kuweka masharti ya ufadhili kwa UNRWA. "Unawezaje kupatanisha ahadi yako ya kupunguza mateso ya wanadamu," Lazzarini aliuliza, "na ukweli kwamba unakataa kupeleka pesa kupitia Shirika kama UNRWA,  ambalo lina alama kubwa zaidi huko Gaza na ndilo mtoa huduma mkuu wa elimu na afya ya umma?" Alisisitiza kwamba usaidizi wa kibinadamu hauzuiliwi na chakula pekee, unahitaji makazi, unahitaji chanjo na unahitaji upatikanaji wa maji safi, zaidi unahitaji upatikanaji  wa elimu ya msingi. Mengi ya haya yanatolewa na UNRWA pekee." Kwa kukuongezea, Lazzarini alibainisha kuwa "Hakuna shaka, kwamba kuna utata kati ya kusema unaunga mkono mwitikio wa kibinadamu huku ukikataa kuunga mkono shughuli mbalimbali muhimu za kibinadamu."

Ukweli uliopo nyuma ya 'kusitishwa kwa mapigano'

Kusitishwa kwa mapigano kumepunguza vurugu za kila siku, lakini Lazzarini alionya dhidi ya kulinganisha utulivu na utatuzi wa mgogoro. "Mgogoro bado unaendelea kila siku," alisema. "Kuna ukiukwaji wa kila siku. Vizuizi vinabaki." Huenda njaa imepungua kidogo, lakini umaskini haujapungua. Mbali na chakula, alisema, "idadi hii ya watu inahitaji karibu kila kitu." Katika muktadha huo, Lazzarini anaamini waandishi wa habari wana jukumu maalum.  Kwa sababu "Gaza na Palestina zimekuwa chini ya vita vya masimulizi. Kumekuwa na taarifa nyingi za uwongo. Jukumu la waandishi wa habari ni kuendelea kuzingatia, kwa umakini, na kuwa na uangalifu kinachoendelea Gaza.  Zaidi ya miaka miwili baada ya vita, hakuna waandishi wa habari wa Kimataifa walioruhusiwa kuingia Gaza. "Hili lazima libadilike," alisisitiza Lazzarini. "Waandishi wa habari wa ndani wamelipa gharama kubwa sana, na wanahitaji kuungwa mkono na waandishi wa habari wa kimataifa."

Usaidizi wa Kanisa

Kwa kuzingatia hisia hii ya kuachwa, usaidizi wa Kanisa kwa Wapalestina wanaoteseka unachukua maana maalum. "Ni ujumbe wa mshikamano kwa Wapalestina, ambao tayari wanahisi kwamba jumuiya ya kimataifa imewapa mgongo. Pia ni ujumbe wa matumaini, kwa wachache katika ukanda mzima. Kwa UNRWA, usaidizi huo pia ni wa vitendo. Tunahitaji kulinda nafasi yetu ya uendeshaji. Tunahitaji kuhakikisha kuchukuliwa kuwa sehemu ya suluhisho, kama vile  rasilimali katika kujenga taasisi za Wapalestina za baadaye. Tusipofanya hivyo, sioni matumaini yatakuwa wapi," alihitimisha Lazzarini.

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku:Just click here

13 Januari 2026, 10:31