Kwa maombezi ya Bikira Maria Bwana asikie kilio cha kimya cha wadogo na aijalie dunia,haki na amani
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Hakuna Noeli bila nyimbo. Kila mahali ulimwenguni, katika kila lugha na taifa. Tukio la Bethlehemu huadhimishwa kwa muziki na nyimbo. Na haiwezekani kuwa vinginevyo, kwa kuwa Injili yenyewe inasema kwamba, Bikira Maria alipomzaa Mwokozi, Malaika mbinguni waliimba: "Utukufu kwa Mungu na amani duniani. "Haya na mengine ni tafakari ya Baba Mtakatifu Leo XIV kwa washiriki wa Tamasha la Noeli ambalo liliainishwa kupitia lugha ya muziki na uimbaji, yenye uwezo wa kuzungumza na akili na moyo katika Kikanisa cha Sistina mjini Vatican, Jumamosi jioni, tarehe 3 Januari 2026. Hii ilioneshwa na sauti za kwaya, iliyoanzishwa zaidi ya miaka 1500, iliyoongozwa na Mwalimu, Monsinyo Marcos Pavan, pamoja na Mwalimu wa Pueri, yaani wa sauti za watoto, Michele Marinelli, wote wawili, ambao Baba Mtakatifu Leo XIV aliwashukuru. Kwa njia hiyo Baba Mtakatifu mara baada ya nyimbo hizo za kusisimua alianza hotuba yake.
Hakuna Noeli bila nyimbo
“Ninapenda kushukuru Kwaya ya Kikanisa cha Muziki cha Sistine(Cappella musicale Sistina,)ambayo katika tamasha hili walitufanya tutafakari juu ya fumbo la Noeli kwa lugha ya muziki na uimbaji, lugha yenye uwezo wa kuzungumza sio tu na akili, bali pia moyo. Ninampongeza Mwalimu Monsinyo Marcos Pavan na Mwalimu wa Pueri Michele Marinelli.” Papa aliendelea kusema, “Hakuna Noeli bila nyimbo. Kila mahali ulimwenguni, katika kila lugha na taifa, tukio la Bethlehemu huadhimishwa kwa muziki na nyimbo. Na haiwezekani kuwa vinginevyo, kwa kuwa Injili yenyewe inasema kwamba, Bikira Maria alipomzaa Mwokozi, Malaika mbinguni waliimba "Utukufu kwa Mungu na amani duniani"(Rej Lk 2,13-14).”
Papa Leo XIV alifafanua zaidi kuwa “Walikuwa ni wakina nani watazamaji na mashuhuda wa "tamasha ya Noeli" ya kwanza? Tunajua Walikuwa, baadhi ya wachungaji kutoka Bethlehemu, ambao, baada ya kumwona Mtoto katika hori, pamoja na Maria na Yosefu, walirudi wakimsifu na kumshukuru Mungu (rej. Lk 2:20).”
Tujifunze kutoka moyo wa Maria
Kwa njia hiyo Papa aliongeza kusema “Na ninapenda kufikiria kuwa walifanya hivyo kwa kuimba na labda kucheza kwa kupiga filimbi ya kawaida. Lakini kuna mahali pengine ambapo muziki wa mbinguni ulisikika kwenye usiku huo Mtakatifu. Mahali patulivu, alipojikusanya, nyeti sana: Kwa asili ninazungumza kuhusu moyo wa Maria, mwanamke aliyechaguliwa na Mungu kuwa Mama wa Neno aliyefanyika mwili. Tunajifunze kutoka kwake kusikiliza sauti ya Bwana katika ukimya, kufuata kwa uaminifu sehemu ambayo Yeye anatukabidhi katika alama ya maisha.”
Watoto waliopitia Noeli bila taa
“Wapendwa, ninapenda kuweka Tamasha hili kwa ajili ya watoto ambao, sehemu nyingi za dunia, wameishi Noeli hii bila taa, bila muziki, bila hata mahitaji ya utu wa binadamu, na bila amani,” Papa alisisitiza na kuongeza: “Bwana, ambaye tulitaka kumwinulia nyimbo zetu za sifa jioni hii, asikie kilio cha kimya cha hawa wadogo, na awape ulimwengu haki na amani, kwa maombezi ya Bikira Maria.” Hatimaye Papa Leo XIV alitoa shukrani kwa Kwaya hiyo: “Asante tena Kwaya ya Kikanisa cha Sistine na ninawatakia heri ya mwaka mpya ninyi nyote!”
Yalisikika makofi mengi, … ambapo Papa Leo XIV pia aliongeza kusema: “Ninathubutu kuwaalika sisi sote kuimba Pater Noster, yaani “Baba Yetu” katika Kikanisa hiki kizuri cha Sistine.” Baada ya sala hiyo Papa aliwatakia “Matashi mema.” Ilifuatia picha ya pamoja na baadaye akaondoka.
Ratiba ya Tamasha na nyimbo
Katika hotuba iliyotangulia kuanza kwa tamasha hilo, hata hivyo Monsinyo Pavan alimshukuru Baba Mtakatifu Leo XIV kwa uwepo wake, uliofafanuliwa “kuwa ni heshima na faraja katika muendelezo wa huduma ambayo waimbaji wa kipapa wamemfanyia mrithi wa Petro kwa miaka 1500." Mpango huu ulianzia katika utayarishaji mtakatifu wa aina nyingi, kuanzia na wimbo wa Gregorian hadi kazi za Giovanni Pierluigi wa Palestrina, ambapo noti mbili zake zinachezwa: Dies Sanctificatus na Hodie Christus Natus Est. Wastaafu wawili wa Muziki wa Kwaya ya Kikanisa cha Sistine walikumbukwa na kisifiwa: Giuseppe Liberto, kwa wimbo wa Magnum Nomen Domini, na Domenico Bartolucci, na wimbo wa Puer Natus in Bethlehem na Christus est qui natus hodie.
Ulifuata wimbo wa: O Magnum Mysterium uliotungwa na Mhispania wakati wa Kipindi cha Kuzaliwa upya, Tomás Luis de Victoria na Quem vidistis, pastores, dicite wa Francis Poulenc, Msanii wa Kifaransa wa karne iliyopita. Kisha ulifuata wimbo mwingine wa Quem pastores laudavere uliotungwa na Mmarekani James Bassi. Mwisho wa Tamasha, hilo nyimbo tatu maarufu za kiutamaduni ziliimbwa: Astro del ciel, Tu scendi dalle stelle zilizotungwa na Mtakatifu Alfonso Maria de’ Liguori na Adeste fideles.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku. Just click here.
