Fumbo la Umwilisho Liwe ni Kiini Cha Imani, Matumaini na Mapendo!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Noeli ni chemchemi ya Injili ya matumaini na furaha ya kweli; ni muda muafaka wa kumshukuru Mungu na utume unaopaswa kutangazwa na kushuhudiwa kwa watu wa Mataifa. Noeli ni Sherehe ya imani, matumaini na mapendo. Tafakari ya Fumbo la Umwilisho, Neno aliyefanyika mwili inatia moyo neno jipya na la kweli katika Kanisa lote kwa kuwataka waamini kutangaza na kushuhudia furaha ya Noeli, ambayo ni adhimisho la fumbo la imani, mapendo na matumaini. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Noeli ni sherehe ya imani, kwa sababu Mungu anakuwa mtu, aliyezaliwa na Bikira Maria. Ni sherehe ya upendo, kwa sababu zawadi ya Mwana mkombozi inatimizwa katika kujisadaka kidugu. Ni sherehe ya matumaini, kwa sababu Mtoto Yesu anawasha tena matumaini ndani ya waamini na hivyo kuwafanya kuwa ni vyombo na wajumbe wa amani. Wakiwa wamesheheni fadhila hizi nyoyoni mwao, kamwe hawawezi kuogopa usiku na kwamba, wanaweza kukabiliana kikamilifu na changamoto ya mapambazuko ya siku mpya.
Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatano tarehe 7 Januari 2026 wakati wa mzunguko mpya wa Katekesi unaojikita katika: Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na Usomaji Mpya wa Nyaraka zake, ili kugundua tena uzuri na umuhimu wa tukio hili la Kikanisa, amewakumbusha waamini kwamba, Katika kipindi hiki cha Sherehe za Noeli, Mama Kanisa anaendelea kulitafakari Fumbo la Umwilisho. Tafakari hii iwe ni dira na mwongozo wa mwaka mpya 2026. Lango la Jubilei ya Matumaini limefungwa lakini amana na utajiri wa Mama Kanisa unaobubujika kutoka katika huruma na upendo wa Mungu bado unaendelea kubaki wazi. Hii ni Jubilei iliyozinduliwa na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 24 Desemba 2024. Kwa hakika mahujaji wa matumaini kutoka sehemu mbalimbali za dunia wamepitia katika Lango hili, ambalo litaendelea kubaki wazi katika maisha ya kiroho kwa wale ambao bado wametia nia ya kuhatarisha maisha yao, wanaosikia hamu ya kuondoka na kutafuta ukweli wa maisha katika Kristo Yesu, Mwana wa Mungu anayejifunua kwa walimwengu.
Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kumwilisha matunda ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo kwa kuhakikisha kwamba, wanakuwa ni vyombo na mashuhuda wa tunu msingi za Kikristo; wakitafuta na kudumisha: haki na amani katika utakatifu. Waamini waendelee kuwa ni chemchemi ya matumaini, dira na mwongozo kwa waamini kukutana na walimwengu ili kuwatangazia na kushuhudia Habari Njema ya wokovu na kwamba, anawatakia maadhimisho mema ya Sherehe za Noeli zinazosheheni furaha ya kweli na amani; tayari kujenga na kudumisha Ufalme wa Mungu Mungu unaosimikwa katika: Upendo, haki na amani. Anawatakia waamini wote amani na utulivu wa ndani. Amewatakia Mapadre heri na fanaka wanapoendelea kubariki nyumba za waamini wao, faraja kwa wagonjwa, maskini na wakaa pweke!
