Ujumbe, Salam na Baraka za Papa Leo XIV: Urbi et Orbi Noeli 2025
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Ujumbe wa Noeli, Salam na Baraka kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, maarufu kama “Urbi et Orbi” ulianza kutolewa kwa mara ya kwanza na Mtakatifu Paulo VI kunako mwaka 1974. Kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii, ujumbe huu unawafikia watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia kwa njia ya mfumo wa matangazo yanayorushwa kwa njia ya satellite saba. Baba Mtakatifu Leo XIV katika Ujumbe wa Noeli, Salam na Baraka zake kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, “Urbi et Orbi” wakati wa maadhimisho ya Sherehe za Noeli tarehe 25 Desemba 2025, maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo amekazia kuhusu: Noeli ya Bwana ni Noeli ya Amani, Fumbo la Umwilisho linapata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, Kristo Yesu ni amani ya watu wake, Hija yake ya Kitume huko Mashariki ya Kati; Amani na faraja kwa waathirika wa vita, kinzani na mipasuko ya kijamii; Mama Kanisa anaanza kuhitimisha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, lakini Kristo Yesu ni Lango la mbingu ambalo daima liko wazi.
Baba Mtakatifu Leo XIV katika Ujumbe wa Noeli, Salam na Baraka kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, maarufu kama “Urbi et Orbi” tarehe 25 Desemba 2025 anasema: Noeli ya Bwana ni Noeli ya Amani, na hasa katika muktadha wa Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo yanayonogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini” na yanalenga pamoja na mambo mengine: kuwahamasisha waamini kuishi kwa matumaini na hivyo kuendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa fadhila ya matumaini inayokita mizizi yake katika imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Mama Kanisa anawaalika watoto wake wote kufurahi katika Bwana, kwa sababu Mwokozi amezaliwa duniani. Leo amani ya kweli imewashukia kutoka mbinguni. Mtoto Yesu amezaliwa na Bikira Maria, ndiye Kristo Bwana, aliyetumwa na Baba yake wa mbinguni kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti; huyu ndiye aliyeshinda giza na ubaya wa dhambi; chuki, uhasama na uadui kwa upendo wa huruma ya Mungu. Ni kutokana na muktadha huu, Noeli ya Bwana ni Noeli ya Amani.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Mtoto Yesu alizaliwa kwenye hori la kulishia wanyama kwani wazazi wake hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni na baada ya kuzaliwa tu, Mama yake akamvika nguo za kitoto, akamlaza katika hori ya kulishia ng’ombe na kwamba, kutokana na upendo wake kwa mwanadamu, Mwana wa Baba wa milele aliamua kuzaliwa na mwanamke, ili kushiriki ubinadamu na kwa njia ya upendo, akaupenda ufukara na hali ya kukataliwa, kiasi cha kujitambulisha na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya mwanadamu, akamtaka kila mwanadamu kuwajibika katika mchakato wa wokovu wake kwa mwamini kutambua na kukiri dhambi zake; akateswa, na kufa Msalabani, mwaliko kwa waamini kuonesha mshikamano na maskini pamoja na wale wote wanaoteseka. Amani inawawajibisha binadamu wote na kwamba, Kristo Yesu ndiye amani ya watu wake, kwa sababu amewakomboa kutoka katika utumwa wa dhambi na mauti na kuwaonesha njia ya kupitia na kwamba, anawaonesha waja wake njia ya kufuata ili kuondokana na kinzani binafsi na zile za Kimataifa. Waamini wanahamasishwa kuwa na moyo huru na wenye kusamehe na kusahau, ili kujenga na kudumisha amani duniani. Kristo Yesu aliteswa, akafa na kufufuka kwa wafu ili amkomboe mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, kumbe, Kristo Yesu ni mkombozi wa Ulimwengu, changamoto na mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kutekeleza dhamana na wajibu, ili kuzuia chuki, uhasama na vita, na hatimaye, wawe ni vyombo na wajumbe wa majadiliano katika ukweli, amani na upatanisho.
Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Leo XIV nchini Uturuki kuanzia tarehe 27 hadi tarehe 30 Novemba 2025 ilinogeshwa na kauli mbiu: “Bwana mmoja, Imani na Ubatizo Mmoja.” Baba Mtakatifu Leo XIV alikazia pamoja na mambo mengine: Umuhimu wa uinjilishaji, Utangazaji na ushuhuda wa Injili yaani “Kerygma” kuhusu: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, chemchemi ya wokovu. Utengano kati ya Wakristo ni kikwazo cha ushuhuda wa Injili ya Kristo Yesu. Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Leo XIV nchini Lebanon kuanzia tarehe 30 Novemba hadi tarehe 2 Desemba 2025 ilinogeshwa na kauli mbiu “Heri wapatanishi; Maana hao wataitwa wana wa Mungu.” Mt. 5:9. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwatakia amani watu wa Mungu nchini Lebanon, Palestina, Israeli na Siria akiwataka wawe na amani katika Kristo Yesu, kwani Yeye ameushinda ulimwengu. Wawe ni vyombo vya haki na amani na kwa hakika watapata amani na utulivu. Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwaombea watu wa Mungu Barani Ulaya na hasa wale wanaotoka nchini Ukraine na kuwataka wajenge moyo wa kijumuiya, mshikamano, huku wakidumisha fadhila ya uaminifu inayokita mizizi yake katika Ukristo, katika historia, mshikamano na ukarimu kwa watu wanaoteseka na hasa watu wa Mungu kutoka Ukraine. Ameitaka Jumuiya ya Kimataifa isitishe vita na kujielekeza katika mchakato wa ujasiri wa majadiliano katika ukweli, uwazi na kuheshimiana. Baba Mtakatifu amewaombea faraja na amani waathirika wote wa vita, kinzani na mipasuko ya kijamii; watu wanaoteseka kutokana na ukosefu wa haki, amani na utulivu wa kisiasa, nyanyaso na madhulumu ya kidini pamoja na vitendo vya kigaidi. Baba Mtakatifu amewakumbuka kwa namna ya pekee watu wa Mungu kutoka Sudan Kongwe na Sudan ya Kusini, Mali, Burkina Faso pamoja na DRC.
Katika Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Matumaini, Mwana wa Mungu aliyefanyika mwili, awe ni faraja kwa watu wa Mungu nchini Haiti, ili kinzani na mipasuko ya kijamii, iweze kukoma na hatimaye, waanze kujielekeza katika njia ya amani na upatanisho wa Kitaifa. Watu wa Mungu Amerika ya Kusini, wenye wajibu wa kisiasa kwa watu wao, wapambane na changamoto mamboleo kwa kutoa kipaumbele cha kwanza katika majadiliano, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na kuachana na itikadi zinazokwamisha maendeleo. Watu wa Mungu nchini Myanmar waone mwanga wa upatanisho wa Kitaifa, Mfalme wa amani awakirimie matumaini vijana wa kizazi kipya, awaongoze watu wote wa Mungu katika njia ya amani, awasindikize watu wasiokuwa na makazi ya kudumu, usalama wa maisha yao, wale waliovunjika na kupondeka moyo kwa siku za usoni. Kristo Yesu, awezeshe kurejesha tena urafiki na mahusiano mema kati ya Thailand na Cambodia, ili waendelee kujikita katika mchakato wa upatanisho, haki na amani. Baba Mtakatifu Leo XIV amewaaminisha watu wa Mungu kutoka Barani Asia na Oceania walioathirika sana kutokana na mabadiliko ya tabianchi chini ya ulinzi na tunza ya Mtoto Yesu. Watu watakatifu wa Mungu wajitahidi kila mtu kadiri ya uwezo wake kuwasaidia watu wote wanaoteseka. Baba Mtakatifu Leo XIV amewakumbuka na kuwaombea watu wanaoishi Ukanda wa Gaza, wanaosiginwa na umaskini, njaa, maradhi na utupu; wanaokimbia makazi yao wakitafuta hifadhi, usalama na maisha bora ugenini nasa Amerika; Vijana wanaotafuta fursa za kazi na ajira; wale ambao utu, heshima na haki zao msingi zinasiginwa. Kwa hakika watu wana kiu ya amani ya kudumu, ili kupata amani ya kweli, hawana budi kumpokea na kumkaribisha Mtoto Yesu katika maisha yao.
Kristo Yesu ndiye Lango la maisha ya uzima wa milele, anayewashirikisha waja wake Fumbo la upendo na huruma ya Mungu isiyokuwa na mipaka; huruma inayowakumbatia binadamu wote pasi na ubaguzi, changamoto na mwaliko wa kuambata toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha. Huu ni mlango unawaohamasisha waamini kujikita katika upendo kwa Mungu na jirani kwa kuambata Injili ya furaha, daima wakimwangalia Kristo Yesu waliyemtoboa kwa mkuki ubavuni, kimbilio la wakosefu na wadhambi; watu wanaohitaji msamaha, amani na utulivu wa ndani. Kristo Yesu ni mlango wa huruma na faraja, wema na uzuri usiokuwa na kifani. Huu ndio mlango wanamopita watu wenye haki. Kristo Yesu ni mlango wa mbingu, unaowaalika wote kushiriki furaha ya uzima wa milele. Yesu anawasubiri kwa moyo wa huruma na mapendo, wale wote wanaomwendea kwa toba na wongofu wa ndani. Bikira Maria, nyota ya asubuhi anawaongoza waamini kwa Kristo Yesu, ambaye ni Lango la huruma ya Mungu.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Makanisa yameanza kufunga Malango ya Jubilei ya Matumaini, kama hitimisho la Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo. Lakini Kristo Yesu ni Lango la Matumaini kwa waja wake, ataendelea kubaki akiwa anaambatana na watu wake, ni Lango linalowapeleka watu wa Mungu katika maisha ya Kimungu. Mtoto aliyezaliwa ni Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, anayekuja kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko uletao maisha na uzima wa milele. Kristo Yesu anakuja kuganga na kuponya madonda yanayo mwandama mwanadamu na kwa wale waliovunjika na kupondeka nyoyo wanapata amani na utulivu wa ndani. “Noeli ya Bwana ni Noeli ya Amani.” Ndivyo Baba Mtakatifu Leo XIV alivyohitimisha Ujumbe wa Noeli, Salam na Baraka kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, maarufu kama “Urbi et Orbi” tarehe 25 Desemba 2025.
Wakati huo huo, Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar Es Salaam, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC katika Kesha la Noeli kwa mwaka 2025 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yosefu amewaalika watanzania kujitosa kupigania haki, na kwamba, haki na mani ni mambo yanayotegemeana na kukamilishana; ni zawadi na wasifu unaofungamana na Kristo Yesu Mwokozi wa Ulimwengu.
