Ibada na Heshima Kwa Jina Takatifu la Kristo Yesu! Mkombozi wa Binadamu!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican & Na Linus Tigiti, SJ, - Roma.
Ibada kwa Jina Takatifu la Yesu inapata chimbuko na asili yake kwenye Maandiko Matakatifu. Lakini hizi hasa zilikuwa ni juhudi za Mtakatifu Bernardino wa Siena (8 Septemba 1380 - 20 Mei 1444), na Yohane wa Capistrano) Watawa wa Shirika la Ndugu Wadogo kuineza sehemu mbalimbali za dunia. Mtakatifu Bernardino wa Siena ndiye anayesadikiwa kutunga herufi IHS, yaani “Iesus Hominum Salvator.” Na kwa lugha ya Kigiriki “ΙΗΣΟΥΣ, Iesûs” “Yesu” na maana yake “Yesu Mkombozi wa Binadamu.” Kwa kuwa Jina Takatifu la Yesu ni sehemu ya vinasaba na utambulisho wa Wakristo, Papa Innocent XIII akaieneza Ibada hii ulimwenguni kote. Na Mtakatifu Yohane Paulo II akatamka iandikwe kwenye Kalenda ya Liturujia ya Kiroma na kuadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 3 Januari. Baba Mtakatifu Francisko katika ufunguzi wa Lango la Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo alisema, Kristo Yesu ni tumaini la waja wake, ndiye Immanueli yaani Mungu pamoja nasi! Huyu ndiye Mungu aliyejinyenyekesha na kuwa mdogo, Mwanga wa Kimungu unaong’aa katika giza nene la ulimwengu; Ndiye utukufu wa Mungu ulionekana ulimwenguni katika umbo la Mtoto mchanga, katika hori la kulishia wanyama, leo hii anazaliwa katika nyoyo za waja wake, tumaini hai linaloyazunguka maisha ya watu wake.
Itakumbukwa kwamba Mwezi Januari umetangwa rasmi na Mama Kanisa kwa ajili ya Ibada na heshima kwa Jina Takatifu la Yesu na Sikukuu ya Jina Takatifu la Yesu inaadhimishwa kwa namna ya pekee na Wayesuit. Lengo la Sikukuu ya Jina Takatifu la Yesu ni kukuza na kudumisha fadhila za Kikristo, kupyaisha na kuboresha maisha ya Kikristo mintarafu tunu msingi za Kiinjili. Kwa namna ya pekee kabisa Mtakatifu Bernardino wa Siena, alitaka kulipyaisha Jina Takatifu la Yesu kama lilivyojulikana kwa Wakristo wa Kanisa la mwanzo. Jina Takatifu la Yesu lilifafanua ndani mwake: Fumbo la Umwilisho linalopata hatima yake katika Fumbo la Pasaka yaani: Mateso, kifo na ufufuko uletao wokovu na maisha ya uzima wa milele. Hili ni jina linalofumbata na kuambata tunu msingi za maisha ya Kikristo: Ufukara, maisha, utume na kazi alizotenda Kristo Yesu kwa ajili ya kufunua na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka kwa waja wake. Maandiko Matakatifu yanakaza kusema “Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao.” Mt 1:21.
Kumbe, hili ni jina kadiri ya Maandiko Matakatifu linalofafanua utume wa Yesu, yaani “Mungu anaokoa." Katika maisha na utume wao, Mitume pamoja na wafuasi mbalimbali wameendelea kutenda miujiza na maajabu mengi kwa jina la Yesu kama Maandiko Matakatifu yanavyofafanua “Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya.” Yn 14:13-14. Mwinjili Luka katika Kitabu chake cha Matendo ya Mitume anakaza kusema, “Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.” Mdo 4:12. Jina la Kristo Yesu ni chemchemi ya: Ushirika, umoja na unyenyekevu: “Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya Msalaba. Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba.” Flp 2: 5-11.
Kutoka kwa Mgogoro hadi Ujasiri: Hadithi ya Wajesuit Kuhusu Jina Takatifu la Kristo Yesu: Kila wakati, binadamu hukumbwa na nyakati za mgogoro mkubwa—nyakati ambapo hofu hutaka kuondoa matumaini, na migawanyiko kuharibu mshikamano wa jamii. Karne ya 16 ilikuwa kipindi kama hicho. Ulaya ilikuwa imejaa migogoro ya kidini, mizozo ya kisiasa, na kutokuwa na hakika ya maisha ya kiroho. Katika mazingira haya, Wajesuit walijitambua kama watu waliotumwa kumtumikia Mungu katikati ya machafuko, wakitangaza na kushuhudia wazi kwamba walikuwa tayari “kumtumikia Mungu kama askari chini ya bendera ya Msalaba” (Formula Instituti, 1.) Kutoka katika dhoruba hii ulitokea ujumbe wa matumaini uliolenga jina moja tu: Yesu. Kanisa, likitambua hitaji la upyaishaji wa maisha ya kiroho, liliweka mkazo juu ya Jina la Yesu kama chanzo cha wokovu, kwa sababu, kama Mtume Paulo anavyosema, “Mungu alimkweza sana na kumpa jina lililo juu ya kila jina, ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe” (Flp 2:9–10.) Moyo wa uhuishaji huu ulikuwa ni Wajesuit, kundi dogo la watu waliokuwa chini ya uongozi wa Mtakatifu Inyasi wa Loyola. Wajesuit walizaliwa katika wakati wa machafuko, na walifanya Jina la Yesu kuwa msingi wa utu wao na dhamira yao. Nembo yao, herufi IHS, yaani “Iesus Hominum Salvator” ni zaidi ya alama—ni tamko la imani hai na thabiti. Nguvu ya Kiroho ya Jina Takatifu: Kwa Mt. Inyasi wa Loyola, Jina Takatifu la Yesu halikupaswa kuheshimiwa kwa maneno tu bali kumwilishwa katika undani wa maisha. Ndiyo maana katika Mazoezi ya Kiroho anawaalika waamini kuomba “maarifa ya ndani ya Bwana wetu, ambaye amekuwa mwanadamu kwa ajili yangu, ili nipate kumpenda zaidi na kumfuata kwa karibu zaidi” (Ignatius wa Loyola, Mazoezi ya Kiroho, 104). Hapa, kumpenda Yesu na kuishi kwa Jina lake kunakuwa chanzo cha mabadiliko ya ndani na ujasiri wa utume.
Kwa Nini Jina Takatifu la Yesu Linabaki Muhimu Hata Katika Ulimwengu Mamboleo?: Dunia ya leo inakabiliwa na migogoro inayofanana kwa namna nyingi na ile ya karne ya Kumi na sita: Vita, ukosefu wa haki, upweke,majanga na hofu. Katika hali hii, Sikukuu ya Jina Takatifu la Yesu inaendelea kuwa mwaliko wa kugundua tena tumaini la kweli. Kuishi kwa Jina Takatifu la Yesu kunamaanisha kuchagua ukweli, haki, na huruma hata pale mazingira yanapokuwa magumu. Wajesuit wanaeleza kuwa imani ya Kikristo haiwatengi waamini na dunia, bali inawatuma ndani ya dunia kwa namna mpya. Kama Mkutano Mkuu wa 32 unavyosema, “Imani yetu katika Kristo haitutoi nje ya dunia, bali inatufunga nayo kwa namna mpya ya uwajibikaji” (GC 32, D.4, 18). Mwito wa Ujasiri na Huruma: Hadithi ya Wajesuit inatufundisha kuwa imani inayojikita katika Jina Takatifu la Kristo Yesu inaweza kubadilisha mgogoro kuwa ujasiri. Ni imani ambayo haikatai makosa ya dunia bali inakutana nayo kwa ujasiri na huruma. Urithi huu unatuita kila mmoja wetu kujiuliza: Ninawezaje kuishi zaidi katika Jina Takatifu la KristoYesu katika Ulimwengu mamboleo? Ninawezaje kuwa chanzo cha matumaini na uponyaji katika familia yangu, jamii yangu, na zaidi? Hitimisho: Kuendeleza Nuru ya Jina Takatifu la Kristo Yesu:Tunaposherehekea Sikukuu ya Jina Tukufu la Yesu, tukumbuke imani thabiti ya Wajesuit—imani ambayo iliwapa nguvu ya kubadilisha historia. Jina la Takatifu la Kristo Yesu liwe kimbilio letu na nguvu yetu. Litupe ujasiri wa kuishi kwa moyo mkuu, upendo wa kujitoa na kujisadaka, na hatimaye kujikita katika huduma yenye unyenyekevu. Katika dunia inayotamani: haki, amani na ukweli, Jina Takatifu la Kristo Yesu linaangaza kama taa ya mwanga na hivyo kutoa mwaliko kwa waamini kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya rehema na neema za Mungu.
