Tafuta

Ni Mapokeo ya Kanisa kwamba, Sikukuu ya Mtakatifu Agnes, wanabarikiwa kondoo ambao manyoya yao yatatumika kutengenezea Pallio Takatifu. Ni Mapokeo ya Kanisa kwamba, Sikukuu ya Mtakatifu Agnes, wanabarikiwa kondoo ambao manyoya yao yatatumika kutengenezea Pallio Takatifu.  (AFP or licensors)

Kumbukumbu ya Mtakatifu Agnes: Manyoya ya Kondoo: Pallio Takatifu

Sikukuu ya Mtakatifu Agnes, wanabarikiwa kondoo ambao manyoya yao yatatumika kutengenezea Pallio Takatifu, wanazovishwa: Papa, Maaskofu wakuu na Mapatriaki katika maadhimisho ya Sikukuu ya Mtakatifu Petro na Paulo Mitume, inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 29 Juni. Ni katika Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Mtakatifu Agnes, Bikira na Shahidi, Papa Leo XIV amebariki wanakondoo wawili ambao manyoya yao yatatumika kutengenezea Pallio Takatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 21 Januari anaadhimisha kumbukumbu ya Mtakatifu Agnes, Bikira na Shahidi, aliyeuwawa kunako karne ya tatu; akaonesha upendo wa pekee sana kwa Kristo Yesu mchumba wake wa daima kiasi cha kuyasadaka maisha yake, ili asiuchafue ubikira wake. Yesu mwenyewe alitambulishwa na Yohane Mbatizaji kama Mwana Kondoo wa Mungu anayebeba na kuondoa dhambi za ulimwengu. Ni Mapokeo ya Kanisa kwamba, Sikukuu ya Mtakatifu Agnes, wanabarikiwa kondoo ambao manyoya yao yatatumika kutengenezea Pallio Takatifu, wanazovishwa: Papa, Maaskofu wakuu na Mapatriaki katika maadhimisho ya Sikukuu ya Mtakatifu Petro na Paulo Mitume, inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 29 Juni.

Pallio Takatifu
Pallio Takatifu   (VATICAN MEDIA)

Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Mtakatifu Agnes, Bikira na Shahidi, Baba Mtakatifu Leo XIV Jumatano tarehe 21 Januari 2026 amebariki wanakondoo wawili ambao manyoya yao yatatumika kutengenezea Pallio Takatifu. Pallio Takatifu ni kitambaa cha sufi safi kinachovaliwa na Baba Mtakatifu, Maaskofu wakuu wa majimbo ya Kanisa Katoliki pamoja na Mapatriaki, kilicho pambwa kwa Misalaba sita ya sufi nyeusi. Hii ni alama ya Kristo mchungaji mwema aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Pallio Takatifu huvikwa: Papa, Maaskofu wakuu na Mapatriaki
Pallio Takatifu huvikwa: Papa, Maaskofu wakuu na Mapatriaki   (AFP or licensors)

Kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu, Mchungaji mwema, hata kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, Maaskofu wakuu na Mapatriaki wanahamasishwa kuwabeba kondoo wao kama kielelezo cha wachungaji wema; wakumbuke kwamba, wameteuliwa si kwa ajili ya mafao yao binafsi, bali kwa ajili ya kondoo wa Kristo Yesu. Papa, Maaskofu wakuu na Mapatriaki wanapaswa pia kusadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Pallio takatifu ni alama ya umoja na mshikamano kati ya Khalifa wa Mtakatifu Petro, Maaskofu wakuu na Mapatriaki.

Pallio Takatifu
21 Januari 2026, 14:45