Tafuta

Dominika ya Neno la Mungu na tarehe 25 Januari 2026 ni Dominika ya Saba ya Neno la Mungu tangu kuanzishwa kwake na Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2019 Dominika ya Neno la Mungu na tarehe 25 Januari 2026 ni Dominika ya Saba ya Neno la Mungu tangu kuanzishwa kwake na Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2019  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Maadhimisho ya Dominika ya Saba ya Neno la Mungu 25 Januari 2026

Hati ya Kusikiliza kwa Uchaji Ufunuo wa Neno la Mungu “Dei verbum” inagusia kwa undani kuhusu: Ufunuo wenyewe; Urithishaji wa Ufunuo wa Kimungu; Uvuvio wa Kimungu na Ufafanuzi wa Maandiko Matakatifu; Agano la Kale, Agano Jipya; pamoja na Maandiko Matakatifu Katika Maisha ya Kanisa. Papa Leo XIV anasema, Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kristo Yesu, Ufunuo wa Baba wa milele, anazungumza na wanadamu kama mtu anavyo zungumza na rafiki yake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Barua yake Binafsi, Motu Proprio “Aperuit illis” yaani: “Aliwafunulia akili zao wapate kuelewa na Maandiko” (Lk 24:45.” iliyochapishwa kunako tarehe 30 Septemba 2019 alianzisha Dominika ya Neno la Mungu na tarehe 25 Januari 2026 ni Dominika ya Saba ya Neno la Mungu. “Aliwafunulia akili zao” kitendo hicho ni kati ya vitendo vya mwisho alivyovitenda Kristo Yesu, Bwana mfufuka, kabla ya kupaa kwake mbinguni. Alionekana kwa wanafunzi wake walipokuwa wamekusanyika pamoja, akamega mkate pamoja nao, akawafunulia akili zao wapate kuelewa na Maandiko Matakatifu. Kwa watu wale waliokuwa wameshikwa na hofu na kukata tamaa, aliwafunulia maana ya Fumbo la Pasaka: yaani kwamba, kadiri ya mpango wa milele wa Mungu Baba, Kristo Yesu alipaswa kuteswa, kufa na hatimaye, kufufuka kwa wafu ili awajalie watu wote: toba, wongofu na msamaha wa dhambi (taz. Lk. 24:26.46-47); pia aliahidi kumpeleka Roho Mtakatifu atakayewapa nguvu ya kuwa mashahidi wa Fumbo hili la wokovu (taz. Lk 24:49.)

Neno la Mungu lipewe uzito wa pekee katika maisha na utume wa Kanisa
Neno la Mungu lipewe uzito wa pekee katika maisha na utume wa Kanisa   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Lengo kuu ni kulihimiza Kanisa kukumbuka umuhimu wa Neno la Mungu kama zawadi ya bure inayotoa uhuru, amani na matumaini, akisisitiza kwamba Kristo Yesu huweka huru watu kutoka katika minyororo yote ya ndani, na Baba Mtakatifu Francisko akawakabidhi Wakatoliki Biblia, akisisitiza uhai na nguvu ya Neno la Mungu. Hati ya Kusikiliza kwa Uchaji Ufunuo wa Neno la Mungu “Dei verbum” inagusia kwa undani kuhusu: Ufunuo wenyewe; Urithishaji wa Ufunuo wa Kimungu; Uvuvio wa Kimungu na Ufafanuzi wa Maandiko Matakatifu; Agano la Kale, Agano Jipya; pamoja na Maandiko Matakatifu Katika Maisha ya Kanisa. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kristo Yesu, Ufunuo wa Baba wa milele, anazungumza na wanadamu kama mtu anavyo zungumza na rafiki yake. Huu ni mwaliko kwa waamini kujenga na kudumisha utamaduni wa kusoma, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao pamoja na kujikita katika maisha ya sala!

Waamini wajenge utamaduni wa kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno!
Waamini wajenge utamaduni wa kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno!   (Vatican Media)

Mtakatifu Jerome (Jina kamili ni Eusebius Sophronius Hieronymus) kwa agizo la Papa Damasi wa kwanza, kwa muda wa miaka 23 alifanya kazi ya kutafsiri na kupanga vitabu vya Biblia kwa lugha ya Kilatini, maarufu kama “Vulgata” iliyopitishwa na Mababa wa Mtaguso wa Trento (1545-1563) kwamba inafaa kufundishia imani. Alifariki dunia tarehe 30 Septemba 420 akiwa ameliachia Kanisa utajiri mkubwa wa Maandiko Matakatifu. Mama Kanisa tarehe 30 Septemba 2020 aliadhimisha kumbukizi ya miaka 1600 tangu Mtakatifu Jerome alipofariki dunia. Wakati huo huo, Tarehe 30 Septemba 2020, Sikukuu ya Mtakatifu Jerome, Padre na Mwalimu wa Kanisa, Hayati Baba Mtakatifu Francisko alitia “mkwaju” kwenye Waraka wa Kitume Unaojulikana kama: "Scripturae Sacrae Affectus" Yaani “Waraka wa Kitume Juu ya Upendo Kwa Maandiko Matakatifu, Miaka 1600 Tangu Alipofariki Dunia Mtakatifu Jerome.” Mtakatifu Jerome, Padre na Mwalimu wa Kanisa aliyeweka Maandiko Matakatifu kuwa kiini cha maisha yake, awasaidie waamini kupyaisha ndani mwao ari, moyo na upendo wa kusoma, kutafakari na kumwilisha Maandiko Matakatifu katika uhalisia na vipaumbele vya maisha yao.

Papa Leo XIV: Kristo Yesu Neno wa Baba wa Milele ni Ufunuo wa Mungu
Papa Leo XIV: Kristo Yesu Neno wa Baba wa Milele ni Ufunuo wa Mungu   (ANSA)

Waamini wajenge utamaduni wa kujadiliana na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Maandiko Matakatifu. Utambulisho wa Wakristo unafumbatwa kwa namna ya pekee, katika mahusiano ya dhati kati ya: Kristo Mfufuka, Maandiko Matakatifu na Jumuiya ya waamini. Ndiyo maana Mtakatifu Jerome anasema “Kutojua Maandiko Matakatifu ni kutomfahamu Kristo.” Liturujia ya Kanisa na Sala ni fursa ya kuzungumza na Mwenyezi Mungu. Hii ni sehemu ya: sera na mbinu mkakati wa Mama Kanisa kuendelea kujikita katika mchakato wa uinjilishji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Lengo ni kuwahamasisha waamini kujenga na kudumisha utamaduni wa kupenda kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika vipaumbele na uhalisia wa maisha yao mintarafu maisha na utume wa Kanisa.

Dominika ya Saba ya Neno

 

22 Januari 2026, 16:28