Maombi ya Papa kwa ajili ya waathirika wa Kimbunga Kristin nchini Ureno
Isabella Piro na Angella Rwezaula–Vatican.
Ukaribu na maombi, ndizo hisia zilizotolewa na Papa Leo XIV katika ujumbe uliotumwa kwa Askofu José Ornelas Carvalho, wa Jimbo Katoliki la Leiria-Fátima na Rais wa Baraza la Maaskofu wa Ureno (CEP). Katika ujumbe uliosainiwa na Katibu Mkuu wa Vatican Kardinali Pietro Parolin, Papa anatoa salamu za rambirambi kwa waathiriwa wote wa Kimbunga “Kristin,” "akiungana kiroho na huzuni ya familia zao.” Kimbunga, kilichofika pwani ya Atlantiki ya Ureno ,usiku kati ya Jumatano na Alhamisi Januari 28 na 29, chenye upepo wa zaidi ya kilomita 170 kwa saa, kimeacha "eneo baya sana," ambapo Papa alibainisha, akielezea “huruma yake kwa waliojeruhiwa, waliokimbia makazi yao, na wale ambao wameathiriwa vibaya na uharibifu mkubwa uliosababishwa na dhoruba hii."
Mshikamano na Matumaini
Askofu wa Roma anaomba "kwa ajili ya mamlaka ya kitaifa na serikali za mitaa, pamoja na taasisi za kiraia, kijeshi, na kidini zinazoungana kuwasaidia," akitoa shukrani "kwa kujitolea kwa mashirika ya kanisa, bila kusahau mshikamano wa hiari wa kila raia." Hatimaye, Papa anamwomba Mungu "manukato ya mshikamano na mwanga wa matumaini ya Kikristo," akitoa baraka zake za kitume.
Sote tunatambua mateso ya kimwili na kihisia
Askofu Ornelas Carvalho, katika ujumbe kwa Jimbo la Leiria-Fátima, pia alionesha mshikamano na wote walioathiriwa na dhoruba hiyo. "Sote tunatambua mateso ya kimwili, kihisia, na kiroho ambayo hali hii imesababisha. "Hamuko peke yenu kwa wakati huu." Kiukweli Jimbo "linafuatilia kwa karibu hali hii ngumu, katika parokia na mashirika ya ndani, kwa kadiri mtandao wa mawasiliano unavyoruhusu, ikitafuta kutoa msaada halisi na uwepo wa kichungaji katika Jumuiya zilizoathiriwa, ikitenda kwa uratibu na mamlaka za misaada mahalia, na kitaifa na kurejesha hali ya maisha katika maeneo yaliyoathiriwa."
Tusimame pamoja ili kupunguza mateso na kujenga upya jamii
Kupitia Caritas mahalia, Askofu Ornelas Carvalho aliendelea, mshikamano wa Kanisa pia unaenea hadi Majimbo mengine yaliyokabiliwa na matatizo kama hayo. Tunatambua kujitolea na mateso ya wale wote katika maeneo ya jirani ambao wameathiriwa na hali hii mbaya. Wakati huo huo, askofu anawashukuru wote ambao, tangu mwanzo, walikimbilia eneo hilo kutoa msaada: Ni ishara chanya sana ya mshikamano wa kibinadamu ambayo itabaki katika kumbukumbu zetu za pamoja, alisisitiza. Katika nyakati kama hizi, tumaini la Kikristo linakuwa mwanga unaoongoza. Tumeitwa kumtumaini Mungu na kuimarisha vifungo vya ushirika na mshikamano miongoni mwetu," anahitimisha rais wa CEP. Kila ishara ya msaada, kila sala, kila uwepo wa kirafiki huchangia ujenzi upya na kupunguza mateso."
Mfuko wa Dharura wa Caritas Waundwa
Kujibu dharura, Caritas Leiria-Fátima ilitangaza kuundwa kwa "Mfuko wa Dharura wa Kijamii wa Kuwasaidia Waathiriwa wa Dhoruba ya Kristin," ili kuimarisha uwezo wake wa kukabiliana na dharura huku ikiendelea kukusanya mahitaji ya msingi na vifaa vya dharura. Mpango huu, alielezea Ana Mota, "utaharakisha usaidizi kwa familia zilizoathiriwa. Mshikamano ambao tayari tumeanza kuonesha ni ishara ya matumaini." Kwa hivyo, wito wa kubaki na umoja, kwa sababu pamoja tutaweza "kujenga upya, kusaidia, na kurejesha heshima ya kila mtu aliyeathiriwa."
Waathiriwa 5 na manispaa 60 zilizoathiriwa
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa ni kwamba, wilaya zilizoathiriwa zaidi na Dhoruba ya Kristin ni Leiria, Coimbra, Santarém, na Lisbon. Karibu manispaa 60 zimeathiriwa. Hadi sasa, kumekuwa na vifo vitano, pamoja na mafuriko, maporomoko ya ardhi, kufungwa kwa barabara na reli, na kukatika kwa umeme kwa zaidi ya knyumba 850,000. Kimbunga hicho pia kimesababisha ajali zaidi ya 3,000 nchini kote, huku barabara zikiwa zimeziba miti na vifusi na majengo mengi yakiharibiwa.
Mahali Patakatifu pa Fatima pia pameathiriwa
Miongoni mwa uharibifu mkubwa wa vifaa ni ule ulioripotiwa katika Kituo cha Anga cha Monte katika wilaya ya Leiria, ambapo vifaa kadhaa na ndege mbili za kivita za F-16 ziliathiriwa na vifusi vilivyoanguka kutokana na upepo mkali. Madhabuhu ya Fátima pia pameathiriwa: upepo mkali ulibebwa hasa mierezi na misonobari kando ya njia za "Kizuizi cha Maombi," pamoja na baadhi ya maeneo yaliyo nyuma ya Basilika ya Mama Yetu wa Rozari na katika eneo la Valinhos.
Hali ya janga imetangazwa hadi Februari 1
Serikali ya Ureno imetangaza hali ya janga katika maeneo yaliyoathiriwa zaidi, kuanzia usiku wa manane Januari 28 hadi saa 11:59 jioni tarehe 1 Februari 1. Waziri Mkuu Luís Montenegro, ambaye alitembelea Leiria Alhamisi 29 Januari, alitangaza kwamba Ureno inawasiliana na Tume ya Ulaya ili kubaini "aina bora ya ufadhili ili kusaidia familia na biashara zilizoathiriwa. Kwa upande wake, Rais wa Tume ya Ulaya Bi Ursula von der Leyen, katika chapisho kwenye X, alielezea "rambirambi zake za dhati" kwa waathiriwa na uharibifu uliosababishwa na dhoruba hiyo, akihakikisha kwamba EU "iko tayari kusaidia nchi hiyo kupona."
Tahadhari pia nchini Hispania
Wakati huo huo, baada ya kuvuka Ureno, Kimbunga Kristin kilielekea mashariki hadi Hispania, kikileta theluji katika miinuko ya chini, mvua, na upepo mkali. Huko Andalusia, huduma za dharura ziliripoti takriban matukio 2,000 yanayohusiana na hali ya hewa. Mamlaka ya Hispania ilitoa maonyo kwa mawimbi makubwa kando ya pwani na kutabiri dhoruba za upepo za hadi kilomita 90 kwa saa kwenye kisiwa cha Ibiza.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku: Just click here
