Tafuta

Askofu mkuu Carlo Roberto Maria Redaelli wa Jimbo kuu la Gorizia, Italia ameteuliwa na Baba Mtakatifu Leo XIV kuwa Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa Kwa Ajili ya Makleri. Askofu mkuu Carlo Roberto Maria Redaelli wa Jimbo kuu la Gorizia, Italia ameteuliwa na Baba Mtakatifu Leo XIV kuwa Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa Kwa Ajili ya Makleri.  (Vatican Media)

Askofu Mkuu Carlo. M. Redaelli: Katibu Mkuu Baraza La Kipapa Kwa Ajili ya Makleri

Papa Leo XIV, tarehe 22 Januari 2026 amemteua Askofu mkuu Carlo R. M. Redaelli wa Jimbo kuu la Gorizia, Italia kuwa Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa Kwa Ajili ya Makleri. Alizaliwa tarehe 23 Juni 1956, huko Jimbo kuu la Milano, Italia. Tarehe 14 Juni 1980 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tarehe 8 Aprili 2004 akateuliwa kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo kuu la Milano na kuwekwa wakfu tarehe 5 Juni 2004. Tarehe 28 Juni 2012 akateuliwa kuwa Askofu mkuu wa Gorizia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kutangaza na kushuhudia Injili ni dhamana na utume ambao Kristo Yesu amewakabidhi Mitume wake. Huu ni utume wa kwanza unaopaswa kutekelezwa na Mama Kanisa kwa kila mtu na kwa ulimwengu mzima. Utume huu unatekelezwa kikamilifu na Mama Kanisa anapotangaza na kushuhudia Injili ya upendo inayomwilishwa katika huduma makini kwa binadamu wote: kiroho na kimwili. Upendeleo wa pekee ni kwa maskini, wagonjwa na wadhaifu ndani ya jamii. Katika muktadha huu, Kanisa linapaswa kujikita katika wongofu wa kimisionari, kwa kuwa ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu. Kanisa lijitambulishe na kueleweka kuwa ni Fumbo la Ushirika unaomwilishwa katika dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 19 Machi 2022, Sherehe ya Mtakatifu Yosefu Mume wake Bikira Maria, aliridhia Katiba mpya ya Kitume inayojulikana kama “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu.”

Baraza la Kipapa Kwa Ajili ya Makleri ni muhimu sana katika utume wa Kanisa
Baraza la Kipapa Kwa Ajili ya Makleri ni muhimu sana katika utume wa Kanisa   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Kutokana na mabadiliko haya, Baraza la Kipapa kwa Ajili ya Makleri, limepewa dhamana nyeti sana inayogusa kiini cha maisha na utume wa Kanisa; kwa kuangalia malezi na majiundo ya Makleri; Kanuni na nidhamu ya maisha; utumishi wa mapadre unaoundwa na Makanisa mahalia, kwa kuzingatia ubora wake; Kwa kuwasaidia Maaskofu Jimbo kushuhughulikia kikamilifu: huduma ya kichungaji, nidhamu, na masharti yanayohitajika kutekelezwa ili huduma hii iweze kuwa ya kweli na inayozaa matunda yanayokusudiwa, kwa kukazia malezi na majiundo ya miito ya Kipadre ndani ya Seminari. Baraza linawasaidia  Maaskofu ili majimbo yaweze kukuza shughuli za kichungaji kwa kuangalia: juu ya maisha ya jumuiya na utawala wa seminari, ikithibitisha ulinganifu wao na mahitaji ya malezi ya kipadre kwa kujikita katika uadilifu.

Baraza la Kipapa Kwa Ajili ya Makleri: Muhimu katika maisha na utume
Baraza la Kipapa Kwa Ajili ya Makleri: Muhimu katika maisha na utume   (@VATICAN MEDIA)

Mwongozo wa Malezi ya Kipadre: “Ratio Fundamentalis Institutionis Sacerdotalis” unatoa kwa muhtasari wa sheria na kanuni msingi ambayo yanapaswa kuzingatiwa kwa ajili ya malezi na makuzi ya wito wa Daraja Takatifu ya Upadre. Unabainisha wajibu wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki; Waratibu wa Seminari kitaifa na kimataifa pamoja na mwongozo wa malezi ya Seminari moja moja. Baraza pia lina jukumu la kuratibu maisha na nidhamu ya Mapadre; malezi ya awali na yale ya kudumu; changamoto ya uhaba wa Mapadre unaoathiri ushiriki wa waamini walei katika Maadhimisho na Ushiriki wa Ekaristi Takatifu, hivyo ni sehemu ya kazi ya Baraza kuhakikisha kwamba, kuna kuwepo na uwiano mzuri wa Mapadre katika huduma za kichungaji. Baraza linashughulikia pia uongozi wa Makanisa mahalia. Katika mfumo huu, jukumu la Katibu Mkuu wa Baraza la Kipapa kwa Ajili ya Makleri ni nyeti na muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu: utawala wa shughuli za kichungaji, nidhamu, kanuni, taratibu, maisha na utume wa Kanisa.

Katibu Mkuu wa Baraza la Kipapa Kwa Ajili ya Wakleri ni muhimu sana.
Katibu Mkuu wa Baraza la Kipapa Kwa Ajili ya Wakleri ni muhimu sana.   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Leo XIV, tarehe 22 Januari 2026 amemteua Askofu mkuu Carlo Roberto Maria Redaelli wa Jimbo kuu la Gorizia, Italia kuwa Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa Kwa Ajili ya Makleri. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Carlo Roberto Maria Redaelli Katibu Mkuu wa Baraza la Kipapa Kwa Ajili ya Makleri alizaliwa tarehe 23 Juni 1956, huko Jimbo kuu la Milano, Italia. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 14 Juni 1980 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre mikononi mwa Hayati Kardinali Carlo Maria Martini, kwa wakati akiwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Milano.Tarehe 8 Aprili 2004 Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo kuu la Milano na kuwekwa wakfu tarehe 5 Juni 2004. Tarehe 28 Juni 2012 Baba Mtakatifu Benedikto XVI akamteuwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Gorizia, Italia na kusimikwa rasmi tarehe 14 Oktoba 2012. Tarehe 22 Januari 2026, Baba Mtakatifu Leo XIV akamteuwa kuwa ni Katibu Mkuu wa Baraza la Kipapa kwa Ajili ya Makleri. Katika huduma na utume wake wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kama Askofu msaidizi na hatimaye kama Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Gorizia amelitumia Kanisa kwa moyo wa ushirika, akitoa kipaumbele cha pekee kwa Makleri; Usikivu wa kichungaji; akajipambanua katika kukuza na kudumisha uwajibikaji wa Kikanisa; kwa kuhamasisha na kulea miito; kwa kujikita katika majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa watu wa Mungu aliopewa jukumu la kuwaongoza. Kwa uteuzi huu, Askofu mkuu Carlo Roberto Maria Redaelli Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa Kwa Ajili ya Makleri anaitwa kushirikiana na kushikamana katika kulinda, kutunza na kudumisha zawadi ya Daraja Takatifu; kwa kukuza huduma ya ushirika wa Kikanisa, huku akiweka mang’amuzi yake ya  shughuli za kichungaji, nidhamu na kanuni katika huduma ya Kanisa la Kiulimwengu.

Uteuzi
23 Januari 2026, 15:12