Tafuta

Tarehe 23 Januari 2026 Vatican na Brazil zimeadhimisha Jubilei ya Miaka 200 tangu zilipoanzisha uhusiano wa kidiplomasia tarehe 23 Januari 1826 Tarehe 23 Januari 2026 Vatican na Brazil zimeadhimisha Jubilei ya Miaka 200 tangu zilipoanzisha uhusiano wa kidiplomasia tarehe 23 Januari 1826 

Jubilei ya Miaka 200 ya Uhusiano wa Kidiplomasia Kati ya Brazil Na Vatican: 1826-2026

Tarehe 23 Januari 2026 Vatican na Brazil zimeadhimisha Jubilei ya Miaka 200 tangu zilipoanzisha uhusiano wa kidiplomasia kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa watu wa Mungu kutoka ndani na nje ya Brazil kwenye Kanisa la Bikira Maria Mkuu, lililoko Jimbo kuu la Roma. Miaka mia mbili imekuwa ni hija ya maisha ya diplomasia mintarafu huduma kwa: utu, heshima na haki!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Vatican na Brazil zimedumisha uhusiano wa kidiplomasia tangu tarehe 23 Januari 1826, muda mfupi tu baada ya Brazil kujipatia uhuru wake yaani kunako mwaka 1822. Baba Mtakatifu Leo XII akapokea hati za utambulisho kutoka kwa Monsinyo Francisco Corrêa Vidigal, aliyekuwa ametumwana Mfalme Petro wa kwanza mjini Vatican, ili kuomba uhuru wa Brazil, uweze kutambulika. Diplomasia ya Vatican na Kanisa katika ujumla wake, kimsingi inakazia kwa namna ya pekee kabisa: huduma makini ya maendeleo fungamani ya binadamu; kusimama kidete kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Mambo mengine msingi ni: amani na maridhiano kati ya watu; huduma makini kwa wakimbizi na wahamiaji duniani; elimu, afya, biashara, mawasiliano, ushirikiano na mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa pamoja na haki miliki ya kiakili.

Jubilei ya Miaka 200 ya Uhusiano wa Kidiplomasia: Brazil na Vatican
Jubilei ya Miaka 200 ya Uhusiano wa Kidiplomasia: Brazil na Vatican   (@VATICAN MEDIA)

Hizi ni kanuni msingi zinazofumbatwa katika Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayotoa dira na mwongozo makini kwa Jumuiya ya Kimataifa katika mchakato wa kukuza na kudumisha utamaduni wa amani, haki, ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu. Hii ni sehemu muhimu sana ya utangazaji na ushuhuda wa Habari Njema ya Wokovu miongoni mwa Jumuiya ya Kimataifa. Vatican katika masuala ya kidiplomasia inafuata kwa makini sana: Sheria za Kimataifa, taratibu na kanuni za Jumuiya ya Kimataifa sanjari na kuendelea kuwa ni sauti ya kinabii inayojikita katika kanuni maadili na ushirikiano unaosimamiwa na kuratibiwa na kanuni auni. Amani haiwezi kufikiwa mara moja kwa daima, bali inadaiwa kujengwa siku kwa siku. Amani ni matokeo ya haki inayomwilishwa katika upendo, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Rej. GS 78.

Papa Leo XIV akizungumza na Rais wa Brazil
Papa Leo XIV akizungumza na Rais wa Brazil   (@Vatican Media)

Amani ya kweli inakolezwa katika urafiki wa udugu wa kibinadamu. Upatanisho ni mchakato unaopania kuboresha maisha ya mbeleni na unafumbatwa katika toba, msamaha na wongofu wa ndani, ili kujenga na kudumisha utamaduni wa upendo, chemchemi ya amani ya kudumu. Vatican na Brazil kunako mwaka 2008 zikapyaisha Mkataba wa mahusiano yao, kwa kufafanua hali ya kisheria ya maisha na utume wa Kanisa Katoliki nchini Brazil. Tarehe 23 Januari 2026 Vatican na Brazil zimeadhimisha Jubilei ya Miaka 200 tangu zilipoanzisha uhusiano wa kidiplomasia kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa watu wa Mungu kutoka ndani na nje ya Brazil kwenye Kanisa la Bikira Maria Mkuu, lililoko Jimbo kuu la Roma. Miaka mia mbili anasema Kardinali Parolin, imekuwa ni hija ya maisha ya diplomasia kiroho mintarafu huduma kwa: utu, heshima, haki msingi za binadamu, ustawi na maendeleo.

Jubilei ya Miaka 200 ya Uhusiano wa Kidiplomasia kati ya Vatican na Brazil
Jubilei ya Miaka 200 ya Uhusiano wa Kidiplomasia kati ya Vatican na Brazil

Tangu wakati huo, Brazil imepokea Mabalozi wa Vatican 34. Hii ni changamoto kwa Brazil kujikita katika mchakato wa ujenzi wa haki, amani na maridhiano kati ya watu wake kwa kuendelea kujikita katika: huruma ya Mungu, Uongozi unaosimikwa katika sheria, kanuni, utu na haki msingi za binadamu na kwamba uongozi kadiri ya Mafundisho Jamii ya Kanisa ni huduma inayofumbatwa katika unyenyekevu, sadaka na majitoleo kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Uongozi unapaswa kuwa ni jicho la huduma ya upendeleo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii na kwamba, hii ni sehemu ya Fumbo la Msalaba! Hii ni changamoto kwa watu wa Mungu nchini Brazil kuungana na kushikamana katika unyenyekevu, ili kukoleza: imani na matumaini ya watu wa Mungu nchini Brazil, yanayosimikwa kwa Ibada kwa Bikira Maria, ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo za madonda na makovu ya kijamii, changamoto zinazoendelea kuibuliwa katika sekta ya elimu, afya, sanjari na kusimama kidete katika misingi ya haki na amani.

Diplomasia ya Vatican: Utu,  heshima na haki msingi za binadamu, haki na amani
Diplomasia ya Vatican: Utu, heshima na haki msingi za binadamu, haki na amani   (AFP or licensors)

Changamoto zote hizi zinapaswa kushughulikwa kwa: Ujasiri, furaha na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, kwa kujitahidi kuishi katika amani na utulivu; kwa kuzingatia na kuheshimu tofauti zao msingi kama amana na utajiri wa watu wa Mungu nchini Brazil. Katika kipindi cha miaka mia mbili ya uhusiano wa kidplomasia kati ya Vatican na Brazil, kumekuwepo na mabadiliko makubwa ya kisiasa, kijamii, kiuchumi na katika maisha ya kiroho. Daima uhusiano huu wa kidiplomasia umejikita katika utu, heshima na haki msingi za binadamu; binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza. Brazil inapaswa kujikita katika kupambana na mifumo mbalimbali ya umaskini mamboleo, ili kuweza kujikita katika msingi ya haki, amani, ustawi na maendeleo fungamani ya binadamu anasema Kardinali Parolin. Jubilei hii, iwe ni mapambazuko ya uhusiano mpya wa kidiplomasia, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watu wa Mungu nchini Brazil. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, ameziweka nchi hizi mbili chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Afya ya Waroma na Mama Yetu wa Aparecida.

Parolin Jubilei Miaka 200
24 Januari 2026, 17:38